BURIANI PADRI DESIDERY
KASHANGAKI 1911 – 2011.
Tarehe 26.10.2011, padri
Desidery Kashangaki, aliaga dunia na kuzikwa Rubya-Bukoba tarehe 28.10.2011
akiwa na umri wa miaka miamoja na miezi mitano! Mungu amlaze mahali pema
peponi.
Kuna mambo mengi ya
kuandika juu ya padri huyu mzalendo, maana miaka 100 si haba. Ni watu wachache
wanaobahatika kufikisha umri huu. Jambo la kwanza juu ya padri huyu ni kwamba
yeye ndiye padri wa kwanza wa Bukoba kufikisha umri wa miaka miamoja. Pili ni
kwamba padri huyu alilitumikia kanisa na taifa la Tanzania kwa kipindi cha miaka sitini (60). Mbali na kazi zake za
kiroho, yeye alikuwa mwalimu wa chuo cha walimu cha Butimba Mwanza. Alifundisha
pale muda mrefu na kwa njia hiyo amewafundisha walimu wengi hapa Tanzania. Kwa
Tanzia hii basi wanafunzi wake popote walipo wapate habari kwamba mwalimu wao
hatunaye tena duniani.
Tatu, ni padri
aliyependa elimu. Mbali na masomo yake ya theolojia, alisoma digrii ya Elimu ya
watu wazima Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, akiwa na umri wa miaka 60. Kupenda
kwake kusoma kulimfanya abaki kijana muda wote. Ingawa alikuwa mtu mzima wa
miaka 100, maongezi yake na uelewa wa mambo ulikuwa ni kama wa kijana mdogo.
Nilipomtembelea mwezi wa tano mwaka huu wakati alipofikisha miaka 100,
nilishangaa sana kuona anavyofahamu dunia inavyokwenda. Alikuwa na redio yake
ndogo, akisikiliza habari za dunia.
Nne, alikuwa mshauri wa
kiroho wa Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hata masomo yake ya chuo
kikuu cha Dar-es-Salaam, alilipiwa na Mwalimu.
Tano , ni mtu aliyekuwa
amejaliwa afya ya pekee. Hakuwai kuugua katika maisha yake yote. Anakumbuka
kudungwa sindano mwaka wa 1935 kule Katigondo Uganda. Hakukumbuka ulikuwa ni
ugonjwa gani. Lakini baada ya hapo yeye hakujua malaria au magonjwa mengine
kama shinikizo la damu, kisukari na mengine. Daima aliuliza dalili za malaria.
Hata kifo chake hakikutokana na ugonjwa, tarehe yake ilifika tu akaitika kwa
Muumba wake.
Sita, alikuwa
mtanashati, mtu wa majivuno, mwenye kiburi cha elimu, lakini mwenye kuipenda na
kuiheshimu kazi yake ya upadri. Majivuno yake na kiburi havikuigusa roho yake
ya wema, ucheshi na kuwapenda watu. Alipenda sana lugha ya mafumbo, na maisha
kwake lilikuwa ni fumbo la imani. Aliwachukia watu waliotumia lugha ya wazi na
kuyachukulia maisha kuwa ni kitu cha wazi. Alisisitiza umuhimu wa kuyafumba
mambo na kuyafumba maisha! Alitaka kuishi kwa staha, alikula kwa staha na
kunywa kwa staha, asingeweza kunywa bia zaidi ya mbili na chakula kama hakuna
uma na kisu, basi hawezi kula!
Saba, na labda hii ndiyo
sehemu mbaya na ngumu sana katika maisha yake; aliadhibiwa na Askofu wake,
akiwa na umri wa miaka 80. Inashangaza
na kusikitisha, lakini ndio ukweli wenyewe. Askofu wake hakuweza kumsamehe kwa
zaidi ya miaka 20, hadi juzi siku mbili kabla ya kifo chake. Maana yake ni
kwamba Askofu, kiongozi wa kiroho, alitunza hasira moyoni mwake zaidi ya miaka
20. Swali la kujiuliza ni je, kama Askofu hawezi kusamehe, Wakristu wengine
watafanya namna gani? Je hii ndiyo imani ya Yesu wa Nazareti, aliyetwambia
tusamehe saba mara sabini; na kwamba mtu akikupiga shafu la kushoto umgeuzie na
la kulia? Ni imani ya Mungu wetu wa upendo na huruma?
Chanzo za adhabu yake ni
nini? Padri Desidery Kashangaki, alipostaafu kazi ya kufundisha Chuo cha Ualimu
na kurudi nyumbani kwao Bukoba, akiwa na umri mkubwa, maisha ya Parokiani
yalikuwa magumu. Posho aliyokuwa akiipata akiwa mwalimu hakuipata kule
parokiani. Alianza kufuatilia na kuuliza juu ya maisha ya mapadri wanaoishi parokiani
na hasa mapadri wazee kama yeye. Baadaye aligundua kwamba Roma kila mwaka
inatuma pensheni ya mapadri waliofikisha miaka 60. Yeye alikuwa na miaka 80,
bila kupata pensheni. Ina maana pensheni yake ya miaka 20 ilikuwa inaingia
mfuko gani? Alianza mchakato wa kudai pensheni yake kwa Askofu wake. Hiki
ndicho chanzo cha magomvi yake na Askofu wake, Askofu Nestory Timanywa, wa
Jimbo Katoliki la Bukoba.
Magomvi ya Padri
Desidery Kashangaki na Askofu Timanywa, yalikuwa makubwa kiasi cha Askofu
kuomba msaada wa polisi ili kumwondoa Padri Kashangaki kwenye nyumba za kanisa.
Adhabu yake ilikuwa kwenda kuishi nyumbani kwao alikozaliwa. Mtu mwenye miaka
80, na amelitumikia kanisa miaka 60, tukio hilo la kumfukuza kwenye nyumba za
kanisa halikuwa la kawaida. Iliwashangaza watu wengi, hata kama Padri Desidery
Kashangaki, alitumia kiburi na majivuno kudai pensheni yake, umri wake na miaka
aliyolitumikia kanisa ilitosha kumchukulia alivyo, kuliko kumfukuza na kumtupa
mitaani.
Watu wengi walijitokeza
kumwombea msamaha Padri Desidery Kashangaki kwa Askofu wake, lakini jitihada
hizo ziligonga mwamba. Askofu hakutaka kusikia wala kupatanishwa na padri wake.
Alikuwa na hasira kubwa ambayo iliibua hata makosa ambayo Padri Desidery
Kashangaki, aliyatenda akiwa kijana wa miaka 40.
Bahati nzuri, Askofu wa
jimbo la jirani la Rulenge, wakati huo, siku hizi linaitwa Rulenge-Ngara,
Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, alimwonea huruma Padri Kashangaki na
kumkaribisha jimboni kwake. Hivyo Padri Kashangaki, aliishi kama “Mkimbizi”
kwenye jimbo la Rulenge. Waswahili wanasema Ng’ombe wa masikini hazai…. Mwaka
1996, Askofu Mwoleka, alistaafu. Roma ilimteua Askofu mwingine, Mheshimiwa sana
Askofu Severine NiweMugizi, ambaye kwake maisha ni sheria. Hakuna hekima,
busara wala utu – sheria ni msumeno. Ni lazima kufuata sheria. Kuna ushahidi wa
kutosha kwamba hata yeye mwenyewe anashindwa kuzifuata baadhi ya sheria, lakini
anataka wengine wazifuate sheria. Aliposhika utawala wa Jimbo Katoliki la
Rulenge, alimfukuzia mbali Padri Desidery Kashangaki, maana hakuwa Jimboni
Rulenge Kisheria. Askofu Mwoleka alimpokea Padri Kashangaki, kiubinadamu maana
alikuwa mkimbizi. Kumtakisha mkimbizi hati ya kusafiria, ni uwendawazimu.
Ingawa Padri Kashangaki, alifukuzwa na Askofu wake, mtu aliyefanya dhambi kubwa
ni yule aliyemfukuza mara ya pili; aliyemfukuza mkimbizi. Hata sheria za
Kimataifa, ukiachia mbali hekima na busara, zinazuia kumfukuza mkimbizi. Hivyo
Padri Desidery Kashangaki, alihama kutoka nyumba za kanisa la Jimbo Katoliki la
Rulenge na kuishi mitaani. Aliishi maisha magumu. Watu wengi Wakristu kwa
Waislamu walijitokeza kumsaidia na hasa wanafunzi wake. Hata hivyo kipindi
kilikuwa ni kirefu kiasi cha wale waliokuwa wakimsaidia kuanza kuchoka.
Miaka ya mwisho ya
maisha yake, kwa kushirikiana na mapadri waliokuwa na roho ya utu, walimsaidia
“kuitekea nyara” parokia ya Bugene Karagwe na kuishi pale. Lengo lake na
matumaini yake ilikuwa ni kurudi kwao Bukoba kudai pensheni yake.
Nilipomtembelea mwezi wa tano mwaka huu, aliniambia kwamba atakwenda Bukoba
kudai pensheni yake. Bahati mbaya mauti yamemkuta kabla ya kulipwa pensheni
yake. La kumshukuru Mungu, ni kwamba amezikwa nyumbani kwao Bukoba, kama
alivyokuwa akitamani. Mungu, amlaze mahali pema peponi rafiki yetu, ndugu yetu
na Mtanzania mwenzetu padri Desidery Kashangaki.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment