MWANA MAMA,


MAIMUNA KANYAMALA.

Mama Maimuna Kanyamala, ni mwanamke wa nne kupokea tuzo ya mwanamke jasiri inayotolewa na Balozi wa Amerika, Tanzania. Wakati akipokea tuzo hiyo, alitoa maneno yanayoonyesha kwamba tuzo hiyo hakuipata kwa bahati mbaya bali alistahili asilimia mia moja

“…ukatili dhidi ya wanawake unawaumiza, unawaletea ulemavu na kuwaua wanawake wengi zaidi ya malaria, vita, kansa na ajali za barabarani”

Wimbi kubwa la mauaji ya wanawake vikongwe yamefanyika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Mauaji ya albino yamefanyika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Lakini pia kumekuwepo na ukatili wa kutisha wa wanawake katika mikoa ya kanda ya ziwa, hasa Musoma, Mwanza na Shinyanga. Mama Maimuna Kanyamala, amefanya kazi katika mazingira haya ambayo mfumo dume umesimika mizizi na amepigana bega kwa bega na wanaharakati wengi kutokomeza vitendo hivi vya kuwanyanyasa na kuwatesa wanawake.



Mama Maimuna Kanyamala ni miongoni mwa wanawake sita walioamua kuanzisha shirika la Kivulini mnamo mwaka 1999 na amekuwa mkurugenzi mtendaji wa shirika hili hadi leo hii. Shirika hili ni la kutetea na kulinda haki za wanawake Mkoani Mwanza na maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria. Juhudi za mama huyu, zilimpelekea kuchukiwa na wanaume na kumpachika majina kama “Adui wa wanaume” na mtu “anayewapatia kichwa kikubwa wanawake” .



Baadhi ya watu wanafikiri hawa wana mama wanaojitolea kutetea haki za binadamu hawana ndoa. Wanafikiri wanaweza kusimama na kukemea vitendo vya unyanyasaji wa wanawake kwa vile wao hawana wanaume. Jambo hili si la ukweli. Mama Kanyamala, alikuwa na ndio yake nzuri mpaka pale alipofiwa na mme wake siku za hivi karibuni. Ni mama wa watoto watatu, aliowalea vizuri na kuwapatia maadili bora.



Mama Maimuna Kanyamala ana uzoefu mkubwa na amesomea masuala ya maendeleo ya Jamii.

Ana digrii ya uzamili katika taaluma za maendeleo aliyoipata katika chuo cha Holly Ghost College, Kimmage Manor, Ireland.



Mama huyu pia amesomea mambo ya ustawi wa jamii katika chuo cha Ustawi jamii na kupata cheti daraja la kwanza. Pia ana diploma ya uongozi na katibu muhtasi kutoka chuo cha biashara cha Shinyanga.



Pia mama Huyu amesoma mambo mbali mbali ya kuendesha mashirika yasiyokuwa ya serikali kutoka sehemu mbali mbali kama vile chuo cha MS-TCDC , USIS & USAID Tanzania, Catholic Relief Services Tanzania, World Bank Institute, REPOA Dar es Salaam

: Jinsia na Haki za binadamu, Ushawishi na utetezi, uhamasishaji, usimamizi wa fedha na utawala, bajeti na matumizi, tathimini nk



Kabla ya kuanzisha KIVULINI, alikuwa na uzoefu wa kufanya kazi sehemu mbali mbali, Uzazi wa mpango wa Taifa, na afisa utawala katika mradi wa kuendeleza makao makuu Dodoma na kuongoza kitengo cha utetezi katika shirika la kutetea haki za watoto la Kuleana.



Hata hivyo uwezo mkubwa na ujasiri wa mama Maimuna Kanyamala umeonekana kwenye kuliongoza shirika la Kivulini, ambalo kwa maoni ya wengi shirika hili limekuwa sehemu ya maisha ya mama huyu. Utetezi wa haki za wanawake na watoto, ni kitu kilicho kwenye damu yake.



Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wanawake lenye makao yake makuu jijini Mwanza linalokutanisha watu wa jinsia zote kujadili, kutafakari na kutafuta suluhisho la ukatili majumbani. Neno Kivulini linalotambulisha shirika hili linatokana na neno kivuli, kwa maana ya chini ya mti au paa ambako watu hukutana na kujadiliana kwa amani juu ya matatizo yao katika jamii. Ndoto za kivulini ni kujenga jamii salama isiyokuwa na ukatili ambayo haki za wanawake zinathaminiwa na kuheshimiwa.

Si kivuli cha maneno, ni kivuli kweli. Ukifika Jijini Mwanza, utakiona kivuli hicho kinachowakusanya watoto, vijana, wazee wake kwa waume, kama si majadiliano juu ya usuluhishi katika familia, watakuwa wanajadili mbinu za kutumia kutokomeza ukeketaji, kupambana na ukatili majumbani, kuomba msaada wa kisheria juu ya mirathi, midahalo juu ya vyanzo vya ongezeko la ukatili katika jamii, kujengewa uwezo juu ya ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa habari.

Ingawa jiji la Mwanza lina mashirika mengi yasiyokuwa ya kiserikali, Kivulini ni shirika pekee lilioanzishwa na wanawake na linalishughulikia kuzuia ukatili majumbani. Pia ni shirika pekee lenye mfumo wa kushirikiana na makundi mbalimbali katika jamii kama viongozi wa mitaa, vijiji, dini, vikundi vya kijamii na wanaharakati wa kujitolea.

Shirika la kivulini linachukua jukumu la kujenga uwezo wa kuelewa madhara ya ukatili unaotendeka majumbani miongoni mwa makundi mbali mbali na kuyaachia makundi hayo kubuni mbinu za kukomesha ukatili majumbani. Wawezeshaji wa Kivulini, hawachagui wala kupendekeza mbinu yoyote. Kazi yao ni kuelekeza ,kushauri, kuchochea, kuhamasisha na kupandikiza mbegu ya ujuzi na utaalam katika mfumo mzima. Maamuzi ya nini kifanyike yanabaki mikononi mwa walengwa!

Jambo jingine la pekee katika shirika hili, ni kwamba wanawaachia uhuru wanajamii kuchagua ni kitu gani wangependa kujifunza kuhusiana na sheria za mirathi, ndoa, jinsia, stadi za maisha, ushauri nasaha, uchumi nk., wakichagua jambo la kujifunza, kivulini inashughulika kumtafuta mtaalamu. Mfano, wanajamii wanaleta maombi juu ya mdahalo wanaoutaka na njia wanayoitaka kuitumia, kama ni kwa njia ya filamu, ziara za kimafunzo, uchoraji, muziki, msaada wa kisheria hasa pale wanawake wanapodhalilishwa. Ikilazimu, wanasheria wao wanakwenda kutoa msaada wa kisheria mahakamani au kutoa ushauri.

Kinachovutia Kivulini na kuleta matumaini ni kwamba wakati mashirika mengi yanakuwa na malengo ya kuhudumia maeneo makubwa, jambo linalozorotesha mafanikio, Kivulini inahudumia maeneo machache. Pia inakuwa rahisi kuunda vikundi vya majadiliano na ushirikishwaji. Kwa njia hii wameweza kupambana na changamoto kubwa ya mtazamo wa dini katika suala zima la kuleta uwiano kati ya wanaume na wanawake, mitizamo ya kimila na desturi, jinsi ya mazoea ya mwanamke na mwanamme ambapo katika baadhi ya maeneo mwanamke anaonekana ni sawa kunyanyaswa na changamoto ya wanandoa kutokuwa wazi juu ya kipato chao na wanakitumiaje. Changamoto hizi wamekutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi kwa vile wanahudumia maeneo machache, wanashirikisha walengwa, wanatengeneza jukwaa la majadiliano, wanasikiliza zaidi kuliko kusikilizwa.

Wanaume wa Mwanza waliichukia Kivulini na Mama Kanyamala, pale shirika hili lilipomsaidia mwanamke kumshitaki mme wake aliyemkata masikio. Mahakama, ilimhukumu mwanaume kwenda jela kwa kitendo hicho.

Lakini kwa ujumla sasa hivi watu wengi wamezielewa juhudi za Kivulini, baada kuona malengo yake ya kutetea haki za wanawake na watoto zinaleta matunda mema. Pia, Kivulini ilionyesha pia kuwatetea wanaume wanaonyanyaswa na wake zao. Imeeleweka kuwa hiki ni kituo cha kutetea haki za binadamu bila ubaguzi wowote ule.

Ingawa jitihada za kuitengeneza Kivulini, ni za wachangiaji wengi, lakini Mama Maimuna Kanyamala, ametoa mchango mkubwa zaidi. Ndio maana safu hii ya Mwana Mama, imeamua kumleta kwenu mama huyu jasiri na mzalendo wa taifa letu.

Na,

Padri Privatus Karugendo.

+255 754 6331 22

www.karugendo.net

































0 comments:

Post a Comment