NYANJURA DOREEN NA BAGAYA IBRAHIM KISUBI, NI KIZAZI KIPYA CHA UGANDA NA AFRIKA?
Tarehe 11 mwezi wa nne ni siku yenye kumbukumbu nzito kwa nchi za Uganda na Tanzania. Tarehe kama hiyo mnamo mwaka 1979, majeshi ya ukombozi ya Tanzania na Uganda (Wapiganaji wa msituni) yalifanikiwa kumtimua Iddi Amin kutoka Kampala, na kuandikwa historia ya kumaliza utawala wa kimabavu uliodumu Uganda zaidi ya miaka tisa. Wakati ule ilionekana Iddi Amin, alikuwa amekaa miaka mingi madarakani. Leo hii Rais Yoweri Kagura Museveni, anakaribia kufikisha miaka 20 akiwa madarakani. Wameziba midomo ya watu wengine kusema na kuhoji na hili halikuwa ni lengo Rais Museveni, alipokuwa akiingia madarakani.
Ingawa ushindi huo wa 1979 ulipokelewa kwa furaha na wanganda pamoja na ndugu zao Watanzania, bado kuna ukweli ambao hadi leo hii bado unaishia ndani ya mioyo ya wanganda. Pamoja na mabaya yote yaliyoandikwa na kutangazwa juu ya Iddi Amin, ukweli unabaki kwamba huyu ni rais pekee wa Uganda ambaye hakuwa na mali binafsi, hakuwekeza fedha nje ya nchi; alitumia fedha ya Uganda kwa maendeleo ya Uganda.Hakuwa na fedha nje ya nchi, aliamini fedha zote ni zake na kama zake yeye Rais, basi fedha ni za waganda. Alipokuwa akiikimbia Uganda, alikuwa na uwezo wa kubeba vitu vingi, lakini hata ndege ya Rais ambayo eti walienda kuinunua akiwa na fedha kwenye mkoba na uwa mtu wa kwanza kununua ndege kwa mtindo huo, hakuondoka nayo, aliicha maana aliamini si mali yake bali ni mali ya Waganda. Inasemekana kwamba nyumba za Ubalozi wa Uganda katika nchi nyingi zenye uhusiano na Uganda zilijengwa na Iddi Amin. Hata nyumba nzuri za Mapolisi zilijengwa na Iddi Amin. Ingawa Iddi Amin, alikuwa mtu ambaye hakuwa na elimu ya juu, lakini alipenda elimu. Vijana wote waliomaliza kidato cha sita wakati wa utawala wake na kushinda kwa daraja la kwanza, aliwapeleka wote kwa nguvu kujifunza ualimu, ili warudi na kuwafundisha watoto wengine. Walimu wengi walipoikimbia Uganda kwa kuogopa usalama wa maisha yao, Iddi Amin, eti alitumia ndege yake ya Urais, kwenda Ghana, kusomba walimu na kuwaleta Uganda ili wawafundishe watoto wa Uganda. Yapo mengi mazuri aliyoyafanya Iddi Amin, lakini yalifunikwa kwa propaganda za kisiasa. Si lengo la makala hii kumtetea Iddi Amin, bali ni kutolea mfano wa tarehe 11 mwezi wa nne.
Kumbu kumbu nyingine mbaya ya terehe hiyo ya 11 mwezi wa nne ni mwaka huu alipokamatwa na kuwekwa ndani binti mdogo wa miaka 22, Nyanjura Doreen, na kuwekwa ndani kwa kuandika kitabu kinachomkosoa Rais Yoweri Museveni. Furaha ya kumfukuza Iddi Amin, imeanza kuleta machungu na masikitiko katika nchi ya Uganda zaidi ya miaka 31 Iddi Amin kutoka madarakani. Kwa vile Tanzania, ilishiriki kikamilifu kumfukuza Iddi Amin, haiwezi kukaa kimya, historia inapojirudia. Ni lazima watanzania kushirikiana na waganda kulaani kitendo cha serikali ya Uganda kumkamata Binti Mdogo na kumfunga gerezani kwa kitendo cha kuandika kitabu.
Nyanjura Doreen na mwenzake Bagaya Ibrahim Kisubi, wameandika kitabu : “Is It The Fundamental Change?” wakilenga kufichua ukweli uliojificha juu ya maisha na utawala wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda. Wanasema Rais Yoweri, alipoingia madarakani, alitoa ahadi ya kuleta mabadiliko ya msingi. Kinachoonekana leo ni tofauti kabisa. Vijana hawa wawili na wengine wengi nchini Uganda, wamezaliwa wakati Rais Yoweri akiitawala Uganda, wamekuwa wamesoma hadi chuo kikuu, bado Rais ni Yule Yule. Na hili ndilo swali lao kubwa, kwamba mabadiliko ya msingi yanaweza kuwa na maana yoyote ile kwa kumtengeneza Rais wa maisha? Kwa kuizika demorasia na kunyamazisha vyama vya siasa vya upinzani?
Walichofanya vijana hawa ni kukusanya maneno ya Rais Museveni mwenyewe, na kuhoji ukweli way ale yote aliyoyatamka siku akiingia madarakani hadi leo hii. Na jibu ni kwamba wakati umefika wa “Mzee” kupisha kizazi kipya. Kitu ambacho Rais Museveni na serikali yake hawako tayari kukisikia, na ndicho kisa cha Kumkamata na kumuweka Doreen na mwezake ndani.
Ninapoandika makala hii Doreen na mwenzake bado wako ndani hadi tarehe 24.4.2012 watakaposomewa mashitaka. Lakini kuna shinikizo kubwa kutoka kwa wanafunzi wa vyuo vyote Jijini Kampla, kwa kutaka ifikapo Jumatatu tarehe 16.4.2012, Doreen ambaye ni makamu rais wa serikali ya wanachuo wa chuo kikuu cha Makerere Uganda na mwenzake wawe wametolewa gerezani bila masharti yoyote yale mara ifikapo Jumatatu ya tarehe 17.3.2012. Vijana wamehapa kufanya maandamano ya nguvu na polisi wanajiandaa kwa mabomu ya kutoa machozi, maji ya kuwasha, virungu na risasi za moto.
Unapofika wakati vijana wakawa tayari kwa lolote, ni hali ya kugopesha. Kwanza vijana ndiyo asilimia kubwa ya watu duniani. Siku vijana wakikubaliana kuungana na kuwa na sauti moja na kuamua kuingia mitaani; viongozi wanaotaka kuzeekea madarani watapata taabu kubwa sana. Watajikuta nje ya Bunge na ni jambo la kusikitisha kwamba huko vijijni hawatapokelewa
Nilikutana na Nyanjura Doreen, jijini Mwanza siku ya Pasaka, akiwa na nakala chache za kitabu chake cha “Is it The Fundamental Change?” Ni vigumu kuamini kwamba msichana mdogo kama Doreen, anaweza kuwa na maneno ya kuongea; maneno ya kuwaomba viongozi waliokaa muda mrefu madarakani, waachie ngazi vijana chipukizi. Doreen Nyanjura,aliniomba nikifanyie uhakiki kitabu chake na kukiweka kwenye magazeti ya Tanzania. Lengo lake kubwa lilikuwa ni kukisambaza kitabu hicho kabla ya kukizundua Jijini Kampala tarehe 11.4.2012. Nafikiri alijua wazi kwamba uwezekano wa serikali ya Uganda kukizuia kitabu hicho kisizinduliwe na kusambazwa ni mkubwa, hivyo aliamua kusambaza nakala chache nchi jirani.
Na huo ulikuwa ujumbe tosha kwa Serikali ya Uganda kwamba mbinu za kizamani za kuzuia vitabu kusomwa, kuzuia vitabu kuzinduliwa, zimepitwa na wakati. Sasa kitabu kimefika Tanzania, kutoka hapa kitasambaa Kenya, Rwanda , Burundi na nchi nyingi za kiafrika hata na Ulaya na Amerika. Na kitendo cha kuwakamata waandishi wa kitabu hiki na kuwaweka ndani ni mtindo wa kizamani usiokuwa na tija. Hata mtu ambaye alikuwa hana habari juu ya Nyanjara Doreen, sasa amemfahamu na atatake amfahamu vizuri kwa kutaka kufahamu ni kwanini binti mdogo kama huyo akamatwe na kuwekwa ndani, kutafanya kitabu hicho kitafutwe kwa udi na uvumba.
Wakati akinipatia nakala ya kitabu chake alisema “ Karugendo, nisaidie kukitangaza kitabu hiki, maana najua yaliyo mbele yangu. Museveni, atanikamata na kuniweka ndani. Pia anaweza kuamua kuvichoma vitabu vyote”. Nilimsii kwa vile alikuwa Tanzania, na ana hofu ya kukamtwa, basi abaki Tanzania kama mkimbizi wa kisiasa. Jibu laki lilikuwa “ Siwezi kuikimbia nchi yangu, ninajua nina haki zote za kutoa maoni yangu, ni haki yangu kutetea haki na kuhakikisha demokrasia na mabadiliko ya msingi yanatendeka nchini Uganda. Ni bora nikamatwe, nifungwe na hata ikibidi niifie nchi yangu”. Nilishangaa kuona binti mdogo wa miaka 22, akiwa na ushupavu wa kutisha. Na kweli siku mbili baada ya kukutana naye Jijini Mwanza, alikamatwa siku ya kukizindua kitabu chake na kutupwa gerezani.
Uzinduzi wa kitabu chao ulikuwa ni waina yake. Waandishi walivalia nguo za wasomba taka taka na kushikilia mifagio na vyombo vya kukusanyia takataka na kuelekea kwenye uwanja wa Katiba wa jijini Kampala ili kuusafisha waweze kuzindua kitabu chao kwenye uwanja ulio safi. Polisi waliwakamata wakiwa njiani kuelekea kwenye uwanja wa Katiba.
Kwenye kitabu chao wananukuu maneno ya Martin Luther King; “Maisha yanaelekea mwishoni, siku tunapokaa kimya kwa mambo ya msingi” Tafsiri ni yangu. Pia wananukuu maneno ya Napoleon, pale aliposema kwamba “ Dunia inateseka, si kwa sababu ya vurugu na maasi ya watu wabaya, bali ni kwa sababu ya ukimya wa watu wema”.
Nyanjura Doreen na Bagaya Ibrahim Kisubi, hawakupenda kuwa kimya; walitaka kuyashughulikia mambo ya msingi: Kutetea demokrasia, kutetea haki za binadamu, kutetea uhuru wa kujieleza na kumweleza wazi wazi rais Museveni kwamba amekaa sana madarakani wakati umefika wa kuwaachia wengine nafasi ya kuliongoza taifa la Uganda.
Pamoja na ukweli wa kujua kitakachotokea; kukamatwa, kupigwa, kuwekwa ndani na wakati mwingine kupoteza maisha yao, bado waliendelea na mipango yao ya kukizindua kitabu chao kwenye uwanja wa katiba. Hili linashangaza ni ujumbe si kwa Rais Museveni peke yake, bali kwa marais ya Afrika ya mashariki na Afrika nzima: Kwmba mabadiliko ya msingi yataletwa na Kizazi kipya. Matumizi ya silaha yanapitwa na wakati. Mbele yetu ni nguvu ya kizazi kipya mbayo kuizuia ni lazima mtu awe tayari kuwekwa kwenye rekodi ya mauaji ya kimbali.
Nilipomshawishi Nyanjura Doreen, ubaki Tanzania kama mkimbizi wa siasa, alikataa kabisa. Kwa maneno yake mwenyewe alisema: “ acha niende kufungwa, acha nife kama ni kufa kwani mimi ni bora zaidi ya nani? SeptembaI 2009 zaidi ya vijana 40 waliuawa, hawa ni pamoja Kauma Joseph, Nakazi Deborah, Nahumma Brenda, Katum Richard, Kalamba Ronald, Kamoga Sula, Aliwo Abed, Nabakoza Christine, Bisso Steven,Ssango Kyobe, Ikongo Samuel, Mayanja Bruno, Bukenya Faisal, Mukwanga Kaziru, Benjamin Parnot Ateere, Batiibwe Badru, Muganga Huzair,Busulwa Hassan, Bwesigwa, Grace Sserunjogi, Joseph,Muganga Hakim, Kafuma Frank, Nampijja Jackie, Magembe Ali, Lukwago Sulaiti, Karungi Annet, Erimweya Mawanda, Nsereko Robert, Batibwe Abdullah, Nampijja Beatrice, Nahumma Brenda, Ngaba Moses. Vijana wote hawa isipokuwa Batiibwe Badru aliyekuwa na umri wa miaka 39, walikua kati ya miaka 2-25. Na wengine walikufa kwenye Makubiri ya Kasubi, Masaka, Kampala, Gulu, Jinja, Mbale na sehemu nyinginezo”.
Alinielezea haya kwa uchungu mkubwa. Akilalamika kwamba vijana ambao wangepaswa kuwa shuleni wakisoma, wanakamatwa na kuwekwa gerazani. Yeye Doreen na Mwenzake, wako mwaka wa mwisho kwenye chuo kikuu cha Makerere.
Waswahili wana msemo wa “Mwenzako akinyolewa wewe tia maji” Sisi watanzania tunajifunza nini kutokana na tukio la Serikali ya Uganda kuwakamata na kuwashitaki waandishi?
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment