SIKU YA WANAWAKE DUNIANI, TANZANIA TUMEPIGA HATUA? Nianze makala hii kwa maoni ya mhariri wa gazeti moja la Ujerumani: “Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linawataka akina baba wauthamini mchango unaotolewa na wanawake katika maendeleo ya jamii. Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kwamba wanawake ndiyo, wazazi, ndiyo akina mama wa majumbani na pia ni wafanyakazi. Mambo hayo matatu yanashikamana ,anasema mhariri wa Stuttgarter Nachrichten. Kwa hiyo kila siku ingelikuwa siku ya wanawake duniani, laiti pangekuwa na mtazamo sahihi wa -kijamii” Maneno yaliyonivutia kwenye nukuu hii ni: “Kwa hiyo kila siku ingelikuwa siku ya wanawake duniani…” na yale yasemayo kwamba: “ Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kwamba wanawake ndiyo, wazazi, ndiyo akina mama wa majumbani na pia ni wafanyakazi”. Tunapojiandaa kusherehekea siku ya wanawake duniani ni muhimu kuwa na maneno hayo hapo juu kichwani mwetu. Tuache utamaduni wa kusherehekea kwa vile ni ratiba au kwa vile wengine wanafanya hivyo. Ni muhimu kusherehekea tukitafakari chanzo cha sherehe zenyewe, chanzo cha mapambano haya ambayo lengo lake kubwa ni kutetea haki za wanawake. Ni ukweli ulio mbele yetu kwamba kwa hapa Tanzania, kila siku ingekuwa ni siku ya wanawake duniani. Tunaishi na kushuhudia kila siku kwamba hapa Tanzania, wanawake ndiyo wazazi, ndiyo akina mama wa majumbani na pia ni wafanyakazi. Wanawake wanalima, wanapika, wanachota maji, wanazaa na kuwalea watoto. Wanawake wanatunza familia kwa kila hali. Kule vijijini wanawake hawana hata nafasi ya kuyafurahi maisha, kazi yao kubwa ni kuhakikisha familia inafurahi na kuishi kwa amani. Wasichana wanafanyiwa vitendo vibaya ya ukeketaji, kunyimwa nafasi ya kuendelea na masomo na kulazimishwa kuolewa mapema. Wengine wakipona kuozwa mapema na wakati mwingine hawapati bahati ya kuolewa, wanakimbilia mijini na kuanza kujiuza. Wanaishi maisha ya taabu na shida, wanapata fedha kwa mateso makubwa na kuhakikisha fedha hizo zinarudi nyumbani kwenye familia zao ili kuwalea watoto wao na kuwatunza wazazi wao. Wanawake wamekuwa wakisimama kidete kulinda na kutetea dhana ya mshikamano wa dhati; uwazi unaojengeka katika utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kwamba, wamekuwa wakitoa mchango mkubwa wa hali na mali katika maendeleo ya sekta ya elimu, afya na kilimo cha chakula kwa ajili ya familia na Jamii zao. Ni watu wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto ndani ya familia. Wanawake wameendesha mapambano bila kutumia silaha na wameshiriki kikamilifu kupata amani ya kweli, hata katika hali yao ya ukimya. Ugomvi wa kupigania madaraka barani Afrika, ambao umeleta vita na kuzalisha wakimbizi haujawa sehemu ya wanawake hata mara moja. Ugomvi huu unaongozwa na wanaume. Ingawa Tanzania haijakumbukwa na ugomvi wa madaraka kiasi cha kuingia vitani, vitendo vya ufisadi na rushwa kubwa ambavyo vimelitesa taifa letu kiasi kikubwa vimekuwa vikiongozwa na wanaume. Siku ya wanawake duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1911 wakati makundi ya wanawake nchini Marekani yalipokusanyika na kupinga udhalilishaji, ukandamizaji, uonevu na ubaguzi wa kijinsia hususani sehemu za kazi. Kuanzia wakati huo mataifa mbalimbali yalianza kuadhimisha siku hiyo kwa lengo la kupinga mfumo dume ambao uliwabagua wanawake kwa kuwanyima fursa za kusoma, kupata vyeo, mishahara mikubwa na haki ya kushiriki katika shughuli za maendeleo kisiasa, kiuchumi na kijamii. Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kila mwaka tarehe 8 Machi. Madhumuni ya Maadhimisho haya ni kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusu masuala ya wanawake. Aidha, madhumuni mahususi ni pamoja na: Kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani, Kuweka msisitizo na kuhamasisha jamii kuhusu kauli mbiu ya kimataifa wakati wa Maadhimisho ya kila mwaka, Kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali, asasi mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kuwaendeleza wanawake, Kuhamasisha jamii kuhusu utekelezaji wa sera, mipango na ahadi mbalimbali za kudumisha “Amani, Usawa na Maendeleo”. Vilevile, Maadhimisho haya hutoa fursa maalum kwa Taifa, Mikoa, Wilaya mashirika ya dini, vyama vya siasa, mashirika ya hiari, jamii na wanawake, kupima mafanikio yaliyofikiwa kimaendeleo na kubainisha changamoto zilizojitokeza katika kufikia azma ya ukombozi na maendeleo ya wanawake na hivyo kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo. Hapa nchini maadhimisho haya yalifanyika Kitaifa kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2005 na baada ya hapo Serikali ilipitisha uamuzi kuwa yafanyike kila baada ya miaka mitano. Uamuzi huu ulipitishwa ili kutoa muda wa kutosha wa utekelezaji wa maazimio mbalimbali na kuweza kupima mafanikio ya utekelezaji wa shughuli hizo za kila baada ya miaka mitano. Pamoja na umri mkubwa yaliyofikia maadhimisho haya, bado tunachokionja katika jamii zetu ni manyanyaso mbalimbali wanayofanyiwa akina mama duniani. Hali za kuwatumia kinamama katika mazingira ya kivita inasikitisha na kudai tena kutupiwa jicho. Takwimu zinaonesha wazi kuwa bado kuna idadi kubwa sana ya kinamama, na hasa walio katika umri wa ujana wanaendelea kunyimwa haki zao katika mazingira mbalimbali yanayotawaliwa na vita na vurugu. Kwa muda mrefu sasa wanawake wamekuwa ni tabaka linalodai haki dhidi ya mfumo dume, haki ya usawa kijinsia katika elimu, kazi za kiuchumi na kijamii. Haishangazi kuona kuwa wanawake wamekuwa na vyombo vingi vinavyowatetea, zikiwemo asasi za kiraia na za kiserikali, mashirika ya sheria Tangu shuleni wanawake wanapewa upendeleo, ukifika bungeni kuna viti maalum vya wanawake, hiyo yote ni njia ya kuwawezesha wanawake. Lakini kwa nini wanawake wanatetewa kiasi hicho? Je, ni kweli wanawake hawawezi? Mimi nadhani sasa ifike mahali wanawake wajitokeze wapaze sauti yao wenyewe badala ya kusubiri kuwezeshwa. Nasema hivi kwa sababu wanawake ni binadamu yule yule kwa hiyo hana tofauti na mwanaume kiutendaji ukiacha tofauti ya jinsia tu. Mwanamke anaweza kufanya kazi zote zinazofanywa na wanaume bila kupendelewa, sasa kwa nini asubiri kuwezeshwa? Tumeona wanawake wakiendesha hata magari ya mizigo, ndege, meli na treni. Siku hizi tunaona wanawake wakicheza hata mpira wa miguu. Hii inaonyesha kuwa wanawake wanaweza kila kazi. Kuendeleza upendeleo ni hali ya kuonyesha kwamba hawawezi na hii inawatendea kisaikolojia. Makala iliyopita niliandika juu ya wimbo wa Vick Kamata, unaosema kwamba wanawake wameolewa na CCM. Haya ni matokeo ya kuendeleza upendeleo kwao kiasi wanajiona duni mbele ya mfumo dume na kuutukuza kila wapatapo nafasi. Mfumo mzima unawanyima wanawake uwanja wa kujiamini na kujichukulia kama binadamu yeyote yule. Kwa upande mwingine, hapa Tanzania, ukombozi wa Mwanamke unakwamishwa na wanawake wenyewe. Kuna haja ya wanawake Tanzania kujifunza kutoka mataifa mengine. Sherehe kama hii ya siku mwanamke duniani iwe ni fursa ya kujifunza kutoka kwingine. Tanzania ni lazima tupige hatua katika jitihada za kumkomboa mwanamke. Kuna kazi kubwa ya kuvunjilia mbali mfumo dume ambao kwa kiasi kikubwa umejengeka kiasi hata wanawake wanafikiri na kutenda “Kimfumo dume”. Akigombea mwanamke, wanawake wenzake wanakuwa mstari wa mbele kusema kwamba hawezi na wakati ukifika wa kupiga kura wanamnyima kura zao. Ipo mifano mingi ambapo wanawake walishindwa kuwaunga mkono wanawake wenzao na kuwapigia kura wanaume. Hali hii ni hatari. Wanawake ni wajenzi wa amani, taswira ambayo imejionesha kwa namna ya pekee katika siku za hivi karibuni, katika medani za kitaifa na kimataifa, kwa wanawake watatu kutoka Barani Afrika kupewa tuzo la amani kwa Mwaka 2011. Wanawake katika nchi mbali mbali za Kiafrika wamekuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha misingi ya amani na utulivu, lakini mchango wao haukupewa uzito unaostahili kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Leymah Gbowee ni mwanamke ambaye alipambana kufa na kupona, ili kuhakikisha kwamba, vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyokuwa inavuma nchini Liberia kuanzia mwaka 2003 inafikia ukomo. Mama huyu anakumbukwa na Jumuiya ya Kimataifa kama mpigania amani. Fatou Bensouda si mgeni sana katika masuala ya haki na amani kwenye Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda, iliyokuwa na makao makuu yake Jijini Arusha, Tanzania. Bibi Jacqueline Moudeina alikuwa ni wakili wa kesi za dhuluma dhidi ya wanasiasa waliokumbana na ukatili wa utawala wa rais Hussein Habre wa Chad. Ni mwanamke aliyehatarisha usalama na maisha yake. Jumuiya ya Kimataifa imetambua na inaendelea kuthamini mchango makini uliotolewa na wanawake wawili kutoka Liberia: Hawa ni Rais Elle Johnson Sirleaf na Bibi Leymah Gbowee pamoja na Tawwakkol Karman, mwanamke kutoka Yemen. Hawa ndio waliojinyakulia tuzo ya amani kwa Mwaka 2011 na kwamba, kuanzia sasa dhamana na mchango wa wanawake kutoka sehemu mbali mbali za dunia utaendelea kuheshimiwa na kuthaminiwa. Wanawake hawapaswi kuwa ni wahanga wa vita na nyanyaso za kijamii, bali wadau wakuu katika mchakato mzima unaopania kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani duniani. Itakumbukwa kwamba, mwanamke wa kwanza kupata tuzo ya amani kimataifa ni Hayati Professa Wangari Mathaii kutoka Kenya. Aliendesha kampeni ya kijani kibichi nchini Kenya; jambo ambalo lilipelekea msigano mkubwa na viongozi wa kisiasa nchini Kenya, kiasi hata cha kuonja taabu na suluba za gereza. Lakini, akasimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na matunda ya juhudi hizi yanaendelea kuonekana si tu nchini Kenya, bali kwa wapenda amani na watunza mazingira kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wanawake wa Tanu, wakiongozwa na Bibi Titi Mohamed, ni miongoni mwa wanawake waliochangia kiasi kikubwa Uhuru wa taifa letu la Tanzania. Baada ya uhuru, wanawake hawa walitupwa pembeni. Hakupata vyeo, hawakuandikwa kwenye kumbukumbu ya historia ya Tanzania. Lakini wanawake hawa, pamoja na uwezo mkubwa walikuwa nao, hawakuingia msituni kudai haki zao. Walikaa kimya, waliendelea kulima na kufanya kazi ili kuwalea na kuwalinda watoto wa Tanzania. Wanawake wa Tanu ni mfano mzuri wa maneno niliyoanza nayo: “Kila siku ingekuwa siku ya wanawake duniani….” Maana hawa …. “ ndiyo, wazazi, ndiyo akina mama wa majumbani na pia ni wafanyakazi”. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 63 31 22

0 comments:

Post a Comment