AJALI ZINAKATISHA MAISHA
YA WATANZANIA.
Tarehe 14.1.2012 siku
ambayo ajali ya barabarani iliyakatisha maisha ya Mheshimiwa Regia Mtema,
mbunge wa viti maalum kupitia chama cha CHADEMA, ilikuwa ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwangu nikiwa nimefikisha miaka 56.
Ndugu, jamaa na marafiki walinitumia salaam za matashi mema, wengine
walinipongeza kuvuka wastani wa kuishi wa Mtanzania, tunaambiwa kwamba miaka 43
ndo wastani wa kuishi wa Mtanzania? Mimi na wengine tuliovuka wastani wa kuishi
wa Mtanzania tunawajibika kumshukuru Mungu, maana si kwa ubora wetu bali kwa
Neema yake; rafiki zangu wa mtandao wa Facebook ndo walitia fora maana hadi leo
nilikuwa nimepokea ujumbe wa matashi mema ya “Birthday” kutoka kwa watu mia
tatu hamsini. Kati ya hao, rafiki yangu kutoka Tabora alinitumia ujumbe
ufuatao: “ Karugendo, hongera kufikisha miaka 56 ya kuzaliwa, kumbuka kadiri
miaka inavyoongezeka ndivyo unavyolikaribia kaburi..”
Nami nikamjibu; “ Asante kwa matashi mema. Zamani tulifikiri
kulisogelea kaburi inaendana na umri mkubwa, ila siku hizi mambo ni tofauti.
Vijana wanakufa kwa ajali, ukimwi na magonjwa mengine yanayosababishwa na
kemikali zinazochanganywa kwenye vyakula, vinywaji na dawa bandia..”
Kabla sijamaliza kusoma
salaam zangu za “Birthday” nilipata habari za kushutusha na kusikitisha za kifo
cha Mbunge Regia Mtema, kijana ambaye kufuatana na mawazo ya rafiki yangu wa
Tabora, umri wake 32? ulikuwa si wa kulikaribia kaburi. Alikuwa bado mdogo,
alikuwa ana matumaini ya kuendelea kuishi miaka mingi mbele, wanaomfahamu
vizuri wanasema alikuwa amepania mwaka huu uwe ni wa kuwahamasisha vijana
kufanya kazi. Alitaka kuwashawishi vijana kuachana na tabia za kukaa vijiweni na kutegemea miujiza
kutoka Mbinguni. Maisha yake yamekatishwa na ajali ya barabarani. Inasikitisha
sana Taifa kumpoteza kijana aina ya Regia Mtema, ambaye alionyesha wazi kuwa na
hazina kubwa ya kuchangia maendeleo ya taifa letu la Tanzania.
Mbali na kumfahamu
Mheshimiwa Regia Mtema, kupitia kwenye vyombo vya habari na kushuhudia mchango
wake wa mawazo katika matukio mbali mbali na hata Bungeni, alikuwa rafiki yangu
katika mtandao wa “Facebook”. Yeye ni kati ya watu walionitumia ujumbe wa
matashi mema wakati wa kukumbuka ya siku
ya kuzaliwa kwangu. Ni imani yangu kwamba ujumbe huo aliuandika muda
mfupi kabla ya kuanza safari yake hiyo iliyoyakatisha maisha yake. Aliniombea
maisha marefu na kunihakikisha kwamba
vijana wanafuata nyayo zetu sisi wazee katika harakati za kulijenga
taifa letu la Tanzania. Wakati nikiusoma ujumbe wa Regia Mtema, kumbe yeye
alikuwa akiaga dunia.
Mheshimiwa Slaa, Katibu mkuu wa Chadema wakati akitoa
rambi rambi kwenye vyombo vya habari alisema kifo cha Regia Mtema,
kimewasononesha na kuleta huzuni kwa taifa zima, lakini kwa vile ni mpango wa
Mungu, hatuwezi kuhoji. Namheshimu sana Dk Slaa, na ninatambua vizuri uwezo
wake wa kujenga hoja na kuzisimamia. Ninafahamu vizuri kwamba yeye ni mwanateolojia aliyebobea.
Bahati mbaya ni kwamba theolojia yake hii ya “Kazi ya Mungu haina makosa”,
“Bwana ametoa, Bwana ametwaa”, imepitwa na wakati! Kadiri siku zinavyosonga mbele na mwanadamu anakimbizana na
maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia ni lazima tuwe na theolojia
inayokwenda na wakati. Najua siku nikikutana na Dkt Slaa tutabishana juu ya hoja hiii hadi kieleweke!
Mbali na Dkt Slaa,
ukisikiliza ujumbe unaotolewa redioni na kuandikwa kwenye magazeti ni ule ule
wa “Kazi ya Mungu, haina makosa”. Hivyo mawazo kama haya ninayoyatoa
yanayoelekea kuhoji kazi ya Mungu, ni lazima yatapokelewa na hisia tofauti.
Ninalijua hili, lakini ni lazima awepo wa kuanzisha. Na kawaida kuanzisha kitu
si kazi nzuri sana, maana kuna kutukanwa mambo yakienda vibaya. Kitulizo ni
kwamba kilichoandikwa kimeandikwa. Leo watatukana na kuweka pembeni, lakini kesho
na keshokutwa watasoma na kufurahi.
Mambo mengi
yanayokatisha maisha ya watu hapa Tanzania, si mpango wa Mungu na wala si kazi
ya Mungu, bali ni kazi yetu sisi wenyewe. Jambo hili ni lazima tulieleze bila
kuogopa maana kinyume na hapo ni kuendelea kuwapumbaza watu. Ajali kama hii
iliyokatisha maisha ya Mheshimiwa Regia Mtema, si mpango wa Mungu. Ni dhambi
kubwa kusema kwamba huu ni mpango wa Mungu. Kama barabara ya kutoka
Dar-es-Salaam hadi Morogoro, ingekuwa ni ya njia nne, ajali kama hii ya Regia Mtema
na nyingine nyingi zinazotokea kila wakati kwenye barabara hii zisingetokea.
Wataalamu wanasema kufuatana wingi wa magari yanayotoka na kuingia
Dar-es-Salaam kila siku ya Mungu, ni uzembe kuendelea kuwa na aina ya barabara
tuliyonayo kwa sasa ya magari kupishana. Tunataka tusitake ni lazima ajali
zitaendelea kutokea. Ajali zikitokea, tunasema
Mpango wa Mungu hauna makosa? Na kwamba hatuwezi kuhoji kazi ya Mungu!
Theolojia ya aina hii ni ya kuwekwa pembeni kabisa! Mungu anatuumba tuwe na
uzima tena tuwe nao tele! Mpango wa Mungu ni uzima tele, kinyume na hapo ni kutoka kwa yule mwovu!
Tunaachia magari mengi
yanaingizwa nchini, bila kuwa na mpango wa kupanua barabara, tunategemea nini?
Kama si foleni, basi ni ajali za kila siku. Ni makosa makubwa kusema foleni na ajali zinazosababishwa na uzembe
wetu wa kushindwa kupanua barabara zetu miaka hamsini baada ya uhuru wetu, ni
kazi ya Mungu na haina makosa.
Namkumbusha Dkt Slaa,
kitu anachokijua mwenyewe. Ni lazima tusimame na kuhoji ni kwa nini maisha ya watanzania
yanaendelea kupotea kwenye ajali za barabarani. Tukifanya hivyo, haina
maana imani yetu imekwenda tenge,
kuhoji kazi ya Mungu. Ni haki yetu kuhoji tena kwa ukali. Mungu amefanya yote,
ameiumba Tanzania ikiwa na rasilimali nyingi, ametupatia akili ya kuzaliwa na
kipaji cha kujifunza mambo mapya na kuwa wavumbuzi, ametupatia uwezo wa
kuutiisha ulimwengu. Iweje leo hii tunashindwa kuwa na barabara nzuri, kubwa na
pana zinazoweza kuruhusu magari kukimbia bila kukutana wala kugusana. Tatizo
letu ni kupanga vipaumbele. Tukiyaweka maisha ya watanzania kuwa kipaumbele
namba moja, ni lazima ajali za barabarani zitakoma.
Ni lazima tusimame na
kuihoji serikali yetu iliyo madarakani: Je maisha ya watanzania ni kipaumbele
namba moja? Mtu akifa kwa ajali ni lazima tuhoji kwa ukali kabisa, Albino
akichinjwa ni lazima tusimame na kuhoji, hatuwezi kusema kwamba kuyakatisha
maisha ya albino kwa imani za kishirikina ni kazi ya Mungu, mtu akifa kwa
malaria ni lazima tuhoji kwa ukali, watoto wachanga wakipoteza maisha ni lazima
tusimame na kuhoji kwa ukali, mwanamke akipoteza maisha wakati wa kujifungua ni
lazima tusimame na kuuliza kwa ukali kabisa. Katika dunia hii ya maendeleo ya
sayansi na teknolojia mwanamke kupoteza maisha wakati wa kujifungua si kazi ya
Mungu, ni kazi yetu sisi. Ni lazima tuijutie na kupiga magoti kuomba toba kwa
muumba wetu.
Tunaachia dawa bandia
zinaingizwa nchini. Watu wanazitumia dawa hizi, matokeo yake wanaugua kansa na
magonjwa mengine ya hatari. Wakifa, tuseme ni mpango wa Mungu, hauna makosa na
haturuhusiwi kuhoji? Baadhi ya vyakula tunavyonunua madukani vimejaa kemikali
za hatari. Hatuna mpango imara wa kudhibiti vyakula hivi, ili kuhakikisha ni
salama kwa matumizi ya binadamu. Wale wanaohusika na kupima vyakula hivi
wakihongwa vijisenti kidogo wanaachia vinapita na kusambaa nchi nzima. Samaki
wa mionzi kutoka Japan walifika hadi Morogoro! Kesho na keshokutwa vyakula hivi
vikisababisha vifo tuseme ni mpango wa Mungu, kwamba bwana ametoa, na bwana
ametwaa, jina lake lihimidiwe milele! Theolojia hii ni ya kutupwa kabisa na
isionekane tena hapa duniani. Sina lengo la kupinga nguvu za Mwenyezi Mungu.
Ninafahamu kwamba yeye ni Muumba wa Mbingu na nchi, ambaye anaumba
vinavyoonekana na visivyoonekana. Hoja yangu ni kwamba hata yale ambayo Mungu ameyaweka kwenye himaya yetu,
tukishindwa kuyatekeleza kwa uzembe wetu, tunayasukuma kwake.
Tunaruhusu matairi
bandia yanaingizwa nchini. Matairi haya yakipasuka, magari yakapinduka na watu
wakafa, tuomboleze kwa kusema ni mpango wa Mungu: Bwana ametoa, bwana ametwaa? Kusema kweli ajali na vifo vingi
hapa Tanzania ni vya kujitakia na wala si mpango wa Mungu. Tunamsingizia mungu
kwa uzembe wetu na kukwepa wajibu wetu wa kuzipanua barabara zetu.
Tunamsingizia Mungu kwa uzembe wetu wa kushindwa kudhibiti bidhaa bandia.
Tunashabikia magari ya
mitumba na kununua vitu chakavu. Waheshimiwa wabunge walijadili na kupitisha
sheria ya kununua vitu vichakavu. Wanataka tununue magari ya mitumba, meli za
mitumba ndege za mitumba. Vitu hivi vichakavu vikileta hatari na kusababisha
maisha ya watanzania kupotea, tuseme ni Kazi ya Mungu haina makosa? Ni kukwepa
wajibu wetu na kumbebesha Mungu huyu mizigo isiyokuwa ya kwake.
Kifo cha Regia Mtema,
kimetusikitisha na kutuletea majonzi makubwa. Kama alivyosema Mheshimiwa Zitto Kabwe, huyu alikuwa mbunge kijana
ambaye ndo ilikuwa mara yake ya kwanza kuingia Bungeni, alikuwa na mpango wa
kufanya mambo mengi, lakini maisha yake yamekatishwa kwa ajali ya barabarani.
Wale wanaofuatilia mambo ya siasa za Tanzania, watakubalia na mimi kwamba
Mheshimiwa Regia Mtema, alikuwa hafungwi na mipaka ya chama chake. Alikuwa ni
mbunge aliyekuwa akitetea haki za walemavu, vijana na wanawake wote wa
Tanzania, bila kuangalia chama.
Mheshimiwa Rais Jakaya
Kikwete, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na viongozi wengine wa
serikali na vyama vya siasa wamemsifia Marehemu Regia Mtema, kuwa miongoni mwa
wa wazalendo wa Tanzania wenye jitihada binafsi za kuleta umoja na mshikamano
katika taifa letu. Wazalendo wanaolitanguliza taifa mbele kabla ya kitu
chochote kile. Wanatanguliza taifa kabla ya chama chao cha siasa, wanatanguliza
taifa kabla ya tumbo lao na familia
zao.
Hivyo wakati tunamlilia
Regia Mtema, tuache utamaduni huu wa Kazi ya Mungu haina makosa. Tukubali
makosa yetu, tukubali kwamba kwa namna mmoja ama nyingine tumechangia kifo cha
Kijana huyu na wengine wanaokufa kwa vifo vinavyoweza kuzuilika. Uchungu
tulionao utusukume kuanza kufanya maamuzi ya kulijenga taifa letu lenye
viwango. Mungu amlaze mahali pema
peponi ndugu yetu, rafiki yetu, mwanaharakati na mzalendo wa kweli wa Tanzania
Mheshimiwa Regia Mtema. Amina.
Na,
0 comments:
Post a Comment