MAAMUZI MAGUMU NI PAMOJA
NA KUDHIBITI UPORAJI WA ARDHI.
Watanzania wanajua na
dunia nzima inajua kwamba sasa ardhi inaporwa kwa kisingizio cha uwekezaji.
Watanzania wanajua na dunia nzima inajua kwamba uporaji huu wa ardhi ni ufisadi
na wala si kitu kingine kile. Watanzania wanajua na dunia nzima inajua kwamba
viongozi wetu ni miongoni mwa waporaji wakubwa wa ardhi. Watanzania wanajua na
dunia nzima inajua kwamba uporaji wa ardhi ni ukoloni mpya. Watanzania wanajua
na dunia nzima inajua kwamba uporaji wa ardhi utapelekea vijana kutopata ajira.
Watanzania wanajua na dunia nzima inajua kwamba uporaji huu unaongozwa na mfumo
dume. Watanzania wanajua na dunia nzima inajua kwamba watanzania sasa wameamua
kujichulia sheria mkononi ili kuilinda ardhi yao. Watanzania wanajua na dunia
nzima inajua kwamba uporaji wa ardhi umeshika kasi katika serikali ya awamu ya
nne….
Baada ya kukaa kimya kwa
muda mrefu, mheshimiwa Edward Lowassa, ameibukia Bungeni akiwalaumu viongozi
kushindwa kuchukua maamuzi magumu katika maswala ya kitaifa; hata mtoto mdogo aliweza kutambua kwamba Mheshimiwa
Lowassa alikuwa akituma ujumbe wa moja kwa moja kwa ndugu yake Rais Jakaya
Kikwete; bila shaka alimaanisha na maamuzi magumu ya kumfukuza yeye na wenzake
kutoka kwenye chama cha CCM na
kufikishwa mbele ya sheria kujibu tuhuma zote zinazoelekezwa juu yake. Hotuba
yake ilikuwa kwenye mfumo wa ushairi kitu kilichoonyesha kwamba Mheshimiwa
Lowassa ni msanii na mwanasiasa wa kweli. Lakini pia kushangiliwa kwa kila neno
alilolisema, ni dalili kwamba bado ana ushawishi mkubwa ndani ya Bunge, ndani
ya chama chake cha CCM na kwenye jamii ya Tanzania? Ilikuwa ni kumshangilia kwa
kumpongeza au kumtaka asiendelee kusema? Ina maana bado anakubalika kugombea
kiti cha urais na kwenda kinyume na wasia wa Baba wa taifa? Swali hili ni la
kujibiwa na kila Mtanzania mwenye uchungu na taifa letu.
Kwa mtindo wa Watanzania
wanajua na dunia nzima inajua, Mheshimiwa Lowassa, alijitahidi kuyaorodhesha
yale yote yaliyotendwa na serikali
wakati akiwa madarakani (Kama waziri Mkuu); kama vile ujenzi wa Chuo Kikuu cha
Dodoma na uamuzi mgumu wa kuyasafirisha maji kutoka Ziwa Victoria hadi
Shinyanga na labda baadaye hadi Dodoma. Kwa bahati mbaya au kwa makusudi
alisahau kutaja kwamba ni lazima Serikali ifanye maamuzi magumu ya kudhibiti
wimbi la uporaji wa ardhi; maana watanzania wanajua na dunia nzima inajua
kwamba Mheshimiwa Lowassa ni kati ya wanaotajwa kuongoza wimbi hili la uporaji
wa ardhi.
Pamoja na usanii wake,
hoja ya Mheshimiwa Lowassa ni nzito. Tanzania tunahitaji viongozi wa kuchukua
maamuzi magumu; kulinda uhuru wetu, kulinda maliasili na hasa kulinda ardhi
yetu; maamuzi magumu ya kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya utandawazi na si
kumezwa na utandawazi; kulinda lugha yetu, utamaduni wetu na umoja wetu.
Kiongozi wa nchi ni lazima afanye maamuzi na wakati mwingine yasiyomfurahisha
yeye na marafiki zake wa karibu lakini yana manufaa makubwa kwa taifa zima.
Swali la kujiuliza ni Je
Mheshimiwa Lowassa, amechelewa kulitambua hili? Je yeye ni mtu wa kulieleza
hili Bungeni au ana nafasi ya karibu
kulipenyeza kwa Rais wetu ambaye; Watanzania wanajua na dunia nzima inajua
kwamba wao ni kitu kimoja? Au Mheshimiwa Lowassa, anataka kutudhihirishia
kwamba yeye ni msanii wa kweli?
Sina maana ya kuubeza
usanii au kukubaliana na wa wanaosema kwamba: “wasanii ni waundaji wa matatizo
katika jamii”. Hoja yangu ni kwamba Mheshimiwa Lowassa ni msanii aliyeusomea
usanii. Hivyo naongelea dhana nzima ya uigizaji.
Katika ufundishaji wa sanaa
hasa za maonesho, nadharia mbali mbali hutumika. Konstantin Stanislavski (1863-
1938) ni mmoja wa wakongwe wa nadharia za uigizaji ambaye pia alikuwa
mwanzilishi wa Moscow Art Theatre (1897) kundi la uigizaji linalofanya kazi
hadi leo. Yeye anaamini kabisa mbinu
moja wapo ya kuigiza ni kufanya ‘emotional recal’ (kuvuta/kurudisha hisia)
ambayo itapelekea mtu kuweza kuleta uhalisia.
Hapa tunakutana na wale mabingwa wa kutiririsha machozi. Baadhi yao
huweza kuvuta hisia za mambo mabaya (sijui mazuri?) yaliyowaliza kama chanzo
cha kumwaga uchozi kwenye jukwaa au kwenye filamu. Kutiririsha huku kwa
machozi, ni zoezi la kisayansi linalotokana na mwitiko wa mwili. Mwitiko huu wa
mwili ni katika kubana/kubanwa pumzi au kwa kutumia kemikali (kama zile za vitunguu)
ili kufungua mirija ya machozi. Zote ni njia zinazotumika kutiririsha machozi.
Huu ni mfano mmoja tu katika uigizaji. Kuna wengine wanaoona kuigiza ni
‘reality plus one’ yaani ukweli jumlisha moja. Na wengine wamekwenda mbali
zaidi wakasema kuigiza ni zoezi la ‘protrayal of convincing emotions to be real
while it is not’. Naam, naamini hili sasa ndio linalotumika zaidi. Na bila
shaka ndo uigizaji wa Mheshimiwa Lowassa. Ni imani yangu kwamba wakati akiongea
kuna wabunge waliotokwa na machozi na inawezekana na yeye machozi yalikuwa
yakitoka!
Na sasa mimi naendelea
kuchambua uigizaji kama kitendo cha kutoa ujumbe kwa kama ukweli ‘real’ wakati
sio kweli yaani kuigiza kutoka kwenye mzizi wa neno ‘iga’. Nadharia hii ni
ngumu sana kwani ni vigumu pia kujua ukweli unaanzia wapi na usio ukweli
unaishia wapi. Maana hizi za kuigiza ndizo zinazosababisha watu kulinganisha
usanii na uongo. Naomba kusisitiza, sanaa Si uongo labda unaweza kuwa uigizaji,
ambacho ni kipengee kidogo sana katika sanaa.
Kwa mujibu wa kumbukumbu Mheshimiwa Edward Lowasa alipata shahada ya
kwanza ya sanaa za maonesho (performing/theatre arts) katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam. Hii ndio shahada ya ngoma, sindimba au ‘kukata viuno’ kama wengine
walivyopenda kuikejeli. Baadaye shahada ya pili katika masomo ya Maendeleo
(Development studies) toka chuo kikuu cha Bath nchini Uingereza. Mheshimiwa
Lowassa ni kati ya wasanii wachache waliofundishwa na wahadhiri waandamizi
ambao ni magwiji wa sanaa za maonesho nchini Tanzania na katika nyanja za kimataifa.
Lowassa akiwa mwanafunzi aliigiza katika tamthiliya mbalimbali zilizochapishwa
katika vitabu.
Ukitaka kufahamu kuwa Mhe.
Lowassa ana shahada ya uigizaji, soma kwa makini utetezi wake alioutoa Bungeni
wakati wa sakata la Richmond. Alisema, “Mheshimiwa Spika, lakini nimetafakari
kwa makini sana jambo hili nikajiuliza hivi kulikoni mpaka watu wazima wenye
uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la
msingi kama hilo kulikoni? Mimi nadhani there is a wish which I am going to
grant, ni Uwaziri Mkuu. Nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri
Mkuu ndio amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe“.
Swali langu ni kuwa alijuaje kuwa watu
wanauonea gere uwaziri mkuu kama hakuwa na lake jambo? Kwa waliosoma kitabu cha
Mfalme Oedipus, wanakumbuka pale Oedipus alipogundua karaha ya kuwa “amezalia
pale alipozaliwa“ aliamua kujiadhibu kwa kujitoboa macho ili asione. Pia
alilalama sana. Alisema maneno yanayofanana na haya, “Nimefadhaika sana,
nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana katika hili...Mheshimiwa Spika, nimetafakari kwa niaba ya chama
changu, kwa niaba ya Serikali yangu nimeamua kumwandikia Rais barua ya kumwomba
niachie ngazi. Nafanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa ili kuonyesha dhana ya
uwajibikaji lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika kusema uongo ndani ya
Bunge wa kumsingizia mtu“. Kama umesoma
kwa makini alisema kuwa ameamua ’kuachia ngazi’ na mdomo wake haukuwa radhi
kutamka kuwa amejiuzulu, kwani anaamini atendelea kuwa nyuma ya pazia akiangalia
na zaidi kuongoza igizo hili na mengine yatakayofuata.
Mhe. Lowassa alilalama kwa kusema, “Mheshimiwa Spika, wewe ni
Mwanasheria unafahamu suala la Natural Justice. Kwamba Kamati Teule imesikiliza
watu wengine wote pamoja na wanaoita minong'ono ya mitaani, wamesafiri mpaka
Marekani kutafuta mashahidi, lakini mimi ambaye ni mmoja kati ya watuhumiwa mle
hawakunihoji hata siku moja. Mheshimiwa
Spika, nimesimama kueleza masikitiko yangu. Ofisi ya Bunge mpaka ofisini kwangu
hata kama wangeniita ningekwenda kwa miguu kama hamna gari na nilikuwa tayari
kufanya hivyo“.
Alihitimisha uzoefu wake wa kuigiza alisema, “nimpongeze
Dk. Harrison Mkwakyembe, Mwenyekiti wa kamati Teule kwa kuwasilisha kwa
mbwembwe nyingi sana taarifa yake, mbwembwe zilikuwa nzuri kweli“. Ni nani
ambaye angeambiwa kuwa Mhe. Lowassa alikuwa anawaigizia wa Tanzania angekataa?
Na sasa amerudi na uigizaji
mpya wa Watanzania wote wanajua na dunia nzima inajua. Ni wazi tunampongeza kwa
hatua yake ya kuachia ngazi; maana hii ni hatua kubwa katika mchakato mzima wa
kuchukua maamuzi magumu. Lakini Mheshimiwa huyu ametuhumiwa kwa mambo mengine
mengi. Mfano hili la uporaji wa ardhi; ametuhumiwa kupora ardhi kule Arusha na
jijini Dar-es-Salaam. Tumelalamikia kubadilisha sura ya Jiji la Dar-es-Salaam kwa
kujenga majengo marefu bila mpangilio wowote, kuvunja majumba ya kihistoria,
ukiuuliza wanasema Lowassa yuko nyuma ya mpango huu wa kujenga majengo marefu.
Tunakumbuka vizuri sakata zima la jengo refu la Umoja wa vijana.
Tunataka kujua hatua
anazozichukua Mheshimiwa Lowassa, kukisaidia chama chake cha CCM kufanya
maamuzi magumu. Anamsaidia vipi rafiki yake wa karibu Mheshimiwa Rais Dk.Jakaya Kikwete, kudhibiti uporaji wa
ardhi na mengine mengi kama vile biashara ya madawa ya kulevya.
Wakati nikiandika makala hii
kuna mtu amenipiga simu akinijulisha kwamba Mkoa mpya wa Katavi, mwekezaji
kutoka nje ametengewa ardhi yenye ukubwa wa wilaya nzima na kupewa hati miliki
ya mikaka 99! Kule Kilombero kuna mgogoro wa ardhi kati ya serikali na
wananchi, baada ya kijiji kumegwa na kumilikishwa na mwekezaji. Kuna matatizo
na migogoro ya ardhi kila sehemu ya taifa letu.
Vijiji vingi vya Tanzania
havijapimwa. Wananchi hawana hati miliki ya mashamba yao; wakati wowote
wanaweza kutolewa kwenye mashamba yao ili kuwapisha wawekezaji. Ndo maana
tunasema tunahitaji viongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi magumu ya kulinda
ardhi yetu na uhuru wetu.
Hata kama Mheshimiwa Lowassa,
anafanya mchezo wa kuigiza ndani ya Bunge, hoja yake ni ya msingi: Ni bora
kulaumiwa kwa kufanya maamuzi kuliko kulaumiwa kwa kutokufanya maamuzi. Na
wakati mwingine kuchelewa kufanya maamuzi kwa maswala ya msingi kama hili la
uporaji wa ardhi ni chimbuko la migogoro na wakati mwingine umwagaji damu.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment