MIAKA HAMSINI YA UHURU
WETU NI HISTORIA YA WATANZANIA WOTE.
Tunaposherehekea miaka
hamsini ya uhuru wetu ni wakati mzuri wa kuwakumbuka mashujaa waliopigania
uhuru wa taifa letu na ni muhimu pia kuwakumbuka wale wote waliochangia
maendeleo ya taifa letu mara baada ya uhuru hadi leo hii. Kumekuwepo na
michango mingi ya watu binafsi, mashirika ya dini na mashirika yasiyokuwa
kiserikali. Wote hao wamekuwa wakichangia kuijenga Tanzania yetu. Kwa maana
hiyo basi historia hii ya miaka hamsini ya uhuru wetu ni mradi wa pamoja
uliotekelezwa na watanzania wote na utaendelea kutekelezwa na watanzania wote
miaka mingine hamsini na kuendelea.
Ingawa uhuru wetu ni
mradi wa pamoja ni vyema kutambua mchango wa makundi mbali mbali. Katika makala
hii na nyingine zitakazofuata nitajadili mchango wa harakati wa mashirika
yanayotetea usawa wa jinsia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika kipindi
cha miaka hamsini ya uhuru wetu.
Mashirika haya yamefanya
mambo mengi ya kutetea haki za binadamu, usawa wa jinsia na ukombozi wa
mwanamke kama tutakavyoshuhudia kwenye makala hizi: Mfano kusaidia kuiweka
sahihi historia ya taifa letu. Tumekuwa tukisikia majina ya wanaume bila
kutajwa wanawake katika historia ya kupigania uhuru wa taifa letu lakini kwa
kazi iliyofanywa na TGNP ( Mtandao wa Jinsia Tanzania) wa kutafsiri katika
lugha ya Kiswahili utafiti wa Susan Geiger juu ya Wanawake wa TANU, na
kuhakikisha kitabu hiki kinasambazwa na kusomwa na wengi, kumeleta mwanga mpya
wa ukweli wa Wanawake kushiriki kikamilifu katika kupigania uhuru wa taifa
letu. Huu ni mchango mkubwa wa TGNP ambao inawezekana hata na wao hawautambui
maana daima tunaelekeza nguvu zetu kwa mambo makubwa ya dunia hii na kusahau
maisha ya siku kwa siku yanayotuzunguka. Baada ya uhuru mfumo dume ulishika
hatamu, historia ya wanawake waliopigania uhuru ikasahaulika na kufunikwa.
Marehemu Susan Geiger ni
msomi mwanaharakati ambaye alifundisha masomo ya Kiafrika na yale ya Jinsia
katika Chuo Kikuu cha Minnesota/Twin Cities, huko Marekani kwa muda wa miaka
mingi. Alikuja Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa mwalimu wa kujitolea katika
miaka ya 1960. Baadaye aliendelea kurudi katika nyakati tofauti katika kipindi
chote cha maisha yake.
Kazi yake kubwa ya utafiti
ilikuwa juu ya historia ya uchifu wa Wachagga. Utafiti huo ndio uliokuwa
chimbuko la kujipatia Shahada ya Udaktari wa Falsafa. Baada ya hapo alifanya
utafiti mwingine wa makusanyo ya wanawake wanaharakati wapigania uhuru. Susan
alikuwa mwanaharakati aliyejitolea kwa michango ya hali na mali hadi mwisho wa
maisha yake. Alitoa mchango mkubwa kwa wanamtandao wa masuala ya jinsia hapa
nchini ili waweze kuendeleza shughuli zao.
Utafiti wake juu ya
Wanawake wa TANU, uliibua mengi yaliyokuwa yamefunikwa. Mbali na Bibi Titi
Mohamed, mwanamke anayetajwa kwa mbali katika harakati za kupigania uhuru wa
taifa letu, kuna majina ya wanawake wengi waliojulikana kama “Wanawake wa TANU”
waliopigana kufa na kupona kulikomboa taifa letu. Kufuatana na ushuhuda wa Wanawake
wa TANU, ni kwamba chama hiki kilisimikwa na Wanawake, kama alivyonukuliwa Bi
Mashavu binti Kabonge kutoka Tabora:
“ Nikwambie
ukweli, wanawake ndio walioleta TANU. Ukweli ni kwamba wanawake ndio waliofanya
hivyo. Wanaume wengi waliogopa kufukuzwa kazi. Waliambiwa na waajiri wao kwamba
yeyote atakayejiunga na TANU atafukuzwa mara moja…. Lakini wanawake walikuwa
mashabiki wa nguvu wa TANu na wengine waliachika kwa sababu ya sushuli zao za
siasa”
Mashavu binti Kabonge,
ni kati ya wanaharakati wanawake wa Dar-es-Salaam, waliopigana kufa na kupona
kuleta uhuru wa taifa letu, lakini hawatajwi wala kukumbukwa. Hivyo
tunaposherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu kwa vile TGNP imetusaidia
kuyafufua baadhi ya majina ya wapigani uhuru hawa ni bora kuwakumbuka na kuwaenzi.
Pia ni wakati kuendeleza mapambo ya mfumo dume ambao ni hatari kwa mambo mengi
hadi kuifuta historia. Ni wazi majina ya wanawake hawa waliopigania uhuru wa
taifa letu yamefunikwa na mfumo dume! Hakuna maelezo mengine!
Mbali na Mashavu binti
Kabonge, kuna majina mengine mengi ya wanaharakati wanawake wa Dar-es-Salaam:
Tatu Binti Mzee, pamoja na Bibi Titi Mohamed,Tatu Binti Mzee alikuwa mmoja wa
wajumbe wanawake wa kwanza katika chombo muhimu cha maamuzi, yaani, kamati Kuu
ya Chama.
Halima Hamisi, huyu naye
ni mpambanaji wa kuleta uhuru, katika utafiti wa Susan, ananukuliwa akisema “ Tulitembea
kwa miguu siku nzima bila chakula. Ukichukua chai nyumbani na ukijaliwa kupata
karanga, unanunua. Wakati mwingine tuliweza kupata fedha za chakula kutoka ofisi
ya TANU, lakini ilibidi wapige hesabu
kwa makini….”
Wanawake wengine wa
Dar-es-Salaam, walioshiriki harakati za kuleta uhuru na majina yao yamefunikwa
na historia ni: Salima Ferouz, Binti Kipara, Mwasaburi Ali, Fatuma Abdallah na
wengine wengi ambao watafufuliwa na
tafiti nyingine zitakazofanyika kwa kuchochewa na hii ya Susan.
Katika utafiti wa Susan,
Salima Ferouz, ananukuliwa akisema: “ Sisi wanawake tulikuwa na nguvu…
tuliongoza njia kwa sababu ya uonevu wa watoto wetu na jinsi tulivyowekwa ndani…
tulifanya kazi pamoja, tukajiunga na Kitengo cha wanawake na kutumikia TANU,
tukichangisha fedha na kuwahamasisha wengine wengi wajiunge..”
Hata mikoani kulikuwa na
wanawake walioshiriki harakati za ukombozi wa taifa letu. Kule Kilimanjaro
kulikuwa na Halima Selengia Kinabo, Mwamvita Salim, Zainab Hatibu, Morio
Kinabo, Violet Njiro, Elizabeth Gupta, Kanasia Tade Mtenga,Natujwa Daniel
Mashamba na Lucy Lameck.
Hata kule Mwanza
kulikuwa na wanaharakati wanawake waliopigania uhuru wa taifa letu, lakini historia
haiwakumbuki tena. Wanawake hao ni:
Agnes Sahani, Aziza Lucas, Tunu Nyembo, Halima Ntungi, Mwajuma Msafiri, Pili
Juma, Mwamvua Kibonge, Zuhura Mussa na Chausiku Mzee.
Ni wazi wako wanawake
wengine wengi walioshiriki harakati za kuleta uhuru wa taifa letu, ni kazi ya
Mashirika yanayotetea usawa wa jinsia na ukombozi wa mwanamke kwa kushirikiana
na watanzania wanaopenda kuweka kumbukumbu sahihi kuendeleza utafiti na kuibua
majina mengine ya wanaharakati wote walioshiriki kuleta uhuru wa taifa letu. Tusitake
kusherehekea kwa kuimba, kunywa na kucheza bila kuiandika historia sahihi ya
taifa letu.
Ni lazima tujiulize
tumeteleza wapi? Kama huko nyuma
tuliweza kuendesha harambee ya kuchangia harakati za mapambano, shughuli zote
zikaendelea bila misaada ya kutoka nje. Mapato yote ya nchi yakiwa mikononi mwa
mkoloni. Inakuwaje sasa wakati tumeshika mapato ya nchi mikononi mwetu,
tunaendelea kuomba misaada ya kujenga vyoo na vyandarua? Uwezo wa kujitegemea
uliokuwa miongoni mwa wananchi wakati wa kupigania uhuru umekwenda wapi?
Tulipigania uhuru wa kisiasa, ili
tupoteze uhuru wa kujitegemea na kujiamulia mambo yetu wenyewe? Ukipokea
misaada, ni vigumu kukwepa masharti yake!
Makala hii ni mwanzo mzuri wa kuangalia mchango wa
Mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali yanayoshughulikia usawa wa jinsia na
ukombozi wa mwanamke. Swali la kujiuliza ni je, kama Wanawake walikuwa mstari
wa mbele wakati wa kupigania uhuru wetu, ilitokea nini wakawa mstari wa nyuma
baada ya uhuru? Wanawake walichangisha fedha za kuendesha mapambano, walifanya
kazi kwa nguvu kupata fedha, walipika maandazi na wengine walifanya kazi za
kujidhalilisha ili wapate fedha za kukiendesha chama cha TANU. Mapambano ya
kuleta uhuru hayakutegemea misaada kutoka nje. Uwezo mkubwa wa kujitegemea
ulioongozwa na wanawake ulikwenda wapi baada ya uhuru kufikia hatua ya kutafuta
fedha kutoka nje ili kuendesha “ Miradi” ya kuwakomboa wanawake wa taifa letu?
Ni lazima kutafakari kwa kina wakati tukisherehekea miaka Hamsini ya taifa
letu.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment