MWANA MAMA KAROLA KINASHA



Katika safu yetu ya Mwana Mama, leo tunawaletea mwanamuziki mkongwe wa nchini Tanzania, Karola Kinasha. Mwana mama huyu ni mmoja kati ya wanamuziki wa kwanza kabisa wa kike kuvunja mwiko wa kusimama stejini na kuburudisha wapenzi wa muziki. Alianza muziki kipindi kile tasnia hii ikiwa bado imetawaliwa na wanamuziki wa jinsia ya kiume.

Huyu ni mwanamuziki/msanii anayedumisha utamaduni wa Mwafrika. Anajivunia utamaduni wa kabila lake la Wamasai. Usanii wake unabeba ujumbe kwetu sote kupenda na kudumisha utamaduni wetu. Mavazi yake na mwonekano wake, daima unatangaza utamaduni wetu wa Kitanzania na Afrika kwa ujumla. Hivyo huyu si msanii wa kuigiza au kutoka kimaisha, bali ni msanii mwenye malengo ya mbali kwake yeye na kwa taifa zima.

Huyu ni Mwana Mama aliyesomea sheria chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, lakini akaamua kuimba! Ina maana alifanya uamuzi na kuchagua kitu kilichoyagusa maisha yake na wala si kwenda kwenye usanii kwa mkumbo au kutafuta maisha. Alitafuta namna ya kutoa mchango wake kwa taifa kwa kupitia usanii. Ndo maana nyimbo zake zote zimesheheni tafakuri na wala si zile nyimbo za mapenzi tulizozizoea kila kukicha kila msanii anatunga nyimbo za mapenzi.

Karola, si msanii wa kutafuta jina na wala hana majivuno. Ni mtu anayependa kazi yake na kuiheshimu. Ni mnyenyekevu, mkimya kiasi na wala hana maneno mengi. Kikubwa kwake ni kujivunia uafrika wake na kuhakikisha kazi zake na mwonekano wake vinaitangaza Afrika. Ni mtu asiyependa kujitangaza kwenye vyombo vya habari. Dume challenge, ndiyo iliyo iliyomfunua zaidi kwenye vyombo vya habari. Karola, alikuwa jaji wa shindano hilo ambalo washindani walikuwa ni wanaume na majaji wengine walikuwa ni wanaume.

Wale waliopata bahati ya kufuatilia shindano hili la Dume Challenge, watakubaliana na mimi kwamba mama huyu mbali ya kuwa msanii wa nyimbo, bado ana vipaji vingine vikubwa. Kwenye shindano hili, hekima, busara, huruma, upendo vilijitokeza wazi kwa Mama huyu ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu kwa miaka mingi. Alionyesha roho ya umama, kuwajali vijana waliokuwa wakishindana, kuwaelekeza, kuwafundisha na kuwatia moyo, lakini pia alikaripia pale ilipolazimu. Ni miongoni mwa akina mama wengi wa Tanzania, wanaofanya mambo mengi makubwa na mazuri, lakini hawajitangazi na wala hawasikiki!

Ingawa mama huyu hasikiki sana, lakini akipanda jukwaani, akianza kuimba ni nadra mtu kubaki amekaa kwenye kiti. Nilishuhudia mwenyewe Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, wakati wa tamasha la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alipounyanyua ukumbi mzima wa Nkrumah. Sauti yake nzito na ya kukwaruza kidogo, haiwezi kumwacha mtu amekaa. Zaidi ni kwamba anaimba kwa hisia kali na kuonyesha kuguswa na uhai wa Taifa la Tanzania.

Sio jambo rahisi na wanamuziki wasio wengi duniani wanaweza kufanya. Tunazungumzia kuimba na kutumia kifaa chochote cha kimuziki (kama gitaa, piano, ngoma nk) wakati huo huo. Karola ni mmojawapo miongoni mwa wanamuziki tulionao nchini Tanzania ambao wanaweza kufanya hivyo, anaweza kuimba na wakati huo huo kucharaza gitaa. Na baadaye akapata nafasi ya kurudi nyumbani kupumzika na kufurahi na familia yake. Mungu amemjalia watoto wawili. Picha zinazonyeshwa kwenye mtandao, anaonekana ni mama mwema ndani ya familia yake.

Karola Daniel Amri Kinasha alizaliwa Machi, 1970 huko Longido mkoani Arusha. Baada ya kumaliza masomo ya elimu ya msingi huko Longido, alihamia jijini Dar Es Salaam ambako alipata elimu ya sekondari na ya chuo kikuu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Karola amekuwa akijihusisha na masuala ya muziki tangu mwaka wa 1987.Ameshiriki katika miradi na matamasha mbalimbali ya kimuziki, ndani na nje ya Tanzania.



Karola, anatoka kwenye kabila la Wamasai jirani na mpaka wa Tanzania na Kenya. Yeye ni miongoni mwa watoto 8 wa familia yao. Baba yake aliweza kucheza akodiani, kaka yake aliweza kupiga piano na gitaa, mama yake aliimba kwenye kwaya ya kijiji. Inaonyesha jinsi Karola, anavyotoka kwenye familia ya wanamuziki. Lakini pia alishiriki nyimbo na ngoma za wanakijiji na kufurahia mashujaa wa Kimasai walivyokuwa wakiimba na kujigamba.



Ndugu zake na Karola, walipoanza kutoka nyumbani kwenda shuleni, walileta aina mbali mbali ya miziki kutoka dunia nyingine. Kaka zake Esto, Abedi na Oculi, walimletea nyimbo za Calypso, nyimbo za Injili na aina nyingine za nyimbo za Kizungu, nyimbo za Tanzania na za kikongo, wakati Dada yake Juddy, alimletea nyimbo za Afrika ya Kusini.

Rafiki yake wa karibu anasema hivi juu ya Karola:

“Carolla namfahamu miaka mingi. Nilisoma naye Zanaki Girls Secondary School. Alikuwa anapenda sana kuimba wakati huo. Alikuwa anajua nyimbo zote za Boney M na ABBA, tena alikuwa anaziimba vizuri mpaka walimu walichukia na kusema kuimba Kizungu ni kasumba!”

Hivyo haishangazi, baadaye Karola, kuibuka mwimbaji mzuri anayependa na kujivunia utamaduni wa Mwafrika. Bendi yake ya Shada, ilianza kwenye miaka ya mwisho ya 80, ikilenga kutoa muziki wa Kitanzania, wenye maonjo ya Kitanzania. Albamu yake ya pili ijulikanayo kama Maono, iliipaisha bendi ya Shada ndani na nje ya Tanzania.

Karola, kwa namna yake, amekuwa mwanaharakati wa kutetea haki za wanamuziki wa Tanzania. Pia ni kati ya watu waliopambana kurudisha somo la muziki kwenye shule za Tanzania. Mama huyu amepata tuzo ya “MA Africa Awards in South Africa”.

Mama huyu ni Mwanaharakati wa kutetea usawa kijinsia kwa namna yake. Ametumia sanaa, kuonyesha msimamo wake na kutoa ujumbe wa usawa wa kijinsia kwa kutumia nyimbo zake. Lakini pia ameyatumia maisha yake mwenyewe kuonyesha jambo analolisimamia. Kujiingiza kwenye fani ambayo kwa namna Fulani ilionekana ni ya wanaume peke yao ni msimamo wa kimapinduzi na wa kiwanaharakati. Na kama tulivyosema hapo juu, yeye alikuwa mwanamke jaji peke yake ndani ya mashindano ya Dume Challenge. Mama huyu hapigi kelele nyingi kutetea usawa wa kijinsia, matendo yake yanapiga kelele zaidi. Ni mama wa mfano na wa kujivunia kuwa naye katika taifa letu la Tanzania!

Na,

Padri Privatus Karugendo,

www.karugendo.net

+255 754 633122



















1 comments:

Anonymous said...

TheUltimaker s5is a large-sized desktop printer that makes use of PLA and ABS high precision machining plastic. The Ultimaker s5 is a a lot cheaper possibility and will be smart choice|a good selection} for many larger, common purposes. We are joyful to welcome all 3D know-how enthusiasts on our platform, the place could get} a thorough insight into what soon will turn into a groundswell. Now you may be part of of} a3D print market that conscious of} no artistic boundaries, either as a purchaser or seller.

Post a Comment