KWA NINI TUPOTEZE MUDA
MWINGI NA FEDHA NYINGI KUJADILI “NDIYO”?
“Ukisema, ‘Ndiyo’, basi,
iwe ‘Ndiyo’; ukisema, ‘Siyo’, basi iwe kweli ‘Siyo’. Chochote kinachozidi
hayo hutoka kwa yule Mwovu” (Matayo
5:37). Haya ni maneno ya Yesu Kristu wa Nazareti wakati akiwafundisha wafuasi
wake. Somo lenyewe lilikuwa juu ya mtu kuwa na msimamo, uadilifu na uaminifu;
kuwa na msimamo wa mtu binafsi, msimamo wa familia na hatimaye msimamo wa taifa
zima la Israeli; Kwamba mtu ukiamua kuisimamia “Ndiyo” basi aisimamie bila
kuteteleka na akiamua kuisimamia “Siyo” vile vile aisimamie bila kuyumba. Na
kwamba mtu akiisimamia “Ndiyo” ukijua kwamba ni “Siyo” ni unafiki na uovu. Vile
vile akiisimamia “Siyo” ukijua kwamba ni “Ndiyo” ni unafiki na uovu!
Kwa maneno mengine mtu
mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu hawezi kujiwekea kikao cha kujadili
“Ndiyo” anayoijua ni “Ndiyo” na “Siyo” anayoijua ni “Siyo”. Mtu mwenye msimamo,
uadilifu na uaminifu daima anakuwa mbali na unafiki na uovu. Hii ni falsafa ya
Yesu wa Nazareti, aliyowafundisha wafuasi wake; bila kuingilia maswala ya
imani, mtu yeyote anaweza kuitumia falsafa hii katika maisha yake maana ina
msingi chanya wa kuendesha maisha katika jamii yoyote ile.
Wakati Yesu wa Nazareti
akifundisha falsafa hii ya msimamo, uadilifu na uaminifu katika jamii ya
Wayahudi; jamii yenyewe ya Wayahudi ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha
mabadiliko; watawala waliabudu madaraka na mali; walipinduana katika utawala,
walisalitiana na wakati mwingine waliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe;
unafiki na uovu viliongoza maisha yao ya siku kwa siku; kuna wanaojenga hoja
kwamba Yesu wa Nazareti, alikuwa mwanasiasa aliyeguswa na hali ya maisha ya
watu katika jamii yake ya Wayahudi. Kwa wale wanaoipokea imani ya Kikristu bila
kuchimba kwa kina historia, theolojia na elimu ya Biblia, watasema mimi ni
mzushi; lakini ukweli utabaki pale pale kwamba Yesu wa Nazareti alizaliwa
katika jamii Fulani na kuishi akizungukwa na historia, utamaduni na desturi za
watu wake; ingawa sisi hapa Tanzania hatujafikia hatua ya kupigana vita vya
wenyewe kwa wenyewe; hatujabaguana na kushindana kama walivyokuwa wana wa
Israeli; unaweza ukafananisha hali ya Uyahudi ya wakati ule na hali ambayo
taifa letu la Tanzania linapitia hivi leo. Unafiki na uovu vinawaongoza
watawala wetu; hivyo tunahitaji msimamo, uadilifu na uaminifu. Tunahitaji
viongozi watakaosema “Ndiyo” wakimaanisha “Ndiyo” na watakaosema “siyo”
wakimaanisha “Siyo”. Hali ilivyo sasa hivi ni kwamba viongozi wetu wanasema “Ndiyo”
wakimaanisha “Siyo” na wanasema “Siyo” wakimaanisha “Ndiyo”. Tuna viongozi
ambao wanacheka kumbe wanalia, na ambao wanalia kumbe wanacheka! Tuna wabunge
wanaosinzia Bungeni wakisingizia kutafakari; wakibanwa zaidi wanasema huo ni
uchochezi wa waandishi wa habari. Wabunge wetu walipambana kufa na kupona
waitwe “Waheshimiwa” na kusahau kabisa kwamba waheshimiwa ni wananchi
waliowatuma Bungeni.
Katika familia zetu,
katika jamii zetu na katika taifa letu, tunahitaji msimamo, uadilifu na
uaminifu. Hatuwezi kujenga familia, jamii na taifa imara bila kuwa mbali na
unafiki na uovu. Bila kujenga utamaduni wa “Ndiyo” kuwa ni “Ndiyo na
“Siyo” kuwa ni “Siyo”, hatuwezi kupiga
hatua ya maendeleo bila kuizingatia falsafa hii.
Lengo la makala hii si
kujadili “Ndiyo” ni nini katika maisha Mtanzania na “Siyo” ni nini? Kama
inavyofafanuliwa katika falsafa ya Yesu wa Nazareti, maana jinsi mambo
yanavyokwenda ni kwamba sisi kama taifa hatujakubaliana “Ndiyo” ni nini na
“Siyo” ni nini. Na kama makubaliano haya yapo, kitu ambacho sina imani kubwa
nacho, basi ni lazima tukubaliane kwamba msimamo, uadilifu na uaminifu
vimezikwa kaburi moja na Azimio la Arusha! Huu ni mjadala mrefu ambao
ninafikiri unahitaji makala inayojitegemea. Ni mjadala ambao ni lazima
kuendeshwa kwa uangalifu mkubwa ili kukwepa ushawishi wa kuichukulia falsafa
yenyewe kama kichocheo cha udini.
Watanzania wakitaka kupindisha ukweli wanauweka udini mbele. Wakati mwingine
udini ni silaha ya kuifumba midomo ya watu na kulenga kuwatenga watanzania
kwenye makundi ili wasishirikiane kudai haki zao kutoka kwa watawala. Hivyo
falsafa hii ya “Ndiyo” na “siyo” nitaijadili wakati muafaka ukifika.
Hoja ninayoijenga
leo kwenye makala hii ni kule kupoteza
muda mwingi na fedha nyingi kuijadili “Ndiyo” ambayo hata kama watu wengi
wanajua na kuamini kwamba ni “Siyo” lakini watawala na mfumo uliopo unaamua
kwamba ni “Ndiyo”. Tunahitaji muda kuyashughulikia mambo mengine mengi maana
taifa letu bado ni masikini; tunahitaji
fedha kutekeleza mipango mingi ya maendeleo; kwa nini basi muda huu
unaohitajika hivyo na fedha hizi za maendeleo vitumike kujadili “Ndiyo”.
Tunalalamikia ufinyo wa
bajeti. Kila wizara inalalamika kupata mgawo kidogo kutoka kwenye mfuko wa
taifa letu. Watanzania walio wengi wanashauri wizara zote bajeti zao zipanuliwe
na kuongezewa fedha nyingi na hasa fedha inayowalenga watanzania wanaoishi
pembezoni.; badala yake tunawaweka wabunge pale Dodoma kwa kipindi cha miezi
miwili, wakitumia fedha za Watanzania. Siku za kuishi Dodoma zikipunguzwa, ni
wazi fedha nyingi zitapatikana ili ziongezewe kwenye bajeti za wizara mbali
mbali. Ingawa sina takwimu za fedha wanazolipwa wabunge wetu, ni wazi siku
zaidi ya 30 zikipunguzwa kwenye siku
ambazo wabunge wanalazimika kuishi Dodoma, tutapata fedha ya kutosha kufanya miradi
mingine ya maendeleo.
Bajeti yetu ya taifa
inayojadiliwa kila baada ya mwaka mmoja kwa utawala na mfumo uliopo sasa ni
“Ndiyo”. Ijadiliwe isijadiliwe ni lazima ipitishwe. Hata pale inapoonekana wazi
wazi kwamba kuna ulazima wa kubadilisha kama inavyojionyesha kwenye bajeti ya
mwaka huu ya Nishati na Madini, bado bajeti inapitishwa hivyo hivyo maana
wabunge wa chama tawala ni wengi kuliko wa upinzani. Wakati mwingine
inasikitisha zaidi bajeti inapopitishwa hata bila kujadili vifungu vyote kwa
kisingizio cha kukimbizana na muda. Hoja ni kwamba kwa nini wabunge wakae
Dodoma miezi miwili wakijadili “Ndiyo”. Ni busara gani inayotumika? Ni msimamo
gani? Ni uadilifu gani na ni uaminifu gani wa wabunge wetu kutumia muda wote
huo na fedha nyingi hivyo wakijadili “Ndiyo”? Kama lengo ni wabunge kuibariki
bajeti, kwa nini bajeti isisomwe kwa siku mbili au tatu na kupitishwa ili kuokoa muda na fedha?
Bunge letu lina
utamaduni wa kupitisha mambo kwa swali: Wanaokubali waseme “Ndiyo” na
wasiokubali waseme “Siyo”. Kufuatana na utawala na mfumo tulio nao kwa sasa
hivi jibu ni “Ndiyo”. Hata pale ambapo na watoto wadogo wanaweza kutambua
kwamba “Ndiyo” ni “Siyo”, na wakati mwingine sauti za wabunge wanaosema “Siyo”
ni nyingi zaidi ya wale wanaosema “Ndiyo”, Spika na wasaidizi wake watasema wa
“Ndiyo” wameshinda maana vichwani mwao hakuna kitu kingine zaidi ya “Ndiyo”.
Sina magomvi na Spika na
wasaidizi wake kujaza “Ndiyo” vichwani mwao; maana huu pia ni mjadala mkubwa.
Mfumo wetu wa utawala unamlazimisha Spika kuyatanguliza maslahi ya chama chake
kabla ya kitu kingine kile. Spika wetu anatoka chama cha CCM ambacho ndicho
chama tawala, hawezi kwenda kinyume na matakwa ya chama chake; chama kinataka bajeti ipite jinsi
ilivyo; hata kama busara ya Spika inamwelekeza kuunga mkono hoja za wapinzani
zenye kujenga, ni lazima yeye aangukie upande wa chama chake: Kwa maneno
mengine, Spika anakuwa mlinzi na msimamizi wa masilahi ya chama chake ndani ya
Serikali. Hili linaeleweka, hata kama halikubaliki! Magomvi yangu si kwa spika tu
bali kwa Bunge zima: Kwa nini tupoteze muda mwingi na fedha nyingi kujadili
“Ndiyo”?
Mfumo wetu wa utawala,
ni kwamba Mawaziri na manaibu wao ni lazima wawe wabunge. Hivyo Bunge linapokaa
Dodoma miezi miwili kujadili “Ndiyo” mawaziri na manaibu wao wanakuwa Dodoma;
ndivyo inavyopaswa kuwa ingawa wakati mwingine tunashuhudia viti vikiwa wazi.
Wakiwa Dodoma, majukumu yao mengine yanakwamba au yanakwenda kwa kasi ndogo. Na
mbaya zaidi kukaa kwao Dodoma ni matumizi mengi ya fedha, mbali na posho zao wa
kibunge kuna matumizi mengine ya ziada ya kuzitunza ofisi mbili za mawaziri
Dar-es-Salaam na Dodoma kwa wakati mmoja.
Kwa kupendekeza muda wa bunge la bajeti kupunguzwa
kutoka miezi miwili ya sasa hadi siku
tatu, sina lengo la kubeza na kutoutambua mchango wa wale wanaotoa hoja
nzito za kuonyesha kwamba “Ndiyo” inaweza kugeuka na kuwa “Siyo”. Ninaheshimu
sana mchango wa wabunge wa upinzani. Wanafanya kazi nzuri; wanaonyesha msimamo,
uadilifu na uaminifu kwa wapiga kura wao. Nguvu zao hazipotei bure, ingawa wakati
mwingine wanatia huruma; maana mtu kuwaonyesha wenzako mwanga, wakaukataa na
kukumbatia giza ni jambo linaloumiza na kukatisha tamaa, lakini hata hivyo
hakuna hitaji la kukata tamaa maana historia inaandikwa, vizazi vijavyo
vitasoma na kutoa hukumu. Na kusema ukweli wapinzani wanavikalia viti vyao
Bungeni kwa uaminifu, ukilinganisha na wabunge wa chama tawala ambao mara
nyingi viti vyao vinakuwa wazi. Pamoja na kuheshimu na kuukubali mchango wa
wapinzani Bungeni, nafikiri ingekuwa bora kwao kutoa mchango wao kwa maandishi
ili kuepusha kurefusha muda wa Bunge la bajeti. Kufuatana na uzoefu na kwa
mfumo wa utawala uliopo sasa hivi “Ndiyo” itabaki kuwa “Ndiyo”, si busara
kujadili “Ndiyo” hata kama wapinzani wanao mchango mzuri. Ni kiasi cha waziri
kusimama na kusoma bajeti yake; bila majadiliano ikapitishwa. Majadiliano
hayana amaana yoyote wakati kitu kimeamuliwa tayari.
Tumeshuhudia jinsi
wabunge wa upinzani walivyoshikilia bango la kupinga posho za wabunge. Hoja yao imeeleweka na imeungwa mkono na
watanzania wengi. Nafikiri wakati umefika wabunge hawa wa upinzani kushika bango jingine la kupinga Bunge la
bajeti kukaa miezi miwili likijadili “Ndiyo”. Ni imani yangu kwamba na hoja hii
itaeleweka na kuungwa mkono na watanzania wengi na kuchochea kilio cha kutaka
katiba mpya. Wengine wanafikiri katiba si suluhisho la matatizo yetu kama
taifa, ukweli ni kwamba ikiandikwa kwenye katiba kwamba ili “Ndiyo” ifikiwe ni
lazima wabunge wajadili kwa kina na kupiga kura za siri bila shinikizo lolote
kutoka kwenye chama chake.
Ni lazima kushirikiana
sote; vyama vya upinzani, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, mashirika ya
dini na watu wengine wenye nia njema
tuungame kwa pamoja kupinga Bunge letu kupoteza muda mwingi kujadili ”Ndiyo”
Na
Padri Privatus
Karugendo,
0 comments:
Post a Comment