MIAKA HAMSINI YA UHURU MAPAMBANO BADO YANAENDELEA!


Miaka hamsini ya Uhuru wetu, mapambano bado yanaendelea! Kutimiza hamsini ndo mwanzo wa maandalizi ya hamsini mingine. Ndani ya miaka hamsini tumetekeleza mengi na bado kuna mengine mengi ya kutekeleza. Wachambuzi wa masuala ya kijamii wamejitahidi kuchambua nyanja mbali mbali. Binafsi nimejikita katika suala la usawa kijinsia na haki za wanawake; mchango, mafanikio na changamoto ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ndani ya miaka hamsini ya uhuru wetu.

Makala iliyopita tulielezea jinsi Wanawake walivyopambana bega kwa bega na wanaume kuleta uhuru wa taifa letu. Wakati wa harakati za uhuru mfumo dume ulidumaa; Na kwamba baada ya uhuru baadhi ya wanaume walishauri wanawake warudi jikoni na kufanya kazi ya kulea watoto na kuchimba visima. Pendekezo la Mgonja, la kuwarudisha wanawake jikoni lilishika mizizi. Hadi leo hii tunashuhudia chama cha CCM, kilichotokana na TANU, uongozi wake wa juu ni wanaume watupu. Hata nafasi za juu za uongozi serikalini zimeshikiliwa na wanaume, kwa maana ya Rais, Makamu wa Rais na waziri mkuu. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka hamsini ya uhuru wa taifa letu tumempata spika mwanamke kutokana na mizengwe ya kisiasa na wala si kwa nia ya dhati. Lakini hata chama kama vile CHADEMA ambacho tunakichukulia kuwa ni chama cha kimapinduzi uongozi wake wa juu kitaifa ni wanaume watupu! tulishuhudia juzi wakati chama hiki kinafanya majadiliano na Rais Jakaya Kikwete juu ya muswada wa Katiba mpya, ujumbe wao ulikuwa ni wanaume watupu! Chama hiki kina wanawake wenye uwezo mkubwa, lakini kwenye ujumbe wa kujadili mambo mazito ya taifa letu wanawake hawa hawakuonekana. Ni wazi walimezwa na mfumo dume!

Kwa kifupi tunaweza kusema ni miaka hamsini ya kupambana na mfumo dume. Mfumo uliojengwa juu ya tamaduni na mila zetu na kuendelezwa na dini za kigeni zilizokuwa pia zimesukwa na mfumo dume kiasi cha mfumo huu kuzagaa kiasi cha kutisha na kuambukiza kila kiumbe. Kama kuna mapinduzi ya kufanya katika karne hii ni kuupindua mfumo dume na kutengeneza mfumo wenye kuzingatia usawa wa kijinsia.

Pamoja na mwanamke kuambiwa akae jikoni, mazingira yanayomzunguka yaliendelea kuwa ya duni. Kulima kwa jembe la mkono, kuchota maji kichwani, kuchanja kuni na kuzibeba kichwani. Wanawake wapatao 578 hufa kwa kila vizazi 100,000 (utafiti uliofanyika mwaka 2004). Kati ya mwaka 2003 na 2004, wawake 16,000 walikufa kutokana na matatizo yaliyohusiana na ujauzito au kujifungua. Pia, kati ya wawawake 150,000 na 450,000 walipata ulemavu uliosababishwa na matatizo yaliyojitokeza wakati wa kujifungua. Kwa nini hali inakuwa hivi? Ukweli  ni kwamba, wanawake wanne tu kati ya kumi ndio wanaohudumiwa na wakunga waliosomea kazi hiyo. Hii ni mojawapo ya sababu za kuwepo kwa vifo hivyo.

Viwango vya maambukizi mapya ya VVU vinaonyesha kwamba wanawake wako kwenye hatari ya kuambukizwa kuliko wanaume. Imegundulika vilevile kuwa, wasichana wenye umri mdogo na wawawake wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa kutokana na kukandamizwa kiuchumi, kijamii na kimahusiano ya ngono.

Pamoja na mpango huu hasi( wa kuwarudisha wanawake jikoni) juu ya wanawake mapambano yamekuwa yakiendelea kutetea na kulinda haki za wanawake. Mapambano yenyewe yanalenga kutoa fursa sawa za kijinsia, kutoa haki sawa kwa wanaume na wanawake kwa kuwapa nafasi sawa za kupata na kumiliki rasilimali (kiuzalishaji/kiuchumi na -kijamii), na ku kushiriki katika maamuzi na kupata huduma za msingi. Usawa wa kijinsia unamaanisha kuwa mtu anapata haki na fursa mbalimbali kwa kuwa ni binadamu na sio kwa kuwa ni mwanaume au mwanamke. Usawa wa kijinsia pia ni pamoja na kurekebisha ubaguzi utokanao na tabaka/ hali ya kiuchumi, rangi na kabila, mambo ambayo pia yanaweza kuongeza mahusiano yasiyo sawa ya kijinsia.

Watu binafsi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na wakati mwingine hata serikali yenyewe wamekuwa wakijitokeza kuendeleza mapambano ya kutetea usawa wa jinsia kutokana na mashinikizo ya ndani na nje ya nchi. Pia mabadiliko yanayotokea katika dunia yetu ya leo; utandawazi, soko huria na ubeberu unaoingia kwa kasi na kuzivuruga nchi changa, imechochea harakati hizi za kutetea na kulinda haki za wanawake na usawa wa jinsia.
Na hapa ndipo kuna changamoto, maana  bila uangalifu wa kuzingatia agenda ya msingi kuna hatari kutekeleza matakwa ya watu wengine. Mapambano haya ya usawa jinsia yanaambatana na msaada wa kifedha na mara nyingi hakuna uhuru wa kutosha wa wahusika kujiamulia yale wanayoyataka na kuyaamini. Ingawa Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali hapa Tanzania yamefanya kazi kubwa ya kuhamasisha na kuwaelimisha watanzania kuhusu haki zao za msingi na hasa suala zima la usawa wa jinsia, swali ni je ni kiasi gani hitaji hili la uswa wa kijinsia linatokana na watu wanywewe? Je usawa wa jinsia ndicho kipaumbele cha Mtanzania?

Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inazingatia misingi ya haki na usawa; ingawa ni katika marekebisho yaliyofanyika mwaka 2000 ndipo ubaguzi wa jinsia umetajwa waziwazi kuwa haukubaliki kwa mujibu wa katiba. Kimsingi, katiba yetu inatambua haki ya usawa mbele ya sheria kwa kila mwananchi bila kujali tabaka, nasaba wala jinsia. Vile vile, katiba ya nchi inatambua haki ya kila mtu (wake kwa waume) ya utu wake kuheshimiwa na kuthaminiwa bila ubaguzi wa aina yoyote, uwe wa wazi au wa kificho, haki na uhuru wa kuishi kwa usalama kupata na kumiliki mali na rasilimali za uzalishaji, kufanya kazi na kupata ujira wa haki kwa kazi yake, kupata fursa ya kujielimisha kwa kadri ya uwezo wake, kushiriki katika masuala yote ya -kijamii, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika uongozi na ufanyaji wa maamuzi; na kufaidika na huduma za jamii ka ajili ya maendeleo yake.

Msimamo wa Tanzania katika usawa wa kijinsia inaonyeshwa wazi katika Katiba na uwekaji sahihi na uridhiaji wa mikataba mikuu ya kimataifa inayolenga kuimarisha usawa wa kijinsia na haki za binadamu. Tanzania imeweka sahihi na kuridhia mikataba ifuatayo: Azimio la Haki za Binadamu (1948); Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuondoa Aina zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake(CEDAW,1979); Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (CRC,1989), ambao una sehemu mahsusi ya Mtoto wa Kike; makubaliano ya Beijing (1995) hususani katika uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kisiasa, elimu na mafunzo; Azimio la Vienna la Haki za Binadamu (1994), Azimio la Dunia la Malengo ya Milenia (MDGs,2000) ambapo MDG-3 linahusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Katika ngazi ya kanda, Tanzania imeweka sahihi au imeridhia Mkataba wa Muungano wa Afrika na  itifaki yake ya Haki za Binadamu na watu; Mkataba wa Haki za wanawake katika Afrika (Maputo,2003); Azimio la jinsia la SADC(1997) na nyongeza yake juu ya ukingaji wa dhuluma dhidi ya wanawake na watoto wa kusini mwa Afrika (1998); na Itifaki ya SADC juu ya jinsia na Maendeleo(2008).

Ingawa harakati za kumkomboa mwanamke hapa Tanzania zinajikongoja ni kwamba mambo mengi yametendeka na mapambano yamekuwa yakiendelea. Tafiti nyingi zinazofanywa juu ya masuala ya kijinsia na haki za wawake Tanzania inatajwa kufanya vizuri zaidi ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara. Kwa ushawishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayojishughulisha na jinsia na utetezi wa haki za wanawake kimapinduzi Tanzania imepitisha sheria tatu za kitaifa ambazo zinaimarisha uamuzi wake wa kutekeleza maazimio ya CEDAW. Sheria hizi ni pamoja na sheria ya makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya 1998, Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na sheria ya  Ardhi ya vijiji ya mwaka 1999. Pamoja na hayo, sheria hizo zote zinatoa minya ya kuendelea kwa sheria za kimila ambazo baadhi yake zinawabagua wanawake. Na pia haki ya wawake na wanaume kumiliki ardhi ya kijiji au jumuiya imeporwa na kuwekwa chini ya mamlaka ya juu ya serikali, yaani Rais, badala ya kuwa chini ya ngazi ya uwakilishi ya dola, yaani Bunge na Mkutano wa kijiji, kama jumuiya nyingi za kiraia zinavyosisitiza iwe.

Mbali na kushiriki kupitisha sheria hizi mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayojishughulisha na jinsia na ukombozi wa mwanamke yamekuwa yakitoa misaada katika nyanja mbali mbali. TGNP, FEMACT,TAMWA,WLAC, wamekuwa na sauti ya pamoja ya kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wawake walioko pembezoni. Mashirika haya yamekuwa yakifanya uchambuzi wa sera, mipango na bajeti kwa mrengo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi kuanzia ngazi ya serikali za mitaa. Pia mashirika haya yamekuwa mstari wa mbele kufuatilia mgawanyo wa matumizi ya rasilimali zote ikiwemo bajeti ya elimu, afya, maji, kilimo, ajira nk, kwenye serikali za mitaa. Pia yamekuwa yakitoa  Ilani ya uchaguzi. Mfano ilani ya uchaguzi ya mwaka 2000: “Sauti ya wapiga Kura, Haki na Usawa wa Kijinsia”. Pia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005. Hizi zote ni jitihada za mashirika yasiyokuwa kiserikali yanayojishughulisha na jinsia kutaka kuleta mabadiliko katika usawa wa kijinsia.

Mila potovu kama vile ukeketaji, ambazo zilikuwa zikimkandamiza mwanamke hata kufikia kumsababishia ulemavu zimepigwa vita, ingawa tatizo hili halijamalizika kabisa, lakini mashirika kama TAMWA, na Kituo cha Haki za Binadamu yamefanya kazi nzuri na bado yanaendelea kuelimisha jamii juu ya mila hii potovu. Sheria kandamizi zinapigwa vita na ushawishi unajengwa ndani ya jamii ili kuwa na sheria nzuri zinazozingatia usawa wa Kijinsia.

Mashirika haya yamejenga sauti ya pamoja na kwa njia hii huduma nyingi zinapatikana. Wanawake wanapata huduma ya sheria na kujengewa uwezo wa kuzitambua haki zao. Majukwaa ya majadiliano yanayoandaliwa na mashirika haya yametoa matunda; watu wamepata nafasi ya kutoa mawazo yao juu ya maswala mbali mbali kama vile mjadala juu ya  bajeti, katiba mpya, muungano na mambo mengine ya -kijamii. Lengo likiwa ni kuleta usawa wa kijinsia kufika hamsini kwa hamsini katika ngazi zote za maamuzi.

Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122.

0 comments:

Post a Comment