INASHANGAZA, JE TATIZO LIKO WAPI?

Kwa mataifa mengine sikukuu za mwisho wa mwaka huwa ni za kutafakari yaliyotendeka ndani ya mwaka mzima na kujipanga upya kwa maka unaofuata. Sina uhakika kama sisi Tanzania tunafanya hivyo. Katika makala hii najaribu tu kidogo kuangalia mambo yanayoshangaza ndani ya taifa letu na kujiuliza tatizo nini? Ni wazi kuna mambo mengi tunayoyafanya vizuri, lakini kama mtu unataka kuendelea mbele ni lazima kuangalia pale unapojikwaa.

Tumemaliza sherehe za miaka hamsini ya uhuru wetu. Ni vyema kusherehekea kwa mafanikio ama kwa kushindwa kufikia malengo: Miaka hamsini bado kuna mapungufu mengi, la kushangaza hapa ni kwamba tumetumia fedha nyingi kwenye sherehe hizi wakati taifa linayumba kiuchumi na kuna hatari bajeti isiweze kufikia mwisho wa mwaka wa fedha. Kwa nini matumizi makubwa ya sherehe, wakati bado kuna hitaji kubwa la kuboresha huduma za -kijamii? Je tatizo liko wapi hapa? Ni uongozi? Ni kutokuwa na malengo ya mbali au hatuna wataalam wa uchumi?

Baada ya sherehe za uhuru tunawasikia viongozi wetu wakisema kwamba hali  ya uchumi ni mbaya na maisha ni magumu! Inashangaza baada ya kutumia fedha zote hizo kwenye sherehe za uhuru tunalia kwamba maisha ni magumu. Huu ndio utamaduni wetu wa kulalamikia ugumu wa maisha wakati tunateketeza fedha: tunalalamika maisha magumu wakati barabara zetu zimejaa magari hadi foleni hazitembei, magari hayo yanakunywa mafuta! Tunalalamika maisha magumu lakini watu wana simu zaidi ya tatu, simu zote hizo zinakula fedha na kila ukipita watu wote simu masikioni; tunalalamika ugumu wa maisha, wakati sehemu za starehe na nyama choma watu wamejazana kibao; wanakula na kunywa; bei ya bia inapaa na bei ya nyama inatisha; tunalalamika ugumu wa maisha wakati tunachanga mamilioni ya fedha kufanya sherehe za arusi; tunalalamika maisha magumu wakati majumba makubwa yanajengwa usiku na mchana! Inashangaza!

Siku tatu zilizopita mvua ilinyesha kwa nguvu kubwa ndani ya jiji la Dar-es-Salaam na kuleta mafuriko na maafa makubwa. Watu wamekufa na wengine hadi sasa hivi hawana makazi. Amini usiamini, baada ya saa moja mvua hii kubwa kunyesha, nilishuhudia maeneo ya Tabata Chang’ombe watu wakienda kununua maji ya chumvi na kuilaumu idara ya maji kwamba siku hizi haitoi maji. Inashangaza kabisa mvua kunyesha siku tatu mfulizo na watu wakashindwa kuvuna maji ya mvua. Mtu anaweza kujiuliza: Je hapa tatizo liko wapi? Nyumba nyingi zimeezekwa kwa bati, mvua ikinyesa maji yanatiririka kwenye bati, yanaingia barabarani, yanaharibu barabara, yanaleta mafuriko. Tunashindwa kuyatumia maji haya, kupikia, kuoga, kufua na kufanya shughuli nyingine. Nina imani kama tungeweza kuyavuna maji haya ya mvua hii iliyoleta maafa makubwa kwenye Jiji la Dar-es-Salaam, yangetusukuma zaidi ya miezi miwili.

Kule Rwanda, wametunga sheria ya maji ya mvua. Ni kinyume cha sheria maji ya mvua kutiririka kwenda kwa jirani au kuingia barabarani na kuleta uharibifu. Kwa mujibu wa sheria kule Rwanda, kila mtu ni lazima avune maji ya mvua. Sheria hii imesaidia watu kule Rwanda kupata maji ya  kutumia majumbani mwaka mzima,, pia imesaidia kupunguza uharibifu wa miundo mbinu na mafuriko. Nina imani kwamba kama nyumba zote za Dar-es-Salaam zingekuwa na mfumo wa kuvuna maji ya mvua, ni wazi athari ya mvua hizi ingekuwa ndogo.

Lakini jingine linaloshangaza ni madaraja kusombwa na maji barabara mpya ya Mandela, iliyofunguliwa juzi kwa mbwembwe kubomoka. Mtu anaweza kujiuliza, madaraja haya yalijengwa kwa kiwango gani? Na je hii barabara ya Mandela inayobomoka kwa mvua ya siku tatu, itakuwa na hali gani miaka miwili mitatu ijayo? Ni kweli maji yana nguvu kubwa, lakini wanaojenga barabara hawalijui hili? Wanatengeneza mitaro ya kupitisha maji, wakijua kwamba kuna siku maji yanaweza kuja kwa kasi kubwa, la kushangaza ni kwamba mitaro hii ndiyo iliyobomoka!

Inashangaza pia watu kujenga kwenye mkondo wa maji. Watanzania wanaamini kwamba maji yanawakimbia watu! Sasa wametambua kwamba maji hufuata mkondo wake. Maji yamebomoa kuta na kusomba vitu vingi vya thamani. Mtu anaweza kujiuliza je tatizo liko wapi, watu kujenga kwenye mkondo wa maji? Mbona Dar-es-Salaam bado ina maeneo makubwa?

Hadi leo idadi ya watu waliokufa haijulikani. Wengine wanasema ni 20, wengine wanasema ni 50! Serikali inasema ni 20, lakini watu walioshuhudia mafuriko haya wanasema watu waliokufa ni wengi kiasi cha kufikia hata 100. Kinachoshangaza hapa ni kwamba anayeweza kujitokeza kusema ukweli wa jambo hili, ataitwa mchochezi. Gazeti  lolote likijitokeza kuandika ukweli wa idadi ya watu waliokufa inayokinzana na ile ya serikali, litaonekana kuwa ni gazeti la uchochezi na linaweza kufungiwa!

Tukiachana na hili la mafuriko, yako mambo mengine yanayoshangaza sana katika taifa letu na bora kuyatafakari kwa pamoja na kutafuta tatizo lilipo ili tuweze kusonga mbele kama taifa. Kabla ya mvua hii ya mafuriko tulikuwa na tatizo la mafuta. “Wakubwa” wanaouza mafuta waliamua kuyaficha na kuacha kutoa huduma hii. Hatujashuhudia polisi wakiendesha msako wa kuwashika “wakubwa” na kuwapeleka mbele ya sheria; maana hawa ni wachochezi wakubwa wanataka watu waichukie serikali yao na matokeo yake ni kuleta vurugu; watu hawa wanahujumu uchumi wa nchi, siku tatu bila mafuta mambo mengi yanakwama na uzalishaji unazorota. Mtu anaweza kujiuliza tatizo liko wapi? Kwanini polisi wasiwakamate “wakubwa” hawa? Badala yake tunasikia waandishi na wahariri wa vyombo vya habari wanakamatwa kwa uchochezi. Badala ya kuwakamata watu wanaoficha mafuta, wanaopandisha  bei ya sukari, wanaoiba wanyamapori na kuwasafirisha nchi za nje wanamkamata Mwigamba, anayeandika makala katika gazeti hili. Makala kama hii ninayoiandika inaweza kuleta uchochezi zaidi ya mtu anayeficha mafuta na kupandisha bei ya sukari? Tatizo liko wapi hapa?

Ni watanzania wangapi wataisoma makala hii ninayoiandika sasa hivi? Nikikamatwa na kuwekwa ndani kwa uchochezi, ni imani yangu kwamba idadi kubwa ya watu wataisoma makala hii. Kama ilivyotokea kwa Mwigamba; sina uhakika kama mapolisi wengi waliisoma makala ile ilipoandikwa, lakini la uhakika ni kwamba baada ya Mwigamba kushikwa na kuwekwa ndani, makala hiyo imesomwa na karibia polisi wote. Hivyo yule aliyemkamata Mwigamba ndiye  mchochezi kama kweli makala ile ina aina yoyote ile ya uchochezi.

Tanzania ina mambo mengi ya kushangaza. Siku chache kabla ya kamata kamata ya waandishi na wahariri Jukwaa la wahariri Tanzania lilikutana kujadili amani. Mkutano uliwashangaza wengi, maana ulionekana kutokuwa na agenda. Waandishi wa habari wanaweza kudumisha amani kwa kuandika ukweli bila kuongeza chumvi au kuegemea upande mmoja. Hawawezi kuzuia matukio, hii ni kazi ya watu wengine. Ni wazi wao kama watanizaia walikuwa na haki ya kujadili amani ,lakini si kujadili hivyo kama wahariri. Nafasi yao ya kukutana na kujadili ni kama hivi walivyokamatwa waandishi  na wahariri. La kushangaza ni kwamba hatujasikia Jukwaa la wahariri likikutana na kukemea mbinu hizi  mpya za kuwaziba midomo waandishi wa habari.

Nimetaja machache tu yanayoshangaza kwenye taifa letu, lakini yako mengi mfano chama tawala CCM kutembea kifua mbele na kujigamba kwamba kina ridhaa ya kutawala kutoka kwa watanzania; tuko watanzania milioni 40, waliojiandikisha kupiga kura ni milioni 20, waliopiga kura ni milioni 8, na CCM ikawapata kama milioni tano hivi – ni asilimia ngapi ya watanzania? Mtu unaweza kujigamba kwamba chama kinapendwa?

Nimalizie makala hii kwa kutaja pia jambo hili linaloshangaza zaidi la huu ugonjwa wa kutotaka kukosolewa. Huu ni ugonjwa wetu sote watanzania. Ukimkosoa mtu, wewe ni adui! Hatupendi kuambiwa ukweli! Wenye imani zao wanasema Ukweli, utatufanya Uhuru! Basi wakati wa sikukuu hizi za mwisho wa mwaka, tukae pamoja kama taifa na kutafakari na kujifunza kukubali ukweli.

Nawatakia wasomaji wangu Christmas njema na mwaka mpya wenye baraka na mafanikio.
Na,
Padri Privatus Karugendo.

 

0 comments:

Post a Comment