Wasomaji wangu nianze
makala hii kwa kuwatakia Heri ya mwaka mpya. Tumshukuru Mungu kwa wema wake
kutuvusha kuingia mwaka wa 2012. Ni kwa neema
na huruma yake na si kwa ubora wetu tumeendelea kuishi. Ninawashukuru
wote pamoja na Mhariri wangu walionitumia matashi mema ya mwaka mpya kwa ujumbe
mfupi wa simu ya kiganjani, niungame wazi kwamba sikushindwa kujibu ujumbe kwa kila mmoja aliyenitumia
bali naendeleza mgomo wangu niliouanza miaka miwili iliyopita wa kutotuma
ujumbe mfupi wakati wa Christmas na mwaka mpya. Sababu yangu ya msingi ni
kupinga utamaduni huu wa kuyatajirisha makampuni ya simu za viganjani wakati wa
sikukuu. Ni wazi makampuni haya yanatunyonya kila siku, hivyo ni bora kupunguza
mirija yao wakati wa sikukuu. Kama kutojibu ujumbe wenu kuliwakwaza, mnisamehe. Naomba makala hii basi iwe jibu
la ujumbe wenu wa matashi mema ya mwaka mpya.
Kama nilivyotaja hapo
juu tumeruhusiwa kuendelea kuishi hapa duniani kwa neema na huruma ya Mungu na
si kwa ubora wetu. Kuna watu bora zaidi yetu wameshindwa kuiona 2012. La msingi
ni kwamba kwa vile tupo ni lazima tutoe mchango wetu wa kuifanya dunia hii kuwa
bora zaidi kwa kila kiumbe. Ni imani yangu kwamba hatukuruhusiwa kuishi ili
tuendelee kula kunywa tu bila kutoa mchango wowote ule. Hatukurusiwa kuendelea
kuishi ili tuyatafute madaraka kwa gharama zozote zile ili tuwagandamize na
kuwanyanyasa ndugu zetu wanyonge badala ya kuwaongoza na kuwaelekeza. Dunia ya
leo ina changamoto nyingi, bila kujaliwa hekima na busara, tutaivuruga dunia
yetu na tutalivuruga taifa letu. Badala ya kutumia nguvu zetu kutafuta mali,
fedha na madaraka, ni muhimu kuelekeza nguvu zetu zote kutafuta hekima na
busara.
Tanzania, tunauanza
mwaka huu wa 2012 tukiwa na changamoto nyingi; kuna suala la katiba, bunge
kuyumba, uporaji wa ardhi, vurugu ndani
vyama vya siasa, unyanyasaji wa kijinsia, vurugu kwenye vyuo vyetu vikuu,
vurugu kwenye dini zetu, urais wa 2015 nafasi ni moja lakini mamia ya watu
wanaitaka nafasi hii, uhaba wa chakula, mfumuko wa bei na kigugumizi cha
kufanya maamuzi magumu na mengine mengi. Tumeshuhudia serikali ikitaka kutumia
nguvu kubwa kuwahamisha watu wa Jangwani, wakati serikali hiyo hiyo inashindwa
kutumia nguvu hizo kuhamia Dodoma. Mpango wa kuhamia Dodoma ni wa miaka mingi,
lakini hadi leo hii Serikali imeshindwa kuhama kwa visingizio vinavyoelekea
kufanana na vile vya watu wa Jangwani. Swali ni je, watu wa Jangwani wakihama
na serikali ihamie Dodoma? Zile nguvu zitakazotumika kuhamisha watu wa Jangwani
zitumike pia kuihamisha serikali kwenda Dodoma?
Tumeshuhudia Serikali
ikitumia nguvu zake kuwakamata “Wachochezi” waandishi wa habari na wahariri na
kushindwa kutumia nguvu hizo hizo kuwakamata wafanyabiashara wa mafuta
wanaoificha nishati hiyo na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi hadi
kufikia kule Musoma lita moja ya petroli kununuliwa shilingi elfu kumi! Kuna
uchochezi zaidi ya huu wa kuificha nishati hii na kuwachonganisha wananchi na
serikali yao? Usafiri unakuwa taabu na shughuli za uzalishaji zinakwama. Kwa
maneno mengine watu hawa ni wahujumu uchumi. Serikali iko kimya na nguvu zake
hazionekani kuwakamata na kuwaweka ndani hawa wahujumu uchumi.
Tumeshuhudia serikali
ikitumia nguvu zake kuyazuia maandamano ya wananchi wanaotaka kufikisha ujumbe
wao kwa njia ya amani na wakati huo serikali hiyo hiyo inashindwa kuwakamata
wafanyabiashara wanaopandisha bei ya sukari. Serikali ilitamka kwamba bei ya
sukari isiwe juu ya shilingi elfu moja na mia saba. Nenda madukani leo hii uone
bei ya sukari.
Wakati serikali inataka
kutumia nguvu kuwahamisha watu wanyonge wa Jangwani, kila Mtanzania anashangaa
serikali hiyo hiyo kushindwa kuwakamata watu walioingia Benki Kuu na kuiba.
Ilipobainika kwamba kuna wezi, wao wakajitokeza na kukiri kwamba waliiba, na
kwa dharau kubwa “ wakarudisha” fedha walizoziiba, haijulikani pamoja na riba au walirudisha kiasi kile kile?
Hawakukamatwa! Wako huru hadi leo hii. Serikali yenye nguvu, yenye Jeshi la
polisi inashindwa kuwakamata wezi wanaojitangaza wazi, tena wezi wa mabilioni
ya shilingi, badala yake inawakamata
waandishi wa habari na wanafunzi wanaofanya maandamano kudai mikopo ya elimu ya
juu?
Hoja hapa ni kwamba
tumeuanza mwaka na changamoto kubwa. Kwa vile ni nyingi, nijikite kwa suala
hili la Jangwani. Nimemsikia Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam, akisema kwamba “
Watu wa Jangwani wasipokubali kuhama kwenda Mabwepande, watatambua nguvu za
serikali”. Maana yake ni kwamba wataitumia polisi kuwahamisha watu hawa. La
kushangaza hawajaitumia polisi kuihamisha Serikali kutoka Dar-es-Salaam na
kuhamia Dodoma! Hawajaitumia polisi kuwakamata wahujumu uchumi!
Siandiki makala hii
kuwatetea watu wa Jangwani, najua wako pale kinyume na sheria pamoja na ukweli
kwamba viwanja vyao vimepimwa na wana hati miliki, bali mimi naandika kushangaa
jinsi Hekima na Busara kutotumika. Serikali ina makosa, ilivipima viwanja hivyo
ikijua kwamba huo ni mkondo wa maji. Wananchi nao wana makosa kuvikubali
viwanja hivyo wakijua kwamba ni mkondo wa maji. Maafa yametokea, nini
kifanyike? Mungu, anaturuhusu kuendelea kuishi kutumia bunduki na virungu
kuleta amani na maendeleo, au kutumia hekima, busara na majadiliano? Serikali
imesikiliza hoja za watu wa Jangwani? Inajua sababu zinazowasukuma kutaka
kuendelea kuishi pale pamoja na tishio la mafuriko? Tamko la Mkuu wa Mkoa la
kutaka kuwahamisha watu wa Jangwani kwa nguvu linaonyesha wazi kwamba tunaishi
dunia mbili tofauti. Kuna dunia ya wanyonge na dunia ya wakubwa. Mtu ambaye ana
mshahara wake, ana posho zake, ana nyumba ya kifahari ambayo hata mafuriko
yakiingia, maji yananyonywa haraka kwa mashine, ana gari la bei mbaya, manunuzi
yake ni kwenye maduka makubwa na wakati mwingine nje ya nchi, akiugua hata
mafua anakimbizwa India na Uingereza hawezi kuelewa na kuguswa na maisha ya
watu wa Jangani.
Watu wa Jangwani ni wa
hali ya chini, wanaishi Jangwani si kwa kutaka bali kwa kulazimishwa na hali ya
maisha: wanaishi karibu na soko, wanaishi karibu na wateja. Wengi wao ni
mamantilie, ni machinga, changu doa, ni waosha magari, ni mafundi wa magari na
piki piki na kazi nyingine ndogo ndogo ambazo hazipatikani Mabwepande. Hawa
tishio la maisha yao si mafuriko bali ni uwezo wa kuishi siku hadi nyingine.
Kufikiri kwamba wanakataa kuhama kwa ujeuri, ni kuonyesha wazi kwamba hatufahamu
mazingira yao na tunaishi dunia mbili tofauti.
Mtu wa Jangwani anauza
mchicha wake Kariakoo, na kujipatia fedha za kusogeza maisha yake, anapika
chakula na kuwauzia madreva wa daladala. Mtu wa Jangwani anapata kibarua kwenye
majengo haya yanayojengwa usiku na mchana ndani ya Jiji la Dar-es-Salaam, mtu
wa jangwani anapata kazi ya ulinzi, mtu wa Jangwani ni konda kwenye magari, mtu
wa Jangwani anafanya kazi za nyumbani kwenye majumba ya matajiri, mtu wa
Jangwani anafanya usafi barabarani, mtu wa Jangwani inaishi siku hadi nyingine
kutegemea uwanja mkubwa wa matumaini unaomzunguka. Uwanja huu wa matumaini
hawezi kuupata kule Mabwepande. Nguvu za serikali zikitumika kuwahamisha
matokeo yake ni kuzitenganisha familia. Wanawake na watoto watakaa Mabwepande
wakipata shida, wanaume na vijana watarudi Dar-es-Salaam kutafuta maisha kwenye
uwanja mkubwa wa matumaini. Hili likitokea serikali haiwezi kukwepa lawama za
kuwanyanyasa wanawake na watoto.
Hoja kwamba watu wa
Jangwani wamejenga kwenye mkondo wa maji haina msingi kwa dunia yetu ya leo.
Kule Holland, watu wanaishi baharini, si mkondo tu bali wanayafukuza maji na
kutengeneza makazi ya watu. Serikali inayowajali watu wake itaubadilisha mkondo
wa maji kuwa makazi bora kwa kutengeneza miundombinu. Hata Jangwani kama
kungekuwa na miundombinu mafuriko yasingeonekana. Hata hivyo kwa nini wahame
wa Jangwani na wasihame wa Msasani, wa
Sinza, wa Tandale na Tabata Kisiwani? Huku kote yalikuwa mafuriko, watu na mali
zao walisombwa na maji. Kwa nini zoezi la kuhama linaelelekewa kwa watu wanyonge wa Jangwani?
Je wakihama maeneo hayo
yatabaki wazi au tutashuhudia maghorofa yakijengwa? Je haiwezekani hizi ni
mbinu za wajanja wachache kutaka kuwahamisha watu wa Jangwani ili kuliacha eneo
hilo wazi kwa wawekezaji ambao watakuja na utaalamu wa kisasa wa kutengeneza
miundombinu na kuubadilisha mkondo wa maji kuwa makazi bora? Na hili likitokea
Serikali haiwezi kukwepa lawama za kuwatelekeza watu wake na kuwakumbatia
wawekezaji wa nje.
Busara si kuwahamisha
watu, bali ni kutengeneza miundombinu na kuyajali maisha yao. Wakati serikali
inataka kutumia nguvu kuwahamisha watu wa Jangwani kwa lengo la kuwaponyesha
mafuriko, ikumbuke kwamba kule Mabwepande, watakufa kwa magonjwa, watakufa kwa
njaa na wengine watauwa wakiiba, maana bila kazi ya kujipatia kipato na hasa
kwa vijana watajiingiza kwenye ujambazi na mwisho wake ni kifo. Serikali
inataka watu hawa wahamie Mabwepande ndani ya Juma moja kuanzia sasa. Je huko
Mabwepande kuna hospitali? Kuna maji?
Kuna shule? Maana watoto wa Jangwani, walikuwa wakisoma shule za mjini.
Wataweza kutoka Mabwepande, na msongamano na nauli kuja kusoma mjini?
Ni wazi kuna shinikizo
la shule kufunguliwa, maana wahanga wa mafuriko wako kwenye shule. Hata hivyo serikali ina maeneo mengi ambayo
inaweza kuyatumia kuwatunzia watu hawa kwa muda mpaka pale mipango mizuri
itakapo fanyika. Kuna lile jengo kubwa la Machinga, ambalo serikali ilijenga
kwa fedha nyingi lakini machinga kwa sababu zao za msingi( machinga anamfuata
mteja na si mteja kumfuata machinga) wamekataa kuhamia. Jengo hili linaweza
kutumika kuwapatia makazi ya muda wahanga wa mafuriko, ili waendelee na
shughuli zao na watoto wao wasome shule badala ya kutumia nguvu kubwa kuwahamishia Mabwepande, zoezi ambalo matokeo
yake hayawezi kuwa mazuri.
Tunapouanza mwaka huu wa
2012, pamoja na changamoto nyingi, tupige magoti mbele za Mwenyezi Mungu na
kuomba atujalie hekima na busara, atujalie kipaji na uwezo wa kuishi kwa
kufuata sheria za nchi, tuishi kwa kuwaheshimu binadamu wenzetu na kutambua
haki zao za msingi; sote ni binadamu tunahitaji makazi bora, tunahitaji huduma
bora, tunahitaji furaha na amani rohoni. Mungu atujalie uwezo wa kuongozwa na
uzalendo na kulipenda taifa letu la Tanzania. Heri ya mwaka mpya wa 2012.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment