MAREHEMU ASKOFU
CHRISTOPHER MWOLEKA- KUMBUKUMBU YA MIAKA TISA
Wanyakyusa, wana utamaduni mzuri wa kumaliza matanga.
Niliushuhudia utamaduni huu mnamo mwaka wa 1986,nilipoishi Mbeya. Baada ya
mwaka mmoja wa kifo cha marehemu, na
hasa kama mtu huyo alikuwa ni mzee, huandaliwa kikundi cha ngoma kikiandamana
na ndugu, jamaa na marafiki, ambacho huzunguka sehemu zote kijijini ,vijiji vya
jirani na mjini alipokuwa akipendelea kutembea marehemu. Kazi inayofanyika
kwenye sehemu hizo ni kuimba, kucheza, kunywa na kufurahi kwa lengo la kufuta
kabisa kumbukumbu za marehemu. Ni njia ya kujihakikishia kwamba sasa marehemu
hayupo kati yao tena.
Leo tarehe 16.10.2011, ni kumbukumbu ya miaka tisa ya
kifo cha marehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa Jimbo
Katoliki la Rulenge(Sasa jimbo hili limetengwa na kutengeneza majimbo mawili;
Jimbo la Kayanga na Jimbo la Rulenge-Ngara) Labda zamu hii, tofauti na miaka
mingine, utamaduni wa Kinyakyusa ungetusaidia. Tuandae kikundi cha ngoma: Saida
Karoli, Mau,Kakau Band au kikundi cha Taarabu- (Marehemu Askofu Mwoleka,
alipenda kusikia nyimbo na kuangalia mikanda ya taarabu, siku za mwisho wa
maisha yake) tuzunguke sehemu zote alizopenda kutembelea Askofu Mwoleka,
tucheze, tuimbe, tule na kunywa na kufurahi kama njia mojawapo ya
kujihakikishia kwamba sasa Mwoleka hayupo kati yetu tena.
Wasiwasi wangu ni kwamba utamaduni wa Kinyakyusa,
ungeshindwa kufuta kabisa kumbukumbu ya Mwoleka, kwenye nyoyo za watu walioishi
na kufanya kazi naye kwa karibu. Alikuwa ni mtu mwenye matendo yasiyosahaulika
haraka:
Mfano: Mwoleka, alikuwa mtu mwenye ukarimu mkubwa.
Hakujua amsaidie mtu hadi kiasi gani, wakati mwingine kiasi cha yeye kubaki
mifuko mitupu! Hakujua kupima kiwango cha zawadi. Angeweza kumnunulia mtu kilo
25 za nyama, kusalimia msiba au kumpongeza mtu aliyepata mtoto, badala ya kilo
mbili au tatu. Angeweza kumzawadia mtu sukari kilo 50, badala ya kilo nne au
tano. Kwa rambirambi za msiba, ambazo kijijini tunatoa elfu moja hadi tano, yeye
alitoa laki yote! Tulimpachika jina la “Old Man of the Big quantity”.Mtu
aliyekuwa mbali naye angeshawishika kusema, Anafuja mali! Hakuambatana na mali
wala pesa. Aliambatana na wanadamu na Mungu wao!
Yeye alikuwa
hanywi pombe, na si kwamba alikuwa anakunywa na kuamua kuacha baada ya
kushukiwa na Roho wa Bwana! Hakunywa kabisa, lakini nyumba yake ilikuwa na
pombe za aina mbali mbali kwa kuwakaribisha na kuwafurahisha wageni wake. Yeye
alikuwa tofauti na watu wengine ambao
huanzia kwenye ulevi, tena ulevi wa kupindukia wa kuvua nguo nakutembea uchi,
wakishukiwa na Roho Mtakatifu na kuacha ulevi na kuacha kuonja pombe kabisa,
wanakuwa na misimamo mikali ya kuchukia pombe na kuwachukia marafiki zao walevi
waliokuwa wakipigana na kubebana enzi zile za ulevi, Wanafiki wakubwa. Askofu
Mwoleka, hakuwa mnafiki!
Askofu Mwoleka, asingeweza kula chakula bila kuhakikisha
anawahudumia (yeye mwenyewe) wale wote aliokaa nao kwenye meza ya chakula.
Wakati mwingine alihitaji msaada wa kumkumbusha alipokula chakula au kuwakaribisha
watu hotelini, aliendeleza huduma yake huko! Alikuwa ni mtu wa kuwahudumia
wengine. Alikuwa mtumishi, si utumishi wa ishara na maneno, bali matendo.
Aliwafulia watu nguo zao, aliosha vyombo baada ya chakula, aliwalimia watu
mashamba yao, alishiriki kuvuna mazao, kujenga nyumba nk.
Mbali na ukarimu wake, kitu kingine ambacho
hakisahauliki kwa urahisi katika maisha
ya Askofu Mwoleka, ni nia yake ya kutaka kuwajengea nyumba bora na za kisasa
wananchi masikini wa Karagwe,Biharamulo na Ngara.Hakupenda kuishi kwenye nyumba
bora zaidi ya nyumba za wenyeji waliokuwa wakimzunguka. Kama kuna dhambi kubwa
aliyoiacha nyuma yake ni kushindwa kujenga nyumba ya kifahari ya Askofu na wala
hakuwa na mpango. Kilichomsumbua sana ni kuwajengea watu masikini nyumba bora,
imara na za kisasa. Wazo hili lilimchukulia muda wake mwingi. Yeye alikuwa ni
mtaalamu wa kutumia mashini ya kuchapa na kompyuta. Hivyo alichora kwa kutumia
mashini ya kuchapa na kompyuta michoro ya nyumba hizi alizotaka kuwajengea watu
masikini. Kilichomsumbua zaidi ni kujenga nyumba bora na za kisasa kwa gharama
nafuu. Sementi ilikuwa inapatikana kwa shida na kwa bei ya juu. Padre Jacob
Mwenge(marehemu), alimshauri kwamba kulikuwa na uwezekano wa kujitengenezea
sementi, na yeye alimhakikishia kuufahamu mmea fulani unaoashiria kuwepo
sementi kwenye ardhi. Baada ya kuutambua mmea huo, ambao na mimi nilionyeshwa,
Askofu Mwoleka, alianza kuyazungukia mapori yote ya Biharamulo,Ngara na
Karagwe, akitafuta uwezekano wa kupata sementi kwa kuangalia mmea alioonyeshwa
na Padre Jacob Mwenge!
Baadaye walijitokeza wataalamu kutoka Kigoma, sisi
tuliwapachika jina la “Self made geologist”, wataalamu hawa walidai kwamba
miamba ya mlima ulio karibu na Keza, kwenye barabara ya
Nyakahura-Rulenge,ingeweza kutengeneza chokaa. Utaalamu wenyewe ilikuwa ni
kuipasua miamba na kuyachoma mawe kwa moto mkali sana, yakiisha chemka sana
unayamwagia maji na kuyeyuka, vumbivumbi anayotokana na myeyuko huo
inatengeneza chokaa. Mawe alichomwa
kwelikweli. Yalipomwagiwa maji hakuna kilichotokea! Yalibaki vilevile! Mradi
huu ulichukua pesa nyingi bila ya mafanikio yoyote. “Wapelelezi wa Roma”
waliomshitaki Askofu Mwoleka, kwa kosa la ubadhirifu wa pesa, itakuwa waliutaja
na mradi huu na mingine mingi ambayo haikufanikiwa. Ingawa mara nyingi Askofu
Mwoleka, alikuwa hafanikiwi katika miradi yake, lakini daima alikuwa na lengo
la kuwasaidia watu masikini. Hakutumia pesa kwa matumizi binafsi!
Kwa kutaka kukwepa gharama za mabati, alitaka nyumba za
watu wa masikini ziezekwe kwa Vigae. Aliamini watu wangeweza kujitengenezea
vigae. Hii inanikumbusha mwaka 1983, nilipokutana naye Ujerumani na kunielezea
nia yake ya kutaka kujenga nyumba za vigae. Aliwaomba Wajerumani wampatie vigae
viwili vya mfano. Alinificha nia yake ya kutaka kubeba vigae hivyo hadi
Tanzania. Vigae vyenyewe vilikuwa vizito. Siri yake ilifichuka kwenye uwanja wa
ndege wa Munich. Mzigo wake ulizidi uzito. Alipoambiwa kulipia au kupunguza
uzito wa mzigo, alifungua mzigo wake na kutoa vigae viwili na kusema: Ninaomba
mnisaidie, vigae hivi ni vya kufundishia watu wangu masikini, wajue
kuvitengeneza na kujenga nyumba bora, imara na za kisasa. Maneno yake
yaliulainisha moyo wa binti mdogo aliyekuwa anapima mizigo, alicheka tu na
kumruhusu Askofu Mwoleka, kupita na vigae vyake bila kuvilipia. Zoezi la
kujenga nyumba za vigae lilifanikiwa kiasi fulani. Hadi leo zipo nyumba ambazo
chini zimejengwa kwa udongo, lakini paa ni za vigae. Askofu Mwoleka, alinunua
mashini ndogo za kutengeneza vigae na kuzisambaza kwenye vituo mbalimbali.
Bahati mbaya wajanja wachache waliiba hizi mashini na kuzitumia kufanya
biashara kwa kuezeka nyumba za matajiri. Hivyo nia kamili ya Mwoleka ya
kuwajengea maskini nyumba bora ikawa haikufanikiwa kiasi kizima. “Wapelelezi wa
Roma” wakapeleka habari kwamba anafuja pesa!
Askofu Mwoleka, alikuwa mjenzi.
Alikuwa na upeo, karama na roho ya kutaka kuwajengea watu wake nyumba bora,
imara na za kisasa. Aliamini Mungu, anatutaka tuishi vizuri, tule vizuri, tuwe
na afya bora na tushirikiane katika kujenga Ufalme wake. Sambamba na hili,
Askofu Mwoleka, alitaka kujenga jamii bora, imara na ya kisasa. Theolojia yake
ilikuwa Theolojia ya ujenzi. Maoni yake yalikuwa kwamba wamissionari walifyatua
matofali na kuacha marundo. Walileta imani, walibatiza na kugawa sakramenti,
lakini hawakujenga jumuiya za Kikristo. Watu walisali pamoja kanisani, lakini
baada ya hapo kila mmoja alirudi nyumbani kwake na kuendelea kuishi maisha yake
peke yake. Kanisa, halikuunganisha jirani na jirani, familia na familia,
kitongoji na kitongoji na kijiji na kijiji. Waumini walibaki kama rundo la
matofali! Wamissionari Walishughulikia imani ya mtu mmoja mmoja, kwa maneno
mengine waliacha rundo la Wakristu, rundo la matofali, bila kujenga nyumba
bora, imara na ya kisasa. Kazi ya wanateolojia wazawa, ni kuyatumia matofali
hayo, mabaya na mazuri, kujengea nyumba bora, imara na ya kisasa. Kujenga
kanisa la kisasa, lenye sura mpya. Maisha yake yote, Askofu Mwoleka,
alijishughulisha na ujenzi huu wa nyumba bora, imara na ya kisasa. Ni wazi
katika ujenzi kuna makosa ya hapa na pale, kuna kukwama na kuishiwa vifaa! La
msingi ni lengo, na nia.
Tutakukumbuka daima Christopher Mwoleka, uliyekuwa Askofu
wa jimbo Katoliki la Rulenge.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment