TUTAFAKARI JUU YA YESU KRISTU NA UKRISTU
Nianze makala hii kwa kuwatakia wasomaji wangu
heri ya Christmas na mwaka mpya wenye baraka tele. Ni miaka miwili sasa
nimeachana na utamaduni wa kutumiana salaam za Christmas na mwaka mpya kwa
ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani; msimamo wangu ni kukwepa kuyatajirisha
makampuni haya ya simu wakati wa sikukuu hizi za mwisho wa mwaka. Wale wote
watakao ni tumia ujumbe wa sms, nitaupokea lakini sitaujibu, badala yake najibu
kupitia makala hii: Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuhusu kuendelea kuwepo;
si kwa ubora wetu bali kwa neema zake. Hivyo basi kwa vile tumejaliwa bure bila
hata kustahili, tuelekeze nguvu zetu zote katika upendo, amani na kuwahudumia
jirani zetu.
Nitakayoyaandika leo, inawezekana nilikwisha
yaandika miaka iliyopitia. Nitakuwa ninayarudia kama ilivyo kawaida yetu ya
kurudia mambo yale yale kila mwaka. Mfano tukio hili la Christmas tunalirudia
kila mwaka na bila kuwa waangalifu tunaweza kujikuta tunatumbukia kwenye
mnyororo wa kufuata ratiba bila kuwa na tafakuri. Hatari ya kujenga utamaduni
huu ni siku moja kujikuta hatuna majibu ya maswali mengi yanayoweza kujitokeza
kutokana na matukio haya tunayoyarudia kila mwaka. Hivyo katika makala hii kama
nitakuwa nimejirudia, si kwa bahati mbaya bali ni kutaka kujenga utamaduni wa
kuyatafakari matukio haya ambayo yamegeuka kuwa ni sehemu ya maisha yetu.
Tunatumiana salaam wakati wa sikukuu hii ya
Christmas, tunatumiana zawadi, tunakula pamoja na kunywa pamoja, tunafurahi,
tunavaa nguo nzuri na wengine tunasafiri kwenda kupumzika au kuwatembelea ndugu
na jamaa; lakini je, tunatafakari tukio hili la Mungu, kuzaliwa miongoni mwetu,
akaishi na sisi? Tuna tafakari juu ya misamiati tunayoitumia kila siku ya Yesu
Kristu na Ukristu? Je ni kweli kwamba kuna Yesu wa Nazareti na Yesu Mkristu?
Basi nakukaribisha katika makala hii tutafakari pamoja kwa lengo la kuvunja
utamaduni huu wa kuyachukulia matukio haya kama ratiba, bali matuko ya
kuyajenga na kuyaendeleza maisha yetu hapa duniani.
Yesu wa
Nazareti au Yesu Mkristu? Lengo la tafakuri
hii si la kiimani wala kihistoria. Kila mtu anakaribishwa kutafakari
pamoja na mimi. Kila mtu anakaribishwa kutafakari juu ya mtu huyu Yesu Kristo
aliyeishi karne ya kwanza kule Palestina, na kujaribu kumwangalia kwa macho ya
karne ya leo katika mazingira ya Mtanzania. Shauku yangu kubwa ni kumwangalia
mtu huyu kabla ya kutekwa nyara na kutumiwa kama chombo na imani ya Kikristu.
Tafakuri yetu haitaanza na imani katika Kristo,
ingawa nafikiri hitimisho litakuwa hilo. Wala tafakuri yangu haina lengo la
kuutetea Ukristu, hii ni dini kongwe ambayo inaweza kujitetea yenyewe. Pia sina
lengo la kumtetea na kumlinda Kristo, maana yeye ana uwezo wa kujitetea
mwenyewe. Hata hivyo tunaambiwa na wanafalsafa wa zamani kwamba ukweli
hujisimamia wenyewe. Yesu, alipobanwa juu ya Ukweli ni nini, alikaa kimya
ikimaanisha kwamba ukweli ni yeye mwenyewe! Lakini ikitokea baada ya tafakuri
yetu mtu akaamua kumfuata Kristo, nitakuwa sikumshawishi, bali atakuwa
amegundua mwenyewe kwamba Kristo ni
njia ya wokovu. Maana tunasikia katika Injili ya Yohana kwamba Ukweli utatuweka
huru: Yohana 8:32.
Katika tafakuri yetu tutajikita zaidi juu ya Yesu
wa Kihistoria. Lakini pia lengo letu kubwa si huyu Yesu wa Kihistoria.
Hatutafakari kutuliza kiu ya tafiti nyingi za kisomi zilizofanyika juu ya Yesu
Kristo. Lengo kubwa la tafakuri hii ni hitaji muhimu na la haraka. Ni hitaji la
kutafuta mfumo wa kupambana na matatizo yanayomzunguka mwanadamu wa leo.
Mamilioni ya watu wanaishi kwenye mateso kila siku ya Mungu. Kuna njaa, vita,
umasikini, upweke, magonjwa, uonevu, ubaguzi nk. Hapa Tanzania, watu wanakufa
kwa UKIMWI, malaria na magonjwa mengine yanayotibika. Ujambazi, ufisadi, rushwa
na kutowajibika vinasambaratisha uchumi wetu. Namba ya wajane na wagane
inaongeza kwa kasi, watoto yatima, watoto wa mitaani na watoto wanaoishi katika
mazingira hatarishi inaongezeka kwa kasi ya kutisha. Lengo na tafakuri hii
ni tufanye nini kuondokana na mateso na
mambo mengine yanayotishia uhai wa mwanadamu na hasa Mtanzania.
Mamilioni ya watu kwa miaka mingi wamekuwa
wakilitaja jina la Yesu na kumwabudu, lakini wachache kati ya mamilioni ndiyo
waliomwelewa Kristo na namba chache kabisa ndiyo waliofuasa kile alichokitaka
kitendeke. Maneno ya Yesu Kristo, yamebadilishwa na kupindishwa ili yatekeleze
kile watu wanachokitaka, na wakati mwingine maneno yake yamebadilishwa na
kupindishwa yasimaanishe kitu chochote! Jina la Yesu, limetumiwa kubariki maovu
ya kila aina, kama wale waliokuwa wakiongoza vita na kuuwa watu huku
wakitanguliza msalaba na Biblia. Latini Amerika, mamilioni ya watu walipoteza
maisha yao na sehemu nyingine kizazi kilifutika kabisa katika harakati za
kueneza neno na mafundisho ya Yesu Kristo. Lakini pia jina la Yesu, limetumiwa
kuwashawishi na kuwaletea imani kubwa wanaume na wanawake wengi hata kufikia
hatua ya kupumbazika na kufanya matendo ya kijinga, kama kujinyima chakula na
kuitesa miili yao kufikia kiwango cha uwendawazimu. Yesu amekuwa akitukuzwa na
kuabudiwa kwa yale ambayo hakuyalenga, yale aliyo yapinga na kuyakemea kuliko
yale aliyoyalenga, aliyoyahubiri, aliyoyatetea na kuyafia. Jambo la kushangaza
ni kwamba mambo ambayo Yesu, aliyapinga wakati wa uhai wake, yalifufuliwa,
yalihubiriwa na kusambazwa dunia nzima kwa jina lake.
Hatuwezi kumuunganisha moja kwa moja Yesu wa
Nazareti na hii dini kubwa ya Kizungu, inayojulikana kama Ukristu. Yeye alikuwa
mwanzilishi wa dini kubwa zaidi ya hii tunayoifahamu. Yeye anasimama juu ya Ukristu na kutoa hukumu juu
yale yote dini hii imeyafanya kwa jina lake. Hata hivyo Ukristu, hauwezi kudai
mumiliki Yesu Kristo, maana mtu huyu alikuwa ni wa binadamu wote.
Je, hii ina maana kwamba kila binadamu (Mkristu na
asiyekuwa Mkristu) ana uhuru wa kumtafsiri Kristo katika maisha yake jinsi
anavyotaka? Inawezekana kabisa kila mtu akamtumia Kristo anavyotaka kwa mabaya
na mazuri? Lakini yeye alikuwa ni mtu aliyekuwa na imani nzito ambayo alikuwa
tayari kuifia. Je, hakuna namna ya watu, wenye imani na wasiokuwa na imani
kumpatia nafasi takika maisha yao Yesu huyu wa Nazareti, akazungumza yeye
mwenyewe kwenye mioyo yao? Je, hakuna namna ya watu kulinganisha matatizo yao,
nyakati zao na zile za Yesu wa Nazareti?
Hivyo tafakuri yetu inaanza na matatizo mengi
yanayoisumbua dunia ya leo. Tishio lililopo leo si la mtu binafsi, kabila,
taifa au bara. Tishio ni la dunia nzima, ni tishio la ubinadamu. Tumefika
mahali tunachanganyikiwa na kufikiri kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuzuia
tishio la kuumaliza ulimwengu na binadamu. Wapo vichaa kama Kibwetere na
wajinga wengine wanaofikiri kwamba mwisho wa dunia na ubinadamu vinashuka kwa
miujiza, kwamba tunaweza kulala na kuamka tunakuta dunia imekwisha. Huu ni
ujinga mtupu! Mwisho wa dunia, unaletwa na matendo ya binadamu ya muda mrefu.
Matendo ya ubinafsi yasiyozingatia umuhimu wa binadamu na viumbe vingine,
yanaweza kupelekea mwisho wa dunia. Hili si jambo la kutokea leo ama kesho,
lakini mtu anayejali ni lazima kuhakikisha anarithisha dunia hii kwa vizazi
vijavyo. Tunakaa tama kwamba hakuna tena mfumo mzuri wa maisha unaowafaa
binadamu wote. Mfumo wa kuweza kuangalia na kutengeneza maisha bora ya
mwanadamu wa leo na kesho.
Siku za nyuma kidogo tulifikiri labda silaha za
nyukilia zingeweza kutumika kuteketeza ulimwengu. Tumeanza kupunguza woga huu,
lakini mambo mengine mengi kama vile uharibifu mazingira, uchimbaji ovyo wa
madini, upungufu wa chakula na ardhi nzuri ya kustawisha chakula, hatari ya
kupungua kwa maji na ongezeko la binadamu, ni matishio mapya kwa uhai wetu na
ulimwengu tunamoishi. Ukweli kwamba binadamu wanaongeza kwa kiasi cha milioni
80 kwa mwaka, ni tishio kwamba kwa miaka michache ijayo, matumizi ya maji na chakula
yatakuwa katika hali mbaya duniani kote. Ukweli kwamba magazeti, vitabu na
utengenezaji wa karatasi za kuandikia unaitafuna misitu ni tishio la uharibifu
wa mazingira katika enzi hizi tulizomo.
Kuna uharibifu mkubwa katika kila biashara
zinazofanywa kwa lengo la kupata faida. Viwanda vingi vimekuwa vikiharibu
mazingira kwa moshi unaotoka viwandani, lakini pia uchafu unaotiririshwa kutoka viwandani kwenda mitoni na kwenye
maziwa na mabahari umechangia uharibifu mkubwa wa viumbe katika maji. Ni wazi ili
tupone, panahitajika mabadiliko makubwa. Swali ni je ni nani atakubali hasara ya kusimamisha viwanda vyake?
Inakuwa ngumu kuwashawishi watu kubadili mtindo wa
maisha, ili kurefusha maisha yao wenyewe, inakuwa ngumu zaidi kuwashawishi
kufanya hivyo ili kuyarefusha maisha ya watu wengine. Inakuwa ngumu zaidi na
zaidi kuwaambia kufanya hivyo kwa lengo la kunusuru maisha ya mabilioni ambao
bado hawajazaliwa.
Kuna ukweli kwamba dunia hii ina baadhi ya watu, wake kwa waume wenye nia
njema, na wanayaona matatizo yote hayo na wangependa kufanya chochote kuleta
mabadiliko. Lakini wanaweza kufanya
nini? Mtu mmoja, au kikundi cha watu wachache kinaweza kufanya nini kwenye
matatizo haya ya Ulimwengu wa kisasa? Kilicho mbele yetu ni kitu kikubwa, ni
mifumo ya dunia hii iliyojikita na kustawi! Ni mifumo ya ubepari, soko huria na
utandawazi. Mara ngapi tunasikia kilio cha watu kwamba mtu hawezi kupambana
na mifumo?
Hili ndilo tatizo kubwa. Tumejijengea mifumo ya
siasa na kiuchumi kwa kuzingatia mambo fulanifulani, ambapo sasa tunaanza
kutambua kwamba mifumo hii italeta maafa kwa dunia nzima. Ni kama tumefugwa
mikono na miguu, kiasi tunashindwa kubadilisha mifumo na inafika mahali hakuna
kinara kwa kuisimamia na kuiendesha. Na la kushangaza ni kwamba uharibifu wa mifumo
hii, hautambagua mtu yeyote. Mfano uharibifu wa mazingira unaoendelea kuongeza
joto duniani, hautabagua matajiri na maskini, mataifa makubwa na madogo.
Utatuangamiza sote!
Tunaposherehekea sikukuu ya Christmas, ni lazima
kutafakari na kujiuliza maswali: Tunamkumbuka Yesu wa Nazareti au Yesu Mkristu.
Kama tulivyoona kwenye tafakuri yetu ni kwamba Yesu wa Nazareti, alijenga
mifumo ya kupambana na matatizo ya dunia ya wakati wake, matatizo yanayofanana
na matatizo ya dunia ya leo. Baadaye Ukristu ulijenga mfumo unaopingana na ule
wa Yesu wa Nazareti! Hapa ndipo mjadala unakuja; tunataka tusitake ni lazima
tuyajadili haya maana yanagusa maisha yetu. Tuendelee kutafakari wakati
tunakula na kunywa!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment