TUNAWAHITAJI VIONGOZI
AINA YA MAGUFULI.
Siungi mkono kauli
iliyotolewa na Mheshimiwa Magufuli, kwamba watu wa Kigamboni watakaoshindwa
kupata nauli ya shilingi mia mbili wapige mbizi. Na baadaye kwenye vyombo vya
habari tukamshuhudia “kichaa” mmoja akipiga mbizi kutoka Kigamboni hadi
Magogoni. Haikujulikana vizuri kama mtu huyo alifanya hivyo kupinga ongezeko la
nauli. Najua na yeye Mheshimiwa Magufuli
alilisema hilo la kupiga mbizi kwa utani, tukichukulia utani wa miaka
mingi wa Wazalamo na Wasukuma. Kwamba aombe msamaha, nafiki yeye binafsi
atapima na kuona uzito wake. Lakini kwa hoja yake ya msingi ya kupandisha nauli
ya kivuko kutoka mia moja hadi mia mbili, niko naye kabisa. Tunawahitaji
viongozi aina yake, viongozi wanaofuata sheria na kufanya kazi bila kutanguliza
matakwa ya vyama vyao vya siasa na bila
kujitafutia sifa.
Tumeambiwa nauli ya
kivuko cha Kigamboni imekuwa shilingi mia moja miaka kumi na minne. Tujiulize
sote, leo hii unaweza kununua nini na shilingi mia moja? Hata chapati yenyewe
ni shilingi mia mbili. Kilo ya sukari imefikia elfu mbili na mia tano. Mafuta
ya taa, petroli na dizeli ndio bei inaendelea kupaa. Kivuko kinakunywa mafuta
hayo ambayo bei yake inapaa kila siku, kivuko kinahitaji vipuli na wafanyakazi
wanahitaji mishahara, tena mishahara ya kwenda na wakati huu tuliomo. Mapato ya
kivuko ni nauli, hivyo bila nauli hiyo kwenda na wakati, haiwezekani kivuko
hicho kikafanya kazi kwa ufanisi. Ni wakati wa watanzania kuacha kulalamika na
kuangalia hali halisi. Tusipende kuishi kwa kutegemea miujiza.
Magufuli, hapendi porojo
wala kuchanganya siasa na utendaji. Akifanya uamuzi, anakutajia kifungu cha
sheria na mwaka ambapo sheria hiyo ilitungwa. Yeye ni tofauti na watendaji
wengine ambao tumezoea kuwasikia wakisema: “Nimeagizwa na Mheshimiwa Waziri
mkuu” au “ Nimeagizwa na Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa” au “ Hata mheshimiwa Rais
anaunga mkono wazo hili”. Watu wa aina hii hawawezi kukutajia kifungu cha
sheria, wanasubiri kuagizwa kana kwamba hata wakiagizwa kujiweka kitanzi
watatimiza! Sheria zipo ili mambo yaende kwa utaratibu na wala si kwenda kwa
kufuata mapenzi ya mtu fulani hata kama mtu huyo ni Kiongozi mkubwa wa nchi.
Nimeziangalia bei za
kivuko. Kama ni mtu kulalamika, labda kwa upande wa magari na guta. Kwa mfano
inashangaza Guta, kulipishwa shilingi 1,800 wakati gari dogo linalipa shilingi
1,500. Kwa maana zote, kwa kuzingatia uzito na bei ya kifaa, Guta inakuwa bado
chini. Hata kwa hali ya maisha yule wa Guta, huwezi kumlinganisha na mtu mwenye
uwezo wa kununua gari. Na mara nyingi unakuta hawa wenye Guta, wanakuwa
wamekodisha kusombea mizingo. Hivyo shilingi 1,800 ni nyingi! Waheshimiwa
wabunge wetu wa mkoa wa Dar-es-Salaam, wangefanya uchambuzi huo nafikiri
wangeeleweka kwa wengi. Lakini kushikia bango la ongezeko la shilingi mia moja,
ni kuwazomea tu!
Ninaandika makala hii
nikijua kwamba Tanzania leo hii maisha yanaendelea kuwa magumu na mimi nimekuwa
kati ya watu wanaopinga mfumuko wa bei. Lakini kuna vitu ambavyo ni lazima
kukubaliana navyo kufuatana na hali halisi. Tunapima thamani ya fedha zetu kwa
kulinganisha na dola; siungi mkono mfumo huu, lakini ndio ukweli uliopo sasa.
Shilingi yetu inaendelea kudidimia, kiasi kwamba shilingi mia moja hazina
thamani tena. Ndio maana ninakubaliana na Magufuli na wataalamu wake kuhusu
nauli ya Kigamboni. Walichokifanya pamoja na kuzingatia mambo mengine mengi
wakiongozwa na sheria ni kuangalia hali halisi.
Tatizo la Tanzania
tunapenda sana siasa, na tunafanya kosa la kuchanganya siasa na utendaji na
hapo ndipo tunakwama. Magufuli alipotangaza
bei ya shilingi mia mbili, wananchi wa Kigamboni, walilalamika.
Inaeleweka maana mazoea ni vigumu kuyaacha hivi hivi. Walizoea kulipa mia moja,
sasa kuwaambia mia mbili inakuwa nongwa. Walioshangaza zaidi ni wabunge wa CCM
wa mkoa wa Dar-es-Salaam, kushikamana kupinga nauli hiyo ya mia mbili. Mambo
makubwa ya nchi hii yamekuwa yakijadiliwa kule bungeni, hatuzisikii sauti hizi
za Wabunge wa CCM wa Dar-es-Salaam, tunazisikia leo hii nauli inapopanda kutoka
mia moja kwenda mia mbili. Wanaogopa wasiosikika wakisema kitu juu ya nauli,
wakati wananchi wamekuwa wa kwanza kulalamika, watatoswa 2015.
Muswada wa sheria ya
kubadilisha katiba, ulipitishwa kishabiki na wabunge hao hao wa CCM. Hatukusia
sauti ya za wabunge wa CCM wa Dar-es-Salaam, wakisimama kidete kutoa maoni yao
juu ya sheria hii ambayo wataalamu kama Profesa Shivji, wanasema ni sheria
mbaya. Kwa maoni ya wengi, mchakato wa kuipata katiba mpya ni muhimu zaidi ya
hiyo shilingi mia wanayoipigia kelele.
Hatujazisikia sauti za
waheshimiwa wabunge wa CCM mkoa wa Dar- es-Salaam wakiishinikiza serikali yao
kuwashughulikia mafisadi wanaohujumu uchumi wa nchi na kuziweka rasilimali za
nchi hii mifukoni mwao. Kwa maoni ya wengi kupambana na ufisadi ni muhimu zaidi
ya hiyo shilingi mia wanayoipigia kelele.
Magufuli, amesimama
imara na kusema kule jimboni kwake, nauli ya kivuko ni shilingi elfu tatu.
Wapiga kura wake, wamchague , wasimchague nauli ndio hiyo. Anasema hivyo bila
kuogopa, maana yeye hafanyi kazi kisiasa, anafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Anayasimamia yale yatakayoleta manufaa kwa taifa leo na kesho na hata baada ya
yeye kuondoka madarakani.
Tunawahitaji viongozi
aina ya Magufuli, viongozi wanaoiangalia Tanzania ya leo na kesho. Tunawahitaji
wabunge ambao wanaingia bungeni kushiriki kuiweka misingi ya Tanzania iliyo imara leo na kesho na siku za
mbeleni. Wabunge wanaoingia bungeni kujiandalia makazi ya kudumu bungeni
hawatufai! Wabunge wanaoshindwa kutetea ukweli na kusimamia sheria kwa woga wa
kutoswa kwenye uchaguzi mkuu, hawatufai kabisa!
CCM mkoa wa
Dar-es-Salaam imemkalia kooni Magufuli, na jinsi kansa ya kufukuzana
ilivyoingia kwenye vyama vyetu vya siasa, haitashangaza kusikia CCM Mkoa wa
Dar-es-Salaam, ikipendekeza Magufuli kufukuzwa kutoka kwenye chama cha CCM kwa
sababu ya kupandisha nauli ya kivuko cha Kigamboni. Inawezekana, nani alifikiri
Hamad Rashid, Mtu ambaye alipanda kufikia kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani
Bungeni angefukuzwa kutoka CUF? Au Kafulila kufukuzwa kutoa NCCR?
Wakati wabunge wa CCM wa
Dar-es-Salaam, wanashikia bango nauli ya shilingi mia mbili, mkoa wa
Dar-es-Salaam una matatizo kibao ambayo hatujasikia wabunge hao wakiyajadili na
kutafuta ufumbuzi. Kuna suala zima la foleni. Kwa maoni ya wengi, foleni ni tatizo
kubwa zaidi ya hiyo shilingi mia mbili wanayoipigia kelele. Kuna tatizo la
maji, watu wa mkoa wa Dar-es-Salaam, wanatumia fedha nyingi kununua maji. Kwa
maoni ya wengi tatizo la maji ni kubwa zaidi ya hiyo shilingi mia mbili
wanaoipigia kelele. Kuna tatizo la ardhi na utapeli wa viwanja. Baadhi ya
viongozi wamejilimbikizia viwanja na wanaviuza kwa bei ya mabilioni. Kwa maoni
ya wengi tatizo la ardhi mkoa wa Dar-es-Salaam ni kubwa zaidi ya hiyo shilingi mia moja wanayoipigia kelele.
Inashangaza hata Mbunge
wa Segerea, anaungana na wabunge wengine wa
CCM Dar-es-Salaam kupigia kelele ongezeko la nauli ya kivuko cha
Kigamboni wakati jimboni kwake kuna matatizo kibao. Mbali na tatizo la maji
ambalo ni sugu, mafuriko yameharibu miundombinu. Barabara ya Segerea Bonyokwa,
imeharibika kiasi wananchi ndio wanachangishana kuitengeneza. Njia ya dala dala
ya Tabata-Chang’ombe imefutwa kinyemela. Dala dala zimeandikwa Chang’ombe lakini zinakwenda Kimanga na Segerea. Watu
wa Tabata –Chang’ombe wanapata shida. Kutoka Barakuda hadi Chang’ombe mwisho
mtu analipa mia tano hadi elfu moja kwa bajaji na mia tano kwa piki piki.
Hatujamsikia mbunge huyu wa Segerea, akiwahurumia wapiga kura wake, kulipa
nauli ya elfu moja hadi mia tano, badala yake tumemsikia akiibukia Kigamboni
akiwahurumia walioongezewa shilingi mia moja kwenye nauli na kuifanya nauli
hiyo kuwa shilingi mia mbili. Ni maajabu ya Musa!
Wabunge wa
Dar-es-Salaam, wasitafute umaarufu na kubembeleza kura. Wafanye kazi yao na
kujitoa muhanga kama alivyofanya Magufuli, ndipo mambo yataenda. Mfano, wakati
wabunge wetu wakipinga kupanda kwa nauli ya Kigamboni, mbona hatujawasikia
wakipinga kupanda kwa kodi ya pango ndani ya Jiji la Dar-es-Salaam. Wenye
nyumba wanapandisha kodi kila siku ya Mungu, na kuyafanya maisha ya
Dar-es-Salaam kuwa machungu. Chumba ambacho zamani mtu aliweza kupanga kwa
shilingi kumi na tano hadi ishirini, leo hii ni hamsini hadi sitini. Nyumba ya
vyumba vitatu ambayo mtu alikuwa akipanga shilingi laki moja hadi laki na nusu
leo hii ni laki tatu hadi laki nne. Mbona wabunge wetu wasipigie kelele juu ya
suala hili la pango?
Sikukuu za Christmas na mwaka mpya bei ya nyama
ilipanda kutoka elfu nne kilo moja hadi shilingi elfu saba. Sikusikia wabunge
wa CCM wa mkoa wa Dar-es-Salaam, wakipiga kelele kupanda kwa bei ya nyama na
kulalamika kwamba wapiga kura wao watashindwa kufurahia sherehe hizi, badala
yake wanapigia kelele ongezeko la shilingi mia moja kwenye nauli ya Kigamboni.
Bei ya umeme
inaongezeka, ni watanzania wangapi watamudu ongezeko hili? Haya ndiyo
tunayotaka kuwasikia wabunge wetu wa CCM Dar-es-Salaam wakiyatetea na wala si ongezeko la shilingi mia moja kwenye
nauli ya Kigamboni.
Kuna tatizo hili la
wahanga wa mafuriko. Wanahamishwa kupelekwa Mabwepande. Watoto wao watasomea
wapi? Je wao watapata wapi fedha za kujikimu? Wengi wao waliweza kuyaendesha
maisha yao kwa kuwa karibu sana na Jiji la Dar-es-Salaam, Jiji lenye mishe
mishe na uwezekano wa kupata kazi, biashara na mambo mengine mengi ya
kutengeneza fehda. Sasa wanapelekwa mbali na Jiji na sehemu ambayo
haijaendelezwa bado. Hili ni tatizo
ambalo tulitegemea waheshimiwa wabunge wetu wa CCM mkoa wa Dar-es-Salaam
walisemee kwa nguvu zote. Kwa vile ni serikali imetamka, wanafyata mkia. Hawa
hawatufai kama wawakilishi wa watu!
Vyuo vikuu kuna migomo
ya kila siku. Wanafunzi wanahitaji mikopo ili waendelee na masomo yao.
Tunahitaji kizazi kipya kuliendesha taifa letu. Bila kuwapatia elimu bora
tutakuwa tunajimaliza sisi wenyewe. Hivyo tunawategemea waheshimiwa wabunge
wetu wa CCM mkoa wa Dar-es-Salaam, kupambana na serikali ili itoe mikopo kwa
wanafunzi badala ya wao kushikia bango ongezeko la shilingi mia moja kwenye
nauli ya kivuko cha Kigamboni.
Taifa letu liko nyuma
kimaendeleo, tunalazimika kukimbia wakati wengine wanatembea. Tunawahitaji watu
wa kujitolea kufanya kazi kwa nguvu zao zote; watu wenye uwezo na karama ya
kusukuma mambo yakaenda. Mfano kivuko ni lazima kifanye kazi na kuweza
kujiendesha na kutengeneza ziada, ili ruzuku ambayo Serikali ingetoa kuendesha
kivuko hicho ielekezwe kwenye miradi
mingine ya maendeleo. Hivyo akijitokeza mtu aina ya Magufuli, tumpatie
nafasi, tuache utamaduni wa kuingiza siasa kwenye utendaji. Tunawahitaji
viongozi aina ya Magufuli, ili taifa letu lipige hatua na kusonga mbele
kuelekea maendeleo endelevu.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment