UHAKIKI WA KITABU: UTANDAWAZI NA WEWE 1. Rekodi za Kibibliografia. Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni UTANDAWAZI NA WEWE, Kimeandikwa na TGNP. Mchapishaji wa kitabu hiki ni MTADNAO WA JINSIA TANZANIA (TGNP) wenyewe kwa ufadhili wa DANIDA na wamekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987- 600- 14- X Kitabu kina kurasa 33 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. Utangulizi Utandawazi, wengine wanasema ni Utandawizi! Utandawazi kwa Kiingereza ni “globalisation”, ni mchakato unaowezesha nchi mbali mbali duniani kuwasiliana, kuhusiana na kutegemeana. Mazingira hayo yanaleta maingiliano na mifanano kiutamaduni kijamii, kisiasa na kiuchumi. Utandawazi unakuwepo pale mipaka kati ya nchi na nchi inapokuwa si vikwazo kwa biashara na maingiliano mengine ya kijamii, kiutamaduni na hata kisiasa. Mathalani dunia kwa ujumla imekuwa kama kijiji kimoja kwa kuwa watu wa nchi moja wanaweza kuwasiliana na watu wa nchi nyingine na kuwekeza mitaji kwa urahisi. Lakini kwa watu wengi hususani wenye kipato cha chini bado hawawezi kunufaika na maendeleo hayo. Yapo maelezo mengi juu ya utandawazi. Lakini yote hayo ni maneno. Kwa kifupi Utandawazi ni ukoloni mambo leo, utandawazi ni ubeberu. Bila kuwa makini na kuelewa kwa undani mfumo huu, tutatawaliwa tena; zamu hii ni kutawala mawazo yetu na kutuibia rasilimali zetu kwa kisingizio cha dunia kuwa kijiji kimoja. Kijitabu hiki kinalenga kuchangia mjadala kuhusu sera za kimataifa na athari zake kwa sera na mipango ya kitaifa. Pia kinajaribu kubainisha athari za utandawazi kwa wananchi wanawake kwa wanaume, na mapambano dhidi ya ukandamizwaji. Aidha kinaeleza juu ya madhara ya mfumo dume katika jamii, mfumo ambao unapendelea kundi dogo katika jamii. Kitabu kimegawanywa kwenye sehemu tano, kina picha na michoro inayosaidia kufikisha ujumbe kwa haraka. Kabla ya kufanya uhakiki wa kitabu hiki ningependa kuelezea mazingira yanayokizunguka. III. Mazingira yanayokizunguka kitabu Hivi leo duniani kote kuna kilio cha kutaka Dunia mbadala. Hivyo kuna mapambano ya kutaka Dunia mbadala katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Katika ngazi ya kitaifa vita hii inaelekezwa katika kupigania haki sawa kwa wanawake na wanaume, kumiliki, kuendesha na kunufaika na rasilimali za taifa; wananchi kushiriki kikamilifu katika masuala ya uchumi; kushiriki michakato yote ya kitaifa kama vile kuandaa bajeti, kuunda sheria na kutengeneza sera; kuelewa sera za kimataifa na kuzitafsiri katika lugha nyepesi ya kueleweka kwa wananchi wote; kufanya utafiti wa kina juu ya utandawazi na kuelewa vizuri; Kuyaumbua makampuni ya kimataifa ambayo yanahusika na uhamishaji wa mitaji na faida, utajiri na rasilimali zingine au uvunjaji wa haki za binadamu na uharibifu wa mazingira; kujenga nguvu na sauti ya pamoja: kati ya Asasi Zisizo za Kiserikali, Vyama vya wafanyakazi, wanafunzi, wanahabari na wananchi wa vijijini ili kupinga sera za kikandamizaji za utandawazi. Na mapambano haya ya kutaka Dunia mbadala katika ngazi ya kimataifa yaelekezwe katika: Kupigania haki ya kuhakikisha kwamba teknolojia na uvumbuzi mwingine vinakuwa mali ya jumuiya ya kimataifa kwa manufaa ya watu wa nchi zote; tajiri masikini; kinyume na sasa ambapo ujuzi huo unamilikiwa na matajiri wachache na kutumika kama kigezo cha kuwatawala na kuwanyanyasa wengine; Kushinikiza Taasisi za Biashara na fedha ili zizingatie na kujali maslahi ya watu wa nchi masikini; Kushinikiza uwazi na mabadiliko ya namna ya kupata viongozi kwenye Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia; Kupigania kufutwa madeni ya nchi masikini bila masharti; Kudai mazao na bidhaa toka nchi masikini kupata bei bora katika masoko ya kimataifa; Kujenga sauti ya pamoja kupitia mitandao yote duniani inayolilia uhitaji wa Dunia mbadala. Mwalimu Nyerere, alisema “ Tatizo la kweli la dunia ya leo si umasikini; maana tunao ujuzi na mali zinazotuwezesha kuufuta umasikini. Tatizo lenyewe hasa ni mgawanyiko wa binadamu katika tabaka mbili, tabaka ya matajiri, na tabaka ya masikini. Jambo hilo ndilo linaloleta matatizo, vita na chuki kati yetu” TGNP wamekuwa mstari wa mbele katika mapigano haya ya kutaka Dunia mbadala. Kijitabu hiki ni sehemu ndogo ya mapambano yao. Wamekuwa wakifanya mambo mbali mbali kama mijadala ya wazi, matamasha na maandamano ya amani ili kufikisha ujumbe wa uhitaji wa dunia mbadala. Na leo hii ujumbe huu wameupisha katika kijitabu hiki cha Utandawazi na Wewe. Mtandao wa Jinsia Tanzania, TGNP, ni Taasisi huru ya kiraia inayojihusisha na utetezi juu ya masuala ya usawa wa Kijinsia. Mtandao umeanza kazi zake mwaka 1993. Toka wakati huo, TGNP imeimarika na kuwa madhubuti katika ushawishi na kutetea usawa wa kijinsia na mabadiliko ya kijamii ndani na nje ya Tanzania. Maono au taswira ya TGNP ni kuona jamii ya Kitanzania inayozingatia usawa wa kijinsia, kuwepo fursa sawa, na upatikanaji wa umilikaji wa rasilimali kwa raia wote, wanawake kwa wanaume. Tangu 1999, Mtandao wa Jinsia Tanzania, kwa kushirikiana na Wanaharakati wa Jinsia (FemAct), imesisitiza juu ya utengenezaji wa bajeti ya taifa kwa mtizamo wa kijinsia. Mafanikio makubwa ya TGNP na Washirika wake katika kampeni hii ni pamoja na kukubalika kwa mpango huu na Serikali ambapo TGNP wanaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu na kushinikiza uingizwaji wa sauti za wanyonge na vionjo vya kijinsia kwenye sera ya bajeti. TGNP pia imewezesha kuanzishwa kwa harakati za kijinsia katika ngazi za wilaya na mikoa kupitia mitandao ya Jinsia Ngazi ya Kati. Mitandao ya Jinsia Ngazi ya kati iko katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Zanzibar, Lindi, Mtwara, Dodoma. Katika ngazi ya wilaya Mitandao iko Mbeya, Liwale, Kisarawe, Kinondoni na Kondoa. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari. IV. Muhtasari wa Kitabu Kitabu kimegawanyika katika sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza inajadili chanzo na historia ya Utandawazi; hapa tunasikia juu ya Utandawazi ni nini, tunasikia juu ya Uzabizabina wa utandawazi na kupata historia nzima ya utandawazi. Kwa kifupi kapisa katika sehemu hii tunaelezwa kwamba utandawazi ni hatua za kupanga uchumi wa dunia upya kwa ajili ya manufaa na faida ya mabepari wachache. Na kwamba kuna Utandawazi wa kibepari, ambao unajali faida kuliko utu, huu ni ule unaolenga kutaka na kutawala uchumi wa dunia kwa manufaa na maslahi ya makampuni ya kimataifa na nchi tajiri. Kwa upande mwingine kuna Utandawazi wa kiutu, huu ni mchakato unaozileta nchi mbali mbali na tofauti kuwa karibu kwa lengo la ustawi wa nchi hizo; mfano jinsi wafugaji walivyokuwa wakipata chakula kwa kubadilishana mazao ya ufugaji (maziwa, nyama, mbolea) na wakulima. Tungeweza kufanya utandawazi huu wa kiutu kwa kubadilishana teknolojia, ujuzi na maarifa. Katika sehemu hii ya kwanza tunaelezwa pia Uzabizabina wa Utandawazi. Wakati inaimbwa kwamba Utandawazi ni kutengeneza kijiji kimoja. Tunashuhudia kijiji hiki kikigawanyika sehemu mbili ya wababe na wanyonge. Wakati utandawazi unaimba wimbo wa kufungua mipaka ya nchi zote ili tuwe kijiji kimoja, nchi za magharibi zinafunga mipaka kwa kisingizio cha ubora wa bidhaa na usalama. Wakati utandawazi unaimba kuondoa ruzuku kwa wakulima, nchi za magharibi zinatoa ruzuku kwa wakulima wao. Wakati utandawazi unaimba wimbo wa kuheshimu uhuru wa kila nchi, tumeshuhudia nchi kama Iraq, Afghanistan na sasa Libya zikivamiwa kwa maelekezo na faida ya mataifa makubwa. Utandawazi unaimba wimbo wa kutunza mazingira, lakini hadi leo hii Amerika imekataa kupunguza wingi wa viwanda vyake vinavyoongeza joto duniani. Huu ni uzabizabina wa Utandawazi. Pia katika sehemu hii ya kwanza tunaelezwa historia ya Utandawazi kuanzia Pax Britannica hadi Pax Americana. Pax Britanica ulikuwa ni mfumo wa kiuchumi wa Waingereza kuanzia 1789 hadi 1970, walisambaza sera za biashara huria duniani kote bila kujali kama nchi zote zilikuwa makoloni yake. Utandawazi ulichukua sura mpya baada ya vita kuu vya pili vya dunia 1945. Na hii ndiyo ilijulikana kama Pax Americana. Amerika iliendesha mfumo wa uchumi duniani, lakini hadi miaka ya 70 mfumo huu ulianguka kwa sababu ya gharama kubwa ya vita vya Vietnam. Miaka ya 80 Rais Reagan wa Amerika na Waziri Mkuu wa Uingereza Bi.Margareth Thatcher walitoa mwanya wa makampuni kutoa huduma na kuendesha uchumi. Utandawazi wa kibepari ulitanuka na kushamiri kwa sababu ya:  Kuibuka kwa Taasisi za Fedha na Biashara za Kimataifa  Kuporomoka kwa siasa za Kisoshalisti kule Urusi na Ulaya Mashariki  Kuanguka kwa siasa za kibaguzi za Afrika Kusini  Kujiondoa au kupungua kwa majukumu ya serikali katika kusimamia, kuratibu na kuongoza uchumi  Kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano  Kupanuka na kuimarika kwa teknolojia ya usafirishaji  Kuongezeka kwa upinzani Dhidi ya Utandawazi wa kibepari na kibeberu. Sehemu ya pili ya kitabu hiki tunaelezwa juu ya dhana ya Ukweli kuhusu utandawazi: Je, ni kweli kwamba Utandawazi unatuweka katika kijiji kimoja cha dunia? Jibu ni ndiyo na hapana! Teknolojia inapanuka na kuwanufaisha watu wachache. Tumeambiwa kwamba asilimia 14 ya watanzania ndo wanapata umeme, matumizi ya Internet nayo ni kwa wachache. Simu za kiganjani, zimesambaa na kuongeza umasikini mkubwa kwa wale wenye uwezo wa kuzinunua. Ni kuwa kwenye kijiji chenye matabaka! Kwa ufupi ni kwamba Utandawazi ni propaganda za mabepari. Nchi masikini hususani za Afrika ni lazima ziwe makini na propaganda hizi za mabepari na uchu wao wa kuchota utajiri wa Afrika. Rasilimali na utajiri wa Afrika vina ukomo wake kwa kuwa havidumu milele. Hivyo ni vyema kuwa macho kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa maendeleo ya watanzania. Sehemu ya tatu ya kitabu hiki tunaelezwa juu ya vinara wa Utandawazi na madai ya wanaharakati. Hapa tunaelezwa juu ya vinara wa Utandawazi wa kibepari ambao ni: Shirika la Biashara Duniani (WTO),Makampuni ya Kibiashara ya Kimataifa, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF). Taasisi hizi ndiyo hasa huzilazimisha nchi masikini kulegeza masharti ya biashara, kuuza au kubinafsisha viwanda na sekta nyingine za huduma na kuandaa mazingira kwa wafanyabiashara wa kimataifa kupenya na kunufaika na rasilimali za nchi masikini. Asasi za Kiraia zinataka shirika la Biashara duniani liwe shirika lenye kuzingatia demokrasia na usawa kwa nchi zote; mikataba na mazungumzo ya WTO yazingatie kulinda wananchi kaika nchi masikini na tajiri; vyombo vya maamuzi na mikutano ya WTO bado imetawaliwa na mfumo dume zaidi. Hivyo maamuzi yanayofikiwa bado hayazingatii mahitaji na athari za kijinsia zinazotokana na biashara za kimataifa. Pia Asasi za Kiraia zinataka Benki ya Dunia na IMF ziwe na uwakilishi wenye uwiano bora kwenye Bodi zake za utendaji na kuondolea kwa kura ya Veto ya Marekani; kuwepo na uwazi zaidi wa mikutano na shughuli za Benki ya Dunia na IMF, kuwepo na uwazi na nafasi sawa katika kuchagua viongozi kwenye mashirika haya na kutaka kupitiwa upya kwa mahusiano kati ya IMF,Benki ya Dunia na vyombo vya Umoja wa mataifa. Sehemu ya nne tunaelezwa juu ya Utandawazi na Tanzania. Kwamba Utandawazi katika Tanzania unaweza kuangaliwa katika hatua nne: 1500 – 1961, 1961- 1977, 1977- 1985 na 1985 hadi leo hii. Hatua ya kwanza ya Utandawazi ndani ya Tanzania(Tanganyika) ni ile ya biashara ya Waarabu, Wachina na wareno hadi ukoloni. Sehemu ya pili ni ile ya Uhuru na kuendelea kuuza mazao yetu kwa wale waliotutawala. Sehemu ya tatu ni Azimio la Arusha, kuyumba kwa uchumi wa dunia, mafuta kupanda na ukame na kuilazimisha Tanzania kuchukua mikopo kutoka kwenye mashirika ya fedha ya dunia. Na kipindi cha nne ni kujiingiza kwenye soko huria na ubinafsishaji. Matokeo ya Tanzania kuamua kufuata sera na matakwa ya waliotawala utandawazi wa kibepari; ni pamoja na kuongezeka tofauti ya mapato kati ya matajiri na maskini, kushuka thamani ya shilingi kwa asilimia 400, na kuondolewa masharti na vikwazo vya biashara ya bidhaa na fedha. Athari nyingine ni kuanzishwa mpango wa kuchangia huduma za afya na elimu na kubinafsishwa kwa mashirika ya umma, na serikali kutangaza dhamira ya kulipa madeni ya nje. Mzigo wa madeni umeendelea kuwa chambo kingine cha IMF na Benki ya Dunia kuendeleza ubabe na kuzitawala nchi maskini kama Tanzania. Utandawazi umekuwa na athari za moja kwa moja kwa wanawake na wanaume wa vijijini. Kuingia kwa wawekezaji wa kuchimba madini, kuwinda, kuvuna mbao na kulima kumeharibu mazingira, kupora ardhi ya wananchi. Kuna mifano mingi ya Nyamongo, Bulyankhulu, Geita,Mererani na kwingineko. Sehemu ya tano tunaelezwa juu ya harakati za kudai Dunia mbadala. Harakati zimekuwa zikiendelea duniani kote. Hasa maandamano na migomo ya kupinga unyanyasaji unaofanywa na vinara wa utandawazi. Hata Tanzania harakati hizi zimejitokeza kupitia migomo mbali mbali ya wafanyakazi, makongamano na sanaa za maonesho hususani muziki wa rap kuonyesha waziwazi sera za ufukarishwaji za utandawazi. Mwaka 2001 wanaharakati wakiongozwa na TGNP waliandamana jijini Dar-es-Salaam kupinga sera za ukandamizaji za mashirika hayo, wakati Mkurugenzi wa IMF Bwana Horst Kohler na mwenzke wa Benki ya Dunia James Wolfenson walipokuwa na mkutano wa viongozi 12 wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika. Mapambano mengine ni wakulima wa Pamba na Kahawa, kuanza kususia mazao hayo yasiyokuwa na tija na kuanza kulima mazao mengine kama Nyanya, maua na mboga mboga. Wakulima wa Pamba walizichemsha mbegu za pamba kabla ya kuzipanda ili zisiote na kule Moshi na Bukoba wakulima walianza kung’oa kahawa na kupanda mazao mengine. V. Tathmini ya Kitabu Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii iliyoandaliwa na TGNP. Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira wanayoikusudia wanaharakati hawa wa TGNP kitabu chao kinasisimua, kinafundisha na kinafikirisha kutokana na mtindo alioutumia wa kuweka michoro na picha za matukio mbali mbali ya kudai dunia mbadala. Mfano picha kwenye uk 5, inayowaonyesha watu wakiwa kwenye “Super market” wakinunua bidhaa kutoka nchi za nje inafafanua vizuri maneno haya “ Wapo wanaohusisha utandawazi na bidhaa za kimagharibi madukani, lakini utandawazi ni zaidi ya hapo”(uk. 5). Mchoro kwenye uk. 10 unaonyesha jinsi wageni wanavyotuibia na sisi tunabaki masikini “ Afrika inaendelea kusaidia kujazia na kuneemesha utajiri wa nchi tajiri za Magharibi” (uk. 10) Mchoro mwingine uk 17 unawaonyesha watanzania wakiwa wameshikilia simu, radio na luninga huku wamebeba mizigo ya utandawazi na mzungu amekaa juu yao akisema “Tunawasaidia ili muweze kushindana na sisi” (uk.17). Mchoro wa uk.18 unaionyesha Afrika kama ng’ombe anayelishwa vizuri utandawazi, ubinafsishaji na sera nyingine za Benki ya dunia na IMF. Huku vinara wa Utandawazi wakiwa wameshika visu tayari kwa kumchinja Ng’ombe aliyenona “ Hizi ndizo sera za kurekebisha uchumi zinazopigiwa kelele na Taasisi za Fedha za kimataifa” (Uk 18). Pili, ni wazi kwamba TGNP wamefanikiwa kutoa ujumbe kwa wasomaji wao na kwa lugha nyepesi. Utandawazi unaeleweka vizuri. Mtu akisoma kitabu hiki hapana shaka kwamba hatatofautisha Utandawazi na Ukoloni, na utandawazi na ubeberu. Ni lazima atambue na kuelewa kwamba hakuna utandawazi, bali ni ukoloni mambo leo. Hakuna cha Kijiji kimoja ,bali ni kukaribiana na kuingiliana ili kunyonywa kwa karibu zaidi. Tatu, TGNP wamefanikiwa kutufumbua macho juu ya uzabizabina wa Utandawazi. Vinara wa Utandawzi wanahimiza nchi maskini kufungua milango yao, wakati wao wanafunga. Wanataka walete bidhaa zao huku kwetu wakati wao wanafunga masoko yao. Kisingizio ni ubora wa bidhaa zetu na kuogopa kuambukizwa magonjwa. Wao wanatuletea hadi samaki wenye mionzi ya nyukilia kama ilivyotokea juzi kule Morogoro. Nne, TGNP wametuonyesha kwamba kuwa na wingi wa vitu vya nje kwenye maduka yetu siyo utandawazi, bali ni kutufanya sisi soko la bidhaa zao, na wakati mwingine wanaleta bidhaa zilizoshindikana kununuliwa kwenye soko lao. Tano ni changamoto kwa TGNP, je wanahakikisha kwamba kitabu hiki kinasambaa na kuwafikia wananchi wengi kule vijijini? Na si kusambaza kitabu bali kuendesha semina, warsha na mikutano ya kuwapanua watu uelewa juu ya swala zima la utandawazi. Ni imani yangu kwamba watu wakifundishwa na kuelewa vizuri, watasema hapana kwa utandawazi au watafanya mgomo baridi kama kuzipika mbegu za pamba kabla ya kuzipanda na mengine kama hayo. Na changamoto nyingine ni kiasi gani TGNP inawashirikisha watu inapoandaa kitabu kama hiki? Je wataalamu wa TGNP wanasambaa vijijini kukusanya maoni ya wananchi? Je, wanafahamu ni kiasi gani wananchi wanauchukia au kuukumbatia ubeberu? Je elimu yetu inawaandaa vijana kuukataa ubeberu au kuukumbatia? Hizi changamoto ambazo TGNP ni lazima waziangalie na kushiriki kuboresha mfumo wetu wa elimu. VI. Hitimisho Kwa kuhitimisha, nawaomba watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Na kama TGNP bado ina vitabu vingi, ivisambaze vijijini. Wakati watanzania wanafikiria kwa makini kurudi kwenye siasa ya Ujamaa na kujitegemea, ufafanuzi juu ya Utandawazi ni msaada mkubwa. Kuna wanaosema kwamba watanzania ni wavivu wa kusoma. Kama msemo huu ni kweli, basi kuna haja TGNP, wakakiingiza kitabu hiki kwenye maigizo. Ujumbe ulio kwenye kitabu hiki ukaigizwa na kutengeneza CD, ili zisambazwe na watu waweze kujionea. Lakini pia maigizo haya yanaweza kurushwa kwenye televisheni na kwenye redio. Kwa vile mwezi wa tisha kuna tamasha la jinsia kwenye viwanja vya TGNP – Mabibo, ni ushauri wangu kwamba TGNP iandae kitabu hiki na vingine vingi ili visambazwe wakati wa tamasha la jinsia. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment