MUUNGANO NA TANZANIA TUITAKAYO


Juzi Star TV ilirusha kipindi cha mdahalo juu ya  Muungano na Tanzania tuitakayo. Waongeaji wakuu wakiwa ni CCM, CHADEMA na Rais wa chama cha wanasheria wa Tanganyika. CCM kwa upande  wake ilishikilia msimamo wake wa muundo wa muungano wa sasa wa serikali mbili: serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. CHADEMA wao msimamo wao ambao ulielezwa vizuri na Mheshimiwa Mnyika ni ule wa serikali tatu: Serikali ya Zanzibar, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano. Kwa maana hii hoja iliyo mbele yetu ni kuchagua kati ya serikali mbili na serikali tatu. Kuna watu wachache sana wanaojitokeza kushabikia muundo wa serikali moja.

Wakati wa kuunda muungano wa nchi hizi mbili, kila nchi ilikuwa na serikali na kutambuliwa kimataifa. Bada ya muungano, nchi hizi ziliunda nchi moja ya Tanzania. Na kimataifa inatambuliwa nchi hii ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Lakini kiutendaji Zanzibar imebaki kama nchi, ina katiba yake, ina rais wake na   serikali yake na ina baraza la wawakilishi. Tanganyika ilimezwa na kufa kabisa. Hoja ya CCM ni kwamba vijana wengi, ambao ni ndo asilimia kubwa ya watanzania, wamezaliwa baada ya muungano. Hivyo wanachokijua ni Tanzania. Huu ni ukweli kwa upande wa Tanganyika. Lakini kwa upande wa Zanzibar si kweli, maana Zanzibar ilibaki kama ilivyokuwa kabla ya muungano na inaendelea kubaki hivyo. Hivyo hata wale watoto waliozaliwa baada ya muungano wataendelea kuitambua Zanzibar kama Zanzibar. Ni tofauti na wa bara ambao hawakuikuta Tanganyika, labda kuisikia kwenye maandishi kama vile Chama cha Wanasheria wa Tanganyika.
Kama nilivyosema mwanzoni ni kwamba hoja zote zinazotolewa juu ya Muungano ni nzito. Mtu anayefikiri kwamba hoja hizi zinaweza kupita hivi hivi kwa njama za kuzima majadiliano atakuwa na ugonjwa wa akili. La kujivunia ni kwamba hakuna anayependekeza kuuvunja muungano. Ukisikiliza maongezi ya mitaani na vijiweni, hakuna wanaopendekeza kuuvunja muungano. Wale wanaotetea serikali moja na serikali mbili, wanasema hoja ya kutaka serikali tatu lengo lake ni kutaka kuudhoofisha  muungano na hatimaye kuuvunja. Hapo ndipo inaposikika hoja ya kuuvunja muungano; kwamba agenda ya serikali tatu ni njama za kuuvunja muungano; Kwamba Zanzibar wakijadili na kuendesha mambo yao ya ndani na Tanganyika wakajadili na kuendesha mambo yao ya ndani, rasilimali za kuiendesha serikali ya muungano zitatoka wapi? Vuta ni kuvute ya kuiendesha serikali ya muungano ni lazima ilete anguko na muungano kama ilivyotokea kwa Jumuiya ya Afrika ya mashariki.

Pamoja na utangulizi huu, lengo la makala hii si kujadili muungano. Mimi binafsi nina maoni yangu juu ya muungano na isichukuliwe kwamba yale ninayoyajadili kwenye makala hii ndo msimamo wangu. Wakati ukifika na jukwaa la majadiliano likawekwa wazi, mizengwe na siasa uchwara vikawekwa pembeni nitatoa mawazo yangu juu ya muungano. Ninachokijadili leo ni umeme kukatika wakati wa mdahalo.  Kukatika kwa umeme ni jambo ambalo tumelizoea na sasa ni kama utamaduni wetu. Tanzania umeme kuwaka siku nzima bila kukatika ni muujiza. Hakuna aliyetegemea kwamba wakati wa kilele cha sherehe za miaka hamsini ya uhuru umeme ungekatika. Kuna habari zilizoenea kwamba TANESCO iliwapatia motisha wafanyakazi wake kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha tarehe moja hadi tarehe 12 za mwezi huu wa Desemba umeme haukatiki. Wale tuliobaki majumbani na kufuatilia sherehe hizi kwenye luninga, tulishuhudia umeme ukikatika na kushindwa kufuatilia sherehe hizi ambazo ni muhimu kwa taifa letu.

Mdahalo wa Muungano na Tanzania tuitakayo, umerushwa mara mbili na kituo cha Star TV. Mara ya kwanza baada ya utangulizi na mwongeaji wa kwanza aliyekuwa Mheshimiwa Mnyika kumwaga sera za chama chake za Serikali tatu, umeme ulikatika na kurudi mwishoni wakati kipindi kinamalizika. Mdahalo uliporushwa kwa mara ya pili baada ya juma moja, yalitokea yale yale ya kukatika umeme kama ilivyotokea wakati kipindi hiki kikirushwa kwa mara ya kwanza. Kwa maana hiyo ni kwamba wale tuliokuwa tukifuatilia kwenye luninga hatukuweza kusikia hoja za wasikilizaji. Uzuri wa mdahalo ni pale mtu unaposikia hoja mbali mbali. Waongeaji wakuu wakitoa maoni yao, basi mtu unasikiliza na hoja nyingine. Msimamo wa CCM ni wa serikali mbili, msimamo wa CHADEMA ni wa serikali  tatu. Je watanzania wengine wana maoni gani? Umeme ulituzuia mara mbili kufuatilia mdahalo huu. Hili ndilo ninalolalamikia. Tulitaka kusikia watanzania  ambao si wanasiasa, wanasema nini juu ya muundo wa muungano na Tanzania tuitakayo.

