UHAKIKI WA KITABU: SILAHA 100 ZA KIONGOZI; KATI YA HIZO UNAZO NGAPI?
1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA
Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni: Silaha 100 za Kiongozi; Kati ya hizo unazo ngapi na kimetungwa na Pius B. Ngeze. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Kampuni ya Tanzania Educational Publishers Ltd (TEPU) ya mjini Bukoba, Mkoani Kagera na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978-9987-07-005-3. kimechapishwa mwaka huu wa 2008 kikiwa na kurasa 64.Bei ya kitabu hiki ni shilingi 4,000 za Kitanzania. Na anayekihakiki sasa hvi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
11. UTANGULIZI
Kitabu hiki cha Silaha 100 za Kiongozi, ni kati ya vitabu vitano vilivyozinduliwa na Kampuni ya Tanzania Educatinal Publishers Ltd, Mjini Bukoba . Vitabu vingine ni: Ushuhuda wa Muujiza wa 11 Mei 2007, siku ambayo Mzee Pius Ngeze na viongozi wengine wa Chama na Serikali walinusurika kifo baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kwenda Ukerewe ulipo zama katika ziwa Victoria. Vitabu vingine ni Wanyonge Wasinyongwe – kikiwa na utetezi wa biashara ya matumizi ya pikipiki na baiskeli; Mwanzo na Mwisho wa Uongozi na Maisha ya Alhaji Abubakari Rajabu Galiatano. Vitabu vyote hivyo vitafanyiwa uhakiki kwenye safu hii.
Tunaweza kusema kwamba kitabu hiki kinazo sura 100! Maana kila silaha ya kiongozi inayotajwa ni kama sura inayojitegemea. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.
III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.
Tarehe 10/9/2007, Mzee Pius Ngeze, aliamua kung’atuka Uenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera. Lakini pia hakukubali kushika wadhifa wowote katika Serikali inayoongozwa na rafiki yake wa karibu Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Aliamua kuachana na siasa na kuacha utumishi serikalini. Uamuzi huo uliwashangaza baadhi, maana Wazee wenye umri wake bado wanang’ang’ania kwenye utumishi Serikalini. Hawataki kustaafu! Lakini walio wengi waliupongeza uamuzi wa mzee Pius Ngeze. Maana wazee ni lazima wawarithishe vijana uongozi.
Katika kitabu chake cha Silaha za Kiongozi, silaha ya 89 ni Andaa Viongozi wa Kesho: “ Viongozi wa sasa, na wewe ukiwamo, ni wa kupita tu. Si wa kudumu. Hakuna mwanadamu yeyote ambaye ni wa kudumu hapa duniani. Kiongozi yeyote anaweza kuondoka uongozini wakati wowote kutokana na kifo, kujiuzuru, kufutwa uteuzi wake, kumalizika kwa kipindi cha uongozi, kutochanguliwa na kufukuzwa uongozi kutokana na kupungukiwa na sifa za kuendelea kuwa kiongozi. Kutokana na sababu hizi, kiongozi bora ni yule anayeandaa aua anayechangia maandalizi ya viongozi wa baadaye, viongozi wa kesho. Usiandae mtu mmoja au wawili, Andaa watu wengi kwa kila aina ya nafasi. Lengo ni kuwa na benki yenye akiba ya watu wengi wanaofaa kuongoza watu. Kiongozi asiyeandaa viongozi wa baadaye hafai, ni mbinafsi, ni mchoyo na ni mwoga. Si jasiri. Viongozi bora huandaliwa. Nchi yetu inahitaji viongozi walioandaliwa vizuri kushika madaraka. Shiriki kufanya kazi hiyo”. (uk 51-52)
Mawazo kama haya anayaendeleza kwenye Silaha ya 96, inayosema hivi: “ Using’ang’anie uongozi kwa kipindi Kirefu”. Anafafanua zaidi kwa kusema: “ Uongozi ni mtamu. Una heshima na marupurupu mengi. Ukishapewa uongozi, umepewa nafasi ya kuonekana, kujulikana, kusifiwa kukalia kiti cha mbele n.k. Kadiri unavyokaa katika uongozi kwa kipindi kirefu, ndivyo mambo yanavyozidi kukunogea. Lakini, ukikaa kwenye uongozi wa aina moja kwa kipindi kirefu umuhimu na umaarufu wako unapungua sana. Huna jipya. Huna mawazo mapya. Unawazoea sana watu na wao wanakuchoka……..Ushauri wangu ni, ‘Using’ang’anie uongozi kwa kipindi kirefu’. Kipindi kimoja au viwili havitoshi? Fikiria mwenyewe na amua kipindi cha kukaa uongozini”. (uk 56-57)
Mzee Pius Ngeze, ana uzoefu wa zaidi ya miaka 35 kama kiongozi wa familia yake, miaka zaidi ya 38 akiwa kiongozi kazini na miaka 33 akiwa kiongozi wa siasa nchini. Amewahi kugombea uongozi na kushinda mara sita, pia amewahi kugombea na kushindwa mara mbili. Hivyo anajua raha na faraja ya kushinda, pia, anajua masikitiko na uchungu wa kushindwa. Kwa sababu hii, ametengeneza silaha hizi za kiongozi kutokana na uzoefu alionao katika uongozi.
Mzee Pius Ngeze, ni mwandishi wa vitabu wa siku nyingi. Lakini kwa vile ameamua kutumia muda wake wa kustaafu kuendelea kuandika na kuielimisha jamii, ni ushuhuda kwamba huyu alikuwa kiongozi wa kweli.
IV. MUHTASARI WA KITABU.
Silaha 100 za Kiongozi, ni silaha za aina ya pekee na ni maalumu. Hizi ni tofauti kabisa na silaha tulizozoea kuziona au kuzisikia. Silaha hizi zimetengenezwa ili zimsaidie kiongozi kumlinda dhidi ya mashambulizi kutoka kwa “maadui” wake. Silaha zinazozungumziwa katika kitabu si zana wala vifaa, bali ni matendo, tabia na mienendo ya kiongozi. Hizi ni silaha kubwa na nzito zaidi kuliko bunduki, bastola, rungu, mishale, mikuki, mabomu na kadhalika.
Katika kitabu hiki, neno Kiongozi, linajumlisha viongozi wa familia, siasa, serikali, dini, kazi, ushirika, taasisi za serikali asasi zisizo za serikali, asasi za serikali, mashirika ya umma, makampuni na wengine. Viongozi hawa wote wanapigwa vita vya kila namna, kwa hivyo ili waendelee kuongoza wanahitaji kuwa na silaha za kujilinda. Vita hivi vinatoka kwa viongozi wenzao kwa watu wanaowaongoza na hata watu wasiowaongoza. Vita vipo na vya kweli. Asipopigana kwa kutumia silaha hizi ataangamia.
Wananchi nao (watu wasio viongozi) wanahitaji kujua silaha hizi ambazo zimetengenezwa kwa ajili ya viongozi wao. Wakizijua watakuwa wameelewa mambo ya kutegemea kutoka kwa viongozi wao.
Silaha zote kuanzia ile ya kwanza ambayo ni Jitambue, hadi ya mwisho ya 100 ambayo ni: Usiwe mwoga na uwe na moyo mgumu, ni muhimu sana kwa kingozi.
Hata hivyo kuna ambazo zinagusa sana kama ile ya 43: Usiwe mtu wa kulipa Kisasi. Baadhi ya viongozi wanapenda kulipa kisasi, na jambo hili lina kwamisha maendeleo: “ Kisasi ni nia au kusudio la kulipiza ubaya aliofanyiwa mtu. Hupashwi kulipa kisasi. Ukifanya hivyo wewe si kiongozi. Kuudhiwa, kukosewa, kudharauliwa, kutukanwa, kusingiziwa, kuandikwa vibaya magazetini n.k. ni mambo ya kawaida kwa kiongozi….” (27-28).
Nikizitaja zote, nitamaliza utamu wa kitabu chenyewe. Kinunue upate uhondo na kuelimika. Lakini hii hapa ni muhimu na siwezi kuacha kuitaja :-
Silaha ya 23: Uwe Mbunifu, Mwanamikakati, Mwanaharakati na mwenye mawazo mapya, pamoja na mambo mengine inasema hivi: “ Kiongozi lazima uwe mbunifu mwenye mikakati, mwanaharakati na mwenye mawazo mapya. Haiwezekani wewe ukawa ni wa kutekeleza mikakati, mbinu na mawazo ya w atu wengine tu. Ya kwako yako wapi? Je, utakumbukwa kwa lipi? Utasifiwa kwa lipi? Utalaumiwa kwa lipi?.........”( Uk 17)
V. THAMINI YA KITABU
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyofanya Mzee Pius Ngeze.
Awali ya yote lazima niseme kwamba kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana kutokana na mtindo alioutumia wa kutaja kila silaha ya kiongozi na kuielezea. Kila kiongozi atajipima na kuona kati ya silaha hizi 100 za uongozi yeye anazo ngapi? Inawezekana mwingine akaongezea ya 101! Kuzipunguza ni vigumu, maana mwandishi amechimba kweli.
Pili, ni wazi kamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kuzitaja silaha zote 100 kuzitolea maelezo kwa kuzingatia uzoefu wake mwenyewe na uzoefu wa viongozi mbali mbali. Kila kiongozi atakayekisoma kitabu hiki atajipima na kujichambua.
Tatu, mwandishi amefanikiwa kukifanya kitabu chake kiwe cha kuaminika kwa kutoa mfano wake yeye mwenyewe wa kuamua kuacha uongozi ili na vijana waweze kuendeleza uongozi. Alikuwa bado anapendwa, kama angeombea angechaguliwa. Rafiki yake Mheshimiwa Rais Jakaya Kiketwe, angeweza kumpatia kazi hata ya kuwa Mkuu wa Mkoa Lakini aliamua kustaafu ili apate nafasi ya kuandika na kuielimisha jamii.
Nne, Mwandishi wa kitabu hiki ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tanzania Educational Publishers Ltd, alifanya jambo la maana kukizindua kitabu hiki na vingine kwa hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa madhehebu ya dini mbali mbali, serikali na chama cha CCM, waandishi wa habari na wasomaji wa vitabu wa rika zote wakiwemo pia wanafunzi kutoka baadhi ya shule za sekondari zilizomo katika Mkoa wa Kagera. Kwa njia hii anatangaza vitabu na kuwashawishi watu kupenda kusoma vitabu ili kujipatia maarifa.
Hata hivyo, mwandishi na wengine wenye nia ya kusambaza usomaji wa vitabu hadi vijijini bado wana changamoto kubwa. Vitabu havifiki vijijini, lakini hata vikifika huko, maisha ni magumu. Mtu ataamua kununua mafuta ya taa, sukari na chumvi badala ya kununua kitabu. Lazima Serikali ifanye mpango maalum wa kusambaza vitabu vijiji.
VI. HITIMISHO.
Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja ,nawashauri viongozi wote wakitafute kitabu hiki na kukinunua. Kitawasaidia sana katika kazi zao za kila siku. Busara, hekima na uzoefu ulio kwenye kitabu hiki utawasaidia kuwa viongozi bora na kuleta maendeleo katika taifa letu.
Lakini kwa upande mwingie namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jambo moja zaidi la kufanya ushawishi miongoni mwa viongozi wa serikali, viongozi wa dini, viongozi wa mashirika na wafanyabiashara, kuanzisha vituo vya kusoma vitabu vijijini na kuviiimarisha. Kwa njia ya kusoma vitabu, tunaweza kusambaza elimu nchi nzima na kwa njia hii kuharakisha maendeleo ya taifa letu la Tanzania.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment