UHAKIKI WA KITABU: SAA YA UKOMBOZI 1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Saa ya Ukombozi na kimetungwa na Nkwazi Nkuzi Mhango. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Tanzania Educational Publishers LTD na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 9987 07 039 8. Kimechapishwa mwaka jana 2009 kikiwa na kurasa 179. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. 11. UTANGULIZI Kitabu hiki ambacho ni Riwaya, kinachambua dhana nzima ya Uhuru. Na hasa uhuru wa nchi za Afrika. Riwaya, inauweka uwazi kwamba baada ya uhuru viongozi walijinufaisha na kuwasahau kabisa wananchi. Riwaya inawahimiza wananchi kuamka na kudai haki zao. Kwa lugha nyingine Saa ya Ukombozi , ni mapinduzi! Kinyume na mapinduzi tuliyoyazoea ya kumwaga damu, Saa ya Ukombozi inasisitiza mapinduzi ya kutumia haki ya kupiga kura. Tunakumbushwa wananchi, yaani watawaliwa kuhakikisha wanawawajibisha viongozi wao. Mfumo unaopendekezwa ni ule wa watawala kuwatumikia watawaliwa. Nchi zote zilizoendelea zinatumia mfumo huu; ndio maana tunasikia kwamba demokrasia ya kweli ndio inajenga Uhuru wa kweli. Bila Demokrasia, watawala wanageuka na kuwa Miungu watu. Riwaya hii inapinga ufisi, ukuku, umbwa, ukondoo, usindano, ukijiko na tabia nyingine kama hizo; inashajihisha usimba, umizani na utambuzi, utendaji na ulinzi wa haki. Hapo ndipo utamwona mhusika mkuu, Mzee Njema, akipambana na uongozi mbovu kuanzia kijijini mwake hadi wilaya na hatimaye, taifa. Cheche ya shujaa inawasha moto unaouamsha na kuukengeua umma kiasi cha kuangusha serikali dhalimu ya Mizengwe kupitia sanduku la kura. Riwaya, inazo sura 27. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki. III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU. Riwaya hii ni ya kubuni. Hata nchi inayoongelewa ni ya kubuni. Lakini kama anavyoandika Ngugi wa Thiong’o, hata kama nchi ni ya kubuni, jina lake linakuwa na maana ya kufikirisha. Ukisoma vitabu vya Ngugi, bila kufahamu lugha yake ya Kikikuyu, ni wazi unapoteza utamu na ujumbe wa riwaya zake. Kwa Mswahili anayesoma Saa ya ukombozi, anapata utamu na ujumbe wa riwaya, maana hata majina yamebeba ujumbe mzito. Jina la nchi ni Mizengwe. Jina hili linampatia msomaji hamu ya kutaka kujua nchi hii ya mizengwe. Penye mizengwe mambo hayawezi kwenda vizuri. Kufuatana na mila za Kiafrika, majina yanatokana na matukio fulani katika jamii. Kama nchi ni Mizengwe, ni kuna mizengwe au huko nyuma kulikuwa na mizengwe iliyoendeshwa katika nchi hii ya kufikirika. Jina la kijiji kilichozaa Saa ya Ukombozi ni Githakwa, sina habari kamili ya mwandishi anatoka kabila gani, lakini kufuatana na uandishi wake ni lazima jina la kijiji linamaanisha kitu fulani kuhusiana na uhuru wa wanakijiji hicho, maana vuguvugu la mapinduzi linazaliwa hapa. Jina la Mkoa ni Chelewa! Inaonyesha jinsi mkoa ulivyokuwa umechelewa kufikia ukombozi wa kweli. Lakini pia ukiangalia majina ya wahusika, unaona kwamba yanatoa ujumbe: Matatizo, Mafanikio, Huzuni, Njema, Kupata, Furaha nk., yanaongeza si utamu tu wa hadithi bali yanafikisha ujumbe kwa haraka na kumfanya msomaji kutafakari wakati akisoma. Ujumbe unazama zaidi pale kikosi cha kuzuia vurugu kinapopatiwa jina la PPK ( Pinga Pata Kipigo). Msomaji atatambua haraka Mizengwe ni nchi ya namna gani na inaongozwa vipi. Inaonyesha vyombo vya usalama vipo kuhakikisha hakuna mtu mwenye kutoa mawazo huru, kutoa mawazo huru ni kupinga na ukipinga ni lazima upate kipigo. Wataalamu wanasema kwamba fasihi ni kioo cha jamii. Mbali na majina yaliyotumika katika Riwaya hii, matatizo yanayotajwa yanafanana kabisa ya yale hapa Tanzania. Kijiji cha Githakwa, kinakataa ardhi yake kumegwa na kugawiwa kwa mwekezaji wa madini. Haya ni matatizo yanayozikumbuka sehemu nyingi za Tanzania. Loliondo, tumeshuhudia Wamasai wakifukuzwa kwenye makazi yao ili ardhi apewe mwekezaji. Lakini maeneo mengi ya madini, watu wamekuwa wakihamishwa ili kupisha miradi ya madini. Tumeshuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira; kule Musoma maji yenye kemikali kali yameingia kwenye mkondo wa maji wanayotumia wananchi na watu wameathirika. Wataalamu na wachambuzi wa maswala ya kidunia wanasema vita kuu ya tatu ya dunia italetwa na kugombea maji. Lakini nafikiri kabla ya hapo kutazuka vita kali ya kugombea ardhi. Serikali za nchi huru za Afrika, zimefanya uzembe au viongozi wamefumba macho na kuendeleza ufisadi wa Ardhi na kutengeneza bomu litakalowalipukia vizazi vijavyo. Kuwamilikisha wawekezaji wa nje ardhi kwa kipindi cha miaka 99, ni uwendawazimu usiokuwa na mipaka! Ingawa mwandishi anaandika kwa kuficha sana na kutufanya tuamini kwamba anazungumzia nchi ya kufikirika ukweli unabaki kwamba Mizengwe ni Tanzania. Mwandishi huyu ni miongoni mwa watanzania wengi ambao wamekuwa wakifikiri kwamba tunahitaji mapinduzi makubwa katika nchi yetu. Na maoni ni kwamba mapinduzi haya yatalewa na watu wa chini kabisa kule vijijini au watoto wa mitaani waliojazana kwenye miji yetu. Kwa vyovyote vile Saa ya ukombozi haikwepeki! Pamoja na kwamba mwandishi anapenda ukombozi uje kwa njia ya kura, anasahau kwamba umezuka mtindo wa kuiba kura. Yaliyotokea Kenya, si kwamba watu walitaka kuchinjana – bali wizi wa kura ulileta tatizo hilo! Mazingira yanayoizunguka riwaya hii; pamoja na nia njema ya mwandishi ya kutaka kutuaminisha kuleta mapinduzi bila kumwaga damu, utabiri wake unaweza ukawekwa pembeni na hali halisi inayotokea kwenye nchi mbali mbali za Afrika. Uganda mfano haiwezi kuleta mabadiliko au mapinduzi au ukombozi kwa sanduku la kura; sote tunafahamu jinsi Mseveni anavyotumia nguvu zote kubaki madarakani. Tanzania, pia tumeshuhudia mara nyingi ujanja na wizi wa kura. Kuna saa itafika, na bila shaka itakuwa saa ya ukombozi watu watakaposema hapana na kuamua kushika silaha za kumwaga damu. Utabiri wa Saa ya Ukombozi unakuja katika mazingira magumu! Mwalimu Nkwazi N. Mhango, ni pacha wa Mwandishi maarufu Mpayukaji na Msemahovyo katika gazeti la Tanzania Daima. Mwalimu Nkwazi anasoma nchini Kanada. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari. IV. MUHTASARI WA KITABU. Riwaya inaudurusu na kuzulu uhuru na dhima nzima ya kuwa huru. Inaona shaka na uhuru wa baadhi ya nchi barani Afrika unaowanufaisha watawala waliojigeuza miungu pamwe na walamba viatu wao. Watu wa kawaida hawaruhusiwi kutia mkono kwenye deste nao wale halua! Riwaya hii inaualika umma kushika hatamu. Inashadidisha utathimini na kuuhoji upya uhuru wanaoambiwa ni wake si wake. Katika kufanikisha hilo, tofauti waathirika waishio kwa matumaini kuupigania na kuupata uhuru wa kweli kupitia kwenye sanduku la kura. Riwaya inahimiza watawaliwa kuhakikisha wanawajibisha watawala kama sehemu ya uwajibikaji wao. Kila mmoja awajibike kwa mwenzake. Inawataka watawala wawatumikie watawaliwa badala ya kuwatumia kama punda wa kuwabeba wao na mizigo yao. Riwaya inapinga ufisi, ukuku, umbwa, ukondoo, usindano, ukijiko na tabia nyingine kama hizo; inashajiisha usimba, umizani na utambuzi, utendaji na ulinzi wa haki. Riwaya inaielezea nchi ya Mizengwe ambayo ina tabia kuu tatu zinazoweza kufananishwa na nchi yoyote, nazi ni matatizo, mafanikio yake na hamu ya kujikomboa kutoka mikononi mwa adha zote zinazoikabili nchi hii. Tofauti na nchi nyingine iwayo, wananchi wa Mizengwe hasa wanakijiji, wanafanikiwa kuudekua mfumo wa kiunyonyaji na wa ukandamizaji uliokuwa ukiwadhalilisha na kuwadhulumu. Hapo ndipo utamwona mhusika mkuu Mzee Njema akipambana na uongozi mbovu kuanzia kijijini mwake hadi wilaya na, hatimaye, taifa. Cheche ya shujaa inawasha moto unaouamsha na kuukengeua umma kiasi cha kuangusha serikali dhalimu ya Mizengwe kupitia sanduku la kura. Ukiachia mapinduzi ya wafanyakazi nchini Ufaransa, kwa Afrika wanakijiji wa Githakwa wakiongozwa na mzee Njema na wenzake, wanafungua ukurasa mpya kwa kuanzisha na kufanikisha mapambano ya ukombozi kutokea kijijini kwenda mijini na kutoka kwenye mapambano ya bunduki kwenda kwenye sanduku la kura. Pamoja na kwamba wanakijiji walikuwa na uwezo wa kutumia silaha zao kama mapanga, mikuki hata mawe, hawakufanya hivyo. Kwani siyo jibu wala njia ya kistaarabu ya kujikomboa. Riwaya, licha ya kuwatia shime wanyonge watawaliwa, inawapa changamoto. Inalenga kuamsha ari na mori wa kujiletea ukombozi wa kweli. Wakijitambua na kuamua kwa dhati, kila kitu kinawezekana. Wanakijiji wa Githakwa wamejikusuru ili kujinusuru na kushinda hila na njama za wezi wachache wenye madaraka kutaka kubinafsisha kijiji chao kwa tajiri wa Kizungu, Bwana Sucker. Hata baada ya mzee Njema kuleta ukombozi kwa kuondoa serikali ya kidhalimu, hajiungi na serikali mpya; wala hataki kulipwa fadhila wala kusaliti ukombozi. Kwa sababu ukombozi ni jukumu la kila mwanajamii. Anakaa nje ili awapime na kuwapa changamoto viongozi wapya kama nao watalewa madaraka. Hakika riwaya hii inafungua ukurasa mpya ambapo kwa mara ya kwanza, wanakijiji wanatoa somo adimu na adhimu kwa nchi ya Mizengwe. V. TATHMINI YA KITABU Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Mwalimu Nkwazi N. Mhango. Awali ya yote lazima niseme kwamba kwa kuangalia hadhira anayoikusudia mwandishi ya Saa ya ukombozi, kitabu chake kinasisimua sana kutokana na mtindo alioutumia mwandishi. Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kubainisha na kisha kutoa majibu kamilifu ya Saa ya Ukombozi. Tatu, kama nilivyosema mwanzo ni kwamba matumizi ya majina kama vile nchi ya Mizengwe, na wahusika wengine kama vile Matatizo, Mafanikio, Huzuni, Njema, Kupata, Furaha yanafanya kitabu chake kusomeka kwa mvuto na kumsaidia msomaji kusafiri na mwandishi hadi mwisho. Nne, Mwandishi anatabiri Saa ya Ukombozi kwa kupitia sanduku la kura. Amejitahidi sana kukwepa umwagaji damu kama ule anaoutabiri Mwalimu Mkuu wa watu, katika kitabu chake. Ukiangalia kwa makini na kusoma kwa uangalifu, utagundua kwamba riwaya ya Saa ya ukombozi na Mwalimu Mkuu wa Watu, ni mtu na pacha. Nani kamwangalizia mwingine? Nani kaiba kazi ya mwingine? Au hawa ni mapacha wenye mawazo yanayofanana? Hadithi zote mbili zinahusu wawekezaji wa nje, uroho wa viongozi kuwakubali wawekezaji kwa vile wanawajaza matumbo yao bila kuangalia masilahi ya taifa zima, msimamo ya wa wananchi kukataa kuuzwa na kusimama kutetea haki zao. Tofauti ni kwamba Mwalimu Mkuu wa Watu, anamwaga damu wakati Saa ya Ukombozi, ni ukombozi bila kumwaga damu. Ingawa mimi ninayehakiki kitabu hiki nachukia kwa nguvu zote umwagaji wa damu, ninakuwa na mashaka makubwa sana kwa pendekezo la Mwandishi wa Saa ya Ukombozi. Tungekuwa na Demokrasia ya kweli, tungekuwa na sera nzuri ya siasa ya vyama vingi, pendekezo lake lingewezekana. Lakini leo hii hakuna uchaguzi unaofanyika bila kupindishwa. Fedha zinatumika kuwanunua wapiga kura, kununua shahada zao ili wasipige kura na wakati mwingine Tume ya Uchaguzi, inatangaza mshindi si kwa wingi wa kura bali kwa maelekezo ya serikali inayokuwa madarakani. Uchaguzi wa Kenya, ni mfano mzuri. Dunia nzima ilishuhudia jinsi Kibaki, alivyolazimisha ushindi na matokeo yake yalikuwa ni kumwaga damu. Uganda, Mseveni, hakubali kuona chama kingine au mtu mwingine anaitawala Uganda. Huko nako ni lazima mwisho wake uwe kumwaga damu. Tanzania, tumeshuhudia yale ya Mbeya, Busanda, Biharamulo na kwingineko, ushindi unatangazwa jinsi Chama tawala kinavyotaka. Katika hali kama hii ni vigumu Saa ya Ukombozi ikaja kwa amani, ni lazima ije kwa kumwaga damu. Tano, mwandishi ameshindwa kwa kiasi kikubwa kuacha matukio kujisemea. Ameshindwa kuwaacha wahusika kujisemea na kujielezea. Kama ni unyanyasaji kama ni umaskini, ni vizuri kutovielezea, bali vijielezee vyenyewe. Riwaya ni nzuri, lakini mwandishi anamwelezea msomaji yanayokuja, badala ya msomaji kugundua mwenyewe kutokana na mwenendo wa wahusika. Mfano Faslu ya Saa ya Ukombozi na Utangulizi vinavyotokea mwanzoni mwa riwaya, havikupaswa kuwepo. Kwa kusoma sehemu hizi msomaji anapata muhutasari wa kitabu kiasi kwamba utamu unapungua. Ni kazi ya msomaji kusoma na kugundua kwamba riwaya inalenga Saa ya Ukombozi. Ni kazi ya msomaji kusoma na kugundua kwamba watu wa Mizengwe walikuwa wakipinga ufisi, ukuku, umbwa, ukondoo, usindano,ukijiko na tabia nyingine kama hizo. Ni kazi ya mwandishi kuandika katika mtindo wa kumfanya msomaji kuyaona haya mwenyewe na kuamua mwenyewe kwamba hapa ni ufisi au ukuku. Sita, lugha iliyotumika ni sanifu, mwanzoni mwa kitabu kuna cheti kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa, cha ithibati, kuhakikisha kwamba lugha iliyotumika ni sanifu. Hata hivyo, kwa vile mwandishi alishindwa kuficha kwamba yeye ni mwanaharakati na mpambanaji wa Haki za binadamu na utetezi wa wanyonge, anatumia lugha nzito kuwatukana viongozi wanaopora rasilimali za taifa. Na kama nilivyodokeza, lugha hii inakuwa yake mwenye badala ya kuwa ya wahusika anaowachora yeye mwenyewe. IV. HITIMISHO. Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania na wote wanaotumia lugha ya Kiswahili kukinunua kitabu hiki na kukisoma. Lakini kwa upande mwingine napenda kumshauri mwandishi, kwa maandishi yake yanayokuja, kama ni riwaya, ajaribu awezavyo kuwaacha wahusika kujisemea na yeye kama anataka kutoa ujumbe aupitishe kwenye midomo ya hao wahusika. Riwaya inapendeza pale ambapo inajisimamia na kutoa sauti, kuliko mwandishi kutumia riwaya kama jukwaa la kuhubiri. Ni vyema msomaji akisoma aone Njema, aone Matatizo, Mafanikio na wananchi wa Mizengwe. Kusoma riwaya na kuona sura ya mwandishi badala ya wahusika inatoa utamu wa riwaya. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment