BARABARA TUNAZIJENGA, TUTAZITUNZA NA KUZIKARABATI!
Nianze makala hii kwa kuishukuru serikali yetu kwa kazi nzuri ya kuzijenga barabara zetu kuu kwa kiwango cha lami. Nina mashaka kama kuna Mtanzania asiyeona juhudi hizi na kuzifurahia. Ni wazi kila kizuri ni lazima kitaibua na mabaya pia. Wale wanaoguswa na bomoa bomoa ili kupanua barabara zetu na hasa sehemu za mijini ni lazima wazitizame juhudi hizi za ujenzi wa barabara kwa jicho baya. Hata hivyo mwisho wa siku ni lazima Wema uwe juu ya mabaya. Mwanzoni mwa mwezi huu wa nne nimesafiri kwa gari kutoka Dar-es-salaam, hadi Mwanza kwa barabara nzuri ya lami. Pia nimekwenda hadi Sengerema, nikarudi na kusafiri tena kutoka Mwanza, Morogoro, Mbeya hadi Tunduma kwa barabara ya lami. Safari yangu ilikuwa inaishia Sumbawanga. Ingawa kutoka Tunduma hadi Sumbawanga, si barabara ya lami, lakini ujenzi wa barabara hii unaendelea na sehemu nyingine za barabara hii tayari zina lami. Inajengwa barabara ya lami kutoka Tunduma hadi Mpanda.
Mtu unaweza kutoka Mtukula, hadi Tunduma kwa barabara ya lami, unaweza kutoka Songea hadi Arusha kwa barabara ya lami. Pia barabara ya Singida hadi Arusha kwa lami inatengenezwa, na Dodoma Hadi Iringa inatengenezwa. Pia nasikia na Tabora hadi Kigoma iko mbioni kujengwa ama ujenzi umeanza? Hizi ni juhudi za kupongezwa. Ingawa ni muhimu kuwa macho ili juhudi hizi zisimeze hitihada za kuendeleza reli na usafiri wa anga. Nchi nyingi zilioendelea duniani, zimetumia sana usafiri wa reli, maji na anga. Hivyo na sisi ni lazima tuweke juhudi katika njia zote za usafirishaji na muhimu sana ni hitaji la kufufua kwa nguvu zote usafiri wa reli.
Nyongeza ya hapo ni kwamba, ni muhimu pia Serikali yetu kutupia macho barabara za vijijini. Kuna ulazima mkubwa wa kuboresha barabara za vijini ili wananchi wapate njia ya kusafirisha mazao yao kwenda sokoni. Hatuwezi kuongelea kilimo kwanza kabla ya kuboresha usafiri wa vijijini. Mfano Kutoka Wampembe kwenda Namanyere, wilaya ya Nkasi ni kilomita 96, inamchukua mtu masaa matano kusafiri kilomita hizo. Barabara ni mbaya kupita maelezo. Hakuna usafiri wa basi wala magari madogo. Kuna tajiri mmoja ndiye ana lori analolitumia kubeba mizigo na abiria. Mama mja mzito akipatwa na tatizo la kukimbizwa hospitali ya wilaya Namanyere, ni baraa tupu! Kawaida wanatumia radio call, kuita gari la hospitali, maana huko Wampembe hakuna mawasiliano ya simu. Gari linatumia masaa matano kwenda na masaa matano kurudi. Katika hali kama hii ni vigumu kuokoa maisha ya mama na mtoto. Watu wa Wampembe wanasema kwamba Waziri Mkuu Mheshimiwa Pinda, aliwatembelea na kuwahahidi kuwatengenezea barabara na kuwaletea mawasiliano ya simu, lakini hadi leo hii hakuna kilichotendeka. Pia, eti na Mama Pinda, aliwatembelea na kuwahakikishia kwamba usafiri na mawasiliano vitawafikia, lakini bado ni ndoto. Bila kujenga barabara imara na nzuri ni vigumu kuleta maendeleo ya haraka kwa vijiji vya Wampembe, Mwinza na Kizumbi na vijiji vinginevyo vya Tanzania.
Pamoja na ubovu wa barabara ya kwenda Wampembe, pamoja na ukweli kwamba huduma kama vile dawa, maji, walimu, mawasiliano, kutokuwa na soko la uhakika la kuuza mazao yao, bado kuna ofisi ya Mapato (TRA) katika kijiji cha Wampembe. Wapo kule wanakusaya mapato, lakini barabara na maisha ya watu vinabaki kuwa ni vitu vya anasa. Serikali inaendelea kuwakamua na kuwavyonza watu wake bila kuangalia hali ya maisha na kutafuta mbinu za kupambana na ugumu wa maisha.
Ingawa Barabara ya kwenda Kabwe, pia wilaya ya Nkasi, ni nzuri kidogo. Lakini ukishafika huko ziwa Tanganyika, kuna vijiji huwezi kuvifikia kwa barabara mpaka utumie mtumbwi. Usafiri huu wa mitumbwi si salama, maana nyingi haina vifaa vya kuokolea maisha. Lakini pia ni fedha nyingi kukodisha mtumbwi kutoka Kabwe, kwenda vijiji kama vile Mpenge. Bei yake si chini ya elfu 80, kama mama mwenye mimba ana matatizo, kumsafirisha kwa mtumbwi kutoka Mpenge hadi Kabwe na baadaye kwa gari hadi Namanyere, si chini ya laki moja. Ni wananchi wachache wanaoweza kulipa fedha hiyo. Matokeo yake ni mama au kichanga kupoteza maisha.
Natoa mifano ya Sumbawanga na Nkasi, kwa vile naandika makala hii nikiwa Sumbawanga. Lakini ukweli ni kwamba, pamoja na jitihada za serikali yetu kutujengea barabara kuu kwa kiwango cha lami, bado kuna hitaji la haraka la kujenga barabara za vijijini ili wakulima waweze kufikisha mazao yao kwenye soko na hili huduma nyingine kama vile kwenda hospitali ziwafikie wananchi kwa haraka.
Nilipokuwa nikisafiri kutoka Dar- Mwanza, na Mwanza, Mrogoro, Mbeya hadi Tunduma, swali langu kubwa lilikuwa: Tunazijenga barabara hizi, je tutazitunza na kuzikarabati? Swali hili lilinijia baada ya kuona barabara zetu zinaharibika haraka. Sehemu nyingine zinaharibika ndani ya miaka miwili. Mlima wa Sekenke, barabara imeharibika kabisa. Nilishaandika juu ya Barabara kuu ya Chato-Muleba, hii iliharibika kiasi cha kutilia shaka juu ya Mkandarasi na aliyeipokea barabara hii. Kwa msemo wa kisasa, hao wote ni lazima wawajibishwe! Na maeneo mengine ya Morogoro Dodoma, Makambako – Mbeya, imeharibika. Inaonyesha kwamba magari yenye mizigo mizito yanapita kwenye barabara zetu. Inaonyesha kubonyea na kutengeneza matuta. Kuna sababu mbili kubwa za kusababisha jambo hili. Moja, inawezekana makandarasi walijenga barabara zetu chini ya kiwango, pili ni sisi kuruhusu magari yenye mizigo mizito kupita kwenye barabara zetu.
Kama makandarasi walizijenga barabara hizi chini ya viwango vinavyokubalika kimataifa ni lazima atafutwe mchawi wetu. Vinginevyo ni hatari kushindwa kuzikarabati barabara hizi ambazo tumezijenga kwa fedha nyingi. Hili likitokea itakuwa baraa kubwa maana heri mara mia kutumia barabara ya vumbi kuliko kutumiaya lami yenye mashimo.
Lakini pia kama tunaruhusu magari yenye mizigo mizito ni lazima hapa afichuliwe mchawi wetu. Barabara hizi zina vituo vingi vya mizani. Je mizani hii ipo kama mapambo au inafanya kazi yake? Kama gari limezidisha uzito ni lazima kulipa faini. Matumaini yangu ni kwamba faini hizi zingekuwa zinatumika bila kusubiri kufanya ukarabati wa barabara maeneo yanayoharibika kutokana na uzito wa magari. Kusubiri barabara hizi zikaharibika kiasi cha kusababisha msongamano wa magari barabarani ni hatari kubwa. Huku twendako, tutashindwa kuzikarabati barabara hizi.
Mheshimiwa Magufuli, amefanya kazi nzuri ya kutukumbusha ubora na umuhimu wa kuwa na barabara za lami. Lakini kazi hii hawezi kuifanya peke yake. Ni lazima sote, wanawake, wanaume, vijana wasichana na vijana wavulana, kuonyesha hudi za pamoja katika kulijenga taifa letu na hasa kuwa macho kwa wale wanaotaka kutuharibia barabara zetu. Tushirikiane kuwafichua wale wanaohongwa fedha ili kuruhusu magari yenye mizigo mizito kutembea juu ya barabara zetu na kuziharibu.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment