TUWEKEZE KWENYE ELIMU, TUACHE VISINGIZIO
Nimesikia kwenye vyombo
vya habari kwamba migomo inayoendelea kwenye vyuo vikuu inachochewa na vyama
vya upinzani. Na wengine wanakuwa na ujasiri zaidi kiasi cha kutaja chama husika, kwamba CHADEMA ndo kinara wa migomo
ya vyuo vikuu. Nafikiri hivi ni visingizio. Nisingependa kukubali hoja hii
ambayo kwa upande mkubwa inaungwa mkono na serikali. Wahaya wana msemo kwamba
ukishaumwa na nyoka, hata mjusi unauogopa. Serikali yetu ina changamoto nyingi
na kati ya hizi asilimia kubwa zinatoka kwenye vyama vya upinzani, hivyo kila
tukio lenye harufu ya changamoto ni lazima vinyoshewe vidode vyama vya
upinzani.
Kama msemo wa Kiswahili
wa lisemwalo lipo na kama halipo litakuwa njiani linakuja, usemavyo, basi
tuamini kwamba CHADEMA ina nguvu na ushawishi mkubwa hivyo? Vyuo vyote
viendeshe mgomo kwa kushawishiwa na CHADEMA? Maana yake chama tawala hakina
ushawishi tena? Mbona umoja wa vijana wa CCM umejipenyeza kila sehemu kwenye
vyuo vyote?
Tukitaka kuwa wa kweli
na kuachana na visingizio na porojo ni kwamba tumeshindwa kuwekeza kwenye
Elimu. Tungewekeza kwenye elimu kuanzia ngazi ya chini hadi vyuo vikuu, vijana
wakasoma na kupata elimu bora katika mazingira mazuri, tusingesikia migomo na
maandamano. Mfumo wa mikopo ya elimu ya juu ni mbovu kabisa. Migomo karibia
yote inayoendelea kwenye vyuo vikuu inahusu Mikopo ya Elimu ya juu. Vijana
wanaanza vyuo vikuu na kukaa siku nyingi bila kupata mikopo. Wanahitaji fedha
za kununua chakula, wanahitaji fedha za kupanga chumba, wanahitaji fedha za
usafiri, wanahitaji fedha za kununua vitabu nk. Bila kuwapatia fedha hizo kwa
wakati, ni wazi vijana hawawezi kutulia na kusoma. Watafanya maandamano na
kuendesha migomo. Hata wale wanaoikataa migomo na kuonekana tofauti na wengine,
ni wasanii tu. Rohoni wanaumia na wengine wanapata matatizo ya kisaikolojia,
hawawezi kutulia na kujifunza; Bila fedha za chakula, bila fedha za kulipia
chumba, mtu hawezi kutulia na kusoma.
Kama tungekuwa na mfumo
mzuri wa kuwekeza kwenye elimu, kwa maana ya kuandaa mazingira mazuri ya vijana
wetu kusoma, kama tungekuwa na mfumo mzuri wa kuwapatia vijana wetu mikopo kwa
wakati, nina mashaka kama migomo tungeisikia vyuoni hata kama CHADEMA ina
ushawishi mkubwa kupindukia.
Tanzania tumeamua
kutowekeza kwenye elimu kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu. Shule za
msingi hapa Tanzania, ukitoa zile za binafsi zinazowapokea watoto wa matajiri,
hazina madawati, watoto wanakaa chini, nyingine hazina hata vyoo, mishahara ya
walimu inachelewa muda mrefu kiasi cha kuvunja moyo na juhudi za walimu na
matokeo yake ni watoto kumaliza darasa la saba bila kufahamu kusoma na
kuandika. Tumeamua kuua elimu, kama tulivyofanya kwenye kilimo. Tulikuwa
tunaimba kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu. Lakini hatukuwekeza
kwenye kilimo na matokeo yake, kilimo kimekufa kabisa. Tunaamua kukifufua kwa
kuwakaribisha wawekezaji wa nje wenye malengo ya kulima chakula cha nchi zao na
kuendeleza uchumi wa nchi zao. Hakuna mtu atakayetoka nchi za nje na kuja hapa kuendeleza kilimo chetu, ni lazima sisi
kufanya kazi ya ziada ya kuwekeza kwenye kilimo.
Hivyo hivyo hakuna mtu
atakayetoka nje kuja hapa Tanzania kuendeleza elimu yetu. Tumekuwa tukiimba
kwamba vijana ni taifa la kesho, ni
taifa gani hili lenye kuandaliwa na mfumo mbaya wa elimu? Ni lazima sisi
kufanya kazi ya ziada ya kuwekeza kwenye elimu, bila kufanya hivyo tutabaki
watu wa mwisho katika dunia hii ya sayansi na teknolojia. Tukiwekeza kwenye
elimu, tutapata nguvu na uwezo wa kufufua kilimo, kufufua uchumi wetu, kufufua
viwanda vyetu na kuchimba madini yetu wenyewe.
Tumejenga sekondari za
kata kwa wingi bila kuwekeza kwanza, matokeo yake, sekondari zipo, wanafunzi
wapo, lakini walimu , vifaa na vitabu hakuna. Wanafunzi hawa wakianza migono na
maandamano ya kudai walimu na vitabu, tutasema ni uchochezi wa CHADEMA?
Tumeanzisha vyuo vikuu
vingi. Ni kiasi gani tumewekeza kuwaandaa walimu wa kufundisha kwenye vyuo hivi vikuu. Wanafunzi hawa wanaonyimwa
mikopo na kusoma kwa mashinikizo, ndio hao kesho na keshokutwa watarudi
kufundisha kwenye sekondari hizi za kata. Kama hawakuandaliwa vizuri watakuwa
walimu wa aina gani? Wanafunzi hawa
wakifanya maandamano na migomo ya kudai maandalizi mazuri ya elimu yao, tuseme
ni uchochezi wa CHADEMA?
Hata hivyo sina imani
kwamba CHADEMA, inaendesha siasa za uasi au siasa za kuwafanya vijana kuendesha
migomo. Tunachokijua na kukielewa, na
tukiangalia vijana waliochomoza na kujiunga na CHADEMA na kupata nafasi
ya kuingia Bungeni; wanatuonyesha moyo wa uzalendo na nia ya wazi ya kupigania
rasilimali za nchi hii. Kwa wachache wanaofikiri Tanzania ni yao peke yao, wanauchukulia mchango wa vijana wa
CHADEMA kama vurugu na fujo.
Hivyo basi migomo na
vurugu kwenye vyuo vikuu inasababishwa na mfumo mbovu wa kutoa mikopo kwa
vijana wetu. Vigezo vinavyotumika kuwapatia baadhi mkopo na kuwanyima wengine
havieleweki vizuri, tungesema labda wanaangalia uwezo wa familia, kwa mantiki
kwamba familia masikini vijana watapata mkopo asilimia mia moja. Lakini si
hivyo maana tumeshuhudia watoto wanaotoka kwenye familia tajiri wanapata mkopo
asilimia mia moja wakati watoto
wanaotoka kwenye familia masikini hawapati mkopo kabisa, au wanapata asilimia
ishirini, arobaini au sitini kwa kigezo kwamba zinazobaki watafute wenyewe.
Hawa watu masikini wanaolilia nyongeza ya nauli ya shilingi mia moja ya kivuko cha Kigamboni watapata wapi
mamilioni ya kuwalipia watoto wao?
Badala ya kuilaumu
CHADEMA kwa ushawishi hasi kwa vijana
wetu, ni bora tulaumu mfumo wetu wa kutoa mikopo na kuilaumu hali halisi ya
Tanzania. Hoja yangu hapa ni kwamba
hali halisi ya maisha ya Tanzania ina ushawishi hasi kwa vijana kuliko
kitu kingine kile. Vijana wetu wanashuhudia serikali yao ikitumia fedha nyingi
kusherehekea miaka hamsini ya uhuru na baadaye kutoa visingizio kwamba haina
fedha za kutosha kuwapatia mkopo wanafunzi wote.
Mfumo wa kutoa mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu si watanzania peke yake. Duniani kote, wanatoa
mikopo ya elimu ya juu. Hakuna mtu anayejilipia elimu ya juu. Serikali inatoa
mikopo na kuandaa mvumo mzuri wa kurudisha mikopo hiyo baada ya masomo ili na
wengine wanufaike na mikopo hiyo. Nchi
nyingine bajeti ya elimu inakuwa na kipaumbele kuliko wizara nyingine. Wanawekeza
kwenye mikopo, utafiti, vifaa vingine vya elimu na vitabu.
Vijana wetu wanashuhudia
vingozi wakijenga mahekalu na kuendesha magari ya kifahari, wanashuhudia watoto
wa viongozi wakisomeshwa nje ya nchi na wakirudi, maana wengine hawarudi
kabisa, wanapatiwa kazi nzuri serikalini, kwenye mashirika ya kimataifa, benki
kuu na sehemu nyingine nyeti.
Vijana wetu wameshuhudia
litania ya Tanzania ya EPA, DOWANS na mambo mengine kama hayo ya kutorosha
twiga na kuwauza nchi za nje. Kuna orodha ndefu inayoonyesha kwamba visingizio
vya serikali kutokuwa na fedha za
kuwapatia mkopo wanafunzi ni vya uongo. Katika hali kama hii, si lazima
CHADEMA kuingia vyuoni na kushinikiza migomo, bali hali halisi ndo chanzo cha
matatizo yote hayo.
Serikali yetu ikiwa
makini na kupanga vipaumbele, haishindwi kuwapatia wanafunzi wote na mtu yeyote
anayependa kujipatia elimu ya juu mkopo. Uwezo huo upo, tatizo ni kwamba hatuna
nia ya kuwekeza kwenye elimu. Hivyo tuache visingizio na porojo, vurugu za vyuo
vikuu zinasababishwa na mfumo mbaya wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment