MATRAFIKI WA IRINGA NA VITUKO VYAO. Naandika makala hii kuishukuru serikali yetu na kuipongeza kwa kuwawezesha matrafiki kwa kuwapatia Kamera za kudhibiti mwendo kasi wa magari barabarani. Ni imani yangu na ya wengi kwamba hatua hii itapunguza ajali nyingi zinazotokea kwenye barabara zetu kila kukicha. Ajali barabarani zimekuwa nyingi na maisha ya watanzania yanateketea. Ingawa kuna sababu nyingi za ajali hizi, inaaminika kwamba sababu kubwa ni mwendo kasi. Shukrani hizi si za kujipendekeza au “Mapenzi” na chama cha CCM, kama wanavyofikiria wengine. Ninachokifanya ni kuandika ukweli ulivyo. Si kweli kwamba Serikali inafanya mabaya peke yake, au kwamba serikali inafanya mazuri pieke yake. Pale serikali yetu inapofanya vibaya, ni lazima tusimame na kukemea, lakini pale inapofanya vizuri ni lazima tuishukuru na kuipongeza. Msimamo kwamba serikali ya Kikwete, haifanyi kitu, ni wa kipuuzi kabisa! Ndani ya Serikali ya Kikwete, kuna watu wanafanya kazi usiku na mchana, kuna watu waadilifu, kuna watu wazalendo na wenye nia nzuri na taifa letu; na kuna ushahidi kwamba baadhi ya mambo yanakwenda vizuri. Ninajua, kama wengine wanavyojua kwamba nyakati hizi ni za kutaka mabadiliko. Watanzania na hasa vijana, wanataka mabadiliko. Vuguvugu hili la mabadiliko lisituvumbe macho kiasi cha kutoona hata kile kidogo kinachofanywa na watu wenye nia njema. Mabadiliko haya hayawezi kushuka kutoka mbinguni na kuja kwenye ombwe na si ukweli kwamba yataletwa na malaika. Ni watanzania hawa hawa na Tanzania yetu ndo tutaleta mabadiliko. Makosa yanayofanywa na Serikal ya CCM yanaweza kujitokeza pia kwenye Serikali nyingine itakayouundwa na Chama kingine au na wagombea wakujitegemea. Hivyo ni makosa makubwa kufunga fikira zetu kwenye mwelekeo hasi na kuacha mwelekeo chanya hata kama ni kwa matendo machache kama vile barabara na huduma nyingine ambazo zimeanza kusogea kwa watu wa vijijini kama vile umeme na elimu ya msingi na sekondari. Makala yangu ya juzi, katika safu hii ya Tusemezane, nilisifia barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami. Baadhi ya wasomaji wangu walinipongeza kwa makala hiyo, lakini kuna walionitukana kwamba ninajipendekeza kwa Serikali. Msimamo wao ni kwamba Serikali ya Kikwete, haijafanya kitu. Nafikiri msimamo huu ni wa hatari na hauna manufaa yoyote yale kwa taifa letu. Kwa manufaa ya wasomaji wangu, ninakuu baadhi ya ujumbe mfupi nilioupokea kupitia simu yangu ya kiganjani: “Barabara unazoshukuru serikali kujenga ni zipi? Kama ungeona barabara za nchi tulizokuwa tunalingana nazo kwa vigezo vyote vya maendeleo wakati wa kupata uhuru kama Korea Kusini na Malaysia wala usingetoa sifa yoyote kwa hawa jamaa. Hakuna Barabara Tanzania” Na mwingine aliandika: “ Mtu yeyote mwenye hofu ya Mungu hawezi kuisifia serikali hii ya Kikwete, iliyojaa dhuruma, ufisadi,wizi wa pesa za wananchi ambao wanazidi kuwa maskini kila kukicha, itikadi yako ya CCM ndio inayokusukuma uwapongeze”, Na mwingine aliandika: “ Barabara hizo mtazifaidi nyinyi akina Karugendo wenye magari mliopewa kwa ajili ya kueneza propaganda za CCM. Watanzania wana hali mbaya kimaisha. Kama wanaweza kujenga barabara za mabilioni, mbona hospitali huduma mbovu? Elimu duni! Maisha magumu?”. Ninaheshimu sana maoni ya wengine. Lakini siwezi kukubali kupotosha ukweli kwa kutaka kuwafurahisha baadhi ya watu. Siko tayari kuwa kada wa chama chochote cha siasa; atakayefanya vizuri, nitamsifu na atakayefanya vibaya nitasimama na kukemea. Ndo maana hata baada ya kulalamikiwa na kulaaniwa kwa kuandika makala ya kuzisifia barabara za lami, bado ninasimama kuisifia serikali kwa kitendo chake cha kutoa Kamera za kdhibiti mwendo kasi kwa matrafiki wetu. Swali la Kamera hizi zinatumika vipi, si la serikali bali la mtu binafsi anayezitumia Kamera hizi. Katika makala hii nawaongelea matrafiki wa Mkoa wa Iringa. Baada ya pasaka ya mwaka huu, nilisafiri kwa gari dogo kutoka Morogoro hadi Mbeya. Njia nzima tulishuhudia Kamera hizi za kudhibiti mwendo na vituko vyake. Kabla ya kufika Makambako, tulikamatwa na trafiki kwa mwendo kasi. Tulikuwa tunaendesha kwa kasi ya kilomita 90 kwa saa. Tulipokaribia eneo la tukio na baada ya kuona ishara ya kuendesha kilomita 50 kwa saa, tulianza kupunguza mwendo hadi kilomita 60 kwa saa. Tulipokamatwa na polisi, mshale ulikuwa unaonyesha kilomita 59 kwa saa. Na kamera ya polisi ilionyesha tulikuwa tunakwenda kwa kasi ya kilomita 72 kwa saa. Tulibishana na polisi. Sisi tukisema tulikuwa tunaendesha kilomita 59 kwa saa na yeye akisisitiza kwamba Kamera yake imesoma kilomita 72, kwa saa. Tulitaka kujua kama kamera ile ilikuwa na uwezo wa kusoma namba za gari, ili tuwe na uhakika kama kweli Kamera ilisoma gari letu. Polisi alijibu kwamba Kamera hiyo haina uwezo wa kusoma namba za gari. Wakati wa mabishano magari zaidi ya sita yalikamakwa kwa kuendesha kilomita 72 kwa saa. Tulishangaa kuona Kamera hiyo ina uwezo wa kusoma 72 tu! Ina maana hata kama mtu ukiendesha kilomita 30 kwa saa, Kamera za Iringa, zitasoma kilomita 72 kwa saa! Hivi ndivyo vituko vya matrafiki wa Iringa. Wakitaka kukukamata kwa mwendo kasi, huwezi kupona hata kama unaendesha kwa kasi ya kinyonga! Tulilazimika kulipa faini ya silingi elfu kumi, ambazo sikumbuki kuona risiti yake, na wengine wale sita, walilipa hizo shilingi elfu kumi. Kama yanapita magari zaidi ya miatatu kwa siku kwenye barabara hiyo, huyo trafki atakuwa na fedha kiasi gani mfukoni mwake? Ni aina ya rushwa na ufisadi! Kuwa na Kamera za kudhibti mwendo kasi ni hatua nzuri na ya kusifia. Tatizo ni je Kamera hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa au ni njia yingine ya kuwatengenezea ulaji mapolisi wetu? Kuna haja ya kuziboresha Kamera hizi, zikawa na uwezo wa kusoma namba za magari. Hii inaweza kupunguza mabishano na utatata unaojitokeza anapokamatwa mtu kwa kuendesha mwendo kasi. Pia ni muhimu kuwapatia matrafiki wetu semina ya kuzitumia Kamera hizi. Kamera hizi zinatumia bateri, kama bateri hazina nguvu za kutosha ni lazima Kamera isome uongo. Pia, namna ya kuishika kamera yenyewe ni muhimu pia, mfumo wa sasa wa polisi kujificha kichani na kuchomoka kwa kasi kila anaposikia gari linakuja hauwezi kusaidia kupata namba sahihi kwenye kioo cha kamera. Ina maana gani polisi kujificha kichakani kana kwamba anamvizia mwizi? Ni bora mapolisi wakasimama sehemu wazi barabarani na kuyamulika magari yaendayo kwa kasi isiyoruhusiwa. Ni imai yangu kwamba suala hili litafuatiliwa na kuhakikisha mapolisi hawa wanaotumia Kamera za kudhibiti mwendo kasi kujitajirisha wanashughuliliwa na kuwajibishwa. Vitendo vya watu wachache visipotoshe nia njema ya Serikali ya kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua au zinakwisha kabisa. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment