MTOTO WA AFRIKA NA UPORAJI WA ARDHI.
Tarehe 16.6.2011, kama kawaida ilikuwa ni siku ya
Mtoto wa Afrika .Baadhi ya watu wameikumbuka, lakini inaelekea moto wake
unaendelea kupunguka na kubakia ni siku ya watoto wa shule, kukutana na kuimba
nyimbo, kucheza ngoma na maigizo. Watu wazima wanaanza kuikwepa siku hii. Jana
kwenye taarifa za habari ilionekana asilimia kubwa ya watoto na asilimia ndogo
sana ya watu wazima. Pamoja na jitihada za kuikwepa siku hii ukweli unabaki
pale pale kwamba yaliyotokea Soweto miaka hiyo yanaweza kutokea tena popote
kwenye nchi hizi za Kiafrika na Tanzania ikiwemo. Matendo ya ukiukwaji wa haki
za watoto ikiwemo na uporaji wa ardhi yamekuwa mengi. Binafsi nimejenga utamaduni
wa kuandika makala kila tunapoikumbuka siku hii ya mtoto wa Afrika. Ninaamini
mchago wangu huu unaweza usiwanufaishe watanzania wa leo, lakini kama
awasemavyo kwama “Kilichoandikwa kimeandikwa” ni imani yangu kwamba mchango
wangu utawanufaisha hata watanzania wa kesho.
Mnamo mwaka 1976, Kule Soweto, Afrika ya kusini,
maelfu ya watoto weusi wa shule waliingia mitaani na kufanya maandamano ya
zaidi ya nusu kilomita, wakipinga elimu duni waliyokuwa wakiipata na kudai
kufundishwa kwa lugha yao. Walifanya maandamano ya amani kwa lengo la kufikisha
ujumbe kwa serikali ya makaburu. Ujumbe huu ulikuwa mchungu kwa wakubwa na
hawakuwa tayari kuusikiliza. Kama kichaa anavyoweza kutumia bunduki kuua mbu,
ndivyo makaburu walivyofanya kwa wanafunzi hao. Mamia ya wasichana na wavulana
walipigwa risasi na kupoteza maisha yao.
Kwa vile bunduki inaua mwili, lakini fikra na roho vinaendelea kuishi,
maandamano hayo hayakuzimwa kwa risasi! Machafuko yaliyofuatia tukio hili
yalipoteza maisha ya mamia ya watu na kuacha majeruhi kadhaa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshuhudia
matatizo mengi ya watoto. Tunashuhudia watoto wetu wanavyosukumwa kila siku
kwenye daladala, watoto wanavyosoma kwa shida, shule za msingi wengine wanakaa
chini, sekondari wanasoma bila kuwa na walimu wa kutosha, matokeo yake wanafanya vibaya na kushindwa kuendelea na
masomo ya juu. Lakini pia na wale wanaofanikiwa kuendelea na masomo ya juu,
tunashuhudia wanavyonyanyaswa na Bodi ya mikopo. Tunashuhudia watoto wetu
wakikoswa ajira, tunashuhudia watoto wetu wakibugia madawa ya kulevya, wakilewa
pombe, wavulana wakisuka nywele na kujifananisha na wasichana, wasichana
wakitembea nusu uchi na baadhi ya watoto wetu wakiikimbia nchi kwenda kuishi
ughaibuni. Kwa asilimia kubwa maisha ya
mtoto wa Kitanzania, yanakuwa ni ya shida.
Binafsi, nimeamua mwaka huu niandike juu ya Mtoto
wa Afrika na uporaji wa ardhi. Kwanini, nimeamua kuandika hivyo: chanzo cha
siku ya mtoto wa Afrika, ni maasi yaliyofanywa na watoto wa Soweto, kwa kukataa
kunyanyaswa. Walikuwa wakipata elimu duni ukilinganisha na ile ya Wazungu. Pia,
walitaka elimu inayotolewa kwa lugha yao. Kule Soweto, watoto walianza kutambua
kwamba wale waliokuwa wakifundishwa katika shule nzuri ndio waliokuwa wakipata
kazi nzuri na vyeo vya juu katika serikali. Hali ya kutamani hali bora ya
maisha kwa siku za mbele, hali ya kutaka kuwa na vyeo na nafasi nzuri za kazi,
iliwafanya wanafunzi kukataa elimu duni waliyokuwa wakiipata. Hawakuogopa nguvu
za jeshi la Makaburu. Walikuwa tayari kupambana bila silaha – na kweli wengi
wao walipoteza maisha. Watoto wa Soweto, walitambua kwamba kujifunza kwa lugha
za kigeni wasingepata maarifa yenyewe. Walitaka wafundishwe kwa lugha ya kwao,
lugha inayofanana mazingira yao, lugha inayogusa maisha halisi, lugha inayoweza
kuharakisha maendeleo. Hoja yangu ni kwamba Bila kuwa waangalifu, inawezekana
na sisi hapa Tanzania, tunaandaa Tanzania ya kesho yenye maasi kama ya Soweto.
Kumetokea wimbi la uporaji wa ardhi. Watu wenye
fedha wananunua ardhi kubwa kwa kisingizio cha kuwekeza. Matokeo yake vijana
wengi watajikuta hawana ardhi na wataikataa hali hii. Na tunavyosikia kwenye
vyombo vya habari sehemu nyingine hali hii imekataliwa mapema. Tunasikia kule
Manyara jinsi watu wanavyovamia mashamba, kukata mazao na kuwashambulia wanao
miliki mashamba. Tukio la Tegeta, la kukatana mapanga katika harakati za vijana
kufukuzia mbali waporaji wa ardhi, ni la kusikitisha na kutafakarisha; na ni
fundisho pia kwamba vijana wakiamua kudai ardhi yao, patachimbika.
Mgogoro wa ardhi wa Loliondo, tumeshuhudia jinsi
ulivyovuruga amani kwenye maeneo hayo na kupanda mbegu ya maasi na chuki kwa
vizazi vijavyo. Mashirika mbali mbali yasiyokuwa kiserikali yamepiga kelele juu
ya swala hili la uporaji wa ardhi, lakini kelele hizi zimekuwa kama ile sauti iliayo
nyikani. Mashirika haya yamekuwa yakijitahidi kutengeneza majukwaa ya
majadiliano, ili watanzania tukae pamoja na kujadiliana juu ya uhai wa taifa
letu. Tamasha la jinsia ni miongoni mwa majukwaa haya ya majadiliano.
Tamasha la jinsia ni nafasi ya wazi kwa ajili ya
watu binafsi, mashirika na mitandao, walio katika mapambano yanayofanana,
kubadilishana uzoefu, taarifa, kujengana uwezo, kusherehekea mafanikio na
kutathimini changamoto zilizo mbele yao, kujenga na kuimarisha mitandao; na
kupanga kwa pamoja mikakati kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya -kijamii kwa
mtazamo wa kifeminsti, kujengeana uwezo ili kuchangia katika mijadala ya wazi
kuhusu maendeleo ya jamii na binafsi.
Tamasha la jinsia huandaliwa na Mtandao wa
Jinsia Binadamu na Usawa wa Jinsi (FemAct)
pamoja na washirika wao. Tamasha la mwaka huu litafunguliwa kwenye viwanja vya
TGNP Mabibo tarehe 13.9.2011 hadi 16.9.2011, kujadili mada kuu: Jinsia,
Demokrasia na Maendeleo: Ardhi, Ajira na Maisha Endelevu. Wakimlenga mwanamke
aliye pembezoni. Hii ni mada inayomguza moja kwa moja mtoto wa Tanzania na
uporaji wa Ardhi. Tunajua fika kwamba ardhi inapoporwa na matajiri na mafisadi,
anayeteseka kuwalea watoto ni mwanamke aliye pembezoni.
Ardhi ni muhimu sana kwa maisha yetu ya leo na
vizazi vijavyo; uchumi wetu unategemea kilimo; bila ardhi hatuwezi kulima,
hatuwezi kupata chakula na mazao ya kuuza na kujipatia fedha za kigeni. Hivyo
ni muhimu sote kusimama pamoja kupinga wimbi hili kubwa la kupora ardhi yetu.
Tuhakikishe kila Mtanzania ana ardhi yake ya kutosha na kupiga vita kwa nguvu
zote ardhi kuwa mikononi mwa watu wachache.
Tunapoikumbuka siku mtoto wa Afrika, ni bora
tukazingatia umuhimu wa ardhi kuwa ustawi wa mtoto wa Afrika. Tukiilinda ardhi
yetu leo, tunaepusha machafuko ya ardhi kesho na keshokutwa. Lengo la makala
hii pamoja na kuikumbuka siku ya mtoto wa Afrika, ni kuwakumbusha wasomaji
wangu, kwamba tamasha la jinsi liko karibu. Tujiandae kushiriki na kupata
jukwaa la kupaaza sauti zetu, kujadili na kupanga mbinu za kuleta maendeleo ya haraka
katika taifa letu.
Na,
Padri
Privatus Karugendo.
1 comments:
Padre. Ukigomboa (redeem)ardhi wewe mtoto wa miaka 30, je ardhi hiyo inakuwa yako au unairudisha kwenye familia? Huosi udhulumaji? KAMA jibu kuirudisha kwenye familia.
Post a Comment