Ingawa baadhi ya watu wanataka kulilazimisha tamasha la Jinsia kuwa jukwaa
la hoja moja tu ya Ushoga, ukweli utabaki palepale kwamba Jukwaa hili ni la
watanzania wote kujadili mambo yanayohusu maisha yao. Na mwaka huu mada
iliyojadiliwa ni Ardhi, Nguvu Kazi na maisha endelevu. Ushuhuda uliotolewa
kwenye tamasha, visa mkasa vilivyoelezwa vinatoa tafsiri moja kwamba maisha
endelevu ni ndoto bila demokrasia na
utawala bora.
Maendeleo ya haraka katika Taifa letu yatakuja
pale ambapo tutafanikiwa kusimika utawala bora na demokrasia katika ngazi ya
Vijiji, Vitongoji na Mitaa. Utawala bora na Demokrasia ni muhimu katika ngazi
zote za utawala, lakini kwa vile asilimia kubwa ya watanzania inaishi vijijini
na kumekuwepo hali ya kutowekea mkazo utawala bora na Demokrasia kule vijijini
maendeleo ya taifa letu yamekuwa yakikwama mwaka hadi mwaka.
Chimbuko la misingi ya Utawala Bora na utumiaji wa
madaraka na mipaka yake liko kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(1977) na Sheria zilizotungwa na Bunge. Misingi ya utawala bora imeainishwa
katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura ya kwanza,
sehemu 2 na ya 3 ambayo inaeleza misingi mikuu ya malengo muhimu yanayoongoza
uendeshaji wa shughuli za Serikali katika ngazi zote. Malengo haya ya utawala
bora yanasema kwamba: Wananchi ndiyo chimbuko na madaraka ya serikali; katiba
inashika hatamu; Kunakuwepo na utawala wa sheria; Usawa mbele ya sheria na
kutokuwepo na ubaguzi; Kunakuwepo mgawanyo wa madaraka; heshima kwa haki za
binadamu na utu wa mtu; uwajibikaji kwa wananchi; ushiriki wa wananchi katika
vyombo vya dola; utumiaji wa utajiri na vyanzo vya utajiri vya nchi kwa faida
na ustawi wa jamii; Maendeleo ya watu na uondoaji wa umaskini, ujinga na
maradhi; Ni wajibu wa dola kuhakikisha
kwamba utajiri na njia muhimu za uchumi haviingii katika mikono ya watu
wachache binafsi na wajibu wa vyombo vya dola na watendaji wake kuondoa
ukandamizaji, vitisho, upendeleo, ubaguzi na rushwa.
Katika muundo wa sasa wa Serikali za Mitaa nchini,
Vijiji, Vitongoji na Mitaa ni ngazi muhimu zilizo karibu na wananchi. Ngazi
hizi ndipo mahali pa mwanzo wa Serikali na ambapo mikutano inayowajumuisha
wananchi wote hufanyia kwa lengo la kuwapa wananchi nafasi ya kushiriki
kikamilifu katika maamuzi yanayohusu ustawi na maendeleo yao wenyewe na ya eneo
wanamoishi.
Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa ndio
wasimamizi na watekelezaji wakuu wa shughuli za Serikali katika maeneo yao. Ili
Watendaji hawa waweze kutoa huduma bora kwa wananchi hawana budi kuelewa maana,
dhana na msingi ya Utawala Bora na Demokrasia.
Lakini pia kwa vile maendeleo ya nchi yanategemea
sana ushiriki wa wananchi, ni vyema na wananchi wenyewe wakafahamu kwa undani
maana, dhana na msingi wa Utawala Bora na Demokrasia. Uelewa wa Maafisa
Watendaji wa Vijiji na Mitaa na uelewa wa wananchi ni muhimu sana katika kuleta
maendeleo ya haraka.
Utawala bora ni utaratibu wa uongozi wa kisiasa
kutokana na ridhaa ya wananchi unaolenga kuleta amani, utulivu, ushirikiano na
maendeleo ya wananchi kijamii na kiuchumi bila ubaguzi kwa misingi ya jinsia,
kabila, dini, mila na desturi au haiba ya mtu. Uongozi unaofuata misingi ya
Utawala Bora hufanya kila jitihada kujenga heshima, kuthamini na kukuza uhuru
na utu wa wananchi wote kwa namna ambayo inawezesha utumiaji wa rasilimali na
nguvu kazi kwa makini na ufanisi ili kuhakikisha kuwa wananchi au raia wote
wanapata mahitaji yao ya msingi. Mahitaji ya msingi ni kama vile chakula,
mavazi bora, elimu, afya njema na maji safi na salama. Hivyo, kimsingi Utawala
Bora ni utaratibu wa utumiaji wa madaraka ya umma katika kusimamia rasilimali
za nchi katika jitihada za kuinua hali ya maisha ya wananchi. Utumiaji huo wa
madaraka huambatana na ushirikishwaji wa wahusika wote katika kuhakikisha kuwa
shughuli za umma zinaendeshwa kwa kuzingatia mawazo na maslahi ya wengi,
utawala wa sheria, haki, usawa na uwazi na uwajibikaji.
Tumesema kwamba Utawala bora unazingatia Utawala
wa Sheria. Tukumbuke pia kwamba sheria ni utaratibu ambao umewekwa na watu ili
kuwaongoza kwa namna mbalimbali za kufikia malengo yao katika jamii au kati ya
jamii fulani na nyingine. Katika utawala wa sheria kila mtu anapaswa kuzingatia
na kuongozwa na Katiba ya nchi (ambayo ndiyo sheria mama na sheria nyingine
zote zinapata uhalali kutoka kwenye katiba), sheria, kanuni na taratibu
zilizopo katika kuendesha maisha yake mwenyewe, katika uhusiano na watu wengine
na katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali. Hivyo utawala bora ni ule ambao
unafuata sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kuongoza shughuli za
Serikali za kulinda haki za msingi za
wananchi na kudhibiti vitendo visivyotakiwa au kukubalika katika Jamii.
Utawala bora ni lazima uzingatie Uwazi na
Uwajibikaji. Watendaji wa Serikali za Mitaa na Viongozi wa Kuchaguliwa katika
ngazi mbalimbali wapo kwa minajili ya kuwahudumia wananchi na sio kuwatawala na
kuwaburuza. Yamekuwepo malalamiko ya Maafisa watendaji wa Vijiji na Mitaa
kuwaburuza wananchi. Huo si utawala bora.
Mbali na kuzingatia uwazi na Uwajibikaji, utawala
bora ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa pamoja na usalama wa
raia na mali zao. Jukumu la ulinzi na usalama linategemea sana ushirikiano kati
ya vyombo vya dola, watendaji wa serikali na wananchi wote kwa ujumla.
Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa
wanapaswa kuhakikisha kuwa shughuli za ulinzi na usalama katika maeneo yao
zinaimarishwa kwa kujadiliana na viongozi pamoja na wananchi kuhusu mbinu na
mikakati ya kutekeleza jukumu hilo. Pia Utawala bora ni lazima upige vita
rushwa. Tunajua kwamba rushwa ni adui wa haki na haina budi kupigwa vita na
kila mpenda haki. Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa kwa kushirikiana na wananchi ni lazima
wahakikishe kuwa wanapambana na vitendo vyote vya rushwa katika maeneo yao ili
kufanikisha ujenzi wa Utawala Bora nchini.
Jambo la kukumbusha hapa ni kwamba Utawala bora ni
pamoja na Serikali katika ngazi zote kuwawezesha wananchi kuondokana na
umaskini, ujinga na maradhi kwa kuwapatia huduma bora za kiuchumi na kijamii.
Ni kazi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji na Mtaa kusimamia uwezeshaji huu katika
maeneo yao. Kama tulivyosema hapo juu
kwamba watanzania asilimia kubwa wako vijijini na kwenye mitaa, uwezeshaji huu
ukifanikiwa, basi taifa letu linakuwa limepiga hatua ya haraka katika
maendeleo.
Pamoja na yote niliyoyataja hapo juu ni kwamba Demokrasia ni msingi
muhimu sana katika ujenzi wa Utawala Bora. Bila Demokrasia ni ndoto kujenga
Utawala bora katika ngazi zote za Utawala, kuanzia Vijijini, Mitaa hadi
Serikali Kuu. Neno Demokrasia limetokana na lugha ya Kigiriki “Demos” ikiwa na
maana ya watu na “Kratos” ikiwa na maana ya utawala. Ndiyo kusema, demokrasia
maana yake ni Utawala wa watu walio wengi ambapo msingi wa mamlaka yote ya nchi
ni wananchi wenyewe. Kwa maneno mengine, Serikali ya Kidemokrasia ni ile
inayoundwa na watu wenyewe kwa ajili ya maslahi yao. Maana hii ya Demokrasia,
ni muhimu kueleweka kwa Maafisa watendaji wa Vijiji na mitaa, na pia kueleweka
kwa wananchi ili kusaidia kujenga Utawala bora katika ngazi ya Serikali za
mitaa.
Ni imani yetu kwamba Tamasha la Jinsia, linachangia kiasi kikubwa kujenga
uelewa huu( Maisha endelevu, demokrasia na utawala bora) miongoni mwa
watanzania.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment