NI UFISADI, USHAURI MBAYA AU KUTOKUSIKIA?

Vita ya kupambana na mafisadi wa nchi ilianzia mbali, watu wengi wameshiriki vita hii, tumeandika mengi, tumeonya, tumetoa maoni na kutabiri mambo mbali mbali ambayo leo hii yanaonekana. Nakumbuka kuandika makala juu ya wapambe wa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, nikisisitiza kwamba matatizo mengi yanaletwa na wapambe wake, ukweli ambao umejionyesha wazi mbele ya macho yetu. Na ikitokea Rais Kikwete kukwama kabisa, atakuwa amekwamishwa na wapambe wake. Badala ya kumsaidia wanamdidimiza kiasi kwamba akimaliza utawala wake atakumbukwa kwa mgawo wa umeme, maisha magumu, maandamano na mengine mengi asiyopendeza kuandikwa kwenye historia yoyote ile. Katibu Mkuu anayeshutumiwa kuchangisha fedha za kupitisha Bajeti ya Nishati na madini ni miongoni mwa wa pambambe wa karibu sana wa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete.
Hata hatua aliyochukuliwa ya likizo ya siku 10, ili achunguzwe ni kielelezo tosha cha uswahiba wake na Rais. Maana ukiachia mbali shutuma ya kuchangisha fedha za kuhonga ili kupitisha bajeti, bado Bajeti yake imekataliwa. Kitendo cha Bajeti ya wizara kukataliwa kwa vigezo vinavyoonyesha “Uzembe” kama kukosea takwimu na mengine mengi, inatosha mtu kujiuzulu au kuwajibishwa na Bosi wake. Lakini huyu anapewa likizo na tena likizo yenye malipo! Tatizo lenyewe ni kubwa zaidi ya Serikali inavyotaka tuamini. Bajeti haiwezi kufika Bungeni bila kujadiliwa na Baraza la mawaziri na makatibu wakuu wote. Kama bajeti ya Nishati na Madini ilipitia mchakato wote huo na bado ikaonekana ni ya ovyo, basi kuna sababu ya msingi ambayo ni lazima mtu kuwajibika.
Kama kuna mshauri mzuri anayehitajika sasa hivi kwenye taifa letu, ni yule wa kumweleza Mheshimiwa Rais wetu, kuonyesha upande wake katika kupambana na mafisadi. Huu ni wakati wake kujitoa muhanga, huu ni wakati wake kukubali kuwapoteza marafiki ili kuliponyesha taifa zima. Ni kazi ngumu kuwapoteza marafiki – maana kuachana na mtu si kama vile kuvua nguo na kuiweka pembeni. Lakini pia ni kazi ngumu kuirudisha amani ya nchi ikishavurugika. Hapa ni lazima Rais wetu apime na kuchagua fungu lililo bora; kuwapoteza marafiki wachache nchi ikapata amani na utulivu ama kuwakumbatia marafiki wachache na nchi ikaingia katika machafuko. Uamuzi huu ni wa haraka maana tuko nyuma kabisa ya muda; wanaotuhumiwa wanaishi miongoni mwetu; maisha yao yanajulikana; kama wana fedha nyingi zisizokuwa na maelezo watu wanaona na uvumilivu wa kuyapokea machungu ya maisha kupanda utafikia mwisho wakiwaona wanaofikisha hapo wanaendelea kula nchi.
Tunasikia machafuko yameanza kwa jirani zetu wa Malawi. Tusifikiri kuwa sisi ni wa pekee; yanaweza kutufika pia na kwa kujitakia na wala hatuna ulazima wa kumtafuta mchawi kama anavyofanya Mheshimiwa Membe, kwa kutaka kutuaminisha kwamba baadhi ya Mabozi wa nchi za nje wanatumika kuanzisha vurugu hapa kwetu. Mchawi ni sisi wenyewe! Tulikuwa tukiyasikia machafuko na maandamano nchi za mbali kama vile Libya, Tunisia na Misri. Sasa Malawi ni karibu sana na vurugu hizi kusambaa na kuingia ndani ya nchi yetu ni kitu kilicho karibu sana. Machafuko ya Malawi yameletwa na gharama za maisha kupanda. Wananchi wanataka Raisi ajiuzulu. Matatizo ya Malawi  ni sawa na yale tuliyo nayo sisi hapa Tanzania. Bei ya vyakula inapanda, mafuta ya taa yanapanda na tatizo la umeme linaongeza makali ya ugumu wa maisha, ufisadi unaendelea kuwa na nguvu na mafisadi wanakingiwa kifua; kuendelea kumtafuta mchawi ni upumbavu na kujidanganya. Katika hali kama hii ambayo wananchi wengi wanafikiri tumefikia hali hii kwa sababu ya ufisadi mkubwa; ingekuwa vizuri kujua Rais wa nchi yuko upande gani.
Rais ni mtu, ana familia, ana ndugu na jamaa, ana marafiki na wapambe wa kufa na kuzikana, lakini pia ni taasisi wakati huo huo. Kwa hiyo ni vema watu wakaelewa toka mapema kuwa vita ya kupambana na ufisadi nchini Rais wao anasimama wapi. Kwa vyovyote vile upande atakaokuwa Rais wa nchi ndio utakaoshinda. Najua haya si maneno mazuri kuyasema, lakini Tanzania yetu wote tunaijua, kuwa kiongozi wa nchi anategemewa sana kutoa mwelekeo wa vita yoyote.  Raisi anapokuwa na kigugumizi kuwawajibisha watu wenye harufu ya ufisadi kama ilivyotokea kwa Katibu Mkuu wa Nishati wa Madini, inatisha! Kwa nini mtu atumie hongo kupitisha bajeti ya Wizara? Maana yake ni nini? Kuna siri? Kuna mambo ya ovyo? Kuna fedha zilizopangiwa (hewa) kazi isiyokuwepo? Kumkingia kifua Katibu wa Nishati na Madini, kunatia shaka.
Ni kweli kwamba ili kutenda haki, kuna ulazima wa kumpatia nafasi Katibu Mkuu wa Nishati na Madini kujitetea kuhusu shutuma hii ya kukusanya fedha za kupitisha bajeti. Yeye kama watanzania wengine ni lazima alindwe na sheria. Lakini je hili la Bajeti yake kuwekwa pembeni ni nani wa kuwajibika? Au ni nani wa kumwajibisha? Au Bajeti yake imehujumiwa na wabaya wake? Ambao kwa maneno mengine ni wabaya wa Mheshimiwa Rais, maana kuikataa bajeti kunaweza kupelekea “Kura ya kutokuwa na imani”. Hili nalo linawezekana maana makovu mengi hayajaponyeshwa.
 Makovu ya yale yaliyotokea kwenye uchaguzi mkuu wa 2005, hayakutafutiwa dawa. Hivyo baada ya uchaguzi makovu haya yaliendelea na bado yanachimba na kusimika mizizi. Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, alifikiri dawa pekee ni kuendelea kuongoza bila kutibu makovu. Nina mashaka kama alifanya juhudi binafsi za kuyamaliza makundi ndani ya CCM, kuwapatanisha wanamtandao na wale waliokuwa nje ya mtandao. Kutamka kwamba makundi yamekwisha, si dawa! Panahitajika kazi ya ziada. Nafikiri Rais wetu alipaswa kuelekeza kwanza nguvu zake katika kutibu makovu ndani ya CCM na taifa kwa ujumla kuliko kujenga mahusiano yetu na nchi za nje.  Watu kama Malecela, Sumaye, Salim, Mwandosya, Butiku, na wengine walipata makovu makubwa.  Baada ya uchaguzi Rais alifanya makosa ya kiutendaji kwa kuwateua baadhi yao kuingia katika vyombo muhimu bila kwanza kuponya makovu na kuhakikisha yamepona kweli. Hawa ni mwiba na sitaki kusema zaidi. Yeye anadhani wanaongoza kumkwamisha lakini kimsingi yeye anajikwamisha kwa kuamua kufa na tai shingoni.
Najiuliza, tatizo la Rais wetu kushindwa kufanya maamuzi magumu ni kwa vile amezungukwa na mafisadi? Ni ushauri mbaya au ni yeye kuwa na matatizo ya kutokusikia?
Na,
Padri Privatus Karugendo.


0 comments:

Post a Comment