TAMASHA LA JINSIA NI MAFANIKIO YA MIAKA HAMSINI YA UHURU WETU.


TGNP NA FEMACT wamekuwa wakiandaa tamasha la jinsia ambalo limetokea kuwa jukwaa la majadiliano na mkusanyiko wa watu mbali mbali wanaotetea jinsia na haki za wanawake na makundi ya watu wanyonge wanaoishi pembezoni..

Tamasha la Jinsia ni nafasi wazi kwa ajili ya watu binafsi, vikundi, mashirika na mitandao walio katika mapambano yanayofanana; kubadilishana uzoefu, taarifa, kujengana uwezo, kusherehekea mafanikio na kutathimini changamoto zilizo mbele yao, ili kuchangia katika mijadala ya wazi kuhusu maendeleo, kujenga na kuimarisha mitandao, na kupanga kwa pamoja kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya -kijamii kwa mtazamo wa ukombozi wa Wawanawike kimapinduzi.

Tamasha la kwanza la jinsia lilifanyika 1996: Lilikuwa la aina yake likiwa limeandaliwa na TGNP, na zaidi ya washiriki 400 kutoka karibu kila pande ya Tanzania na baadhi ya nchi jirani wakiwakilisha asasi za kiraia, na taasisi za wafadhili. Lengo kuu la  tukio hilo lilikuwa ni kujenga uwezo katika uchambuzi wa masuala ya Kijinsia na kubadilishana uzoefu na taarifa kuhusu masuala ya maendeleo na demokrasia. Pia tama hili lilitumika pia kupanga mikakati ya pamoja juu ya mapambano ya kutafuta usawa. Mada kuu ya wakati huo ilikuwa Jinsia, Demokrasia na Maendeleo na ndio imeendelea kuwa mwongozo wa Matamasha haya hadi leo hii.

Tamasha la mwaka huu 2011, lilifanyika wakati muhimu katika historia ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Tunashuhudia ubadhirifu wa rasilimali za taifa ( ardhi, madini, maji, misitu. n.k) unaofanywa na mashirika ya uwekezaji wa Kimataifa, kwa kuungwa mkono na serikali za nchi za Afrika na wahisani. Wakati huo huo, mapambano dhidi ya unyonyaji yameongezeka kwani miaka 50 baada ya uhuru wa Tanzania bado haijaweza kujitegemea kiuchumi, kisiasa, -kijamii, kijeshi, kidini na kiutamaduni. Tanzania bado imetawaliwa na utegemezi mkubwa kwa nchi za magharibi kupitia makampuni makubwa ya kimataifa ya uwekezaji, na kupelekea taasisi hizo kudhibiti wa kiasi kikubwa sera zetu kuu za uchumi.

Wanawake ndio wanaoathirika na kunyonywa zaidi na mfumo uliopo kwani wengi wao ndio wazalishaji wadogowadogo, iwe ni wakulima, wafugaji au wavuvi. Wao ndio wanaonyonywa zaidi na kuporwa rasilimali kutokana na mwingiliano wa mifumo kandamizi ya kibeberu, kibepari na mfumo dume na kufanya wao kunufaika zaidi iwapo mifumo hii kandamizi  ya uchumi itaondolewa. Hivyo mada kuu ya tamasha la mwaka huu ilikuwa ni Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Ardhi, Nguvukazi na Maisha Endelevu.

Hivyo kwenye tamasha hili sauti za watu kutoka pembezoni zilisikika na ujumbe ulifika serikalini na popote pale ambapo wenye kutaka kusikiliza wapo. Matatizo ya ardhi yalijadiliwa, ukatili majumbani, ubakaji na udhalilishaji wa wanawake.

Nimetaja tamasha la kwanza na la mwisho kwa maana la mwaka huu, ni wazi matamasha yataendelea. Sasa tuyatupie macho matamasha mengine ya hapa katikati. Mfano tamasha la pili la jinsia lilifanyika mwaka 1997. Na tamasha  hili lilihusu zaidi masuala ya -kijamii. Usawa wa Kijinsia na Mgawanyo wa Haki katika mgawanyo wa rasilimali, hususan kuhusu ardhi, elimu, afya na sekta zingine. Lililenga kukosoa mageuzi ya ardhi ambayo yalikuwa yakiendelea wakati huo na kuzindua Mpango wa bajeti kwa mrengo wa Kijinsia ambao unapigania usawa na haki katika mgawanyo wa rasilimali na maamuzi. Tamasha hili lilihudhuriwa na washiriki wapatao 500.

Tamasha la tatu la jinsia liliandaliwa mwaka 1998. Na hili lilijikita zaidi katika ujenzi wa mitandao kama nyenzo ya ujenzi wa uwezo na mabadiliko ya Kijamii. Mada hiyo ilichaguliwa kusisitiza mahusiano kati ya asasi mbalimbali za kiraia na jinsi zinavyohusiana na kufanya kazi za serikali katika kuleta maendeleo, usawa wa Kijinsia na mabadiliko ya -kijamii.

Tamasha la nne la jinsia liliandaliwa mwaka 1999. Na hili pia liliandaliwa kwa mafanikio makubwa likijitia katika mada kuu ya Jinsia na uwezeshaji wa ushiriki Kisiasa katika milenia mpya. Tamasha lilivutia washiriki zaidi ya 600 ushiriki ukiboreka zaidi kutoka mikoani kuliko miaka mingine yote. Ushiriki wa makundi ya wananchi toka mawilayani na vijijini ( hasa mitandao ya Jinsia ngazi ya kati) ulifanya washiriki, wake kwa waume ikiwemo viongozi wa kisiasa, hususan wabunge na madiwani, kufanya tamasha liwe na maana iliyokususiwa kwa mwaka huo.

Tamasha la jinsia la tano lilifanyika mwaka 2001. Na hili lililenga zaidi mada ya Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Mbinu mbadala za kupambana na ufukarishwaji. Kauli mbiu ya tamasha hili ilikuwa “Rudisha Rasilimali kwa Wananchi”. Tamasha lilivutia washiriki wapatao 800 katika siku zote nne za tamasha. Na washiriki zaidi ya 40 walitola Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara na nje ya Afrika

Tamasha la sita la Kijinsia lilifanyika mwaka 2003. Lilifanyika juu ya mada ya Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Dunia Mbadala inawezekana. Cha muhimu zaidi kuhusu tamasha hili la 2003 ni kwamba lilitumia kuadhimisha miaka kumi ya uwapo wa TGNP na lilitoa nafasi ya kusherehekea miaka kumi ya kupigania ukombozi wa Wanawake nchini. Kufanikisha hilo TGNP ilichapisha na kuzindua vitabu viwili muhimu: Dhidi ya Ubeberu: Jinsia, Demokrasia na  Maendeleo na Saudi ya Wanaharakati: Harakati za Wanawake katika kutafuta Dunia Mbadala. Pia vijitabu viwili vilivyoandikwa kwa lugha nyepesi vilizinduliwa: Utandawazi na wewe na Rasilimali, Jinsia na UKIMWI. Tamasha  hili lilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 900 kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Tamasha la Jinsia la saba liliandaliwa mwaka 2005. Hili lilifanikiwa kwa kuwa na watu wengi zaidi. Walifika washiriki 2000 wakiwa ni wanawake na wanaume vijana na wasichana. Mada kuu ya tamasha hili ilikuwa ni Jinsia ,Demokrasia na Maendeleo: Mapambano ya Umma kuelekea dunia mbadala na iliyo bora zaidi. Tamasha liliweza kuleta pamoja washiriki toka sehemu mbali mbali za Tanzania, Afrika na duniani. Ushiriki wa Tanzania pia ulikuwa mkubwa sana na wa kufurahisha. Tamasha lilipambwa na sauti za wazunguzaji maarufu kama Waziri Mkuu wa zamani Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye alikuwa mgeni rasmi, Njoke Njoroge Njehu (Mkurugenzi wa Taasisi inayopigania mabadiliko Kenya) ambaye alitoa mada kuu na wengine wengi.

Tamasha la jinsia la nane liliandaliwa mwaka 2007. Mada kuu ya tamasha hili ilikuwa Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Harakati za Ukombozi wa Mwanamke katika Muktadha wa Utandawazi. Mijadala ya tamasha hili ilizingatia hali ya siasa ya utandawazi wa kibeberu na itikadi ya soko huria, madhara yake kwa maendeleo ya demokrasia nchini, barani Afrika na duniani kote. Tamasha lilivutia washiriki zaidi ya  3000 kutoka sehemu mbali mbali duniani kote.

Tamasha la jinsia la tisa liliandaliwa mnamo mwaka 2009. Tamasha hili lililenga zaidi katika harakati na mapambano kwenye ngazi ya jamii na hasa wanawake walioko pembezoni, kuhakikisha kuwa wanapata haki za fursa sawa katika kufikia na kumiliki rasilimali, katika ngazi zote, hususani katika muktadha huu wa mtikisiko wa uchumi na fedha. Mada kuu ilikuwa Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake walioko Pembezoni.

Pamoja na mafanikio na umuhimu mkubwa wa matamasha haya na majukwaa haya ya majadiliano bado kuna changamoto kubwa ya kuyaendesha kwa ufadhili kutoka nje ya nchi. Wafadhili wakubwa wa majukwaa haya ni HIVOS, SIDA, UNFPA, FOCUS, Well Spring, DANIDA  na Action Aid. Hata Foundation for Civil Society wanatoa mchango mkubwa. Ni kiasi gani mashirika haya ya kigeni yanatoa msaada bila ushawishi wa agenda zao? Ni kiasi agenda ya ukombozi wa mwanamke kimapinduzi inabaki ni agenda ya wanawake wenyewe wa Tanzania bila kuingiliwa na agenda ya za kibeberu na utandawazi wa utandawizi?

Hii ni changamoto ya miaka hamsini ya uhuru wetu. Kama mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanapenda kuendelea kuwepo na kupambana kwa kusimamia agenda zao, basi ni lazima yaanze mbinu za kujitegemea na kuendesha harakati kwa rasilimali zetu tulizonazo hapa ndani ya nchi. Vinginevyo yatakuwa yanatumikia mashinikizo ya ufadhili.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

 

0 comments:

Post a Comment