DAKIKA 45 NA SELEMANI SEMUNYU Kipindi cha dakika 45, kinachorushwa na ITV na kuendeshwa na Selemani Semunyu, ni kipindi muhimu katika jamii yetu. Kwa mtizamo wa haraka kipindi hiki ni kama jukwaa la majadiliano, ni jukwaa ambalo viongozi na watu mbali wanaweza kulitumia kufafanua mambo mbali mbali katika jamii yetu. Tunahitaji majukwaa mengi ya namna hii, na hasa wakati huu tunapoelekea kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya. Selemani Semunyu amejitahidi kukiendesha na kuwauliza maswali ya uchokonozi viongozi ambao hadi leo hii wamejitokeza kwenye kipindi chake na wengine wakirudi zaidi ya mara mbili. Mawaziri na manaibu mawaziri waliohojiwa na Semunyu, wameweza kujibu maswali kwa umahiri mkubwa ingawa si mara zote wametoa majibu ya kuridhisha sana. Viliporushwa vipindi vya kwanza, niliandika makala juu ya kipindi hiki na Selemani Semunyu, alinitumia ujumbe wa barua pepe kunipongeza kwa makala hiyo na kunitaka ushauri juu ya kipindi chake. Nilimshauri ili kipindi kiwe kizuri na kiwavutie wengi, yeye mwongozaji asionyeshe upande wake. Nafikiri amejitahidi sana kwa hilo. Bahati mbaya au nzuri wakati ule sikufahamu vizuri mwelekeo wa kipindi chake, vinginevyo ningeweza kumshauri mengi pamoja na yale nitakayoyaongelea kwenye makala hii. Kipindi cha dakika 45, kilipoanza kilikuwa na mvuto mkubwa, ila kadri siku zinavyokwenda mvuto huu unapungua. Labda haya ni maonjo yangu, lakini nina imani kama kungekuwepo na muda wa watu kupiga simu na kuuliza maswali, kipindi hiki kingeendelea kuwa na mvuto mkubwa. Mara nyingi watu wanavutiwa jinsi mtu anayohangaika kutafuta majibu ya maswali na mvuto unakuwa mkubwa zaidi pale mtu anapoweza kuyajibu maswali ya papo kwa papo kwa umahiri na wakati mwingine akitoa takwimu, majina ya watu, majina ya sehemu mbali mbali, inafurahisha kuona mtu anafahamu kile anachokifanya na kukisimamia. Mpangilio wa sasa wa kipindi hiki wa Selemani na mhojiwa wake, unakipunguzia kipindi hiki mvuto na hasa pale inapoonekana kwamba Selemani anaandaa maswali kabla na kuyajadili na mhojiwa wake. Pia kipindi kinapungua mfuto kwa kuwarudia watu wale wale na kuongea mambo yale yale kana kwamba Tanzania ina upungufu wa watu wa kulitumia jukwaa hili la dakika 45. Kitu kingine kinachopunguza mvuto wa kipindi hiki ni kwamba wote wanaohojiwa au tuseme walihojiwa hadi leo hii ni watu wenye majukwaa mengi ya kutoa mawazo yao. Tanzania kuna watu wengi wasiokuwa na jukwaa la kuongelea. Lakini mawaziri na wabunge wetu wana majukwaa mengi. Bunge letu ni jukwaa kubwa ambalo watu hawa wanaweza kulitumia, mikutano ya Halmashauri ni jukwaa jingine na wana nafasi pia ya kuitisha mikutano ya hadhara, lakini cha kusitisha yale wanayoyasema kwenye kipindi cha dakika 45, hatuwasiki wakiyasema Bungeni na kwenye majukwaa mengine niliyoyataja hapo juu. Kwa nini mtu aonekane mwenye busara na hekima kwenye kipindi cha dakika 45, na kubaki bubu Bungeni? Mipango mizuri na yenye matumaini inayoelezwa kwenye kipindi hiki cha dakika 45, mbona hatuisikii ikielezwa kwenye majukwaa mengine? Mbona hatuwasiki waheshimiwa wakitembelea majimbo yao ya uchaguzi na kumwaga sera kama zile wanazozimwaga kwenye kipindi cha dakika 45? Badala ya kipindi hiki cha dakika 45 kuzungumzia mambo ya -kijamii yanayowagusa watanzania wote, inaelekea kipindi hiki kinalenga kuwajenga watu binafsi kwa malengo yao ya mbele. Hata maswali ya Selemani Semunyu, yanaonyesha kuwa na lengo la kumwongoza mhojiwa kujitangaza na kujinadi. Ni mpango wa Semunyu na wahojiwa wake, au inatokea bahati mbaya? Haya ni maswali ambayo watanzania wakisimama kidete na kuisusia ITV, majibu yatapatikana tu! Tanzania tunashambuliwa na ugonjwa wa mdudu asiyeonekana, mdudu huyu ni mdogo sana kuonekana kwa macho, lakini ni mdudu wa hatari maana anatutafuna pole pole na mwishowe tutabaki mifupa mitupu. Mdudu huyu ni uchu wa madaraka. Kila tukimaliza uchaguzi mkuu wenye uchu wa madaraka hawakai chini kupanga mbinu na mikakati ya kuliendeleza taifa letu, bali wanaanza mbinu mbali mbali za kuingia au kuendelea na madaraka miaka mitano ijayo. Mdudu huyu anakwamisha mambo mengi ya maendeleo. Kama kipindi hiki cha dakika 45, kimekumbwa na mdudu huyu au kilianzishwa kwa lengo la kumsambaza na kumlea mdudu huyu, ni bora watanzania tukakipiga vita na kukisusia. Kabla ya kuandika makala hii, nilimtumia barua pepe Selemani Semunyu, kutaka ufafanuzi juu ya kipindi chake. Bahati mbaya mpaka dakika hii ninapoandika makala hii sikupata jibu la barua pepe. Inawezekana anashindwa kujibu kwa vile yeye si mwanzilishi wa kipindi hiki? Yeye ni mwajiliwa? Anafanya kazi apate mshahara ili aweze kuyaendesha maisha yake na familia yake; watanzania wengi tunafanya hivyo, hatuangalii, kuchunguza na kuyatafakari yale tunayoyafanya kazini kwetu na kwingineko yana manufaa gani kwa jamii nzima. Au labda Selemani yuko “Bize” kama tulivyo watanzania wengi. Natumai Selemani na wote wanaohusika watasoma makala hii na kunipatia majibu. Hata wasiponipatia majibu, maana mimi ni nani? Basi wachukue hatua ya kubadilika vinginevyo siku si nyingi jamii ya watanzania itawasusia! Kama nilivyosema hapo juu, kilipoanzishwa kipindi hiki nilifikiri hili ni jukwaa la majadiliano. Kwa maana kwamba yeyote mwenye mchango wa kulijenga taifa letu anaweza kupatiwa dakika 45, akaelezea mipango yake na mchango wake katika taifa. Nilitegemea viongozi wetu wote wa serikali, wa kidini, wa kijadi, wa vyama vya upinzani na viongozi wa vyama visivyo vya serikali, wangepata nafasi kwenye kipindi hiki cha dakika 45. Tulitegemea kuwaona maaskofu na mashehe wakihojiwa na Selemani Semunyu kwenye kipindi chake cha dakika 45. Tulitegemea pia tuone viongozi wetu wa jadi wakihojiwa na kuelezea misimamo ya imani zao na mchango wao katika jamii yetu ya Tanzania. Tulitegemea kuwaona wanaharakati na viongozi wa mashirika yasiyokuwa kiserikali wakihojiwa na Selemani Semunyu. La kushangaza, na ndiyo maana nauliza, kipindi hiki kimegeuka kuwa cha Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali. Ndiyo maana nilitaka kujua malengo ya kukianzisha kipindi hiki kabla ya kuandika. Kama kilianzishwa kwa lengo la kuwa Jukwaa la Mawaziri na viongozi wa Serikali, swali langu litakuwa tofauti na aswali langu la msingi, na kama labda serikali ndo mdhamini wa kipindi hiki kwa maana kwamba serikali inakilipia, pia swali langu litakuwa tofauti. Hata kama kipindi hiki kingekuwa kinaendeshwa na TBC ambacho ni chombo cha serikali, na ikafanya kama wanavyofanya ITV, kuendeleza propaganda za serikali na chama tawala, swali langu la msingi lingekuwa bado lina uzito. TBC inaendeshwa kwa kodi ya watanzania wote, hivyo si haki kujigeuza kuwa chombo cha propaganda za serikali na chama chake. Hata hivyo chombo cha serikali kazi yake ni kuwaunganisha wananchi kwa kuwapatia haki sawa ya kusikika. Swali langu la msingi ni je Kipindi cha dakika 45 cha Selemani Semunyu ni kipindi cha propaganda kipindi cha kuelezea mafanikio ya serikali? Ni sauti ya serikali na chama tawala? Na kama jibu ni ndiyo, je ni utaratibu wa chombo binafsi kama ilivyo ITV, kuwa chombo cha propaganda kwa serikali iliyo madarakani? Na je chombo hiki kama kinafanya kazi ya kuendesha propaganda, kinashiriki katika kujenga amani na utulivu katika taifa letu la Tanzania. Hapa hoja ya propaganda kuwa nzuri au mbaya si ya msingi. Hoja ya msingi ni chombo binafsi kuruhusiwa au kujiamulia kufanya propaganda za serikali. Wasi wasi hapa ni kwamba kama vyombo vingine vikiamua kufanya propaganda za kidini, propaganda za vyama vya siasa na propaganda za ukabila tutafika? Tunaambiwa kwamba kule Rwanda ,mauaji ya kimbali yalisambaa nchi nzima kwa kuchochewa na vyombo binafsi vya habari vilivyoamua kufanya kazi ya propaganda za serikali. Ni hatari kubwa vyombo binafsi vya habari kujiingiza kwenye propaganda za serikali au kuhubiri chuki za kiimani. Tanzania tunaelekea kufumbia macho hatari hii kubwa iliyo mlangoni. Mbali na ITV kuendesha propaganda za serikali, vimeibuka vyombo vya habari ambavyo kazi yake kubwa ni kuzitukana dini nyingine. Vyombo hivi vipo, vinajulikana na vinaendelea na matusi, serikali imekaa kimya ikisubiri kuwakamata waandishi wa habari wachochezi. Hivi kuna uchoche mbaya kama huu wa vyombo vya habari kutumika kuzitukana imani za watu wengine? Au dhambi hii ya chombo binafsi kuendesha propaganda za serikali iliyo madarakani? Propaganda inaweza kuwa nzuri ama mbaya kufuatana na malengo ya propaganda hiyo. Nchi kama China na Korea, ziliendesha propaganda na bado zinaendesha propaganda kwa lengo la kuendeleza nchi zao, na kusema kweli nchi zao zimeendelea. Sisi hapa Tanzania tunaendesha propaganda kwa faida ya nani? Zingekuwa ni propaganda za kujenga umoja wa kitaifa, mtu atafumba macho na kusema ITV, iendelee na propaganda za Serikali. Zingekuwa ni propaganda za kujenga uchumi, mtu atafumba macho na kusema ITV, iendelee na propaganda za serikali na chama tawala. Uchumi wetu ni mbaya kabisa, serikali iliyo madarakani imeshindwa kufufua uchumi. Shilingi yetu inazama kila siku. Maisha ni magumu na mfumuko wa bei unashika kasi ya kutisha. Migomo ya kila aina imekuwa ni sehemu ya maisha ya watanzania, leo wanagoma walimu, wanafunzi na vituo vya mafuta kesho wanagoma madreva, keshokutwa ni madaktari nk. Tumesikia malalamiko kwamba kuna watu tena ambao ni viongozi wamepewa sumu. Yote hayo ni kugombea madaraka. Tulimsikia Rais wa nchi ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha CCM, akisema ndani ya chama chake kuaminiana kumepungua. Watu wanaogopa kupeana sumu, “kulogana” na kusukiwa mizengwe. Chama chenye matatizo makubwa hivi, kinaweza kuendesha propaganda za kutaka kuendelea kuwa madarakani kutawala kwa faida ya nani? Je, ni mimi mwenye matatizo na kipindi hiki cha dakika 45? Inawezekana wengine wanakiona “Poa”? Au kuna wengine wanaoziona kasoro hizi nilizozitaja na labda kuna kasoro nyingine zaidi? Kama nilivyochukua jukumu la kushika kalamu na kuandika, ndivyo ninavyochukua jukumu la kuwakaribisha wasomaji wangu kushiriki katika mjadala huu wa dakika 45. Je kipindi hiki ni cha propaganda? Tujadili! Na, Padri Privatus Karugendo.

1 comments:

Anonymous said...

The King Casino | Situs Judi Slot Online Terbaik 2021
Play online Pragmatic Play Slots https://septcasino.com/review/merit-casino/ at The King 출장마사지 Casino - Member Baru 메이피로출장마사지 & Terpercaya 2021! Rating: 98% · ‎240,388 바카라사이트 votes

Post a Comment