MIAKA 35, CCM IMESHUGHULIKIA MAMBO YA MSINGI? CCM wanasherehekea miaka 35, ya kuwepo kwao. Miaka hii ni mingi kwa chama kilicho madarakani. Hivyo sherehe zao ni lazima ziwe ni za tathimini na wananchi waruhusiwe kuwahoji yale waliyoyafanya kwa kipindi hiki; je wamefanikiwa kushughulikia mambo ya msingi? Washerehekee kwa kuonyesha mafanikio na changamoto. Ule mtindo wa kutengeneza kadi za vyama vya upinzani na kuzisambaza kwa watu mbali mbali ili siku ya kilele cha sherehe wasimame mbele ya mgeni rasmi na kurudisha kazi za upinzani kwa mamia, umepitwa na wakati. Mafanikio ya chama hayapimwi kwa kukomba idadi kubwa ya wapinzani, bali kinapimwa kwa sera, itikadi na uwezo wake wa kushughulikia mambo ya msingi. Chama kinaweza kuwa na idadi ndogo ya wanachama, lakini kina uwezo mkubwa wa kutekeleza mambo ya msingi zaidi ya chama chenye mamilioni ya wanachama. Muhimu si wingi wa wanachama bali ni utekelezaji. Juzi tumemaliza kusherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu na sasa CCM, chama ambacho kimekuwa madarakani wakati wote, kinasherehekea miaka 35 na bado Tanzania inahesabika katika nchi masikini duniani. Kwa nini hili limetokea? Kwa nini tumeshindwa kukimbia wakati wenzetu wakitembea? Baadhi ya nchi zilizokuwa na hali kama yetu wakati tukipata uhuru, sasa hivi zimepiga hatua kubwa katika maendeleo. Sisi tumepotelea wapi? Labda ni kwa vile CCM na serikali yake hawajayashughulikia mambo ya msingi? Ingawa ni jukumu la watanzania wote kujiuliza kilichotokea, hatuwezi kukwepa kuwahoji kwa namna ya pekee CCM, maana hawa ndo watunga sera, miongozo, itikadi na mwelekeo wa taifa letu kwa miaka yote hii. Ni lazima watoe jibu vinginevyo ni wakati wa kuwatosa! Kwa miaka yote hii walishughulikia vitu vya msingi? Au wamekuwa wakikijenga chama chao, familia zao na matumbo yao? Inaweza ikawastaajabisha baadhi kusikia kuwa tufanye vitu vya msingi kwanza sasa hivi wakati ambapo taifa letu lina miaka hamsini ya uhuru na chama tawala kinasherehekea miaka 35. Baadhi wanaweza kufikiri kuwa tumeshachelewa. Bado kuna nafasi kubwa kuangalia tulipo sasa miaka hamsini baada ya uhuru na kurekebisha sehemu muhimu ili kuwawezesha watanzania kuwa na “kesho bora”. Marekebisho hayo ni pamoja na CCM kujisafisha na kuzaliwa upya na hata ikiwezekana kutoswa! Wakisherehekea kwa mtindo wa kizamani wa kula, kunywa, kucheza na kutamba kwamba wao ni nambari moja na CCM ina wenyewe, dawa yao itakuwa jikoni ikichemshwa! Wakisherehekea kwa kufanya tathimini wanaweza kuleta nuru mpya au kupata heshima ya kuongoza kambi ya upinzani bungeni. Mambo ya msingi ninayoyazungumzia na yanayotakiwa kutiliwa mkazo kwa sasa ni: afya, elimu, kilimo, miundo mbinu, kubana matumizi ya serikali na pengine kuacha matumizi ambayo si ya lazima kwa wakati huu tunaojaribu kufanya mambo ya msingi kwanza. CCM wanaposherehekea miaka 35, hali ya afya iko vipi katika Taifa letu, hali ya elimu iko je, Kilimo tumefikia wapi? Tunawaendeleza wakulima wetu, au tunayakaribisha makampuni ya kibeberu kuja kulima chakula na mazao ya mafuta kwa ajili ya nchi zao? Miundo mbinu ya vijijini imeboreshwa kiasi gani? Ni muhimu kusafiri kwa taxi kutoka Mtukula hadi Songea, lakini pia ni muhimu kuhakikisha mazao ya wakulima yanasombwa kutoka vijijini kwenda kwenye masoko. Tukianza na afya, haihitaji fizikia ya roketi kufahamu kwamba wananchi wenye afya watafanya kazi kwa nguvu zao zote ili kuongeza tija na hatimaye pato la taifa. Kinyume chake ni maafa. Ni muhimu kwa serikali ya Awamu ya Nne kuweka kipaumbele na kufanya jitihada za makusudi kuboresha huduma za afya kwa wananchi si tu kwa kujenga majengo mengi ya hospitali, bali pia kuboresha mazingira ya watumishi wake na upatikanaji wa dawa. Pia kudhibiti baadhi ya magonjwa yanayozuilika (kama kipindupindu n.k) ni jambo la lazima sana. Kuna mpango wa kujenga vituo vya afya kila kata na zahanati kila kijiji. Hili ni jambo zuri, lakini mzigo wasibebeshwe wananchi masikini wakati taifa letu lina utajiri mwingi na pesa nyingi zinaelekezwa kwa mambo yasiyokuwa ya msingi. Inasikitisha kuona kuwa sekta ya afya ni mgogoro mpaka sasa. Huduma za kinga zinatakiwa ziwe ni kipaumbele ili kuweza kuzuia magonjwa yanayozuilika ambayo yakishafumuka hutumia mamilioni kwa ajili ya tiba. Tumeona mfano wa Homa ya bonde la ufa. Ninapozungumzia kinga hapa simaanishi uchapishaji wa fulana na kofia na maadhimisho ya siku za Malaria na Kifua Kikuu. Ninamaanisha elimu ya kinga itakayomwezesha mtu kujua namna ya kujikinga na Kipindupindu kwa mfano. Tumesema tufanye ya msingi kwanza. Tuache kuitisha warsha, semina na makongamano kwa watu ambao wana uelewa wa kinga tayari. Nguvu ielekezwe Buguruni ambapo kila mwaka kunatokea mlipuko wa kipindupindu. Nguvu zielekezwe vijijini ambako magonjwa kama homa ya bonde la ufa yanawashambulia wananchi bila taarifa yoyote. Tukiweza kupanua huduma za kinga kikamilifu, hakuna shaka yoyote kwamba gharama za matibabu zitapungua. Magonjwa yanayotukabili mengi ni ya umasikini yanayohitaji walengwa kuelimishwa kidogo tu juu ya njia sahihi za kujikinga nayo, lakini si kwa kuvaa fulana na kofia. Tukiweza kuimarisha kinga tutaondokana na aibu hii ya mfumuko wa kipindupindu kwa jiji la Dar-es-Salaam kila mwaka. Ni lazima pia jitihada ziendelezwe kupambana na malaria. Tusingoje watu wapate malaria ndio watibiwe. Tuangamize Mbu. Hili linawezekana, kama tukilipatia kipaumbele. Lakini pia madaktari wetu tuwathamini na kuhakikisha wana mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Wawe na vifaa vya kisasa na maisha ya familia zao yawe mazuri. Daktari ambaye hana usafiri, hana nyumba, familia yake haina sukari, chakula cha kutosha na karo ya kumsomesha mtoto kwenye shule bora, hawezi kutulia kazini na kuwahudumia wagonjwa ipasavyo. Mawazo yakimzidi anaweza kusababisha vifo wakati wa upasuaji. Mgomo wa madaktari unaoendelea hivi sasa, umetufumbua macho kwamba bado tunachezea afya za watu. Bado hatujaliona suala la afya kuwa jambo la msingi katika taifa letu. Badala ya kuwasikiliza madaktari, Serikali ilitaka kutumia vitisho kuwalazimisha madaktari kurudi kazini. Na la kushangaza sana ni kwamba hadi naandika makala hii Rais wetu Jakaya Kikwete, hajasema lolote kuhusiana na mgomo huu. Watu wanakufa, watu wanahangaika kutafuta huduma ya matibabu, watanzania wanapigia kelele mgomo wa madaktari, lakini Rais amekaa kimya. Maana yake nini? Hivi kweli Rais wetu anatambua kwamba afya ni jambo la msigi katika taifa letu? Wananchi wenye afya njema hujenga taifa (uchumi) lenye afya. Kwa upande wa elimu, hakuna asiyefahamu kuwa bila elimu katika dunia ya sasa, huna nafasi. Hapa hatuzungumzii vyuo vikuu tu. Elimu kuanzia shule za msingi hadi vyuo vya kati ni muhimu sana ikaendelezwa na kupelekwa waliko wananchi wengi: vijijini. Elimu isichanganywe na kujifunza. Kujifunza si kuongeza idadi ya wanafunzi madarasani, si kujenga madarasa, si kumaliza mitaala. Hatusemi kwamba madarasa yasiongezwe au idadi ya wanafunzi isiongezeke. Suala hapa ni kwamba yote hayo ni muhimu lakini hayatoshi. Kujifunza ni zaidi ya hapo. Ni kuweza kutumia elimu unayopata kwa manufaa ya taifa letu na kutumia rasilimali zilizopo. Ni kuhitimu masomo na kuweza kubuni namna ya kutumia rasilimali zilizopo nchini kuongeza pato la taifa. Ni kuweza kugeuza chelewa ziwe vijiti vya kuchokonolea meno. Ni kutumia pamba tunayozalisha wenyewe kutengeneza pamba za kutolea uchafu masikioni, ni kuweza kutumia mitishamba tuliyo nayo kutibu magonjwa yanayotusumbua na kadhalika. Elimu ya vitendo ndiyo inayozungumziwa hapa Wananchi wenye elimu bora hujenga taifa lililoelimika na kustaarabika. Tangu uhuru tumekuwa tukiimba kuwa Tanzania ni nchi ya wakulima kwa asilimia tisini na kuwa uti wa mgongo wa nchi yetu ni kilimo. Inawezekana ni kweli. Hata hivyo ninadhani kuwa uti wa mgongo huo hauko madhubuti kama unavyotakiwa uwe. Kwa maoni yangu, kuboresha sekta hii ni lazima, kama kweli tunataka kujiita taifa la wakulima. Ni lazima tutatue tatizo la njaa inayojirudia kila wakati kwa kuwekeza katika kilimo. Kama hakutakuwa na mkakati wa kujitosheleza kwa chakula, wimbo wetu wa Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu utakuwa butu. Taifa haliwezi kuwa linategemea msaada wa chakula kila wakati. Siyo Tanzania hii yenye ardhi nzuri kiasi hiki. Wananchi hawawezi kufikiria kitu kingine chochote wakiwa na njaa. Kilimo si kuwa tu na ardhi kubwa, kinahusisha pia kuwa na huduma zote muhimu na miundo mbinu muhimu (ambazo ni jukumu la serikali kuwekeza katika hizo), huduma za ugani, masoko nakadhalika. Iwapo Tanzania ni nchi ya wakulima kwa 90% hakuna sababu ya Mwananyamala au Masaki, kusikokuwa hata na bustani ya nyanya kuwa na barabara nzuri kuliko Njombe au Sikonge. Barabara ni moja ya matatizo ya ki-miundo yanayowakabili wakulima wengi Tanzania, mengine ni pamoja na kutokuwa na taratibu maalum za upashanaji habari na hata kukosekana kwa mikopo kuendeleza kilimo kwa wakulima wadogo wadogo. Pamoja na hayo, tatizo sugu la kutoongeza mazao thamani ni lazima litatuliwe na si la kuishia kuzungumziwa majukwaani tu. Sasa hivi kwa mfano utasita kuwaambia wakulima wa matunda waongeze uzalishaji. Msimu wa machungwa ukiwadia, na kama una “kauzalendo” kidogo si ajabu ukatokwa na machozi. Machungwa yanaharibikia masokoni yanayobaki yanauzwa kwa bei ya chini sana. Sasa unajiuliza hivi uzalishaji ukiongezeka yatapelekwa wapi? Wakati huo huo unakwenda dukani unanunua juisi inayotengenezwa “ARABUNI”. Juisi toka jangwani!!! Mlimani City, imejazana vitu ambavyo tunaweza kuizalisha hapa hapa Tanzania! Kwa kumalizia, ni vyema kwa rais wetu kuwa na busara ili kupunguza matumizi ya serikali. Kinachoshangaza kwa nchi nyingi masikini duniani kama ilivyo yetu, tunapenda kuiga sana staili za matumizi za ma-rais na viongozi wengine wa serikali za nchi tajiri lakini hatupendi kuiga sera zao bora. Tofauti ni kuwa nchi tajiri wanatumia ndani ya uwezo wao wakati sisi tunategemea misaada na mikopo ili kukimu bajeti zetu. Hili si la kuchezea hata siku moja. Ni lazima tutumie kile tulicho nacho. Maisha ya anasa wakati uwezo ni mdogo ni hatari. Hivyo wakati CCM wanafurahia kuwa na wanachama wengi, wanasherehekea kuwa na wabunge wengi na kuiendesha serikali, ni lazima wafanye tathimini ya kina juu ya kuyashughulikia mambo ya msingi katika taifa letu. Kinyume na hapo sherehe zao ni batili na wala hawaruhusiwi kutumia rasilimali za nchi hii kufanya sherehe. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 633122

0 comments:

Post a Comment