MWANA MAMA RHODA KAHATANO
Katika safu yetu ya Mwana Mama, tunawaletea Mama Rhoda Kahatano. Mama huyu aliyeaga dunia mwaka wa 2010, ni miongoni mwa wanawake waliojitoa kulitumia taifa letu kwa nguvu zao zote, mama mzalendo, mchapakazi na mwadilifu lakini machache yameandikwa juu yao.
Mama Rhoda Kahatano, alikuwa msomi, mwanasiasa, kiongozi, mcha Mungu na zaidi ya yote alikuwa “Mama”. Siku za mwisho za maisha yake, yeye na mme wake Mzee Kahatano, walianzisha shule ya Sekondari kule Bunju Dar-es-Salaam. Wanafunzi walimbatiza mama huyu jina la Bibi na mme wake aliitwa Babu. Kwao shule si kitegauchumi kama ilivyo kwa watu wengi wanaoanzisha shule; Familia ya Kahatano inaichukulia shule hii kama familia yao kubwa: Kuwafundisha watoto, kuwapatia elimu na maadili bora. Jinsi walivyowalea watoto wao wa kuzaa ndivyo wanavyolenga kuwalea watoto wote watakaojiunga na shule yao.
Shule hii ya sekondari, ilianzishwa kwa lengo maalumu. Familia ya Mama Kahatano, iliwapoteza watoto wawili wakubwa, waliokuwa wasomi na wenye kuonyesha matumaini ndani ya familia. Misiba hii iliiyumbisha familia ya Kahatano, lakini kwa vile walikuwa na imani isiyoyumba, aliamua kuanzisha shule ya sekondari kama njia pekee ya kuwaenzi watoto wao. Shule hii kwao ni kama fanaka na kitulizo kikubwa. Kwa kujenga shule hii wanaamini Mungu, ameyafuta machozi yao ya kuwapoteza watoto na kuanzisha maisha mapya yenye matumaini si kwa familia ya Kahatano peke yake bali kwa familia nyingi zenye watoto wanaohitaji elimu.
Katika hali ya kawaida misiba ya watoto wao ilitosha kuiyumbisha familia. Lakini Mama Rhoda Kahatano na Mzee Kahatano, kwa vile walikuwa ni watu wa imani na walimwamini Mwenyezi Mungu kwa kila jambo, walimshukuru Mungu kwa matukio hayo ya kuumiza na kuamua kuendelea na maisha. Na hili liliwezekana kwa vile familia hii ilikuwa ni ya mfano: Pamoja na Mama huyu kuwa Mwanaharakati wa kupigania haki za binadamu na haki za wanawake, familia yake ilibaki imara na kuchomoza miongoni mwa familia za kuigwa.
Nina imani Familia ya Kahatano, imezisaidia familia nyingi kwa ushauri. Na kwa baadhi ya viongozi wa serikali walioyumba na kuteteleka katika familia zao, walipata msaada mkubwa kutoka kwa familia ya Kahatano. Hivyo kama walishindwa kuimba sifa za uchapakazi wa mama Kahatano ndani ya serikali, basi wangeziimba sifa za Mama huyu kuwa mfano bora wa familia na mshauri mkubwa wa ndoa nyingi.
Nilipoitembelea shule hii mwaka mmoja kabla ya kifo cha mama huyu, aliniambia kwamba mtaji wa kwanza wa kuanzisha shule hiyo ulitokana na posho zake za Ubunge. Wakati wabunge wakichukua mikopo kununua magari ya kifahari, yeye alichukua mkopo kuanzisha shule. Kwa kusaidiana na mme wake aliyekuwa amestaafu kazi za kuajiriwa na kwa misaada mingine ya ndani na nje ya nchi, shule ilisimama. Yeye na mme wake waliendesha shule hiyo wakati mama Kahatano akiwa anateswa na ugonjwa. Hata hivyo mama huyu hakuonyesha mateso aliyokuwa nayo, aliendelea kuonyesha matumaini kwa wanafunzi na wote walioitembelea shule hiyo kwa kuelezea mipango ya zaidi ya miaka ishirini mbele. Hakuwa mtu wa kukata tama.
Mama Kahatano alifanya kazi mbali mbali katika taifa la Tanzania. Alikuwa mkuu wa Wilaya, Afisa Elimu wa Mkoa, Mbunge, Mwana harakati, Mcha Mungu na alikitumikia chama chake Cha Mapinduzi katika ngazi mbali mbali. Walimu wa mkoa wa Kagera na wanafunzi waliosoma enzi za Mama Kahatano akiwa Afisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, wanakumbuka uchapakazi wa mama huyu ambaye mbali na kuwa kiongozi alikuwa “Mama”. Alielekeza, aliongoza, alishauri, alionya, aliyasikiliza matatizo ya walimu na kutafuta ufumbuzi na aliinua kiwango cha elimu katika Mkoa wa Kagera.
Waliopata bahati ya kukutana na Mama Kahatano, watakubaiana na mimi kwamba mama huyu alikuwa Mama mwenye hekima na busara. Hakuwa mpole ki hivyo kwa watu wavivu, lakini alikuwa na huruma na utu wa kuwajali wote waliomzunguka na wote aliowatumikia. Alijaliwa kipaji cha kumbukumbu, aliwakumbuka karibia watu wote aliokutana nao kazini na kwenye jamii. Yeye Mzaliwa wa Mkoa wa Mbeya, aliyeolewa mkoa wa Kagera na kujizingarisha kiasi cha kuwazidi hata wale wazawa wa mkoa wa Kagera.
Rambirambi za Serikali wakati wa kifo chake hazikutoa picha kamili ya Mama huyu ambaye ni miongoni mwa watu wachache waliolitumikia taifa hili kwa moyo wao wote. Tanzania tumekuwa na utamaduni wa ovyo wa kuwasahau kwa haraka watu wanaolitumika taifa hili. Na bahati mbaya hayajaandikwa mengi juu ya mama huyu. Salaam za Rambirambi kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete zilisema kwa kifupi sana:
“Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za Rambirambi Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, Bibi Sophia Simba, kufuatia kifo cha mmoja wa wanachama wake hodari Bibi Rhoda Kahatano aliyefariki usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake Bunju A, jijini Dar-es-Salaam.
Katika salamu hizo Rais Kikwete amesema amemfahamu na kufanya naye kazi katika chama na serikali na kumuelezea kuwa mwanachama dhabiti, aliyeshirikiana vyema na wenzake na mwajibikaji mkubwa.
“Alikuwa nguzo imara katika kusimamia masuala ya chama na serikali na mwajibikaji ambaye anakumbukwa wakati wote kwa ushirikiano na upendo mkubwa kwa wenzake siku zote”. Rais amesema
“Tutamkumbuka kwa kupenda kutoa ushauri, ushirikiano, upendo na ucheshi kwa watu wote na wakati wote” Rais amesema na kumuomba Mwenyekiti wa UWT, amfikishie rambirambi zake kwa Mume, watoto na wana familia ya Marehemu Rhoda Kahatano kwa kuondokewa na mpendwa wao.
Marehemu Rhoda Kahatano alizaliwa Tukuyu, Mbeya tarehe 15 Desemba, 1941. Aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya mkoani Kagera kabla ya kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka mwaka 1995 hadi 2000.
Amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Mjumbe wa UWT katika kipindi cha uhai wake.
Ameacha mume, watoto na wajukuu.”
Pamoja na shukrani kwa serikali kukumbuka kutoa rambirambi, hatuwezi kusita kusema kwamba mengi hayakusemwa juu ya mama huyu:
Maisha ya Mama Rhoda Kahatano, yanaonyesha ukakamavu aliokuwa nao katika kuishi na kutenda kazi. Ushiriki wake katika makambi ya “GirlGuide” Dar-es-salaam, Zambia na Denmark, ni ushahidi wa kutosha juu ya ukakamavu wake. Pia mama Rhoda alishiriki kikamilifu harakati za Umoja wa mataifa kuwajengea nyumba watu wasiokuwa na makazi na kushiriki mikutano ya harakati hizi nchini Sweden. Na uongozi ndani ya jumuiya za wanawake zilimpeleka hadi Korea ya Kusini na Hawaii. Ni mama aliyechapa kazi bila kuchoka ndani ya serikali, kwenye chama chake cha CCM na ndani ya mashirika ya kidini.
Mwaka 1962 hadi 1963, alikuwa kwenye Umoja wa vijana wa chama TANU. Mwaka wa 1963 mpaka 1966 alikuwa Katibu wa UWT mkoa wa Arusha. Mwaka 1972 mpaka 1975, alikuwa katibu wa UWT tawi la Wizara ya Elimu makao makuu.
Mama Rhoda Kahatano, alikuwa ni msomi aliyepata Diploma ya Elimu ya watu wazima mnamo mwaka 1974 na digrii ya ualimu kutoka Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam mwaka 1980. Mbali na digriini ya ualimu alisoma mambo mengine mbali mbali: Chuo cha Siasa Kivumoni, Diploma ya lishe kutoka Muhimbili, Cheti cha Maendeleo ya jamii kutoka Tengeru na Israel. Cheti ya utawala kutoka Swaziland na cheti cha Kingereza na kutengeneza mitaala kutoka Ethiopia.
Mama Rhoda Kahatano alijiunga na shule ya msingi Rungwe mnamo mwaka wa 1950 hadi 1955, aliingia shule ya msingi ya kati ya Kisa mwaka 1956 hadi 1957. Baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari alijiunga na Chuo cha ualimu cha Mvumi na kupata cheti ya ualimu daraja la pili.
Kazi kubwa ya Mama Rhoda Kahatano, alikuwa ni mwalimu. Mbali na kuwa afisa Elimu wa Mkoa, alifanya kazi kwenye nafasi mbali mbali katika wizara ya Elimu. Alikuwa kiongozi kwenye Umoja wa Wanawake Tanzania na kuiwakilisha Tanzania kwenye mikutano mbali mbali nje ya nchi. Alikuwa Mbunge wa viti maalumu na kuifanya kazi hiyo kwa umahiri mkubwa. Inawezekana serikali imesahau kwa haraka mchango wa Mama huyu, lakini walimu na wanafunzi wake wana wajibu mkubwa wa kuziimba sifa za mama huyu na kuiga kila jema alilolifanya kwenye wizara ya Elimu.
Mungu, amlaze mahali pema peponi Mama yetu Mwalimu Rhoda Kahatano.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment