MBONA TGNP NI JUKWAA LA JINSIA KWA MIAKA MINGI? Kwa kusherehekea Siku ya wanawake duniani, Kipindi cha malumbano ya hoja kinachoendeshwa na ITV, kiliandaa mada inayohusu ukombozi wa mwanamke katika Taifa letu la Tanzania. Wanawake na wasichana walishiriki kwa wingi kwenye kipindi hiki na kusema kweli mada iliendeshwa vizuri kinyume na mada iliyokuwa imepita iliyohusu Mapolisi kuwaua watu wakati wa maandamano. Kwa mtu yeyeyote aliyeangalia mada hiyo, ilijionyesha wazi kwamba ilitekwa na Mapolisi na kutumia kipindi cha mapambano ya hoja kama jukwaa la kuwashambulia wanaharakati. Wanaume kwa wanawake walishiriki mada hii juu ya haki na wajibu wa wanawake katika jamii yetu ya Tanzania. Lengo kubwa lilikuwa ni kusherehekea siku ya wanawake duniani. Meza kuu alikaa Profesa Anna Tibaijuka na dada Gradness Munuo, mwandish i wa habari wa mambo ya jinsia na mwanaharakati wa siku nyingi. Hoja nzuri na za msingi zilitolewa, wanaounga mkono jitihada zinazofanyika za kutetea haki za wanawake walijitokeza na kujieleza kwa mantiki na hoja za nguvu. Binafsi niliguswa na hoja ya Profesa Tibaijuka, alipokuwa akichangia kujibu mchangiajia aliyewalalamikia dada zetu kuvaa nguo fupi. Profesa Tibaijuka, alisema yote hayo ni mwendelezo wa mfumo dume, maana ni nani anaamua aina ya nguo za kuvaa? Wanaume wanatunga sheria juu ya mavazi ya wanawake. Kwa nini iwe hivyo? Kwa nini wanawake wenyewe wasijiamulie nguo za kuvaa? Na akaenda mbali kusema kwamba ni nani anayekuja hapa duniani amevaa nguo?Tunazaliwa uchi na walio wengi wanaendelea kukaa uchi mpaka wanapoanza kwenda shule. Hivyo hoja ya msingi si wasichana kuvaa nguo fupi, bali na matatizo ya kufikiri kwenye vichwa vyetu. Hoja nyingine iliyovutia zaidi ni ile ya wanaume kuwanyoshea wanawake kidole kwamba adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe. Kwamba wanawake hawapendani wenyewe kwa wenyewe. Ukija uchaguzi akasimamishwa mwanamke na mwanaume, atachanguliwa mwanaume kwa kura nyingi kutoka kwa wanawake. Lakini pi na hoja kwamba wasichana wanaofanya kazi za majumbani wanateswa na wanawake wenyewe. Wanaume walishikilia bango hoja hii kwa kusema kwamba manyanyaso yanayoendelea majumbani, kwa kiasi kikubwa yanaendeshwa na wanawake wenyewe. Ziko hoja nyingi zilizoibuliwa kwenye kipindi cha malumbano ya hoja cha Alhamisi ya tarehe 8.3.2012 siku ya w anawake duniani. Lakini si lengo la makala hii kujadili yale yaliyotokea kwenye kipindi cha malumbano ya hoja. Lengo lilikuwa ni kudokeza tu ili niweze kujadili kwa kirefu jambo moja lililojitokeza kwenye mjadala huo. Kuna mama mmoja aliyejitambulisha kama kada wa CHADEMA kutoka Dodoma na yuko kwenye chama cha wanawake wa CHADEMA. Hoja yake ya msingi ni kwamba hakuna jukwaa la kuwaunganisha wanawake Tanzania. Kwa maana kwamba jukwaa ambalo si la kichama, si la kidini na wala la kikabila. UWT ni chama cha wanawake wa CCM, na vyama vingine vya siasa vina vyama vyake vya wanawake. Mama huyu wa CHADEMA alisikitika sana kuona wanawake hawana sauti mmoja ya kuwasaidia kutetea haki zao. Kwa maoni yake, kule kugawanyika kwenye vyama vya vya kisiasa, vyama vya kidini na vinginevyo kunakwamisha juhudi za wanawake kujikomboa maana hawana sauti moja. Kwa kuguswa na hoja hiyo Profesa Tibaijuka, alitumia kipindi cha malumbano ya hoja, kuwatangazia watanzania kwamba BAWATA, chama cha wanawake kilichokuwa kimieanzishwa miaka mingi iliyopita kwa lengo la kuwaunganisha wanawake wa Tanzania, kikapigwa vita na kufungiwa, sasa kimeshinda kesi na shughuli zake zitaanza hivi karibuni. Kwa maneno mengine Profesa Tibaijuka, alikuwa na habari njema kwamba jukwaa la kuwaunganisha wanawake sasa liko njiani. Sina lengo la kumpinga Profesa Tibaijuka, mbali na kumpongeza kwa kupambana miaka yote hiyo kuhakikisha BAWATA, inafufuka na kufanya kazi. Napenda kuwakumbusa watanzania na hasa yule mama wa Dodoma, kwamba tumekuwa na majukwaa ya kuwaunganisha wanawake, lakini tuna macho hatutaki kuona na tuna masikio hatutaki kusikia. Mfano mzuri tarehe 7.3.2012 Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Mtandao wa Mashirika yanayotetea haki za binadamu, ukombozi wa wawanawake kimapinduzi na masuala ya jinsia (FemAct) pamoja na wanaharakati wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS) walishirikiana kuaadhimisha siku ya wanawake duniani kwenye viwanja vya Mabibo yalipo makao makuu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania. Jukwaa hili la Mtandao wa jinsia, lipo siku nyingi. Na kusema kweli si jukwaa la kisiasa, si jukwaa la kidini na wala si jukwaa linaoangukia kushoto wala kulia. Ni jukwaa linalowashirikisha watu wote wenye nia njema ya kutetea haki za wanawake na haki za binadamu kwa ujumla. Juzi hiyo ya tarehe 7, tulishuhudia wenyewe wasichana na akinamama walivyosimama kidete kutoa hoja zao juu ya kudai kupewa haki ya kupiga kura, kushika ngazi za uongozi na maamuzi, kupinga unyonyaji wa jasho lao na ubaguzi kaika ajira na unyanyasaji wa kijinsia na hasa kuonyesha nia ya wazi ya kutaka kupambana na uporaji wa rasilimali za nchi hasa ardhi, maji na madini. Mbali na jukwaa hili la siku ya wanawake duniani, Mtandao wa Jinsia Tanzania, umekuwa na utamaduni wa kuandaa tamasha la jisnia kila baada ya miaka miwili. Huu ni uwanja mpana ambao una uwezo wa kuwaunganisha wanawake wote wa Tanzania. Kawaida wanaalikwa wanawake kutoka mikoa yote ya Tanzania kuja pale Mabibo, kushirikishana mapambano ya kutetea haki za binadamu na haki za wanawake. Inawezekana baadhi ya watu wasifahamu kuwepo kwa jukwaa kama hili la Mtandao wa Jinsia, haya ni makosa madogo madogo, ambayo ni lazima Mtandao wa jinsia wajisahihishe na kuhakikisha jukwaa lao linafahamika kiasi kikubwa. Lakini hatuwezi kusimama na kusema kwamba wanwake wa Tanzania hawana jukwaa la kuwaunganisha. Mbali na Tamasha la jinsia, kila Jumatano, pale makao makuu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania, kuna mjadala wa wazi saa za jioni. Wadau wanakutanika hapo na kuendesha majadiliano. Kawaida mada zinaandaliwa, na wataalamu wa kuchokoza mada wanakaribishwa. Washiriki wanakuwa na uhuru wa kujieleza na kusikilizwa. Ni wakati mzuri wa kusikiliza yanayotokea kwenye jamii yetu na hasa kuhusu unyanyasaji wa kijinsia. Matokeo ya mijadala hii ya jumatano, yanajionyesha taratibu kwa wanawake na wasichana kujengewa uwezo wa kujiamini wakati wa kujieleza, lakini pia wanawake wengi wamejengewa uwezo wa kutambua haki zao na kujua ni wapi pa kwenda wakati wanapokumbana na matatizo ya unyanyasaji. Hoja ninayoijenga kwenye makala hii ni kwamba si kweli kwamba Tanzania hakuna jukwaa la kuwaunganisha wanawake. Majukwaa yapo, la msingi ni kujiuliza ni kwanini majukwaa haya hayaonekani? Au ni kwa nini yanatumiwa na watu wachache? Kwa vile kaulimbiu ya mwaka huu ni vijana chachu ya maendeleo, basi uwepo mkakati wa kuwajengea utamaduni vijana wetu na hasa watoto wa kike kuyatumia majukwaa yaliyopo kama hili la Mtandao wa jinsia, ili kuleta mabadiliko. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment