MIAKA HAMSINI YA KUPAMBANA NA MFUMO DUME.

Makala hii ni mwendeleo wa makala iliyopita iliyo beba kichwa cha habari “ Miaka 50 ya uhuru, ni historia yetu sote”. Ni wazi ndani ya miaka hamsini tumefanya mengi kama taifa. Hakuna anayeweza kutubeza kwamba hatukufanya kitu. Wachambuzi wengine wataelezea hatua tulizopiga katika mambo mbali mbali, na kwa upande wangu nitajikita kuchambua hatua tuliyoifikia katika masuala ya jinsia na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi.

Katika makala iliyopita tulielezea jinsi mfumo dume ulivyodumaa wakati wa kupigania uhuru na kufufuka tena  baada ya uhuru. Tulitoa mfano wa majina mengi ya wanawake waliopigania uhuru wa taifa letu, ingawa hadi leo hii majina haya yamesahaulika. Ukweli unabaki kwamba wakati wa kupigania uhuru wawawake walipigana bega kwa bega na wanaume. Hivyo tunaweza kusema kwamba miaka hamsini ya uhuru wetu imekuwa ni miaka ya mapambano; kupambana na umaskini wa kifikra na kipato, kupambana na maadui wa nje na ndani ya taifa letu na juu ya mada hii tuliyo nayo ya Ukombozi wa mwanamke kimapinduzi yamekuwa ni mapambano ya mfumo dume.

Imeelezwa vizuri katika kitabu cha Wanawake wa TANU, kwamba mfumo dume ulifufuka kwa nguvu zote pale aliyekuwa Waziri wa wa  Maendeleo ya Jamii, Bwana Mgonja alipotoa ushauri kwamba baada ya kupigania uhuru wanawake warudi jikoni na kuendelea kufanya kazi ya kuwalea watoto: “Akizungumza kwenye mkutano siku ya pili, Waziri wa Maendeleo ya jamii, Bwana Mgonja, alizungumza katika njia iliyofifisha ari ya siasa kwa wanawake na kuimarisha mamlaka ya serikali. Wakati wa kitengo cha wanawake kilikuwa kinahamasisha wanawake wajiunge katika harakati za kujenga taifa, Mgonja aliwaambia wanawake kwamba wakilea watoto watakuwa wamelea taifa zima. Aliwasifu wawake kwa juhudi zao katika kupigania huru lakini kwa sasa walichotakiwa kufanya ni kulima, kufuga kuku, kuchimba visima na kupanda miti…”

Na kusema kweli wanawake wakarudishwa jikoni na mbaya zaidi hata historia ikafutika. Wanawake waliopigania uhuru kwa nguvu zote wakatupwa pembeni. Wanaume wakateuliwa kwenye uongozi ngazi mbali mbali na wanawake wakaendelea kulea watoto, kulima na kuchota maji. Mbali na dhambi kubwa ya kufukia vipaji, tunaendelea kutafunwa  kwa nguvu zote na ile dhambi ya wanaume ya uchu wa madaraka.

Katika kitabu hiki cha Wanawake wa TANU, ananukuliwa Bibi Titi, akilalamika juu ya hatua hii iliyochukuliwa na serikali ya taifa huru kufanya uamuzi wa kuwarudisha jikoni wanawake waliopambana  na wanaume bega kwa bega kuleta uhuru: “ Wakawakusanya wanawake pamoja na kuwafundisha usafi, upishi, malezi ya watoto…. Elimu ya watu wazi na ususi…. Vitu vyote hivi havikuwepo katika Kitengo cha Wanawake  cha TANU. Hatukuwa na muda wa kufanya vitu hivi..” kwa maneno haya ya Bibi Titi, ina maana kwamba wakati wa kupigania uhuru wanawake walifanya kazi sawa na zile za wanaume.

Wanawake walishiriki mapambano ya kuleta uhuru si kwa kutafuta madaraka na fedha, bali walikuwa wakitafuta maisha bora ya watoto wao na vizazi vijavyo kama anavyonukuliwa akisema Mwamvita kwenye kitabu cha Wanawake wa TANU: “ Tulikuwa tunatafuta maisha bora ya baadaye kwa watoto wetu na tulitaka uhuru, uhuru wa kuamua tulichotaka…. Tulitarajia uhuru ulete amani…. Usawa, tuwe pamoja na tuishi kwa amani. Hatukutarajia kupata fedha. Hata kama sio matajiri, hatuna nyumba kubwa, tunapaswa kuwa na umoja na tuheshimiane…”

Pendekezo la Mgonja, la kuwarudisha wanawake jikoni lilishika mizizi. Hadi leo hii tunashuhudia chama cha CCM, kilichotokana na TANU, uongozi wake wa juu ni wanaume watupu. Hata nafasi za juu za uongozi serikalini zimeshikiliwa na wanaume, kwa maana ya Rais, Makamu wa Rais na waziri mkuu. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka hamsini ya uhuru wa taifa letu tumempata spika mwanamke kutokana na mizengwe ya kisiasa na wala si kwa nia ya dhati. Lakini hata chama kama vile CHADEMA ambacho tunakichukulia kuwa ni chama cha kimapinduzi uongozi wake wa juu kitaifa ni wanaume watupu! tulishuhudia juzi wakati chama hiki kinafanya majadiliano na Rais Jakaya Kikwete juu ya muswada wa Katiba mpya, ujumbe wao ulikuwa ni wanaume watupu! Chama hiki kina wanawake wenye uwezo mkubwa, lakini kwenye ujumbe wa kujadili mambo mazito ya taifa letu wanawake hawa hawakuonekana. Ni wazi walimezwa na mfumo dume!

Wanawake wamesukumwa nje ya vyombo vya kufanya maamuzi na kutunga sera. Labda ndo maana inashangaza kwamba pamoja na Tanzania kupiga hatua kubwa katika mambo ya teknolojia, bado wanawake wanabeba maji na kuni vichwani, wanatumia jembe la mkono, wanasafiri mwendo mrefu kwa miguu kwenda hospitali na wengine wanafia njiani.

Watu binafsi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wamekuwa wakipambana na mfumo huu dume ulio chipuka kwa nguvu zote mara tu baada ya uhuru wetu. Mashirika kama TGNP na FEMACT yamekuwa mstari wa mbele kupambana na mfumo dume. Mapambano yenyewe yanalenga kutoa fursa sawa za kijinsia, kutoa haki sawa kwa wanaume na wanawake kwa kuwapa nafasi sawa za kupata na kumiliki rasilimali (kiuzalishaji/kiuchumi na -kijamii), na ku kushiriki katika maamuzi na kupata huduma za msingi. Usawa wa kijinsia unamaanisha kuwa mtu anapata haki na fursa mbalimbali kwa kuwa ni binadamu na sio kwa kuwa ni mwanaume au mwanamke. Usawa wa kijinsia pia ni pamoja na kurekebisha ubaguzi utokanao na tabaka/ hali ya kiuchumi, rangi na kabila, mambo ambayo pia yanaweza kuongeza mahusiano yasiyo sawa ya kijinsia.

Tunapoangalia mchango wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na hasa haya yanayoshughulikia usawa wa kijinsia na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi ndani ya miaka hamsini ya uhuru wetu, hatuwezi kuacha kulitaja  hili la kupambana na mfumo dume. Watu wote niliowahoji juu ya suala hili na hasa wale waanzilishi wa mashirika ya mashirika ya kutetea usawa wa kijinsia na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi walilitaja hili la mfumo dume. Ni wazi yako mengi kama jitihada za kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wanaoishi pembezoni ambao idadi yao kubwa ni wanawake, kuzuia ukatili wa kijinsia kama vile ukeketaji, ubakaji na ndoa za utotoni. Hata hivyo yote haya yanasimamiwa na mfumo dume.

Changamoto kubwa ni nani anaongoza mapambo haya ya mfumo dume na kwa faida ya nani? Agenda hii ya kuuondoa mfumo dume iko wazi kwa wapambanaji wote? Ni agenda inayotokana na hitaji la jamii yenyewe au ni agenda inayoshinikizwa  na nguvu nyingine za ndani na nje ya nchi?

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment