KILIO CHA TAIFA LETU;
NANI WA KUTUVUSHA?
Kuna uvumi kwamba
mapacha watatu; Lowassa, Rostam na Chenge, wamejipanga vizuri kutumia kila njia
kujisafisha; kosa la mwenyekiti wa CCM kushindwa kuwafukuza na kuwaachia uhuru
wa kupima wenyewe na kuondoka; umekuwa ni wakati mzuri kwao kufanya mbinu za
kujisafisha; wana fedha za kufanya hivyo na wana watu wengi nyuma yao ( Watu ni
fedha, maana watanzania tunanunuliwa kama bidhaa mnadani – mwenye fedha nyingi
ni lazima awe na watu wengi nyuma yake) wanaamini ni haki yako kujisafisha
maana ndani ya CCM kuna wachafu zaidi yao. Inawezekana kabisa kwamba hoja hii
ya Kikwete kuandaa watu wake ambao wametajwa tajwa kama vile Asha-Rose na
Hussein Mwinyi; ambao wote ni waisalimu, ni ya kutungwa kwa lengo la kumchafua
Kikwete; hoja ihame kutoka kwa mapacha watatu na kuanzisha mjadala mpya wa
Waislamu kupokezana vijiti. Na kete hii imsaidie Lowasa ( ambaye ni
Mkrisut-Mlutheri) kusafishwa na hatimaye kutimiza ndoto zake za muda mrefu za
kuingia Ikulu. Lakini pia yawezekana ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais wetu ana
mpango huo wa kuhakikisha kiti chake kinakaliwa na mtu atakayemhakikishia
usalama wakati wa kustaafu kwake. Yote yanawezekana maana “uchu” wa madaraka katika
taifa letu ni mkubwa kuliko “uchu” wa maendeleo ya wananchi.
Hata hivyo Kikwete,
amwandae nani ndani ya chama chake cha CCM? Waliomsaidia yeye kuingia
madarakani, walitegemea angewaachia nao wakale “Utamu”, lakini dalili
zinaonyesha wazi kwamba amewazidi kete; walifikiri wako njia moja kumbe
walikuwa njia mbili tofauti. Walifikiri wanaijenga Tanzania yenye umoja na
mshikamano; kumbe mwenzao alikuwa na agenda nyingine. Hakuna mashaka na
utendaji kazi wa Lowassa. Hakuna mashaka na uwezo wa Lowassa kuiongoza au
kuitawala nchi; huyu ni mtu makini na mwanasiasa kweli kweli; ana wafuasi wengi
ndani ya chama na mashabiki wa kutosha nje ya chama. Pamoja na tuhuma zote
alizonazo leo hii ukiitisha uchaguzi wa aina yoyote ile ndani ya chama, Lowassa
ataibuka mshindi, ndo maana wengine wanafikiri labda anataka kufanya ya
Zuma!; tatizo lake kubwa ni kujiingiza
kwenye mnyororo wa uporaji wa mali ya umma; kashfa kama ile ya Richmond na
utajiri mkubwa usiokuwa na uwiano na kipato cha mtumishi wa umma unautia doa
uzalendo wake. Ni nani ndani ya CCM anaweza kusimama na kumnyoshea mwenzake
kidole? Majina yote tunayoyajua na kuyasikia kila wakati yamechafuka! Nani
ndani ya CCM ameshinda uchaguzi bila kutumia fedha? Ni nani kiongozi wa CCM
anaishi maisha ya kawaida ya wananchi kama viongozi wale wa enzi za Mwalimu?
Nafikiri tatizo kubwa
ambalo ni lazima sote tulifanyie kazi ni: Nani atalivusha taifa letu kutoka
hapa lilipo? Hiki ndicho kilio kikubwa cha Taifa letu! Ni mtu gani huyu
atakayeweza kulirudisha taifa letu katika njia sahihi aliyoiandaa Mwalimu
Nyerere? Taifa letu likawa juu ya “Udini”, taifa letu likawa juu ya ukabila na
ukanda? Serikali yetu ikawa ya wakulima na wafanyakazi badala ya hali ya sasa
hivi ya kutekwa na wafanyabiashara na wenye fedha? Ni mtu gani atakayevunja
utamaduni huu kwamba ni lazima Tanzania iongozwe na chama kimoja cha siasa
(CCM). Ni mtu gani huyu atakaye vunja utamaduni huu uliyojengeka wa
kushughulikia mchakato wa kuingia madarakani badala ya kushughulikia mchakato
wa kuleta maendeleo? Tumemaliza uchaguzi mkuu mwaka jana, leo hii watu wameanza
mchakato wa madaraka; badala ya kukazania mchakato wa kuleta maendeleo; nguvu
zote zinaelekezwa kwenye mbio za kutafuta madaraka. Fedha zinatafutwa kwa nguvu
zote kwa lengo la kufanikisha mchakato huu na hiki ndicho chanzo cha mikataba
mibovu na fedha chafu na haramu zinazoingizwa kwenye taifa letu.
Sasa hivi makundi
yanajengwa na fedha zinatafutwa. Wanaoutaka ubunge wanaanza kujiandaa,
wanaoutaka Urais wanaanza kujiandaa. Fitina zinaanza, chuki na wakati mwingine
hata maisha ya watu kupotea. Maana hawa wanaotafuta fedha nyingi, wako tayari
hata kujiingiza kwenye madawa ya kulevya. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba
Tanzania ni njia ya kupitishia madawa ya kulevya. Kuingilia mtandao huu wa
madawa ya kulevya kwa lengo la kuusimamisha ni kutafuta kifo kama ilivyotokea
kwa Amina Chifupa. Wanaofanya biashara hii wanajulikana, lakini hawakamatiki?
Rais Kikwete, alitwambia kwamba ana orodha ya majina yote ya mtandao huu wa
kuuza madawa ya kulevya, lakini hadi leo hii orodha hiyo haijawekwa wazi.
Mtandao huo unaendelea na fedha hizo chafu zinawaingiza watu madarakani.
Ni mtu gani atavunja
utamaduni uliojengeka wa kutumia fedha kuingia madarakani? Mtu akachaguliwa kwa
uwezo wake na uzalendo wake? Tumejenga utamaduni kwamba wananchi hawawezi
kujichagulia mwakilishi wao kwa uhuru bila kununuliwa.
Hili ndio tatizo letu
kubwa na hiki ndicho kilio cha taifa letu la Tanzania. Tunaongozwa na fedha
badala ya kuongozwa na fikira! Tumepotea njia, tuko gizani na tunahitaji mwanga
mpya! Na mwanga huu si kazi ya mtu mmoja. Kikwete peke yake hawezi kuleta
mwanga huu, CCM na ukongwe wake haiwezi kuleta mwanga huu peke yake na wala
vyama vya upinzani peke yake haviwezi kuleta mwanga huu. Mwanga mpya katika
taifa letu la Tanzania ni mradi wa pamoja. Ndo maana watanzania wanataka kuwa
na Katiba mpya. Katiba itakayo weka msingi na kuhakikisha Taifa letu linakuwa
juu ya “Udini” juu ya Ukabila na Ukanda. Katiba itakayo hakikisha Taifa letu
linaongozwa kwa misingi ya Sheria.
Katiba itakayohakikisha kwamba hata mbinu zikifanyika za kumwingiza “zuzu”
madarakani. “Zuzu” huyo atabanwa na kuongozwa na Katiba.
Kama tungekuwa na katiba
imara isiyokuwa bubu kwa baadhi ya mambo ya msingi kwa nini tuwe na wasi wasi
kwamba Kikwete, ana njama za kumwachia Urais Mwislamu mwenzake? Katiba mpya
itatusaidia kuondoa fikra potovu kwamba kuna watu waliozaliwa kutawala;
Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40; miongoni mwao hao watu wengi mmoja tu
anaweza kuwa Rais wa nchi kwa kipindi Fulani. Na mtu huyo hakuzaliwa kutawala
bali anachaguliwa kufuatana na uwezo wake wa kuongoza na uzalendo wake kwa nchi
yake.
Hivyo kazi kubwa iliyo
mbele yetu si kulalamika kwamba Kikwete, anawaandaa watu wake. Ni kushirikiana
kwa pamoja kuhakikisha tunakuwa na Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Nguvu na fedha ambazo mapacha watatu wanatumia kujisafisha, wazitumie
kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unakwenda vizuri. Tutapata mwanga mpya
katika taifa letu, tukipata Katiba mpya! Wa kulivusha taifa letu hapa lilipo si
mwingine bali ni katiba mpya. Wakumaliza kilio cha watanzania si mwingine bali
ni Katiba mpya!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment