EMILIANA ALIGAESHA MAMA SHUJAA WA CHAKULA – MAISHA PLUS 2012.






Katika jitihada za kuwaletea wasomaji wetu wasifu wa Mwana mama leo tumeamua kwenda vijijini. Wiki iliyopita tulikuwa Singida, na sasa tumesogea mbali kidogo hadi mkoa wa Kagera. Lengo ni kuwaletea habari za mama zetu wanaoishi pembezoni sambamba na wale wanaoishi mijini, wasomi, wanasiasa, wafanyakazi, wafanyabiashara hata pia wanawake wa ndani wanaochangia maendeleo katika taifa letu. Hata hivyo kila mama ana mchango mkubwa; wa kuzaa, kulea na kutunza familia; mafanikio ya familia, mafanikio ya mtu binafsi na hata mafanikio ya taifa, nyuma yake kuna mwanamke!

Mwana mama aliyeshika nafasi ya pili katika shindano la Mama shujaa wa Chakula Maisha Plus 2012, ni Emiliana Aligaesha, kutoka Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Karagwe. Mama huyu mwalimu mstaafu mwenye umri wa miaka 69, ni mkulima wa migomba, mahindi, maharagwe na kahawa. Anaendesha kilimo hai na kuwa mfano kwa ndugu, jamaa na marafiki wanaomzunguka.

Kilimo hai, ni kulima kwa kutumia mboji, bila kutumia mbolea za kemikali. Kutandaza nyasi kwenye shamba na kuhakikisha matumizi ya jadi kupambana na wadudu ili kuepukana na matumizi ya dawa za kemikali. Mazao yanayotokana na kilimo hai, yanakuwa na bei kubwa nje na ndani ya nchi. Mfano kahawa iliyolimwa kwa mfumo huu wa kilimo hai, inakuwa na bei ya juu kwenye soko la dunia, maana wenzetu wanaepuka matumizi ya dawa za kemikali ambazo zimeonyesha kuwa na athari kubwa kwa afya ya binadamu, viumbe, ardhi na mazingira pia.

Mbali na kilimo, mama huyu pia ni mfugaji. Ana ng’ombe sita wa kisasa. Anazalisha maziwa na kuuza. Anapata kipato, lakini pia anachangia kuboresha afya ya jamii inayomzunguka. Pia mifugo hii inamsaidia kupata mbolea ya kuweka kwenye shamba lake na kuepukana kabisa na matumizi ya mbolea ya chumvi chumvi

Msimamo wake, aliourithi kutoka kwa mama yake ni kwamba “ mtu yeyote anayeingia shambani, akakata ndizi na kwenda kuipika bila kuangalia magugu yaliyo shambani, anakuwa ni mwizi”. Huo ni msimamo wa mtu mchapakazi. Maana yake ni kwamba, kabla ya kukata ndizi shambani ni lazima kuhakikisha magugu yanapaliliwa! Watu wote, na hawa wa wilaya ya Karagwe, wakifuata msimamo huo wa kupalilia kabla ya kukata ndizi, watakuwa na mashamba mazuri na kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara.

Mama huyu amekuwa mjane, tangia mwaka 1992. Mshahara wake wa ualimu usingemtosha yeye na familia yake, hivyo aliamua kuingia kwa nguvu zote katika kilimo na kufanya uamuzi wa kufuata kilimo hai. Ana ekari sita ambazo anazilima kwa mfumo huu wa kilimo hai na kuzalisha kahawa kwa wingi. Kilimo hiki cha kilimo hai kimemwezesha kuwasomesha watoto wake tisa hadi kwenye ngazi ya vyuo.

Pamoja na kilimo hiki cha kukuza kipato cha familia yake, mama huyu pia amekuwa akizalisha miche ya kahawa na mazao mengine na kuwauzia wakulima wengine. Amekuwa ni mtafiti katika suala zima la kilimo hai na kusaidia kuendesha mafunzo ya wakulima katika vijiji vya wilaya ya Karagwe.

Mama huyu amefuta mawazo ya wengi kwamba wakulima wadogo wadogo hawana faida na kilimo. Yeye ni mkulima mdogo, lakini kwa vile analitunza vizuri shamba lake, ameweza kupata faida kubwa. Kwa kutambua jitihada zake chama cha Ushirika cha Kahawa cha Karagwe (KDCU) mnamo mwaka wa 2005, kilimteua mama huyu kuwa mjumbe wa Halmashauri ya Ushirika huo, akiwa ni mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 9 ya nyuma.

Wilaya ya Karagwe, inazalisha kahawa kwa wingi. Hili ndilo zao kuu la biashara la Wilaya hii. Na kama ilivyo kwa mfumo dume, kazi nyingi za kuhudumia zao hili zinafanywa na wanawake, lakini mapato yanakwenda kwa wanaume. Imani kwamba wanaume ndo wana uwezo wa kupanga matumizi na kutunza familia. Bahati mbaya kwa asilimia kubwa wanaume wamekuwa wakifaidi asilimia kubwa ya mapato ya kahawa kuliko wanawake na watoto.

Mama Aligaesha, ameweza kuonyesha wazi kwamba hata wanawake wakipata nafasi, si lazima iwe kwa kuwa mjane kama yeye, wanaweza! Yeye ameweza kuyatumia vizuri mapato ya kahawa kwa kuwasomesha watoto na kutengeneza maisha bora kwa familia yake na jamii inayomzunguka.

Mbali na kuwa mwanachama wa chama cha Ushirika cha Kahawa cha Karagwe, mama huyu pia ni mwanachama wa shirika la KADERES. Shirika hili linaendesha umoja wa kuweka na kukopa. Na limefanya kazi kubwa kuviendeleza vikundi hivi na kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu vijijini. Pia shirika hili la KADERES, limekuwa mstari wa mbele kuendeleza Kilimo hai na kutafuta soko zuri la kahawa nje ya nchi. Shirika hili sasa hivi limeanzisha kampuni ya kuuza kahawa nje ya nchi. Mwaka huu, shirika hili limewalazimisha watu wanaonunua Kahawa wilaya ya Karagwe kupanga bei nzuri, baada ya shirika hili kupitia kampuni yake ya kuuza kahawa kutangaza bei nzuri ya shilingi elfu moja miatano kwa kilo. Mama Emiliana Aligaesha, amekuwa ni mwanachama hai wa shirika hili la KADERES, na ni mmoja wa wale wanaofaidi soko la nje la Kampuni hii ya KADERES.

Pia shirika la KADEES, lilimuunga mkono mama Emiliana Aligaesha, kwenda kwenye shindano la mama shujaa wa chakula-Maisha plus. Haikushangaza mama huyu kuchukua nafasi ya pili kwenye mashindano haya, maana huyu ni mama aliyetoka kwenye mazingira ya kuchapa kazi na ni shujaa kwa miaka mingi. Huyo ndiye Mama Emiliana Aligaesha, mshindi namba mbili ya Mama Shujaa wa chakula – Maisha pulus 2012.

Na,

Padri Privtus Karugendo.









0 comments:

Post a Comment