Swali langu ni je ni matatizo ya umeme au ni njama? Kuna kishawishi kikubwa kukubali kwamba ni njama. Kwa nini tatizo la umeme lijitokeze mara mbili kwenye tukio lile lile? Kwa wale waliofuatilia kipindi hiki watakuwa waligundua kwamba umeme ulikatika wakati ule ule kama ulivyokatika kwenye kipindi cha kwanza na kurudi wakati ule ule; haiwezekani haya yakawa ni matatizo ya kiufundi, kwa akili za kawaida nasema hapana, labda kama kuna nguvu za giza au hujuma. Inawezekana kuna wakubwa ambao hawapendezwi na midahalo kama hii? Hawapendi watu wajadili mambo mazito ya taifa letu? Inawezekana kuna mtu anatoa amri umeme ukatwe? Nchi hii ina watu wazito, watu wenye fedha, watu ambao wakitaka kitu kinakuwa, wakitaka umeme ukatwe unakatwa, wakitaka mvua inyeshe inanyesha, wakimtaka mbunge anakuwa, wakimtaka waziri anakuwa; tuna miungu watu ndani ya taifa letu.

Nakumbuka kuna wakati Mheshimiwa Dkt Slaa, alikuwa akichangia Bungeni, na watu walisubiri mchango wake kwa hamu. Ilipofika zamu yake ya kuongea, umeme ulikatika nchi nzima! Ni vigumu kujua kama ilikuwa ni tatizo la umeme ua kuna mkubwa Fulani alitoa amri umeme ukatwe.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010, pale Jangwani, CHADEMA walipotoa maneno mazito ya kuishambulia Serikali. Mitambo ya TBC ilizimika kwa kisingizio  cha umeme kukatika. Wachekeshaji wa Ze Komedi ambao daima vichekesho vyao ni juu ya matukio yanayotokea kila siku kwenye jamii yetu, nakumbuka kuna wakati walionyesha jinsi wafanyakazi wa TANESCO wanavyoamua kukata umeme. Hata kama hakuna matatizo yoyote ya kina cha maji kupungua na mitambo ya gesi kuharibika, kama kuna sherehe inaendelea ambayo wafanyakazi wa TANESCO hawakupata mwaliko, umeme unakatwa.

Habari za kuaminika ni kwamba pamoja na matatizo ya kina cha maji kupungua na ukweli tunaoujua kwamba baada ya Mwalimu Nyerere, hakuna serikali iliyofanya uwekezaji kwenye sekta ya umeme, matatizo mengi ya umeme; mgawo na umeme kukatika ovyo ovyo ni hujuma. Ni wazi mitambo ni ya zamani na mfumo mzima wa umeme umechoka; bila ukarabati na kuwekeza ni lazima tupate matatizo ya umeme. Wataalamu wanakubali kuna tatizo, lani si kubwa hivyo kiasi cha kukata umeme wakati mdahalo unaendelea na wakati watu wanasherehekea miaka hamsini ya uhuru wao. Mbaya zaidi ni kwamba umeme unazimwa na kuwashwa kisiasa. Mshabiki wa hoja ya serikali mbili, kama ana uwezo wa kuifikia mitambo ya TANESCO, anaweza kuizima ili mjadala wa serikali tatu usisike! Hii ni hatari maana kuwasha na kuzima umeme bila tahadhari inaleta uharibifu na wakati mwingine kupoteza maisha ya watu mfano umeme ukizimika wakati  upasuaji, hospitali zina genereta za dharura, lakini Tanzania hii usishangae genereta ikakosa mafuta!


Tanzania tuitakayo ni ya watu wanaowajibika. Wahuni wanaozima umeme ili kuzima hoja za wapinzani, wanaozima umeme ili kuhujumu uchumi na kuangusha utendaji wa serikali iliyo madarakani, hatuwataki na kusema ukweli hawawezi kutufikisha mbali.

Tukubali tusikubali, tutaijenga Tanzania kwa majadiliano, kuvumiliana na kusikiliza hoja tofauti. Umefika wakati wa kukubali maamuzi ya wengi. Kule nyuma, watu wachache wangeweza kufanya maamuzi kwa niaba ya taifa zima. Mfumo huu sasa umepitwa na wakati. Karne hii ya demokrasia, utandawazi na maendeleo ya kasi ya tekinolojia, hakuna tena maamuzi ya mtu mmoja. Watanzania wakitaka serikali tatu, ni lazima itakuwa hivyo hata ukifanyika uhuni wa kuzima umeme ili kuzuia midahalo. Kama ni lazima kuwa na serikali mbili au moja, basi hoja ijengwe na watu waikubali.

Na,
Padri Privatus Karugendo
+255 754  633122

0 comments:

Post a Comment