TUZO ZA UANDISHI WA HABARI NA MASWALI MENGI YA KUHOJI
Ni wapongeze wale wote waliopata tuzo. Na pia Gazeti letu Raia Mwema, lilipata tuzo, ingawa si nyingi kama za vyombo vingine vya habari, lakini tumetuzwa. Siandiki kulalamika au kuonekana nina kinyongo. Hoja ninayoijenga hapa ni ile ambayo nimeijenga siku za nyuma. Na hapa naongelea “Ukanjanja”.
Labda kabla sijaiingia kwenye hoja ya ukanjanja, niweke wazi wasi wasi wangu wa chombo kimoja cha habari – Mwananchi, kupata zawadi 10, kati ya 19 zilizotolewa. Kwa uandishi, na kama MTC walivyotueleza kwamba walipata washindani zaidi ya 750, ni vigumu sana kitu kama hiki kutokea, labda tukielezwa kwamba washiriki wengi walitoka Mwananchi. Kila mwandishi ana namna yake ya kuandika, na kila mwandishi ni tofauti na mwingine. Kila chombo cha habari kina sera zake na namna yake ya kuandika habari. Haiwezekani sera na namna ya kuandika ya chombo kimoja iwavutie zaidi waamuzi, bila waamuzi hao kuwa washabiki na washirika wa chombo hicho cha habari? Labda swali la kawaida, washindi hao, wamekuwa wakichomoza katika magazeti kwa habari zao hizo muhimu kiasi cha kuchomoza miongoni mwa washindani 750.
Msomaji wangu kutoka mbeya alinipigia simu na kusema “Mbona kati ya wale wanaopiga vita ufisadi, sijasikia hata mmoja amepewa tuzo? Je Jembe langu Kubenea amepata tuzo au ametoswa?”
Je tushawishike kusema kwamba MCT, wanafanya kazi kwa maelekezo maalumu ili kuhakikisha wale wanaopata tuzo ni wa msimamo wa kati? Wakati mwingine ni vigumu kukwepa vishawishi kama hivi!
Na katika hali nyingine ya kawaida ni vigumu katika ushindani mkali wa washiriki zaidi ya 750, mtu mmoja akanyakua zawadi zaidi ya tatu. Sitaki kuamini kwamba wale wengine wote wameandika pumba!
Nina imani kwamba hili zoezi la kumtafuta mwansihi bora lingewashirikisha wasomaji wa magazeti, tungeshangaa matokeo. Nina mashaka makubwa kama hawa walioptishwa kama washindi, ndo wangechaguliwa na wasomaji. Ndo maana kuna pendekezo kwamba MCT, watuchapishie makala zote zilizoshinda, ili tuzichambue na kukubali kwamba washindi ni washindi kweli. Mara zote mlaji ndo yuko kwenye nafasi nzuri ya kutambua uzuri na ubaya wa kinachozalishwa. Kwa maana hiyo, zoezi la kumtafuta mwandishi bora bado lina udhaifu. Jopo la wataalamu, haliwezi kuwaamulia watanzania wote ni nani mwandishi bora. Ni imani yangu kwamba, jinsi tunavyosonga mbele tutafanikiwa kupata mfumo mzuri wa kuwachagua waandishi bora wa Tanzania.
Unajua kujifunza hakuishi, mtu akikuta waandishi walioshinda ndo mabingwa wa kuandika habari bora,basi atajifunza kwao. Nina imani si lengo la MCT, kukusanya makala hizo na kuziweka tu kwenye maktaba yao. Ziwe ni sehemu ya kujifunza. Wawakusanye waandishi wote walioshiriki zoezi hili, wakae pamoja na kuanza kuchambua makala baada ya nyingine. Kwa kufanya hivyo watakuwa wameelimisha jamii nzima, maana baada ya zoezi hili waandishi wataanza kutoa makala bora na zenye kujenga.
Pendekezo jingine ni kwamba, MCT, ingewakaribisha washiriki wote kwenye sherehe hizi za kutoa tuzo. Ina maana gani kuwakaribisha watu wengine wasiokuwa washiriki na kuwaacha washiriki? Kama lengo ni kutoa motisha kwa waandishi wetu, basi na kitendo cha kuwakaribisha kwenye sherehe ni cha kutia moyo na kuwajenga kwa namna mmoja ama nyingine.
Sasa nigeukie “Ukanjana” sina jipya sana zaidi ya kuridia yale ambayo nimesema siku za nyuma. Wakati Rais Kikwete akihutubia kwenye sherehe za kuwapatia zawadi waandishi bora, aliibua tena neno “Kanjanja” kwamba uandishi wa habari hapa Tanzania umevamiwa na Makanjanja. Mjadala wa Makajanjanja na ukanjanja, umeendelea muda mrefu katika taifa letu. Nimekuwa nikijizuia kujiingiza kwenye mjadala huu, maana ninaamini msemo wa Kiswahili usemao “ Chema chajiuza na kibaya chajitembeza”. Ninaamini kwamba mtu daima anapimwa kwa kile anachokitoa. Mtu akitoa pumba badala ya mchele, hata kama ni msomi wa kupindukia, huyo ni kanjanja. Hivyo nimekuwa mbali na mjadala huu maana ninaamini wasomaji wa magazeti wanatambua ni nani kanjanja na ni nani si kanjanja.
Wengine wana maaoni kwamba makanjana ni wale wanaoivamia taaluma ya uandishi bila kuisomea.Wanasema, makanjanja waache kulalamika na badala yake waende “Open University” na kusoma uandishi wa habari kwa kipindi cha miaka mitatu. Ili nao waitiwe wasomi wa uandishi wa habari! Maana yake wasome digrii! Siamini kama kuna mtu anayeivamia taaluma hii bila kusoma kidato cha nne au cha sita. Hivyo tunaposema kusoma katika makala hii maana yake ni digr
Raafiki yangu mmoja ana mawazo kwamba “ Sikubaliani na wanaotaka taaluma hiyo ilindwe kwa mabavu na vitisho dhidi ya wale wasiotakiwa, ambao kwa namna moja au nyingine ndio wanaoonekana kuivamia taaluma hiyo, japo wao wanajiweka karibu kutokana na mapenzi yao kwenye taaluma hiyo na hivyo kuamua kuiunga mkono.
“Ili taaluma iheshimike, haina budi kujilinda yenyewe kwa wanataaluma kuonyesha kile kinachaoifanya ikaitwa taaluma, ambacho kwa tafsiri yingine kinapaswa kiwe nje ya upeo wa wale wasio na taaluma. Madhalan, maandishi yenye kufikirisha ambayo si kila mmoja mwenye kuelewa kuandika anaweza kuyarukia na kujaribu kuyaandika. Kinyume chake, wanataaluma ya uandishi wanashindwa kukifanya kile ambacho kingeifanya taaluma yao ikaheshimika na kuogopeka badala yake wanafanya mambo ambayo kila mmmoja anajiona ana uwezo nayo. Kwa hilo wa kujilaumu ni wana taaluma ya uandishi wenyewe..”
Huko nyuma nimesema: “ Wakati wengine, wanakazania “Kusoma”, wengine wanasisitiza “heshima” ya taaluma. Wote wawili ninawaelewa vizuri na kukubaliana na hoja zao. lakini kwa upande wa wale wanaokazania “Kusoma”, nafikiri kuna kuchanganya kati ya Kusoma na kuelimika au kuelevuka.
Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kupinga kusoma. Kusoma ni lazima. Swali ni unasoma nini? Unasoma wapi? Unasoma kuelimika na kuelevuka, au unasoma kuwa na cheti? Unaiba mitihani? Unanunua cheti? Kuna malalamishi mengi ya mitihani na vyeti kununuliwa hapa Tanzania. Kuna habari kwamba mtoto wa mkubwa fulani pale Muhimbili alipatiwa cheti cha Udaktari wakati alishindwa mitihani. Shinikizo lilitoka juu! Mpaka leo hii Tanzania, hatuna chuo cha uandishi wa habari kinachowafundisha waandishi wa habari kuelevuka au kuelimika. Kama kipo ningeomba kukifahamu. Na hili si kwa uandishi wa habari tu, bali karibia vyuo vyetu vyote vya juu, vinafundisha kwa lengo la kutoa vyeti. Ndo maana kwa miaka yote hii baada ya uhuru hatujafanikiwa kuwa na wavumbuzi na kuwa na watu wa kututengenezea mifumo bora ya kuleta maendeleo ya haraka. Huu nao ni majadala unaojitegemea”
Kwa maoni yangu, si kila aliyesoma ameelimika au kuelevuka. Mtu aliyesoma na kuelevuka au kuelimika ni lazima afuate mfano wa Socrates. Ni lazima awe tayari kufa akitetea ukweli. Mtu aliyesoma na kuelevuka au kuelimika ni lazima kwake nyeupe iwe nyeupe na nyeusi iwe nyeusi. Msomi ambaye kwake mbwa anaweza kugeuka na kuwa mtu, huyo atakuwa amesoma, lakini hakuelimika.
Hata hivyo kuelimika au kuelevuka si lazima kukaa darasani kama wanavyopendekeza wale wanaokazania “Kusoma”. Tunaambiwa kwamba Komredi Jacob Zuma, hakukaa kwenye dara lolote katika maisha yake. Leo hii ni Rais wa ANC, na Rais wa taifa kubwa la Afrika ya Kusini. Anaheshimika Dunia nzima, akisimama na kuzungumza anaonekana ni mtu mwelelevu na mtu aliyeelimika. Hiki ndicho kitu kinachotakiwa: Kuelimika na kuelevuka, na wala si mzigo wa vyeti!
Pia siku za nyuma nilisema hivi: “ Tanzania tuna wasomi wengi wenye dingrii zaidi ya tatu. Tuna madaktari na maprofesa. Pamoja na ukweli huo taifa letu limeingia kwenye mikataba mibovu. Usomi , haukuwasaidia watu wetu kuwa makini, haukuwasidia watu wetu kuwa wazalendo, haukuwasaidia watu wetu kuwa na malengo ya kujenga taifa lao. Badala yake wanafikiria kuchota fedha na kuzificha nje ya nchi. Maana yake ni kwamba wamesoma, lakini hawakuelimika wala kuelevuka.
Nchi zilizoendelea, ni kwamba watu wao walisoma na kuelevuka, walisoma wakawa wavumbuzi na kutengeneza mifumo mizuri ya kuendeleza nchi zao.Ndo maana wanalinda maslahi ya mataifa yao. Ndo maana wanavumbua njia mbali mbali za kuendeleza mataifa yao.
Hivyo kwa maoni yangu, Makanjanja, si wale ambao hawakwenda darasini kuusomea uandishi wa habari, bali ni wale waliousomea lakini hawakuelimika wala kuelevuka.
Katika taifa letu tumeshuhudia matukio ya kifisadi, rushwa na wizi ambayo mjinga tu ndiye anayeweza kuyatetea. EPA, Buzwagi na mengine ni mambo ya wazi kabisa, ni wizi wa wazi wazi. Mwanahabari anayeshindwa kuyaandika haya kwa uwazi naye ni Mwizi! Mfano Richmond, ilishindwa kabisa. Haikuwasha umeme. Watu walioshiriki kuipitisha Richmond, wanafahamika na wametajwa kwa majina. Kuna ushahidi wa kutosha kabisa kwamba watu hawa walishiriki kuliingiza taifa letu kwenye hasara kubwa. Lakini waandishi wa habari “wasomi” wanaandika kuwatetea watu hawa kwamba wanapakwa matope. Wanafanya kazi ya kuwasafisha kwa malipo makubwa! Wanalazimika Nyeupe, kuiita Nyeusi. Hawa ndio makanjanja!”
Mtu yeyote anayehongwa fedha, nyumba au gari ili aisaliti taaluma yake, ni kwamba mtu huyu alisoma, lakini hakuelimika wala kuelevuka. Tatizo kubwa lililo kwenye kwenye taaluma ya uandishi ni kwamba imevamiwa na watu “wasomi” wanaotaka utajiri wa haraka haraka kama walivyo baadhi ya watanzania wanaotaka kuwa matajiri bila kufanya kazi. Badala ya kufanya kazi yao ya Kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha, waandishi wetu wa habari wanafanya “Ukanjanja” wa kutafuta fedha kwa njia zozote zile.
Magazeti makubwa yanayoaminika kuongozwa na waandishi “wasomi”, yanafanya kazi ya kuwajenga watu binafsi, kuwabomoa watu, kuvijenga vyama vya siasa na kuvibomoa vingine. Yanakuwa magazeti ya propaganda na kuuficha ukweli. Lakini magazeti yanayoaminika kuongozwa na waandishi “makanjanja” yanaibua mambo mazito, yanaibua ufisadi, yanahabarisha, yanaelimisha na kuburudisha!
Hatuwezi kukwepa kusoma, ni lazima maada dunia ya leo ni ya kisomi, lakini mwisho wa yote kinachomoza ni uzalendo, kujituma, kusema ukweli, kama alivyosisitiza Mhesimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Ni imani yangu, Rais wetu anaposema Ukweli, anaanisha ukweli, si ukweli wa kutengeneza ili kuilinda himaya inayokuwa madarakani. Kanjanja siku zote atakuwa mtu anayeukimbia ukweli na kukubali kuhongwa ili kuisaliti nchi yake. Mtu huyu anaweza kuandika vizuri kupindukia kiasi cha kupokea tuzo, lakini hawezi kukwepa hukukmu ya historia!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment