JE UKIMWI SI JANGA LA KITAIFA TENA?
Dunia nzima, imeutangaza ugonjwa wa UKIMWI kama janga, na Serikali ya Tanzania, kupitia kwa Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, iliutangaza UKIMWI kama janga la kitaifa. Vita dhidi ya ugonjwa huu ilitangazwa na serikali iliunda Tume ya kudhibiti ugonjwa huu. Njia mbali mbali za kuepukana na ugonjwa huu ziliweka wazi kufikia hatua ya kuleta migongano kati ya Serikali na viongozi wa dini waliopinga kwa nguvu zote matumizi ya Kondomu. Hata hivyo kondomu, ilipitishwa na kukubalika na wengi kuwa ndiyo njia ya kuaminika zaidi kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Jinsi miaka ilivyokuwa ikipita na ugonjwa huu kuendelea kuwa tishio kubwa kwa maisha ya binadamu, hata viongozi wa dini waliokuwa na misimamo mikali na kupinga matumizi ya Kondomu kwa nguvu zao zote walianza kulegeza misimamo yao kwenye mazingira fulani fulani na wakati mwingine wakilipokea wazo la matumizi ya kondomu kwa kiasi kizima nyuma ya mapazia. Na Baba Mtakatifu Benedict wa kumi na sita, bila kelele nyingi alianza kujadili na kukubali kiasi Fulani; kwa mazingira Fulani matumizi ya Kondomu. Wakatoliki wenye msimamo mkali walimpinga; lakini kwa vile ni imani yao kwamba Baba Mtakatifu akiwa kwenye kiti cha Mtakatifu Petero, hawezi kupotoka wala kupotosha, walinywea wenyewe na sauti ya Papa haikuchomoza kwa ukali kuunga mkono sauti zilizotangulia kuona umuhimu wa matumizi ya Kondomu.
Sina lengo la kuelezea historia ya mampambano ya UKIMWI katika makala hii.Huko nyuma tuliandika mengi juu ya suala hili na msimamo uko wazi wazi. Naandika makala hii kuuliza swali: JE UKIMWI SI JANGA LA KITAIFA TENA? Ukwimi si tishio, na watu tumeanza kuishi kana kwamba haupo au tumezoea na kuliona ni jambo la kawaida? Inashangaza miaka zaidi ya ishirini ya kupambana na ugonjwa huu hapa Tanzania, kuna watu hawana habari na ugonjwa huu. Si kutia chumvi wala kulenga kumfurahisha mtu fulani au kumchukiza mwingine.Ni ukweli nilioushuhudia kwenye wilaya nilizozitemblea mwezi wan nne mwaka huu. Haina maana kwamba ugonjwa huu haupo kwenye maeneo yao, haina maana kwamba watu hawafi kwa ugonjwa huu kwenye maeneo yao; wale wanaokufa kwa ugonjwa wa Ukimwi, wanakufa kama wengine wanaokufa kwa malaria, kwa kuharisha, mama wajawazito kufa wakati wa kujifungua kwa sababu ya kushindwa kufika kwenye vituo vya afya kwa vile barabara ni mbaya au hakuna usafiri kabisa. Wanaokufa kwa ugonjwa wa Ukimwi, wanakufa kama wale wanaozama majini kwa vile wanasafiri kwenye vyombo visivyokuwa salama, wanakufa kama wale wanaokufa kwenye ajali za barabarani. Habari za ugonjwa wa Ukimwi hazijafika kwenye maeneo yao! Inashagaza lakini ni kweli. Pamoja na ukweli kwamba kila wilaya inakuwa na kamati ya Ukimwi na kila kijiji kinakuwa na kamati ya Ukimwi,bado kuna watu hawana habari juu ya ugonjwa huu wa hatari.Ni Janga la kitaifa ambao halijasambaa ili watu wote walijue na kujikinga nalo. Pamoja na tume ya taifa ya kudhibiti Ukimwi, pamoja ma mashirika yote yanayojishughulisha kuelimisha, kuhamasisha na kupambana na ugonjwa huu, bado kuna watanzania hawana habari juu ya ugonjwa huu. Je, ni kweli ugonjwa huu ni Janga la Kitaifa?
Mwezi wa nne mwaka huu, nilitembelea wilaya nne za mikoa miwili ya Tanzania Bara, wilaya mbili kila mkoa kwa utafiti tofauti na mada hii ninayoiandika kwenye makala hii. Kwa vile hili ninaloliandika la Ugonjwa wa Ukimwi, liliibuliwa na “Uchokonozi” wangu; nilifanya majadiliano na vijana na watu wazima kwa makubaliano ya kutowataja majina yao wala wilaya zao, nimeamua kuwa mwaminifu. Sintotaja majina ya watu na wilaya zao, katika makala hii, lakini kwa mtu yeyote anayetaka kulifuatilia jambo hili kwa manufaa ya taifa letu, nitakuwa tayari kutaja wilaya,bila kutaja majina ya wahusika.
Katika wilaya hizi nne, nimekutana na watu wasiokuwa na habari juu ya ugonjwa wa Ukimwi. Vijana kwa wazee, wanaishi bila kuwa na habari ya ugonjwa huu. Watu wanakufa, wanazikwa na wengine wanaendelea kuishi maisha yao kama kawaida. Wakielezea magonjwa yanayosababisha vifo katika jamii yao, utagundua haraka kwamba na Ukimwi ni miongoni mwa magonjwa yanayowasumbua. Wanaendelea kuishi, na wao wako Tanzania, nchi ambayo imetangaza Ukimwi kama janga la Kitaifa.
Lakini la kushangaza zaidi ni kwamba hata na wale wanaofahamu juu ya Ukimwi, wanaishi kana kwamba Ukimwi haupo tena. Vijana waliniambia “ Siku hizi tumeachana na Kondomu. Ya nini kutumia mipira wakati dawa zipo”? Mwanzoni sikuelewa wanamaanishi nini? Dawa ya kutibu Ukimwi au dawa gani? Kumbe walimaanisha dawa za kurefusha maisha.
Kumbe dawa za kurefusha maisha kwa upande mwingie ni janga jingine la kitaifa? Vijana wa wilaya hizi nilizotembelea, wanaamini kwa vile kuna dawa za kurefusha maisha hakuna haja ya kutumia kinga, hakuna haja ya kuepuka wapenzi wengi. Katika kijiji kimoja, wavulana waliniambia “ Asilimia zaidi ya 99 katika kijiji hiki vijana hawatumii kondomu. Wanaamini kwamba dawa za kurefu maisha ni kinga tosha. Wanasafiri hadi vijiji vya mbali kutafuta dawa za kurefusha maisha. Wakishazipata, wanaendelea na maisha kama kawaida. Wanatembea na wasichana bila kujali. Na wasichana wetu hapa, hawataki kutumia kondomu, wanaamini ni uchafu!”.
Pia kuna imani mpya kwamba mtu akitahiri, hawezi kuambukizwa Ugonjwa wa Ukimwi. Imani hii imenea vijijini, na kwenye wilaya hizi nilizozitembelea, vijana wote wanafanya jitihada binafsi za kutahiri. Na huu ni mradi kwa baadhi ya watu, maana kutahiri mtu analipa kuanzia shilingi elfu 20. Wengine wanafanya kitaalamu na wengine ambao hawana fedha za kulipa wanatumia njia za kienyeji ambazo ni hatari kwa maisha yao. Vijana waliniambia “ Ni vigumu kumpata msichana, kama hukutahiri, kama kuliko kutovaa kodomu. Kabla ya kufanya kitendo, ni lazima uvue nguo zote msichana akugague. Akikuta hujatahiri, hata kama utakuwa na kondomu anakataa kufanya kitendo. Imejengeka imani kwamba mtu aliyetahiri hawezi kuwa na virusi. Na hii pia imechangia kiasi kikubwa vijana kuacha kuvaa kondomu”.
Kwamba dawa za kurefusha maisha zinachukuliwa kama kinga ya kudumu ya Ukimwi, ni jambo lililoishutua sana, lakini ukweli ni kwamba katika wilaya nne nilizozitembelea ni jambo la kawaida. Watu wanaamini, hii ni kinga, maana kama unaweza kurefusha maisha, unataka nini duniani? Vijana wanasema “ Bora maisha mafupi yenye raha, kuliko maisha marefu yenye taabu na mateso”. Na kwa maoni yao, uvumbuzi wa dawa za kurefusha maisha, umereudisha “Furaha” ya maisha. Maana kitendo cha ngono, bila kondomu ni burudani iliyokamilika.
Nilishuhudia kondomu zilizopitwa na wakati wake kwenye maduka. Wenye maduka, waliniambia wanasubiri kuziteketeza maana hazina wateja tena, labda wageni wanaopita kwenye vijiji hivyo. Wenyeji, wanaamini dawa ya UKimwi imepatikana: Dawa za kurefusha maisha! Kwa uelewa huu ni vigumu sana kupamba na maambukizi mapya. Wenye virusi wanaendelea kuvisambaza. Swali la kujiuliza ni je pale serikali itakaposhindwa kuzinunua dawa hizi za kurefusha maisha na kuzisambaza hali itakuwa vipi?
Na je, uelewa huu wa kwamba dawa za kurefusha maisha ni dawa ya Ukimwi imetokana na nini? Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi, imeshindwa kufanya kazi yake vizuri? Elimu juu ya Ukimwi imesambazwa vibaya? Maelezo juu ya dawa za kurefusha maisha yametolewa vibaya? Kosa limetokea wapi? Kuna haja ya kufanya utafiti wa suala hili kwenye wilaya nyingine ili kubaini kama hizi wilaya nne nilizozizungukia zina matatizo ya kuelewa au hili ni tatizo la vijana wote wa Tanzania? Je, kuna vijana wengine katika wilaya nyingine wanaoamini kwamba dawa za kurefusha maisha ni kibali cha kuishi kana kwamba hakuna ugonjwa wa Ukimwi? Kama hali ni hii, basi hatuwezi kusema tena kwamba Ukimwi ni janga la kitaifa.
Tunajua kwamba Kondomu si kwa ajili ya ukimwi peke yake, bali pia ni kinga kwa magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa. Kwa vijana hawa, magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa si tatizo maana kuna dawa za asili. Walitaja mizizi ya Mpapai dume, kuwa ni tiba ya magonjwa ya zinaa. Kwamba ukichemsha mizizi ya Mpapai dume na kunywa lita tano ya dawa hii, huwezi kuwambukizwa magonjwa ya zinaa na wengine wanaamini kwamba dawa hii inazuia pia maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Nilionyeshwa Mipapai dume, iliyokauka kwenye kijiji hicho kwa vile mizizi yake imechimbuliwa na kutumika kama dawa ya kuzuia magonjwa ya zinaa.
Kwa upande wa mimba zisizotarajiwa, niliambiwa kwamba kabla ya kitendo cha ngono, mtu anakoroga gilasi mbili za majivu, anakunywa moja na nyingine anampatia msichana wake. Wanasema hata kama ni siku za kutunga mimba, ukinywa gilasi ya majivu ni vigumu kupata mimba.
Katika kijiji kingine, niliambiwa kwamba kuna dawa ya kufunga kwenye ushanga wa mwanamke kiunoni, hata kama ni siku za kutunga mimba, msichana hawezi kupata mimba. Kwa kutumia mizizi ya Mpapai dume, majivu na dawa ya kufunga kwenye ushanga, vijana wanafanya ngono bila kuogopa magonjwa ya zinaa, bila kuogopa mimba zisizotarajiwa na bila kuogopa Ukimwi kwa vile kuna dawa za kurefusha maisha. Hii ni hatari kubwa kwa taifa ambalo limeutangaza Ukimwi kama janga la kitaifa.
Changamoto ni kwa watifiti wetu wa tiba na Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi. Je Mizizi ya Mpapai Dume ni dawa kweli? Je majivu yana uwezo wa kuzuia mimba? Ni nini kifanyike kuwaelimisha watu hawa wanaoamini kwamba dawa za kurefusha maisha ni tiba ya Ukimwi?
Janga jingine katika vijiji hivi nilivyovitembelea ni Piki piki hizi zinazojulikana kama Boda boda. Mbali na ajali za kila siku zinazowaacha vijana wakiwa wamekatika mikono na miguu ni chanzo kingine cha kueneza Ukimwi. Vijana wanaofanya kazi hii ya Boda boda waliniambia “ Wateja wetu, na hasa wasichana wanapopungukiwa nauli, tunaamua kuingia kichakani na kulipana. Wakati mwingine msichana anaamua kusitisha safari yake, tunaingia nyumba ya kulala wageni. Safari inaendelea kesho yake”. Waliniambia kwamba huo ni mchezo wa Boda boda wote hata wa vijii vya jirani. “Hatuogopi Ukimwi, serikali yetu imetujali kwa kutuletea dawa za kurefusha maisha, hivyo kazi iliyobaki ni kuyafurahia maisha”.
Ni imani yangu wanaohusika wataisoma makala hii na kuchukua hatua. Niko tayari kwa ushirikiano.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment