Tumezoea
kushuhudia vibaka wakichomwa moto; hili ni jambo linaloendelea na tunaelekea
kulikubali katika utamaduni wetu! Ni utamaduni wa kutisha maana tutafika mahali
kila kero wananchi wanajichukulia sheria mkononi kama ilivyosikika juzi Jijini
Dar-es-Salaam vijana wakitishia kuviweka moto vituo vya mafuta kwa kitendo cha
vituo hivyo kusitisha huduma hiyo ili kuishinikiza serikali kubadilisha bei ya
mafuta. Vituo vya mafuta vilijichukulia sheria mkononi (Mgomo), na vijana
walitaka kujichukulia sheria mkononi (Kuvichoma vituo vya mafuta), ni hatari!
Zamani,
wengine watahoji zamani ya lini? Sina maana zamani ya mwaka 2000, kwa wengine
ni zamani!, Sina maana zamani ya miaka ya tisini au thamanini katikati,
ninamaanisha zamani ya miaka ya 50,60,70 na 80 mwanzoni, kulikuwepo na wahalifu
wa aina mbali mbali: majambazi, wezi, vibaka, wahaini nk. Walikamatwa, walifikishwa
polisi, polisi walifanya kazi yao kwa
uaminifu na uzalendo na wahalifu walifikishwa mahakamani na sheria ilichukua
mkondo wake kwa msingi wa haki. Wahalifu walipatiwa haki yao ya kikatiba ya
kusikilizwa na kujitetea. Mwamwindi, alinyongwa baada ya kesi yake kusikilizwa
kwa muda wa kutosha na baada ya jitihada za serikali za kuhakikisha kama Mwamwindi, alikuwa na akili timamu
wakati wa kitendo cha mauaji aliyoyafanya ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa. Baada ya mauaji hayo ya kwanza na ya
aina yake hapa Tanzania, ya kiongozi wa ngazi
ya juu katika serikali, Mwamwindi, alijisalimisha mwenyewe na kuubeba
kwenye gari mwili wa marehemu hadi kwenye kituo cha polisi. Polisi,
hawakujichukulia sheria mkononi, kwa kumpiga risasi Mwamwindi, hapohapo. Alikuwa
amefanya kosa kubwa la mauaji ya kiongozi wa serikali. Aliwekwa ndani na kesi
yake iliendelea na kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Hakukuwepo na siri hadi
kila mtu aliamini kwamba haki ilitendeka!
Wale waliotaka kuipindua
serikali ya Kambarage, na njama zao
kugundulika dakika za mwisho, kesi yao iliendelea kwa miaka mingi na kutaganzwa
kwenye vyombo vya habari. Karibu wahaini wote waliachiwa huru.
Zamani hizo wahalifu waliopatikana na makosa,
walipatiwa adhabu ya vifungo. Baadhi yao kifungo ilikuwa ni nafasi ya
ukarabati, elimu na toba. Wengi walijifunza mambo mbali mbali kama ufundi,
kilimo, ufugaji na lugha mbali mbali. Baada ya kifungo majambazi, wezi na
vibaka waligeuka na kuwa raia wema na kuendelea kutoka mchango wao katika
kulijenga taifa letu la Tanzania.
Ipo mifano mingi
inayoonyesha kwamba zamani kila raia alikuwa na haki sawa mbele ya sheria kama
inavyosema katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania:
Ibara 13(1) “Watu wote
ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na
kupata haki sawa mbele ya sheria.
13(3) “ Haki za raia, wajibu na
maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamriwa na mahakama na
vyombo vinginevyo vya mamlaka ya nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.”
13(6) “Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria,
mamlaka ya nchi itaweka taratibu zinazofaa
au zinazozingatia misingi kwamba :-
(6) a) “ Wakati haki na wajibu wa
mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kinginecho
kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa
ukamilifu, na pia haki ya kukata rufani au kupata nafuu nyingine ya kisheria
kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo kinginecho kinachohusika;
(6) d) “ Kwa ajili ya kuhifadhi
haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote
zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai na katika shughuli
nyinginezo ambazo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika kuhakikisha
utekelezaji wa adhabu;
(6) e) “ Ni marufuku kwa mtu
kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.”
Leo hii majambazi, wezi
na vibaka wanahukumiwa kifo bila kufikishwa polisi au mahakamani. Wananchi
wenye hasira wanajichukulia sheria mkononi. Mtu asiyekupenda, mwenye chuki
binafsi nawe, akikunyoshea kidole na kusema wewe ni mwizi, katikati ya jiji la
Dar-es-Salaam, Mwanza au miji mingineyo ya hapa nchini, atakuwa anakutakia
kifo; utavikwa tairi shingoni, utamwagiwa petroli na kuchomwa moto! Matukio
kama haya ni mengi kiasi cha mtu kuwa na maswali mengi juu ya umuhimu wa kuwa
na katiba. Watu, ambao wengi wao ni vijana wa kulijenga taifa hili wanapoteza
maisha yao kwa kukwapua saa, mikufu ya dhahabu, pesa, simu nk.
Hakuna mtu anayeunga
mkono matendo ya ujambazi, vibaka na wezi. Haya ni matendo yanayovunja amani na
utulivu katika jamii. Jambo muhimu la
kujiuliza ni je, jambazi, kibaka au mwizi hana haki ya kujieleza mbele ya
sheria kama inavyotajwa kwenye katiba ya nchi yetu? Je, jamii yetu haina la
kujifunza kutokana na matendo haya? Je, jamii haina la kuwafundisha na
kuwakarabati majambazi, vibaka na wezi? Je, jambo la msingi ni kuwaua watu hawa
au ni kutafuta chanzo cha matendo yao kiovu na kutafuta mbinu za kuyaponya? Vibaka
na majambazi wana mangapi ya kuilaumu na kuishutumu jamii yetu? Wana kero ngapi
ndani ya roho zao? Ni mangapi yamewazunguka na kuwalazimisha kutenda yale
ambayo wasingependa kuyatenda? Je, wanaiba ili kuwapeleka watoto shule? Wanaiba
ili kupata pesa za kulipia matibabu? Wanaiba ili kupata pesa za kununua viwanja
na kujenga nyumba za kuishi? wanaiba ili wanunue nguo, chakula na kuishi maisha
bora? Je, wanaiba ili watoe sadaka na zaka kwenye dini zao - maana pesa
zafanana, ziwe za wizi au zile zilizopatikana kwa njia za halali – viongozi wa
dini wanapokea tu bila kuhoji – kwao la msingi ni pesa! Wanaiba kwa vile hawana
kazi? Au wanaiba kwa vile karibu watanzania wote ni wezi – kama si majambazi wa
kuvamia, basi wanaiba na kupora mali ya taifa! Je, bila ya kuwapatia majambazi,
vibaka na wezi nafasi ya kuwasikiliza tunawezaje kugundua chanzo? Mbona kadri
majambazi, vibaka na wezi wanavyouawa na wananchi wenye hasira ndivyo ujambazi
na matendo mengine ya uovu yanavyoongezeka kwa kasi ya kutisha? Je, si kweli kwamba
majambazi, vibaka na wezi wanakuwa na watu wengi nyuma yao? Je, si ukweli
kwamba matendo haya ya uovu yanaongozwa na vigogo? Vigogo hawa, si wanaendelea
kuishi na kuyafurahia maisha wakati watu wanyonge wanakamatwa na kuchomwa moto?
Je, kama uchumi wa nchi
unakuwa mikononi mwa watu wachache, tunawezaje kuthibiti ujambazi? Wananchi
wanasema majambazi, vibaka na wezi ni kero kubwa katika jamii ya leo. Tofauti
na zamani ambapo vibaka na majambazi walikuwa wanashughulikiwa na sheria, siku
hizi wakikamatwa baada ya siku mbili au
tatu wanakuwa tena mitaani wakienelea na vitendo vyao viovu. Rushwa na hongo
inatumika kuwaachia. Hivyo wananchi wanaona njia pekee ya kumaliza kero hii ni
kifo. Serikali yetu inayaona haya yakitendeka, badala ya kuyakemea na kuielimisha
jamii juu ya kuifuata katiba, utawala wa kisheria, elimu ya uraia na kuheshimu
haki za binadamu, inashikwa na kigugumizi. Viongozi wetu kama vile waheshimiwa
wabunge wanaogopa kuwakemea wananchi wanaojichukulia sheria mkononi ili
wasinyimwe kura. Wanatanguliza maslahi binafsi, bila kutanguliza maslahi na
heshima ya taifa letu.
Jambo tunalolisahau wote
ni kwamba Tanzania, kuna kero nyingi. Je, kila kero wananchi wakiamua
kujichukulia sheria mkononi mwao, ni nani atakuwa salama? Waheshimiwa Wabunge
hawatakuwa salama, viongozi wa serikali hawatakuwa salama, viongozi wa kidini
hawatakuwa salama, matajiri hawatakuwa salama na sisi sote hatutakuwa salama!
Mifano ni mingi. Rwanda, Maaskofu walichinjwa, mapadre, masista, viongozi wa
dini mbalimbali, viongozi wa serikali, matajiri na kila mnyarwanda hawakupona.
Ni hatari wananchi wakiamua kujichukulia sheria mkononi. Ni bora kuthibiti
mapema hali hii inapojitokeza katika jamii.
Msemo wa Waswahili wa: “
Usipoziba ufa utajenga ukuta” utufikirishe. Ilianza kero ya vibaka. Wananchi
walichoka na kuamua kujichulia sheria mkononi. Sasa hivi imekuwa ni desturi
ambayo ni kazi ngumu kuizuia! Akikamatwa kibaka anavikwa tairi shingoni,
anamwagiwa petroli na kuchomwa moto! Ikafuata kero ya majambazi. Wananchi
walichoka na kuamua kujichukulia sheria mkononi. Ukisikiliza taarifa ya habari,
utasikia jinsi wananchi wanavyowazingira majambazi na kuwaua. Baada ya hapo
utasikia pongezi za polisi! Ni muhimu kufuata sheria, kuongozwa na katiba na
kuheshimu haki za binadamu, vinginevyo ni hatari kubwa!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment