MUUNGANO WETU NA UTANZANIA WETU. Ninaandika makala hii nikiwa Tanganyika! Nisieleweke vibaya. Mimi siko kwenye kikundi cha wale wanaotaka serikali tatu: Ya Muungano, Ya Tanganyika na ya Visiwani. Mimi ni mfuasi wa wale wanaotaka serikali mbili, ya Muungano na ya Visiwani. Pamoja na msimamo wangu huo, ukweli ni kwamba sasa hivi niko Tanganyika! Wakati wa kuunda muungano wa nchi hizi mbili, kila nchi ilikuwa na serikali na kutambuliwa kimataifa. Bada ya muungano, nchi hizi ziliunda nchi moja ya Tanzania. Na kimataifa inatambuliwa nchi hii ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Lakini kiutendaji Zanzibar imebaki kama nchi, ina katiba yake, ina rais wake na serikali yake na ina baraza la wawakilishi. Tanganyika ilimezwa na kufa kabisa. Hoja ya CCM ni kwamba vijana wengi, ambao ni ndo asilimia kubwa ya watanzania, wamezaliwa baada ya muungano. Hivyo wanachokijua ni Tanzania. Huu ni ukweli kwa upande wa Tanganyika. Lakini kwa upande wa Zanzibar si kweli, maana Zanzibar ilibaki kama ilivyokuwa kabla ya muungano na inaendelea kubaki hivyo. Hivyo hata wale watoto waliozaliwa baada ya muungano wataendelea kuitambua Zanzibar kama Zanzibar. Ni tofauti na wa bara ambao hawakuikuta Tanganyika, labda kuisikia kwenye maandishi kama vile Chama cha Wanasheria wa Tanganyika. Swali, linakuja, je tuimarishe Tanganyika na utanganyika? Tuimarishe Zanzibar na uzanzibari au Tuimalishe Tanzania na utanzania? Bahati mbaya ni kwamba walio wengi wanakazana kuwaimarisha watanzania na kusahau kuuimarisha utanzania! Maana yake ni nini?Karugendo, anashughulikia maendeleo yake na tumbo lake, Kalimanzila, naye anaangaalia tumbo lake, furaha yake, usalama wake na maendeleo yake. Karugendo ni mtanzania, leo yupo na kesho hayupo! Kalimanzila ni mtanzania, leo yupo na kesho hayupo! Watanzania wanakuja na kupita, lakini utanzania unabaki na kudumu milele! Wito wa mwanadamu, jinsi alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu, ni kushughulikia vitu vinavyodumu milele na kuacha kupoteza muda wake kwa vitu vinavyokuja na kupita. Mfano sisi watanzania wito wetu mkubwa ni kushugulikia utanzania wetu usiopita zaidi ya kuyashughulikia matumbo yetu yanayopita na kupotea. Inawezekana leo ninaelekea kujadili mada inayochanganya kidogo. Ili kuijadili vizuri mada hii nitamtumia mwanafalsafa Plato, aliyeona kwa mara ya kwanza ukweli juu ya vivuli na vitu halisi. Nitatumia kwa karibu maneno ya Adolf Mihanjo,Phd, yanayopatikana katika kitabu chake cha Falsafa na Usanifu wa Hoja-Kutoka Wayunani hadi Watanzania (Waafrika) Plato ndiye mwanafalsafa aliyeanzisha Astria ya Pango. Asria hii ndiyo iliyoendelea hadi kuonyesha ukweli kwamba kuna vitu vinavyodumu na vile vinavyopita. Kwamba vingine ni vivuli na vingine ni vitu halisi, ukweli na vitu visivyobadilika milele yote. Mfano, upendo ni kitu kinachodumu milele yote. Watu wanaopendana wanakuja na kupita, lakini upendo upo pale pale. Au ubaya. Watu wanatenda ubaya na kushiriki ubaya. Watu hawa wanakufa na kupita, lakini ubaya unabaki palepale. Hata kama tungefanikiwa kuwamaliza wabaya wote, ubaya utabaki katika wazo la ubaya, na endapo atachipuka tena mtu mbaya, atashiriki ubaya katika wazo la ubaya! Plato katika nadharia ya asitiria ya Pango, anajaribu kutengeneza picha ya watu ambao walizaliwa pangoni au shimoni na wanaishi huko kuanzia utoto wao hadi ukubwa wao. Huko pangoni wapo peke yao.Na maisha yao yote ni ya pangoni. Nje ya pango kuna watu wakiwa na mishumaa ikiwaka wanapita huku na huko. Mwanga wa mishumaa huakisi sura za hao watu wapitao na kutoa vivuli vyao. Vivuli hivyo hutokea katika ukuta wa shimo au pango ambamo wamo watu waishio humo maisha yao yote. Ingawa hivi vivuli huashiria uwepo wa watu nje ya hilo pango, wao huona hivyo vivuli kama ndio watu wenyewe. Hii inatokana na ukweli kuwa katika maisha yao, hawajawahi kuona tofauti kati ya watu na vivuli vyao. Kwa maoni ya Plato, watu hawa waishio kwenye pango, wataamini daima kwamba vivuli ndo vitu halisi. Hii astaria ya pango ilimfikisha Plato, katika hatua ya nadharia ya mawazo. Hii inajulikana kama Nadharia ya Plato ya Mawazo. Kwa ujumla nadharia ya mawazo ni ule ukweli ambao haubadiliki au una hali ya umilele na haina hali ya umaada ambapo vitu vyote vijavyo kwetu katika hali ya umaada huja kama vivuli vyake. Katika nadharia ya mawazo Plato anasema kuwa wazo ni kitu ambacho hakibadiliki, kipo milele na wala hakuna sura ya mwili. Na kutokana na hili wazo, vitu vyote tuvionavyo ni vivuli vya hilo wazo au hayo mawazo. Tukitaka kubaki kwenye mfano wetu ni kwamba Utanzania, ndilo wazo lisilobadilika. Utanzania ndio ukweli. Hali ilivyo, utanganyika na uzanzibari ni kujidanganya na kukimbiza upepo. Hivyo basi watanzania ni vivuli vya utanzania. Na hapa bila kwenda mbali au kuumiza akili zetu ni kwamba kivuli hakiwezi kuwa cha muhimu kuliko kitu halisi.Picha ya mtu si muhimu kuliko mtu mwenyewe! Kama nilivyosema hapo juu ni kwamba kwa bahati mbaya sisi wadamu au niseme kwamba sisi watanzania tunapenda au tumezoea kushughulika na vivuli kuliko ukweli usiobadilika. Mfano tunashughulika na watu wanaopendana badala ya kushughulika na upendo wenyewe.Hili wazo la upendo lisilobadilika, linalodumu milele yote, tunalishughulikia kiasi gani, kulifahamu na kulielewa vizuri. Tunakwenda kiasi katika kuutafakari upendo? Au tunashughulika na wau wazuri, bila kushughulika na uzuri wenyewe. Watu wazuri wanakuja na kupita, lakini uzuri unabaki pale pale. Hata watakaozaliwa miaka mia ijayo watashiriki uzuri ule ule. Mfano Karugendo ni mtanzania, hicho ndicho tunachokiona na kuamini kwamba huo ndo ukweli. Sisi tunaamini hivyo na yeye Karugendo, anaamini hivyo. Atafanya kila kitu kwa kujiangalia na kuamini kwamba yeye ndo ukweli. Ataishi kwa kuamini kwamba yeye ndo ukweli. Na kwa vile yeye ndo ukweli, basi ana haki zote, atatumia kila kitu kilichotolewa na Mwenyezi Mungu kwa kujiangalia yeye mwenyewe. Kwa njia hii Karugendo, hawezi kuwa na upeo wa kuangalia vizazi vijavyo. Ukweli kwamba Karugendo, ni kivuli cha utanzania. Kwamba utanzania ndicho kitu cha kweli, kwamba utanzania ndicho kitu kinachodumu milele yote, hauoni. Kuuona ukweli huu, kamba utanzania ndicho kitu halisi ni kukubali kutengeneza Tanzania ya vizazi vijavyo. Tukirudi kwenye mfano wetu wa mtanzania na utanzania, au Karugendo na utanzania. Kama Karugendo, pamoja na elimu yake na shahada zake, bado ana imani kwamba yeye ndo ukweli, na utanzania ndo kivuli, basi Karugendo, hana elimu yoyote ile, bado yuko gizani, pangoni. Mtu aliyeelimika ni yule anayetambua kwamba Karugendo ni kivuli cha utanzania. Mtu aliyeelimika ni yule anayetambua kwamba utanzania ndicho kitu kinachodumu milele yote. Ni yule anayetambua kwamba kinachotangulia si Karugendo, bali ni utanzania. Mfano mwingine ni kwamba mtu aliyeelimika ni yule anayetambua kwamba wapendanao ni kivuli cha upendo. Kwamba upendo ndo kitu halisi, upendo ndo ukweli, na upendo ndo kitu kisichobadilika. Wapendanao wanaweza kuachana, wanaweza kufa, lakini upendo upo palepale. Upendo hauwezi kupungua au kuongezeka kwa vile watu wengi au watu wachache wamependana. Sisi tutapendana na vizazi vijavyo watapendana. Ni kiu cha kudumu milele yote. Mtu, aliyeelimika ni yule anayeshughulika na vitu visivyopita. Ni mtu yule anayeshughulikia heshima, kuliko kushughulikia watu wanaoheshimiana, ni mtu anayeshughulikia upendo kuliko wapendanao, na ni yule anayeshughulikia utanzania kuliko kuwashughulikia watanzania! Si kwamba anawapuuza watanzania, hapana, ila kwake kitu cha msingi ni utanzania. Mtu anayetanguliza utanzania, atawahudumia watanzania wote bila kuangalia kabila, sura,cheo au hali ya mtu. Mtu, anayetanguliza utanzania, atatenda haki wakati wote, atawapenda watanzania wote na atawahudumia watanzania wote. Sote tukishughulika na utanzania, Tanzania yenye neema inawezekana leo, kesho na keshokutwa. Tanzania yenye neema kwa vizazi vijavyo inawezekana pia!Hivyo ni muhimu kwetu sote kukazana kuisaka elimu, elimu ya kweli ya kutuletea mwanga na kututoa gizani Nchi zote zilizoendelea zilitanguliza utaifa, mfano Ujerumani ilianguliza Ujerumani, kuliko mjerumani, Amerika ilitanguliza Umarekani, kuliko mmarekani, nchi zote hizi zilizoendelea zilitanguliza vitu visivyobadilika, vitu halisi na vitu ambavyo ndio ukweli wenyewe. Kwa kufanya hivyo waliweza kuwa na mipango ya miaka zaidi ya miambili mbele.Na njia hii waliianza kwa kutafakari na kuikumbatia falsafa. Kwa kusoma na kutafakari, kwa kusoma na kufanya majadiliano, midahalo na kwa kusoma na kushikirishana. Walitafuta elimu ya kweli. Utanzania wetu ni kudumisha Muungano wetu! Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment