UTETEZI WA JINSIA NA
UKOMBOZI WA WANAWAKE KIMAPINDUZI NDANI YA MIAKA HAMSINI YA UHURU WETU.
TGNP,FEMACT na mashirika mengine yanayoshughulika na
utetezi wa jinsia na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi wanatukaribisha
kutafakari pamoja juu ya mchango wao na changamoto walizokumbana nazo ndani ya
miaka hamsini ya uhuru wetu. Mashirika mengi ya kutetea Jinsia na ukombozi wa
mwanamke kimapinduzi yameanzishwa baada ya Beijing. Hivyo yaliyo mengi
yanatekeleza maamuzi ya mkutano huo wa Beijing. Kwa namna moja ama nyingine
tunapozunguzia mchango wa mashirika haya ni kutaka kujua mafanikio na
changamoto ya kutekeleza maazimio ya Beijing. Kwa upande mmoja mawazo haya ni
sahihi kabisa, lakini kwa upande wa historia ya Tanzania, harakati za kijinsia
na ukombozi wa mwanamke zinakwenda nyuma hadi kwenye kupigania uhuru wetu.
Tulipigana kwa pamoja
kumwondoa mkoloni na kushindwa kufuta kabisa vikaragosi vya ukoloni. Mashirika
yasiyokuwa ya kiserikali yanajaribu kupambana na vikaragosi vya ukoloni. Mfumo
wa Soko huria na nguvu za kutisha za ubeberu vinatufanya kuwa na “Uhuru” wa
bendera. Serikali yetu inaelekea kuwa tegemezi mno kwa wale wale waliotutawala,
wakiwemo Wajerumani, Waingereza, Wamarekani, Japani na nchi nyingine za “Kundi
la nchi nane”. Hivyo serikali yetu inajikuta haina uhuru wa kuamua mambo yake
yenyewe, kwa mfano uwezo wetu wa kufanya maamuzi kuhusu mambo ya msingi ya
jinsi ya kugawa rasilimali zetu ni mdogo na umefifishwa na hali yetu ya
utegemezi.
Mfano mwingine unahusu
mapambano yetu kuhusu umilikaji wa ardhi, jambo ambalo ni kati ya yale
yaliyowasukuma Watanganyika kusimama kupigania uhuru wao. Muda mfupi baada ya
uhuru, Serikali ilipitisha sera ya ardhi ambayo ilitambua umiliki wa ardhi kuwa
wa jamii na kuwazuia wageni wasimiliki ardhi. Sera hii ya ardhi imekuwa
ikipigwa vita na wawekezaji na watanzania wenye uroho tangu miaka ya 1980, na
hatua kwa hatua, Serikali imekuwa ikiruhusu matumizi ya ardhi kwa wageni katika
sekta za kilimo, utalii, uchimbaji wa
madini na mabenki yanayowekeza hapa nchi. Hivyo basi, suala la ardhi limeanza
kuibuka upya na wanaharakati pamoja na jamii katika sehemu mbali mbali wameanza
kujipanga upya ili kulipinga.
Utafiti uliofanywa na
Susan Geiger, juu ya Wanawake wa TANU, unaonyesha wazi kabisa kwamba wakati wa
kupigania uhuru, wanawake walipambana bega kwa bega na wanaume. Kitabu hiki
kilichotafsiriwa na TGNP katika lugha ya Kiswahili kinafichua ukweli kwamba
wakati wa kupigania Uhuru, wanawake walikuwa mstari wa mbele; walitembea nchi
nzima wakihamasisha watu kujiunga na TANU, walichangisha fedha za kuendesha
chama na harakati nyingine za kupigania uhuru, walifanya kazi mbali mbali za
kupata kipato ili waweze kupata fedha za kuendesha chama. Hivyo tunapoangalia
utetezi wa jinsia na ukombozi wa Mwanamke kimapinduzi ni lazima tuangalie mbele
zaidi ya kabla ya Beijing.
Kitabu cha Susan Geiger,
kinatupatia majina mengi ya wanawake waliopigania uhuru. Majina haya hayasikiki
tena. Yamezikwa na kufunikwa na mfumo dume. Ingawa jina la Bibi Titi Mohamed
linasikika kwa mbali, majina ya
wanawake wengine alioshirikiana nao Dar-es-Salaam, hayasikiki kabisa. Hata
mikoani kulikuwa na wanawake walioshiriki harakati za ukombozi wa taifa letu.
Kule
Kilimanjaro kulikuwa na
Halima Selengia Kinabo, Mwamvita Salim, Zainab Hatibu, Morio Kinabo, Violet
Njiro, Elizabeth Gupta, Kanasia Tade Mtenga,Natujwa Daniel Mashamba na Lucy
Lameck. Hata kule Mwanza kulikuwa na wanaharakati wanawake waliopigania uhuru
wa taifa letu, lakini historia haiwakumbuki
tena. Wanawake hao ni: Agnes Sahani, Aziza Lucas, Tunu Nyembo, Halima
Ntungi, Mwajuma Msafiri, Pili Juma, Mwamvua Kibonge, Zuhura Mussa na
Chausiku Mzee.
Ni wazi wako wanawake
wengine wengi walioshiriki harakati za kuleta uhuru wa taifa letu, ni kazi ya Mashirika
yanayotetea usawa jinsia na ukombozi wa Mwanamke kuendelea kufanya tafiti na
kuibua majina mengine ili kuweka kumbukumbu sahihi ya historia ya taifa yetu.
Kama tutakavyoona wakati
wa kutafakari juu ya mchango wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
yanayojishughulisha na masuala ya jinsia na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi ni
changamoto ya utegemezi. Mashirika mengi au tuseme yote yanategemea fedha
kutoka nje ya nchi. Utafiti juu ya Wanawake wa TANU, unatufichulia “siri”
kwamba wakati wa kupigania uhuru na miaka michache baada ya uhuru Wanawake wa
TANU, walikuwa na uwezo wa kuendesha mambo yao bila msaada wowote kutoka nje au
kutoka kwa serikali ya mkoloni. Msimamo huu wa kujitegemea uliwawezesha
wanawake kuunda vyama vyao vyenye nguvu kiasi cha kuwatishia “Usalama” wanaume.
Uamuzi wa serikali wa kuvivunja vyama hivi vya wanawake mara baada ya uhuru na
kutengeneza chama kimoja cha UWT, ambacho kilikuwa chini ya serikali na kupata
ruzuku kutoka serikalini ni ishara tosha kwamba vyama hivi vilikuwa na nguvu za
kutisha.
Kwenye kitabu cha Susan
Geiger, Bibi Titi Mohamed, ananukuliwa akielezea yaliyotokea “ Tarehe 2
Novemba, mwaka 1962, Mheshimiwa Nyerere aliagiza kwamba vyama vyote vya
wanawake Tanganyika vivunjwe; yaani, YWCA, Baraza la Wanawake Tanganyika na
UMCA, ili viungane kuunda Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT)”
Kwa maoni ya Bibi Titi
Mohamed, kuvunjwa kwa vyama vya wanawake na kuanzisha chama kimoja cha UWT
kilichokuwa chini ya CHAMA na Serikali
kulidhoofisha maendeleo ya kasi ya ukombozi wa wanawake na usawa wa kijinsia
katika taifa letu huru. Utegemezi uliminya uhuru wa wanawake kutoa maoni na
kufanya mambo yao kwa uhuru. Wanawake wengi wa TANU, hawakuwa na elimu ya juu,
waliongozwa na hekima, busara, kuona mbali lakini hasa na uzalendo. Pamoja na kutokuwa na elimu ya juu wanawake wa TANU
waliona wazi tishio la kuwa tegemezi;
walilipinga wazo hilo kwa nguvu zote, lakini walizidiwa nguvu na vijana wasomi.
Usomi wao haukuwasaidia kuona tishio kubwa la utegemezi. Kama anavyoelezea Bibi
Titi “UWT ilitaka wizara ilipie semina na walimu waliokuwa wakitoa
mafunzo kwa wanawake”. Ukaanza ugonjwa wa posho na kutegemea misaada hadi leo
hii.
Bibi Titi anaendelea
kuelezea makosa yaliyopelekea kudhoofisha nguvu za wanawake wa TANU; “
Wanawake wengi, vijana na wasomi waliokuwa kitovu cha uongozi UWT, waliteuliwa
kutoka taasisi na wizara za serikali, kutafuta fedha, kutoa miongozo katika
mafunzo na warsha za uongozi, na katika miradi ya lishe…”
Hivyo kwa njia hii ule
uwezo wa wanawake wa kujitafutia fedha za kuendesha mambo yao wenyewe ikawekewa
kizingiti.
Susan Geiger, katika
kitabu chake anasema hivi kuhusu hali hiyo:
“ Sasa ni dhahiri
kwamba UWT haikuwa mwendelezo wa harakati za wawawake wa TANU. Mkutano Mkuu wa
Wanawake wa Afrika uliofanyika Dar-es-Salaam mwaka 1962, uliweka wazi katika
rasimu ya katiba yao kwamba UWT ni ya kupigania ukombozi wa wanawake ili waweze
kushiriki katika shughuli za -kijamii na za kisiasa Afrika. Lakini Nyerere
na washauri wake waliamua kwamba wanawake walihitaji kuendelea na kuendelezwa,
na kwamba vikundi vilivyokuwa tayari vinafanya kazi hii viungane
chini ya chama kimoja kitakachoshirikisha wawawake wote na kudhibitiwa na
serikali. Msomi mmoja alipatwa na mshangao kuwa mara baada ya uhuru, wanawake
wamekuwa wajinga na walio nyuma kimaendeleo. Suala la namna ya kuhamasisha
wanawake likawa tatizo mara baada ya uhuru. Hiyo ilikuwa kejeli”.
La kustaajabisha zaidi
ni mfumo dume uliodumaa wakati wa kupigania uhuru na kuibuka tu mara baada ya
Uhuru. Katika kitabu cha Susan Geiger,
Bibi Titi, ananukuliwa akieleza mawazo ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii
wakati ule juu ya wanawake: “ Akizungumza kwenye mkutano siku ya pili, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Bwana
Mgonja, alizungumza katika njia iliyofifisha ari ya siasa kwa wanawake na
kuimarisha mamlaka ya serikali. Wakati kitengo cha Wanawake kilikuwa
kinahamasisha wanawake wajiunge katika harakati za kujenga taifa, Mgonja
aliwaambia wanawake kwamba wakilea watoto watakuwa wamelea taifa zima.
Aliwasifu wanawake wa juhudi zao katika kupigania uhuru, lakini kwa sasa
walichotakiwa kufanya ni kulima, kufuga kuku, kuchimba visima na
kupanda miti pamoja na kushiriki katika
kisomo cha watu wazima. Mgonja alionya kwamba itabidi utamaduni wa Kiafrika
ukuzwe, kwani wakoloni waliudharau”.
Mgonja, alikuwa
akiufufua Mfumo Dume, uliokuwa umedumaa wakati wa kupigania uhuru. Kwa maoni
yake kuukuza utamaduni wa Mwafrika ni kuendeleza mfumo dume. Inaelekea hapa
ndipo tulipoteleza katika suala zima la usawa wa kijinsia. Anavyosimulia Bibi
Titi Mohamed, katika kitabu cha Susan Geiger, ni kwamba idadi kubwa ya wanaume
waliunga mkono msimamo wa Mgonja, wa wanawake kurudi jikoni baada ya kupigania
uhuru. La kushangaza zaidi ni kwamba hata wanawake vijana wasomi waliunga mkono
mawazo ya Mgonja, maana wanawake wa TANU waliopigania Uhuru walikuwa tishio.
Bibi Titi Mohamed
anaelezea: “ Kati ya viongozi wanaume, aliyeunga mkono wazo la usawa kwa
wanawake alikuwa Nyerere. Yeye alikuwa ameshuhudia wanawake. Hata tuliposema
huko bungeni kwamba wanaume waadhibiwe kwa kuwapa wasichana mimba, Nyerere
alisimama kidete nyuma yetu…. Kati ya
wanawake wachache bungeni (tuliopigania suala hili) tulikuwa mimi, Lucy,
Barbara Johansson na mwanamke mwingine aliyekuwa ameolewa na Mgoa huko Amboni,
Tanga. Wanaume walitukasirikia, Nyerere alisema ni lazima sheria hiyo ipite,
ili wanaume wanaolaghai wasichana na kuwapa mimba walipe faini, wafungwe au
watunze hao watoto”
Hivyo wakati wa
kutafakari miaka hamsini ya Uhuru wetu, ni lazima tuchunguze kwa makini yale
yaliyopelekea kufuta na kufunika historia ya ukombozi iliyoongozwa na wanawake.
Kwa nini mfumo dume ulidumaa wakati wa kupigania uhuru na kuibuka mara tu baada
ya Uhuru? Harakati za wanawake wa TANU zilisambaa hadi vijijini, je haraka za
siku hizi zinakwenda hadi vijijini?
Kama tutakavyoona kwenye
tafakuri yetu ni kwamba kati ya changamoto kubwa ya Mashirika mengi yasiyokuwa
ya kiserikali ni kujikita mijini na kusahau kabisa kutandaa hadi vijijini.
Wakati inaanzishwa UWT, Oscar Kambona alionya umoja huo kutandaa hadi vijijini.
Bibi Titi, anaeleza katika kitabu cha
Susan Geiger:
“Oscar Kambona,
aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa, ndiye pekee aliyezungumza kumuhimu wa
Kitengo cha wanawake, ….Alisema kuwa wanawake wanahitaji kufanya kazi kwa
bidii, kwani hakuna taifa linalodhaniwa
kuendelea kama wanawake hawajaendelea. Kambona alisisitiza kwamba maendeleo ni
lazima yawe ya vijijini na mijini. Viongozi wa UWT walishauriwa kurudi vijijini
kuweka mipango ya shughuli na siyo kukazania sehemu za mijini tu”
Ushauri wa Oscar Kambona,
haukufuatwa na UWT na hadi leo hii mashirika mengi yanayotetea usawa wa Jinsia
na ukombozi wa Mwanamke kimapinduzi yamejikita mijini. Ingawa si kawaida kuanza
tafakuri na hitimisho, ni vyema kuzingatia ushauri wa Oscar Kambona, wakati
tunajiandaa kuanza safari nyingine ya miaka hamsini ya Uhuru wetu.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment