NCHI YETU TANZANIA
Tarehe 19.8.2011 Maa
Media Centre ilizindua vipindi vya televisheni
vya Nchi yetu vitakavyoanza kuonyeshwa hivi karibuni kwenye TBC.
Uzinduzi huu ulifanyika kwenye ukumbi wa New World Cinema (Nyerere Gallery
–Mwenge). Mgeni rasmi katika uzinduzi huu alikuwa Waziri wa Habari, utamaduni
na Michezo Mheshimiwa Nchimbi.
Ni jambo la kufurahisha
na kusifia Waziri anapotambua wajibu wake kama alivyofanya Mheshimiwa Nchimbi
kuzindua shughuli zilizo chini ya wizara yake. Kazi za Mawaziri si kukaa
maofisini, bali ni kuzunguka nchi nzima kuhakikisha sera za chama chao na
mipango ya serikali inatekelezwa. Kasoro iliyojitokeza (nilivyoona mimi) ni
Mheshimiwa Nchimbi, kuwa Dar-es-Salaam, akizindua vipindi vya Maa Media Centre,
wakati alitakiwa kuwa Bungeni Dodoma akiwawakilisha wapiga kura wake katika
Bunge la Bajeti. Labda ufunguzi huu ungesogezwa mbele hadi mwisho wa Bunge la
bajeti. Hata hivyo si Mheshimiwa Nchimbi peke yake, tumekuwa tukishuhudia baadhi
ya Mawaziri wakiwa Mikoani, Dar-es-Salaam au nje ya nchi wakati Bunge
likiendelea. Hata wabunge wengine ambao si mawaziri tunashuhudia wakiwa nje ya
Dodoma wakati Bunge likiendelea. Ni vigumu kuwa na wabunge wote asilimia
miamoja wakati Bunge linaendelea; kuna wagonjwa na wengine wenye sababu za
msingi ambazo ziko juu ya uwezo wa mwanadamu; lakini Bunge linapofikia hatua ya
kuwa hata chini ya nusu, inatisha na kutia mashaka. Je kanuni za Bunge
zinalegea sana inapofikia kwenye mahudhurio?
Au ni makosa tunayoyafanya ya kuwapatia wabunge wetu uwaziri na
kuwachagua wabunge wenye shughuli nyingi binafsi ambazo haziwezi kuwaruhusu
kukaa Bungeni muda wote?
Watu wengi wakiwemo na
baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, walifika pale Mwenge
kushuhudia uzinduzi wa vipindi hivi vilivyoandaliwa na Maa Media Centre ambao
pia ndio wanaoandaa na kurusha kipindi cha Dala Dala.
Vipindi hivi vya Nchi
yetu vitajikita kwenye Haki za binadamu ndani ya nchi yetu ya Tanzania na
vitarushwa na TBC kwa miezi mitatu
mfululizo. Ni vipindi vilivyofanyiwa utafiti wa kina na kuandaliwa si chini ya
miezi sita kwa ufadhili wa Tanzania Media Fund, mfuko unaolenga kuboresha na
kuinua kiwango cha kuandika habari za uchunguzi katika taifa letu la Tanzania.
Kwa kuzindua vipindi
hivi Maa Media Centre walionyesha kipindi kimoja wapo cha ukatili majumbani
kati ya vingi walivyoviandaa; matukio
ya ukatili yaliyotokea Zanzibar, Jijini Mwanza na Magu-Mwanza. Kule Zanzibar
mama mmoja alipigwa na mme wake hadi akawa kipofu na kule Magu – Mwanza, mama
mwingine mme wake walimkata pua na masikio na Jijini Mwanza, mama alipigwa na
mme wake akiwa na mtoto mgongoni. Ni ukatili wa kutisha, hata hivyo ni ukweli
ambao tunaishi nao katika nchi yetu ya Tanzania. Ukatili majumbani unasababisha
vifo vya wanawake na watoto, kuvunjika kwa ndoa, ukosefu wa amani na utulivu
katika familia, watoto wa mitaani na watoto wanaoishi kwenye mazingira
hatarishi.
Kwenye hotuba yake ya
uzinduzi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Nchimbi,
aliwapongeza Maa Media Centre kwa mafanikio yao ya kutengeneza vipindi vizuri
vinavyoelimisha na kuwataadharisha wasiige mifano ya wale waliotengeneza
utamaduni wa kuonyesha na kuandika juu ya mambo mabaya tu katika taifa letu. “
Kuna wale wanaotuonyesha wanafunzi wamekaa chini, hivi kweli hapa Tanzania
hakuna wanafunzi wanaokalia madawati? Mbona hawaonyeshwi? Kwa nini itolewe
mifano ya walimu wanaofundisha vibaya? Kwani hapa Tanzania hakuna walimu
wanaofundisha vizuri? Kwa nini tunataka kujenga utamaduni wa kuonyesha mabaya
tu katika Taifa letu?” Alihoji Mheshimiwa Nchimbi. Alisema kwamba kati ya
vipindi ambavyo Maa Media Centre wameandaa kuna kipindi kinachoelezea maisha ya Mwalimu mmoja aliyeanza
kufundisha mwaka 1972 na kuendelea kuishi maisha duni hadi leo hii anamiliki
kiti kimoja kwenye nyumba yake. “Msituletee mifano hii, mtu ambaye alianza
kufundisha mwaka 1972, hadi sasa ameshindwa kuyaboresha maisha yake ni mlevi
tu, hakuna maelezo mengine. Mimi, baba yangu alikuwa mwalimu, kama angekuwa
aina ya huyo wa kiti kimoja basi na mimi nisingekuwa hapa leo hii….Tuonyesheni
mifano ya walimu waliofanikiwa na wala si mifano ya wale walevi walioshindwa
maisha….Tuonyesheni na mambo mazuri katika nchi yetu, msituonyeshe mabaya tu..”
Alisisitiza Waziri Nchimbi.
Kwa Maoni ya Waziri
Nchimbi, ni kwamba vitengenezwe vipindi vinavyoonyesha familia zinazoishi kwa
amani. Waonyeshwe wanaume wanaopenda wake zao na kuishi bila kupigana ili watu
wengine waige. Yeye anaamini kwamba familia hizo zipo. Vitengenezwe vipindi vinavyoonesha
watoto wamekalia madawati na walimu wanafundisha vizuri. Anaamini Tanzania kuna
mambo mazuri yanayotendwa na watu na serikali yao.
Maa Media Centre,
waliijibu hotuba ya Waziri Nchimbi kwa unyenyekevu mkubwa. Walisema lengo lao
si kuonyesha mabaya bali ni kuibua hali halisi; watu waone, wajadili na
hatimaye kwa pamoja tutafute suluhu na kuyabadilisha maisha yetu: “ Ni vigumu
kuwaridhisha watu. Tuliandaa kipindi cha Mwalimu Nyerere, kiliporushwa watu
walilalamika kwamba tulionyesha mazuri
peke yake…sasa Mheshimiwa Waziri anatutaadharisha tusionyesha mabaya peke yake…
tunajitahidi na kuamini kwamba kwenye mijadala uwiano utajitokeza. Tunaamini
kwa kuonyesha hali halisi watu wanaweza kujifunza na kuyabadilisha maisha
yao..” Alisema Furaha wa Maa Media Centre.
Vipindi vya Maa Media
Centre, vitakuwa vinaonyesha ukiukwaji wa Haki za Binadamu. Inawezekana kabisa
kuandaa vipindi vinavyoonyesha watu wanaozingatia haki za binadamu. Hapana
shaka kwamba vipindi hivi vinaweza kusaidia kufundisha na kuyabadilisha maisha
ya watu. Hili wala halina mjadala. Inawezekana kabisa kuandaa vipindi
vinavyoonyesha kwamba Tanzania ni nchi ya neema, nchi yenye mafanikio, nchi
yenye utulivu na amani; tunaweza kutengeneza vipindi kama vile vya Libya,
vilivyoonyesha mazuri matupu kumbe chini ulifunikwa moto mkali ambao sasa
umeripuka na kuleta maafa makubwa. Tunaweza kutengeneza vipindi vizuri vya
kuelezea mafanikio yetu kama vile vya Idi Amin Dada wa Uganda hadi kufikia
kutengeneza fedha nyingi zaidi kama shilingi yetu inashuka thamani; Iddi Amin,
aliyafunika mabaya na kutangaza mazuri, wakati ulipowadia hakuweza kuyafunika
tena! Hoja ya wanaharakati wa Haki za Binadamu ni kwamba kuna ukiukwaji mkubwa
wa Haki za Binadamu hapa Tanzania. Mfano ukatili majumbani na udhalilishaji wa
watoto wadogo ni mambo ambayo huwezi kupambana nayo bila kuyafichua na kuyaweka
wazi. Ardhi inaporwa, mazingira yanaharibika, maisha ya watu yanaendelea kuwa
magumu; ni mazuri yapi ya kutangaza? Kwamba shilingi yetu inaendelea kudidimia?
Kwamba miaka hamsini baada ya uhuru hatuna hata kiwanda cha kutengeneza nyembe?
Au kwamba watawala wetu wanatembelea
magari ya milioni mia mbili wakati wagonjwa wanabebwa kwenye machera kwenda
hospitalini?
Baada ya onyesho la
uzinduzi wa vipindi vya Nchi yetu kulikuwa na majadiliano. La kushangaza ni
kwamba hoja ya Waziri Nchimbi ya kuonyesha mabaya tu haikuungwa mkono kwa maana
kwamba hakuna mchangiaji yeyote aliyeirejea. Inawezekana Mheshimiwa Nchimbi,
anaiona Tanzania kwa macho yake yaliyofunikwa na miwani yenye giza nene? Wakati
anamshangaa mwalimu kufundisha miaka yote hiyo na kushindwa kuyaboresha maisha
yake, walimu wanatishia kufanya migomo kudai malipo yao? Walimu hawana nyumba,
walimu hawana usafiri, walimu wanafundisha kwenye mazingira magumu kiasi kwamba
mshahara wao ni mdogo kuweza kuyakabili
maisha yao magumu? Mwalimu anayetegemea mshahara wake kuwasomesha watoto wake,
kununua chakula, kulipia matibabu na matumizi mengine ya nyumbani atakuwa na
fedha ya ziada? Walimu hawana posho, walimu hawana bahasha na walimu wenye
maadili bora ya kazi yao hawapokei rushwa wala hongo. Au Mheshimiwa Nchimbi
hajasikia ukweli kwamba mishahara ya Tanzania bila mtu kuwa na vyanzo vingine;
miradi midogo, rushwa, ufisadi na fedha chafu haitoshi kiasi cha mtu kuweza
kuyaboresha maisha yake? Umeme unapanda, mafuta yanapanda, karo inapanda na
bidhaa nyingine zinapanda wakati mshahara unabaki pale pale au kupanda kwa
nyongeza ya shilingi elfu mbili tu! Ni watanzania wangapi wenye mshahara wa
kuweza kununua gari, kujenga nyumba na kuwasomesha watoto?
Miaka ya nyuma, mtafiti
kutoka nchi ya Ujerumani, baada ya utafiti wake ndani ya Jiji la Mwanza,
alibaini kwamba kulingana na gharama za maisha kuwa juu, watanzania wengi wenye
kufanya kazi za kuajiriwa watakuwa ni wezi maana mishahara yao ilikuwa chini
sana kulinganisha na matumizi yao ya mwezi. Hata leo hii ukilinganisha matumizi
ya Mtanzania kwa mwezi na kipato chake, unashangaa fedha ya ziada inatoka wapi?
Gharama za maisha ziko juu sana wakati kipato kiko chini. Hivyo haishangazi mtu
kuwa mwalimu kwa miaka mingi akawa hana uwezo wa kujijengea nyumba. Hata
waheshimiwa wabunge wetu tunaoamini wana mshahara mkubwa, bado tunasikia
wanalalamika na kupiga kelele za kuongezewa mshahara wao na posho. Hizo ni dalili kwamba mishahara ya watanzania
bado iko chini. Kama wabunge wanalalamika, walimu je?
Badala ya kuunga mkono
hoja ya Waziri Nchimbi, mjadala ulichukua mkondo mwingine; washiriki wengine
walikubali kwamba “mabaya” yapo katika taifa letu. Mfano ukatili majumbani ni
ukweli ambao hata mtu akijitahidi kuufunika utajitokeza tu. Hoja iliyojengwa na
washiriki wengine ni ushauri kwa Maa Media Centre kuonyesha pande mbili za
matukio wakati wa kuandaa vipindi vyao. “Tumeonyeshwa ukatili aliofanyiwa mama
huyu wa Zanzibar, hatukuonyeshwa upande wa pili, kujua ni kwa nini mme wake
alifikia hatua hiyo. Lazima kuna chanzo. Maa Media Centre, wangefanya jitihada
kumtafuta mme wa mama huyu na kumhoji”. Alidokeza mshiriki. Na mshiriki
mwingine alichangia hoja hiyo hiyo kwa upande wa ukatili aliofanyiwa mama wa
Magu: “Ingekuwa vizuri kama mme wa huyu mama angepatikana na kuhojiwa. Kitendo
alichokifanya ni kibaya, lakini tungependa kujua ni kwa nini alifikia hatua
hiyo?”
Maa Media Centre,
walipokea ushauri na kuahidi kuendelea kuviboresha vipindi vyao. Kwa wakati huo
walichokuwa wamekiandaa ndicho hicho tulichokiona na ambacho watanzania wengine
watakiona siku za hivi karibuni. Kwa mtu yeyote aliyeshiriki uandaaji wa
vipindi hivi, atakubaliana na mimi kwamba Maa media Centre wamejitahidi sana
ukilinganisha na changamoto nyingi walizokumbana nazo; kutokuwa na umeme wa
uhakika, kutokuwa na wataalamu waliobobea wa kuchukua picha na uchanga wa
kuandaa vipindi kama hivi; hata hivyo pole pole ndio mwendo kama wanavyoamini
wao. Kazi yao ni nzuri na ya kupongezwa. Ubunifu wao ni wa kuigwa na vijana
wengine wa nchi yetu ya Tanzania.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment