MWALIMU
NYERERE MIAKA KUMI NA MIWILI SASA
Tarehe
14/11 kwa mara nyingine itakuwa ni siku ya mapumziko kwa watanzania wote ikiwa
ni siku aliyofariki Mwasisi wa taifa letu Mwalimu Julius K. Nyerere. Kwa wengi
pengine walimjua mwalimu kama rais mstaafu tuu. Mwalimu alikuwa zaidi ya hapo.
Mwalimu alikuwa Mwanazuoni mashuhuri,
Mwandishi wa vitabu na maandiko ambayo leo yananukuliwa dunia nzima. Mwalimu
alikuwa mpigania haki za wanyonge si kwa Tanzania tu bali kwa Afrika na dunia
nzima. Zaidi ya hapo alikuwa mwanafalsafa mwenye mawazo yanayojitegemea na
aliyeweza kujenga shule yake ya mawazo. Japo Mwalimu hayupo nasi tena, mawazo
yake, busara zake na hekima zake bado zinakumbukwa na wengi. Maandiko yake yapo
katika maktaba duniani kote yanasomwa, yananukuliwa na yataendelea kusomwa
Kuna
mambo mengi ambayo mwalimu aliyasema miaka mingi iliyopita, lakini hadi leo hii
viongozi wetu wameshindwa kuyatekeleza. Mfano mwaka 1995, Mwalimu aliongea kwa
wazi kabisa juu ya jukumu la Serikali kukusanya kodi. La kushangaza ni kwamba
hadi leo hii serikali yetu haijafanikiwa kukusanya kodi kiasi cha kutosha.
Mwalimu
aliongea kwa uwazi kabisa kwamba chama kinachoshinda uchaguzi kitafakari kwa
makini kuvishirikisha vyama vingine vinavyokuwa vimepata kura nyingi na wabunge
wengi. Kwa kujenga umoja wa taifa changa, na kwa kuepusha migawanyiko isiyokuwa
ya lazima; kama vile ukabila, udini na mambo mengine ya kuelekea kuvunja
muungano. Mwalimu, aliona mbali kwamba kuiga mifumo ya mataifa ya nje, bila
kutilia maanani hali yetu na uchanga wetu hatuwezi kufika mbali.
Lakini
pia Mwalimu, aliongea juu ya mgombea
binafsi. Kwa ukali alisema kwamba kila raia ana haki ya kupiga kura na kupigiwa
kura, hivyo kutokuwa kwenye vyama vya siasa kusiondoe haki ya raia kupigiwa
kura. Pamoja na Mwalimu kulisisitiza hili la Mgombea binafsi, hadi leo hii bado
halijaruhusiwa.
Ingawa
Mwalimu alikuwa mwanachama wa CCM, na alikuwa Mwenyekiti wake, lakini hakusita
kukisema chama chake na kukikosoa pale alipohisi chama hicho kinafanya madudu.
Sote
tunakumbuka jinsi Mwalimu, alivyowakumbusha wanasiasa kwamba hata kama chama
kina nguvu namna gani, kikipuuza maoni ya wananchi, chama hicho hakiwezi
kusimama. Na kwamba vyama vinaposimamisha wagombea, na hasa kiti cha urais, ni
lazima kuwa na umakini mkubwa, maana rais si wa chama bali ni wa nchi nzima.
Umaarufu
wa mwalimu mpaka leo unadhihirika ndani na nje ya mipaka yetu. Chuo Kikuu cha
Western Cape kila mwaka kina mhadhara wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambao lengo
lake ni kuenzi juhudi za mwalimu katika kufuta ujinga Tanzania na mchango wake
katika falsafa ya elimu kwa wote. Hii
ni heshima kubwa kwa Mwalimu na nchi yetu kwa ujumla. Mchango wa mwalimu ambaye
kwake elimu ni njia ya kumkomboa mwanadamu na usawa katika jamii unatambulika
ma kuheshimika. Zaidi ya hayo mchango wake wa elimu ya watu wazima na maendeleo
umekuwa chachu kwa watu na taasisi duniani kote; nchi tajiri na nchi masikini
Amerika,
Jumuiya ya watanzania wanaoishi kule pamoja na wenyeji wanaikumbuka siku ya
kifo cha Mwalimu. Wanakutana na kujadiliana juu ya mawazo ya mwalimu na mchango
wake katika dunia nzima.
Rwanda,
nao wanaisherehekea siku ya Mwalimu kwa uzito mkubwa. Wao wanasema Mwalimu ni
rafiki wa Wanyarwanda. Sote tunaijua historia ya Rwanda miaka ya nyuma.
Wakimbizi wa Rwanda waliokimbilia DRC, Burundi, Uganda na Kenya, hawakupata
uraia, lakini wale waliokimbilia Tanzania, walipata uraia. Mwalimu Nyerere,
hakuona sababu ya Waafrika, jirani zetu kukaa kwenye makambi ya ukimbizi.
Aliamua kuwapatia uraia na kuwaruhusu kuishi popote Tanzania. Walichanganyika
na watanzania; mpaka leo hii uhusiano huu mkubwa hauwezi kufutika.
Upendo
wa mwalimu kwa taifa lake na kwa watu wake, kutopenda kwake matabaka na
kuhubiri usawa miongoni mwa watu wote wakati mwingine kulifanya falsafa zake
kupindishwa kwa makusudi, ama kwa watu kutosoma aliyokuwa akiandika kwa kina
ama kusoma na kutoelewa ama wakati mwingine kusoma na kuelewa na kupindisha kwa
makusudi. Kuna watu mpaka leo wanamlaani sana mwalimu kwa ajili ya ule msemo wa
“ Fedha si msingi wa Maendeleo”.
Wanasema mwalimu aliwakataza watu wasiwe matajiri. Wanasema aliendekeza
umasikini. Lakini ukisoma kwa undani maana ya ule msemo na ukauelewa ndio
utaona ni kwa nini fedha si ndio maendeleo kweli. Suala kamili la msemo ule ni
jinsi ambavyo kila mtu angetamani apate fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo.
Kila mbunge akienda bungeni anataka waziri wa fedha ampe fedha kwa ajili ya
maendeleo ya jimbo lake. Kila waziri angetaka fedha kwa ajili ya Wizara yake
ziongezeke. Lakini hizo fedha zitatoka wapi? Kiuchumi fedha ni lazima
zizalishwe. Sio zizalishwe kwa kuchapwa kiwandani. Zizalishwe kwa kuongeza
uzalishaji viwandani, mashambani, mauzo ya bidhaa nje nakadhalika. Kwa hiyo
chanzo cha fedha ni uzalishaji. Kama hujazalisha hakuna fedha. Unaweza ukawa
mpumbavu ukazichapisha kiwandani. Matokeo yake ni cha moto. Mfumuko wa bei utakuwa wa ajabu kabisa. Utakuwa na
makaratasi yasiyo na thamani. Kama huwezi kuongeza uzalishaji inabidi upate
hizo fedha mahali pengine. Chanzo kikuu cha fedha isiyozalishwa ni misaada ya
nje. Misaada ipo ya aina mbili. Mikopo na zawadi. Ukichukua mkopo ni lazima
ulipwe baadaye. Utalipwaje? Ni kwa kuongeza uzalishaji. Kwa hivyo pesa ni
lazima izalishwe. Ukikopa leo lazima kesho ulipe. Kama si mkopo utapata zawadi
ambayo ni kama Sadaka. Hii inakupotezea uhuru wako. Unakuwa huna maamuzi, huna
mamlaka na fedha unazopewa ndio maana zinakuja na masharti mengi sana. Unakuwa
mtumwa katika nchi yako mwenyewe. Isitoshe, anayekupa msaada leo, kesho na keshokutwa
unatarajia iwe bure tuu? Ni lazima kutakuwa na sababu ya msingi kabisa ya
kukupa fedha. Kila mfadhili ana malengo
yake ama ya mazuri au mabaya. Lakini kwa vyovyote wafadhili wengi wana malengo
ya muda mrefu yatakayowanufaisha wao.
Tunapopumzika
kumkumbuka Mwalimu ni lazima tujikumbushe yale mambo ya msingi ambayo ni muhimu
kwetu, aliyoyapigania hadi kifo chake, mambo ambayo hayajapitwa na wakati
kabisa na yatachukua muda kupitwa na wakati. Kupumzika bila kujadili hoja zake
hakutasaidia kitu. Tumuenzi kwa kukumbuka busara na mchango wake katika nchi ya
Tanzania, bara la Afrika na duniani kwa ujumla.
Changamoto
iliyo mbele yetu wakati tunakumbuka
miaka 12 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ni je ni Kweli tumethubutu, tumeweza na
tunasonga mbele? Sifa ya Tanzania ya kuwa kimbilio la mataifa, sifa ya Tanzania
ya kuwa kisiwa cha amani, sifa ya Tanzania ya kutokuwa na ubaguzi bado ipo?
Na,
Padri
Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment