“EBYENZU” NA “OBUTURA” NI HATARI KWA UCHUMI WA MKOA WA KAGERA. Msimu wa kuuza kahawa mkoani Kagera umeanza. Ni wakati wa neema kwa wakulima wa kahawa, madalali, makampuni ya kununua kahawa, halmashauri za wilaya Bukoba, Muleba, Misenye, Karagwe na Kyerwa. Pia huu ni wakati wa neema kwa wafanyabiashara wote maana mzuguko wa fedha unakuwa mkubwa wakati huu wa msimu wa kahawa. Kahawa ndilo zoa kuu la biashara Mkoani hasa katika Wilaya za Bukoba, Muleba, Karagwe na Ngara. Kwa hiyo, haiwezekani kuzungumzia maendeleo yoyote ya kiuchumi na ya kijamii yaliyowahi kupatikana katika wilaya hizi bila kutaja KAHAWA. Msingi wa maendeleo ya elimu na kijamii yaliyopatikana miongoni mwa wananchi wa wilaya hizi, ni kahawa. Umaarufu wa maendeleo ya Ushirika katika Mkoa huu tangu zama za ukoloni ulitokana na kahawa. Kwa hiyo mifumo (Ebyenzu, Obutura na magendo) na matukio yanayoathiri uzalishaji wa kahawa mkoani Kagera ni matukio ya kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wanaotegemea zao hili. Hali kadhalika, hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa ili kuwezesha kufufua na kuongeza uzalishaji wa kahawa mkoani ni hatua za kuwakomboa wananchi wa mkoa huu. Kwa kufanya hivyo, uchumi wa wananchi utaimarika. Naandika makala hii nikiwa Karagwe, nikishuhudia jinsi watu wanavyoanza kukimbizana kuuza na kununua kahawa. Mhudumu(Msichana) wa kuuza pombe alisikika akipiga simu huku na kule (Bukoba, Mwanza na Kahama) akiwahamasisha wenzake kuhamia Karagwe: “…Nawambia mje haraka huku Kayanga-Karagwe, tukazitafune fedha za wanyambo. Msimu umeshika kasi, leta “vimini” na “vitopu” vya kutosha”. Makampuni ya kununua kahawa yanaanza kusambaza wakala na madalali vijijini kununua kahawa. Wakulima nao wanaanza kuvuna kahawa na kuwa na matumaini ya kupata fedha ili waweze kupambana na maisha. Ni wazi zao la kahawa linachangia kiasi kikubwa uchumi wa mkoa wa Kagera na taifa zima kwa ujumla. Na kama serikali ingesimamia vizuri kuuza na kununua kahawa, maisha ya wakulima wa kahawa yangeboreka zaidi na serikali ingekushanya mapato ya kutosha kutokana na zao hili la kahawa. Sasa hivi uzimamizi wa kuuza na kununua kahawa ni mbaya ndiyo maana wakati bei ya kahawa inaendelea kupanda katika soko la dunia, wakulima wanaendelea kuuza kahawa yao kwa bei ya chini na serikali haipati mapato ya kutosha kutokana na kahawa. Jambo la kusikitisha ni kwamba mawakala, madalali, makampuni na vyama vya ushirika vinanufaika kiasi kikubwa kutokana na zao la kahawa kuliko wakulima na serikali. Makampuni na vyama vya ushirika wanapanga bei ya kununua kahawa kwa mkulima kutokana na bei ya soko la dunia na kwa vile usimamizi ni mbaya, mkulima hapati taarifa ya bei ya kahawa kwenye soko la dunia. Mawakala na madalali nao wanapanga bei zao kutokana na bei iliyopangwa na makampuni na vyama vya ushirika. Ni wazi mkulima ndiye anayepata bei iliyo chini kabisa na mpaka sasa hivi hakuna chombo cha kumtetea mkulima ili apate bei nzuri. Mbali na makampuni na vyama ushirika kumnyanyasa mkulima kwa upande wa bei ya kununua kahawa, kuna mambo kama matatu yanayowanyonga wakulima wa kahawa. Mambo haya ni “Ebyenzu”, “Obutura” na Magendo. “Obutura” ni mfumo wa kuuza kahawa ambayo haijavunwa na wakati mwingine ambayo hata haijakomaa. Na wakati mwingine kuna wakulima wanaoaamua kuuza kahawa yao miaka mitatu mbele. Anapewa fedha ya miaka mitatu. Ina maana kwa kipindi chote cha miaka mitatu, mkulima anakuwa na kazi ya kutunza shamba, ukifika w akati wa msimu, madalali wa kununua kahawa wanakuja kuvuna na kuuza kahawa kwa makampuni na vyama vya ushirika. Kutokana na ugumu wa maisha,baadhi ya wakulima wa kahawa wanaamua kuuza kahawa yao kwa mfumo huu wa “Obutura”. Mawakala na madalali wa kununua kahawa wanathamanisha kahawa iliyo shambani kwa kufuata bei ya msimu uliopita. Msimu ukifika, wao wanaivuna kahawa hiyo na kuuza kwa bei ya msimu mpya. Kwa vile bei ya Kahawa, inapanda kila mwaka, mkulima anayeuza kahawa yake kwa njia hii ya “Obutura” anapata hasa kubwa. Yeye anaiuza kahawa yake shambani kwa bei ya msimu uliopita, wanaoinunua wanaiuza kwa bei ya ya juu ya msimu mpya. Watu wengine (Makampuni, madalali na vyama vya ushirika) wananufaika kutokana na jasho lake. “Ebyenzu” ni mfumo wa kuuza kahawa unaofanana kidogo na “Obutura” lakini kuna tofauti. Huu ni mfumo wa kuuza kahawa iliyoiva tayari, lakini bila kuikausha. Sheria ya kuuza kahawa, inamtaka mkulima avune kahawa yake, aikaushe na kuiuza. Kutokana na ugumu wa maisha, wakulima wa kahawa wanaamua kuuza kahawa yao bila kuikausha. Sasa hivi, wanunuzi wa kahawa wananunua gunia la “Ebyenzu” kwa bei ya shilingi elfu hamsini. Kahawa hiyo hiyo, kama mkulima angeikausha mwenyewe na kuiuza angepata shilingi laki moja. Hivyo kutokana na mfumo huu wa “Ebyenzu” mkulima anapoteza shilingi elfu hamsini au tuseme mkulima anayeuza kahawa kwa mfumo huu anapoteza nusu ya mapato yake ya msimu mzima wa kuuza zao la kahawa. Mbali na wakulima kupata hasara kubwa kwa kuuza kahawa kwa mfuo huu wa “Ebyenzu” hata na jamii nzima inapata hasara. Kahawa ikiuzwa kwa mfumo huu haina makato ya kuchangia huduma za kijamii kama ilivyo kwa kahawa inayouzwa kupitia vyama vya ushirika. Kahawa ikiuzwa kupitia vyama ushirika, kuna makato ya kuendeleza vyama hivyo na michango mingine ya kutunisha mfuko wa Halmashauri za wilaya ili ziweze kutoa huduma za kijamii kama kujenga mashule na kuboresha barabara za vijijini. Makampuni na madalali wanaonunua kahawa, wanapendelea mfumo huu wa “Ebyenzu” maana wao baada ya kukausha kahawa wanayoinunua kwa mfumo huu, wanakuwa na faida mara mbili au zaidi. Magendo, ni mfumo wa kuiuza kahawa nje ya nchi. Mfumo huu umekuwepo kwa miaka mingi. Kwa wingi kahawa ya mkoa wa Kagera inauzwa kwa magendo nchi jirani ya Uganda. Kwa kiasi kidogo inauzwa Burundi na Rwanda. Inaaminika kwamba nusu ya kahawa inayozalishwa mkoa wa Kagera inauzwa kwa magendo. Wakulima, wanaupenda sana mfumo huu wa kuuza kahawa kwa magendo, maana wanapata bei nzuri. Kila mwaka bei ya kahawa nchi za jirani inakuwa juu zaidi ya bei yetu. Na hiki kinakuwa kishawishi kikubwa kwa wakulima kuuza kahawa yao kwa magendo. Magari mengi yaliyozagaa Karagwe, yamepatikana kwa kuuza kahawa Uganda kwa njia za magendo. Majumba mazuri yaliyo karagwe yamepatikana kwa kuuza kahawa Uganda kwa njia za Magendo. Na mafanikio haya, si kwa vile watu wanapenda kufanya magendo, hapana, ni kwa vile Bei ya Uganda ni nzuri.Bei iko juu! Labda kama bei ya kahawa, hapa kwetu ingekuwa nzuri, watu wasingefanya biashara ya magendo. Kusingekuwa na haja ya kutumia polisi kudhibiti uvushwaji wa kahawa. Kwa kutokujua, wakulima wanapendelea sana mfumo huu wa magendo na wanaushabikia sana. Ukweli ni kwamba mfumo huu ni mbaya zaidi, maana kahawa ikiuzwa kwa magendo, taifa letu linapoteza fedha za kigeni. Bila kuwa na fedha kigeni uchumi wa taifa utayumba, na uchumi wa taifa ukiyumba kila mtu anaguswa ,hata huyule anayeuza kahawa yake kwa magendo na kupata fedha nyingi. Jambo la kusisitiza hapa ni kwamba, kahawa inayouzwa kwa magendo si ile iliyo kaushwa tu, bali hata “Ebyenzu” na “Obutura”. Watu kutoka nchi jirani, wanaingia mkoani Kagera, na kununua mashamba ya kahawa kwa miaka miwili au mitatu. Msimu ukifika wanakuja kuvuna na kuivusha kahawa “yao” nchi jirani. Hata sasa hivi ninapoandika makala hii, hapa Karagwe, kuna watu kutoka nchi jirani wanavuna kahawa “yao”. Serikali mkoani Kagera, imeimarisha ulinzi wa kuzuia magendo. Mtu yeyote anayetaka kufanya biashra ya kununua kahawa mkoani Kagera, kwa maana ya kupata kibali kutoka halmashauri za wilaya, ni lazima achangie shilingi milioni moja za kulimarisha ulinzi wa magendo. Inasemekana kwamba kuna na michango mingine ya shilingi laki moja ya vikao vya kujadili mbinu za kudhibiti magendo. Mmoja wa wanunuzi wa Kahawa niliyehojiana naye kwa sharti la kutolitaja jina lake kwenye makala hii, alilalamikia michango hii ya kuimarisha ulinzi wa magendo, alisema “…bila kuwa na bei nzuri ya kahawa hapa kwetu, bila serikali kufanya jitihada ya kuhakikisha mifumo ya “Ebyenzu” na “Obutura” inakomeshwa ni vigumu magendo kuisha. Wakulima wataendelea kutafuta bei nzuri. Ni vigumu kutumia bunduki kulinda magendo katika nchi ambayo karibu kila mtu ana ugumu wa maisha. Askali wetu nao wana maisha magumu, ni lazima watalainishwa na fedha ya magendo ya kahawa. La msingi ni kuweka mifumo mizuri ya kuuza na kununua kahawa na magendo itakufa yenyewe”. Watu wengi nilihojiana nao kuhusu swala hili la magendo ya kahawa, walikuwa na mawazo yanayofanana, kwamba kulinda magendo kwa mtutu wa bunduki ni kupoteza wakati, maana kadiri ulinzi unavyoimarishwa ndivyo kasi ya kuuza kahawa kwa magendo inavyoongezeka. Kama alivyosema mnunuzi wa kahawa hapo juu kuna haja ya kutengeneza mfumo mizuri wa kuuza na kununua kahawa na kuhakikisha bei ya kahawa ni nzuri zaidi ya ile ya nchi za jirani. Kwa njia hii tunaweza kupambana na magendo ya kahawa na inawezekana ikaisha kabisa. Pia kuna haja kubwa ya serikali kukomesha mifumo hii ya “Ebyezu” na “Obutura” ili wakulima masikini wa vijijini waweze kunufaika kiasi kikubwa na zao hili la Kahawa. Nina imani wananchi wakiona kahawa zao zinachangia kujenga Zahanati, zinachangia kujenga mashule, zinachangia kutengeneza barabara nzuri, zinachangia kuleta maji na maendeleo mengine hawawezi kuziiuza tena kwa magendo , “Ebyenzu” ua “Obutura”. Bei ya kahawa ikiwa nzuri, watu wakapata fedha za kujenga majumba ya kisasa na kuishi maisha bora hawawezi kuuza kahawa yao nje ya nchi. Hakutakuwa tena na haja ya kutumia Polisi, kudhibiti uvushwaji wa kahawa kwenda Uganda. Lakini wananchi wasipoona matunda ya kahawa yao, bei ikiendelea kuwa chini wakati nchi ya jirani bei iko juu, ni lazima wataendelea kuivusha! Wanaweza kufikia hatua ya kusema liwalo na liwe. Na, Padri Privatus Karugedo. +255 754 6331 22

0 comments:

Post a Comment