KIFO CHA MUAMMAR GADDAFI
NI KIFO CHA UHURU WA AFRIKA
Jumapili iliyopita
yalitokea makosa katika safu yangu ya Tusemezane. Makala iliyotokea hapo juu ya
Muammar Gaddafi, haikuwa yangu. Nafikiri ni kazi ya mhariri kuwaelezea wasomaji
kilichotokea. Nilipokea simu na sms nyingi. Wengine wakinipongeza, wengine
wakinilaumu na kunitukana. Kilichonisikitisha, pamoja na makosa ya uhariri, ni
kwamba makala iliyowekwa kwenye safu yangu ilikuwa na mawazo na msimamo tofauti
na wa kwangu juu ya maisha ya Muammar Gaddafi. Maana yake wale waliokuwa
wananipongeza kwa makala nzuri, ni kwamba mimi si sitahiri hizo pongezi na wale
walionitukana walinionea bure! Sikuweza kuwajibu wote; hivyo nina imani makala ya
leo ni jibu. Huu ndio msimamo wangu juu ya kuawa kwa Muammar Gaddafi.
Afrika tulitawaliwa na
tuliuzwa sokoni kama bidhaa nyinginezo. Utumwa na ukoloni ni historia mbaya
katika historia ya dunia yetu. Hadi leo hii wakoloni, walishindwa kuomba
msamaha kwa dhambi kubwa walizotutendea. Inajulikana wazi kwamba walitupatia
uhuru shingo upande na kuendelea kututawala kwa njia mpya za utandawazi, soko
huria na ukoloni mambo leo kama ilivyojitokeza juzi kwa Waziri Mkuu wa
Uingereza kutamka wazi kwamba bila kuukubali ushoga hatutapata misaada!
Viongozi wa Afrika
walioonyesha kuwa na mwanga wa kutaka uhuru kamili walizimwa. Mfano mzuri ni wa
Patrice Lumumba. Hata akina Nkrumah, kupinduliwa kwao kulikuwa na msukumo wa
hawa mabwana wakubwa. Wana ujanja wa kutumia misemo kama Demokrasi, haki za
binadamu, kulinda maisha ya watu na upuuzi mwingine mwingi, huku wakiuma na
kupuliza. Lengo lao ni kuwapumbaza
Waafrika, kuendelea kuwatawala na kuwafanya soko lao kubwa na sehemu ya
kuchuma rasilimali nyingi kama vile mbao, madini, ardhi ya kulima chakula na
kuzalisha nishati, sehemu za kupumzikia na mengine mengi.
Kilele cha hujuma za
wakoloni kimejionyesha wazi kwa kifo cha Muammar Gaddafi, aliyekuwa rais wa
Libya. Shutuma zote juu yake kwamba alikuwa dikteta, kwamba alikuwa anawaua
watu wake, kwamba alikuwa akisaidia makundi ya kigaidi ni uongo mtupu. Gaddafi,
alikataa kuwauzia mafuta Wazungu kwa dola, yeye alitaka awauzie kwa dhahabu.
Walete dhahabu awapatie mafuta. Gaddafi, alikataa makampuni ya kigeni kuja
Libya kuchimba mafuta. Alisimama imara na kusema wao wana makampuni yao ya
kuchimba mafuta. Wazungu, waje wanunue mafuta na si kuja kuchimba mafuta Libya.
Gaddafi, alitaka Afrika kuungana. Alitaka Afrika iwe na serikali moja, ili bara
letu liwe na nguvu na kuweza kushindana na hawa wakoloni. Alikuwa tayari kutoa
fedha ili kutekeleza mradi huu mkubwa na wenye manufaa makubwa kwa bara zima la
Afrika. Wakoloni hawakuyataka mawazo yake haya na sasa wamehakikisha ameondoka
na kufutika! Ni unyama ule ule wa Ukoloni na utumwa.
Kifo cha Gaddafi,
kimewasikitisha wengi na hasa Waafrika ambao wanatambua mchango wake mkubwa.
Kama alivyosema Waziri Membe, ni kichaa peke yake anayeweza kusimama na kusema
kwamba Gaddafi, hakufanya kitu. Sote tunakumbuka alivyoligeuza jangwa kuwa
kijani, sote tunajua jinsi ambavyo watu wake wasiokuwa na kazi walivyokuwa
wakipata posho ya kujikimu, tunajua jinsi alivyowajengea wananchi wake makazi
bora ya kuishi, sote tunajua jinsi alivyoigeuza Libya kuwa ni nchi yenye
maendeleo makubwa ndani ya bara la Afrika. Ametoa michango mingi kwenye nchi
mbali mbali za Afrika. Amekuwa akitoa fedha za kuuendesha mikutano ya Umoja wa
Afrika. Ni mtu aliyewapenda watu wake wa Libya na ni mtu aliyelipenda bara letu
la Afrika. Kifo cha kinyama kilichomfika ni aibu na laana kubwa kwa watu wa
Libya kukubali kutumiwa na wakoloni kutekeleza adhima yao.
Kama kweli wakoloni walikuwa na nia njema, mbona
nguvu zilizotumika Libya kumuondoa Gaddafi, hazitumiki mashariki ya kati? Mbona
Syria, kuna maandamano ya kuikataa serikali iliyo madarakani kuondoka na watu
wengi wamekufa, lakini hatujaona nguvu kubwa zikitumika kama zile zilizotumika
Libya?
Wanataka mafuta ya
Libya! Wanataka rasilimali za Afrika, wanataka soko la Afrika; wanataka Afrika
isiungane na kuwa na nguvu ili waendelee kutugawanya na kututawala. Wanataka
kuendeleza ukoloni na utumwa, wanataka kuzirudia sera za mababu zao
zilizoliteketeza bara la Afrika.
Wapo watanzania wenzetu
wanasema Gaddafi, alikuwa mbaya maana alishirikiana na Iddi Amin kuivamia nchi
yetu. Ni kweli alifanya vibaya, hata yeye alijuta na kuomba msamaha. Hizo
zilikuwa ni siasa. Hata sisi Tanzania wakati wa vita ya Biafra, pamoja na
msimamo wa Tanzania wa kutaka umoja, tulisimama upande wa Biafra wa kutaka
Nigeria igawanywe vipande viwili.
Mwalimu Nyerere, alikuwa na hoja nzuri na alijielezea vizuri. Msimamo wetu huo
juu ya Biafra, haukutufanya tuonekane maadui wa Nigeria. Hata hivyo kwani ni
Gaddafi peke yake alimsaidia Iddi Amin wakati wa vita ya Kagera?
Hakuna anayesema kwamba
Gaddafi, alikuwa mtakatifu. Alikuwa na mapungufu yake kama binadamu wengine
wote. Lakini kwa suala la kujenga taifa huru lenye maamuzi yake, kwa suala wa
umoja wa Afrika, kwa suala la
rasilimali za Afrika kuwanufaisha Waafrika wenyewe, hakuwa na mfano wake. Kama
tuna bishi tusubiri utawala mpya wa Libya ndo tutatambua kazi kubwa iliyofanywa
na Gaddafi.
Kwamba alikuwa akieneza
Uislamu, hilo si kosa maana kila muumini ana wajibu wa kuieneza dini yake.
Miaka mingi Waislamu na Wakristu wameeneza dini zao ndani ya bara la Afrika, lakini
ukweli usiopingika ni kwamba hadi leo hii bado kuna Waafrika wanaoamini bado
dini zao za jadi. Hawakukubali kuingia kwenye Uislamu ama Ukristu. Kueneza na
kupokelewa ni vitu viwili tofauti; watu wakikubali kupokea imani fulani, maana
yake ni kwamba wameilewa na kuipenda; kama si kuwalazimisha watu kwa upanga
kama ilivyofanywa miaka ya nyuma katika Bara letu la Afrika na Amerika ya kusini, hakuna tatizo la mtu
kuipokea imani anayoamini itaboresha utu wake na kumwongoza kuishi vyema na
binadamu wenzake.
Kifo cha Gaddafi,
kitufumbue macho. Ni lazima Waafrika kushikamana na kusema hapana! Ni lazima
kukataa mbinu hizi za wakoloni kutaka kutuchagulia viongozi. Ni lazima
kuwakataa hawa vibaraka wao na kuwa tayari kulilinda bara letu la Afrika, ili
liwe salama kwa vizazi vijavyo. Ni bora kufa tukilitetea bara letu kuliko
kuliacha likachukuliwa na hawa wakoloni wajanja wanaojifanya wanaipenda sana
Afrika kumbe ni mbinu za kuhakikisha bara letu linabaki gizani na kuendelea
kunyonywa. Uhuru wetu unakufa ni lazima tusimame kidete kuutetea.
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment