MWANA MAMA AMINA CHIFUPA.

Kati safu yetu ya Mwana Mama, leo tunawaletea mwana mama Marehemu Amina Chifupa. Ni mwana mama aliyeishi miaka michache hapa duniani, lakini alitoa mchango mkubwa katika taifa letu na kupendwa na watu wengi. Kifo chake kilitufundisha kwamba sila lazima kukaa miaka mingi duniani ndipo mtu atoe mchango wake. Mtu anaweza kuishi miaka michache na kuacha makubwa nyuma yake, ndivyo ilitokea kwa mwana mama Amina Chifupa.

Mchango wake mkubwa ni kujitokeza wazi wazi kupambana na dawa za kulevya. Kitu kikubwa ambacho watanzania wengi wanakumbuka ni pale Amina Chifupa, aliposimama Bungeni na kusema “ Hata kama ni mume wangu anauza dawa za kulevya, nitasimama na kumtaja bila kuogopa”. Iliaminika alikuwa na majina ya wauza unga, na habari za kuaminika ni kwamba majina hayo aliyapeleka Ikulu. Na kuna wakati hata Rais Kikwete, alitamka kuwajua watu hao, ingawa hadi leo hakuna aliyewekwa ndani kwa biashara hii inayoharibu vijana.

Tutamkumbuka Amina Chifupa kwa ucheshi na uwezo mkubwa wa kujenga hoja mbalimbali ndani na nje ya Bunge. Katika kipindi kifupi akiwa Mwanasiasa kijana, aliweza kusimama na kujipembua na wabunge wengine kwa kusimama kidete kupiga vita biashara ya mihadarati ambayo aliamini inaua vijana ambao ni viongozi wa kesho.

Kwa ufupi Amina Chifupa alikuwa ni mbunge ambaye alisimama kidete kutoboa siri za biashara za mihadarati na kuna wakati alipata kutishiwa na Polisi na kulazimika kumpa ulinzi kwa muda kutokana na vitisho hivyo. Amina alifariki akiwa na msuguano na baadhi ya viongozi wa UVCCM ambao walituhumiwa kumwona kuwa tishio katika nafasi ya uenyekiti wa Umoja huo ngazi ya Taifa.



Taarifa za madaktari wa Lugalo zilionyesha kuwa Amina alifariki kutokana na shinikizo la damu na kisukari, magonjwa ambayo haikuwahi kushuhudia wakati wa uhai wake. Wengine wanadai kilichomuua Amina, mmoja ni kujitoa kwake mhanga katika vita dhidi ya mihadarati kwa maana ya dawa za kulevya. Kifo chake kiliacha maswali mengi na kila mtu alikuwa na la kwake.

Kuna uvumi kwamba alikuwa na siri nyingi, na baadhi ya vigogo waliogopa siri hizo kuwekwa wazi. Maana kama alikuwa tayari kutoboa siri hata za mme wake, angeficha siri za nani? Ujasiri wake, wengine waliuchukulia kuwa ni “Uchizi”. Na Chizi si mtu wa kuamini! Mungu ndiye anajua, lakini kifo cha Amina Chifupa, kiliacha mengi nyuma yake.



Majuma mawili kabla ya kifo chake Spika wa bunge la 9 Samuel Sitta aliwatangazia wabunge kuhusu kuugua kwa Amina na akawaomba wabunge wamwombee aweze kupona haraka Na hapo ndipo habari zikazagaa Tanzania juu ya ugonjwa wa Amina Chifupa Hata hivyo watu hawakuamini kwamba ugonjwa huo ungeyatoa maisha ya Amina Chifupa, mwana mama aliyekuwa amejitengenezea jina kubwa kwa kusimama kidete kutetea maisha ya vijana.



Tarehe 26, 2007 ilikuwa ni siku ya Jumanne ambayo kwa watunza kumbukumbu za matukio yanayogusa jamii ni siku ambayo haitosahaulika kirahisi nchini Tanzania kufuatia Taaarifa za kushtua, baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Amina Chifupa Mpakanjia kufariki dunia. Na jambo la kushangaza, alikufa siku kupinga dawa za kulevya duniani. Yeye alipiga vita kwa nguvu zote dawa hizo za kulevya na Mungu akamchukua siku hiyo hiyo.



Amina Chifupa alifariki akiwa na umri wa miaka 26 majira ya saa 3:00 katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) Lugalo Dar es Salaam kwa maradhi ya mfadhaiko wa akili yaani “depression”. Kuugua kwa Amina kulianza kama mzaha huku kukigubikwa na habari za yeye kutalikiwa na mumewe Mpakanjia.



Msiba wake Dar-es-Salaam na Njombe alikozikwa ulikusanya watu wengi:

Miongoni mwa waombolezaji waliojumuika na familia ya Chifupa, ni Mama Maria Nyerere, Mwanasiasa Mkongwe Mzee Rashid Kawawa (marehemu), Profesa Mark Mwandosya wakati huo akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Katibu wa CUF Maalim Seif Shariff Hamad, John Mnyika wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Vijana CHADEMA, baadhi ya wabunge, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi wa kawaida.



Maelfu ya wakazi wa Jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake siku ya Jumatano ya Juni 27, 2007 walifurika pembezoni mwa barabara za Bagamoyo na Kambarage wakiwa wameduwaa, wenye majonzi wakiupokea mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM Amina Chifupa.



Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam wakati huo Hemed Mkali alisema kuwa kifo cha Amina kimedhihirisha kuwa kweli alikuwa anaumizwa na matatizo ya dawa za kulevya nchini kwani kimetokea siku iliyotengwa na dunia kupiga vita dawa za kulevya.



Meya wa Jiji la Dar wakati huo Adama Kimbisa alisema Amina alikuwa kijana mwenye kusimamia ukweli, haki na maadili. Kimbisa alisema katika vikao mbalimbali jambo na kulitetea kwa kufuata misingi ya haki.



Mkurugenzi wa Clouds FM Joseph Kusaga alimwelezea Amina Chifupa ilikuwa ni hazina kwa taifa hasa kwa wasichana wadogo kutokana na kipaji alichojaliwa kujiamini katika maisha yake tangu utotoni.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) wakati huo Profesa Mark Mwandosya alisema kifo cha Amina kimeacha changamoto kubwa kwa serikali na wadau wengine kushughulikia tatizo la kushamiri kwa dawa kulevya nchini.



Kwa upande wake Maalim Seif Shariff Hamad Katibu Mkuu wa CUF alisema Amina alishughulikia kero mbalimbali zinazoiathiri jamii bila kujali itikadi za kisiasa, alikuwa mwanasiasa chipukizi aliyejitolea kushughulikia kero za wananchi bila woga.

Amina alizaliwa Mei 20, 1981 mjini Dar es Salaam, alisoma Shule ya Msingi Ushindi, Mikocheni Dar (1988-1994) kabla ya kujiunga na masomo ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Wasichana ya Kisutu, Dar (1995-1998). Elimu ya Juu ya Sekondari alisoma katika shule ya Makongo (1999-2001) kabla ya kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habri cha Royal (2001-2003) ambako alifuzu Diploma ya Uandishi wa Habari.



Mwaka 1999 alianza kazi ya Utangazaji wa Kituo cha Redio cha Clouds FM cha Dar na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mama Shughuli.



Katika CCM aliwahi kuwa Kamanda wa CCM wa umoja wa Vijana katika tawi la Mikocheni A jijini Dar na alikuwa Katibu wa Kamati ya Uchumi ya UVCCM mkoa wa Dar, aliwahi kuwa Mama Mlezi wa UVCCM na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) matawi ya Bunju na Mbagala.



Amina Chifupa, anakumbukwa kwa kutetea maisha vijana bila kuangalia itikadi. Aliyatetea maisha ya vijana wote wa Tanzania. Hakupenda dawa za kulevya kutumia kuharibu maisha ya vijana wa Tanzania. Huyu alikuwa Mwana Mama jasiri, ambaye hata kama ni marehemu anastahili kutunukiwa tuzo ya Mama Jasiri, inayotolewa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania.



Na,

Padri Privatus Karugendo

www.karugendo.net

+255 754 633122

















0 comments:

Post a Comment