UHAKIKI WA KITABU: PESA ZA MAWE
1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA
Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Pesa za Mawe na
kimetungwa na Oscar Ulomi. Mchapishaji wa kitabu hiki
ni E&D Limited na amekipatia namba ifuatayo katika
sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 411 38 X.
Kimechapishwa mwaka 2006 kikiwa na kurasa 70. Na
anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. UTANGULIZI
Pesa za Mawe, ni kitabu cha hadithi ya kubuni.
Hadithi hii imejikita katika mambo yanayotokea kwenye
taifa letu. Malezi mabovu, ulevi na ujambazi,
ushirikiano wa polisi na majambazi. Pesa, ngono na
starehe ni vitu vinavyojitokeza na kuonyesha
vinavyokwamisha maendeeleo. Hadithi inatuchorea
barabara ya biashara haramu ya madini inayovuka mipaka
ya nchi, kanda na hatimaye kufika katika masoko
makubwa ya dunia. Hadithi inaonyesha jinsi maliasili
yetu ya madini inavyoweza kuishia katika mikono ya
watu wachache, watu wanaoabudu pesa na ufisadi.
Kitabu kinazo sura nane. Katika aya zifuatazo nitaoa
muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza
mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.
III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.
Tanzania ni nchi yenye madini mengi. Na madini
mengine kama Tanzanite, yanapatikana Tanzania tu.
Madini haya yamekuwa kiuzwa kwa njia za magendo na
kuzifanya nchi kama Kenya na Afrika ya Kusini, zisizo
na madini ya Tanzanite, zihesabiwe miongoni mwa nchi
zinazozalisha Tanzanite. Hili limetokea kwasababu
Tanzanite inavushwa kwa njia ya magendo.
Jeshi la polisi linalalamikiwa kushirikiana na
majambazi na kushiriki kuvusha biashara ya magendo.
Malezi ni kitu kinacholisumbua taifa letu. Kelele
zinapigwa kila siku juu ya maadili. Kama wazazi
wanalewa na kufanya mambo yanayokwenda kinyume cha
maadili, ni lazima watoto watarithi maadili mabovu.
Kwa njia ya hadithi ya Pesa za Mawe, Osca Ulomi,
anamtumia mhusika mkuu Rasta Kala Ndezi, kutufunulia
ukweli wa mambo matatu yaliyotajwa hapo juu. Kala
Ndezi, anakoswa dira akiwa mdogo. Kazaliwa kutokana na
mzazi mkatili na mlevi. Uhalifu ukawa kitu cha kawaida
kwake, naye akawa mtu muafaka wa kutumika katika
uhalifu. Anashiriki mauaji na kuikimbia polisi.
Alipoingia katika biashara ya kuuza “Mawe”, alijikuta
ndani ya mkondo wa maisha ya kichinichini ya ufisadi
uliokithiri. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu
chenyewe kwa muhtasari.
IV. MUHTASARI WA KITABU
Sura ya kwanza na ya pili zinaelezea maisha ya
familia ya Kala Ndezi, malezi yake na mazingira
yaliyomzuka tangia anazaliwa hadi kuwa mtu mzima:
“..Alipoingia darasa la pili alibadili tabia na kuwa
mkaidi hakupenda masomo na alisumbua walimu sana na
wanafunzi wenzake… aliendelea hivyo hadi darasa la
sita, hali ikawa mbaya zaidi, kwani alishaingilia
uvutaji bangi, kunywa pombe, kulala nje ..” (uk 5-6).
Maisha ya Kala, yanakuwa mabaya hadi anakuwa jambazi
sugu. Anashiriki mauaji ya Polisi, na kujificha.
Maisha yake yanakuwa ya kujificha ficha.
“Kala alikuwa na fedha kiasi mfukoni. Alimfuata
Merinyo akamwelezea mkasa mzima, Merinyo akamwongezea
nyingine. Alimwendea Mwarabu aliyesaidia kumtorosha
hadi Chekereni, nje kidogo ya mji wa Moshi…. Chakachui
naye aliposkia mkasa mzima ulivyokuwa alimpeleka kwa
rafiki yake mwingine upande wa Kenya” (Uk 11).
Sura ya tatu na ya nne, inatuonyesha safari za Kala,
kule Tanga, Dar-es-salaam na Tabora. Kala, anaanza
kushirikiana na wafanyabiashara. Anaanza biashara ya
dhahabu. Hata tunapata mbinu zinazotumika kununua na
kuuza madini kwa magendo.
“Kala hakupinga, kwani alikuwa na hamu ya kufahamu
Dar-es-salaam. Walielekea Dar-es-salaam na walienda
kuishi kwa jamaa yake Mwarabu aliyekuwa maarufu kwa
kuuuza gongo na madawa ya kulenya huko manzese Uzuri”
(uk 14).
“Huko machimboni walifika raia wa nchi za nje kulangua
dhahabu hasa wakitokea Kenya, Mali, Ivory Coast,
Nigeria na Ghana. Maarufu kuliko wote walikuwa raia wa
Senegal waliojulikana kama Masenesene”(uk 17)
“Walipokaribia mpakani kiasi cha kilometa moja, Jabiri
alisimamisha gari, akawaacha wateja wake wakipumzika
garini, akaazima baiskeli ya mkulima mmoja ili
akachunguze kulikuwa na maofisa wangapi wa uhamiaji na
wangehitaji posho kiasi gani” (Uk 21).
Sura ya tano hadi ya nane, tunaingizwa kwenye biashara
yenyewe ya madini. Kala, anavuka mipaka na kwenda
Zambia hadi Zaire. Hapa tunachorewa barabara ya
biashara ya madini na biasha nyingine inayofanyika
kimagendo. Biashara hii inawakusanya watu wa kutoka
nchi mbali mbali kama Senegal na nchi nyingine za
Afrika. Biashara, inatanuka hadi Mashariki ya Mbali.
Tunaelezwa jinsi rushwa inavyotembezwa kwenye mipaka
ili kuruhusu magendo kupita. Na jinsi watu
wanavyopitia njia za panya kuvusha pesa na vitu
vingine:
“ Mousa na Kala walivuka mpaka kupitia njia ya panya
kuwakwepa maofisa wa ushuru wa mpaka ni wasizishtukie
feha zao nyingi zilizokwa ndani ya mbabegi”( Uk. 22).
V. TATHMINI YA KITABU.
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya
kazi hii aliyoifanya Oscar Ulomi.
Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia
hadhira anayoikusudia, hadithi yake inasisimua sana.
Amefanikiwa kutuchorea barabara ya Pesa za Mawe. Kwa
kusoma hadithi, mtu anakuwa na mwanga jinsi madini
yetu yanavyopotea na kutajirisha nchi za jirani. Hii
ni hadithi ya kubuni, lakini waswahili wanasema
lisemwalo lipo, kama halipo liko njiani.
Pili, mwandishi amefanikiwa kuonyesha jinsi familia
inavyochangia maisha na maendeleo ya mtoto. Kama
wazazi wana maadili mabovu, ni lazima na mtoto atakuwa
na maadili mabovu. Familia ni msingi wa malezi ya
mtoto na msingi wa maadili ya taifa zima.
Tatu, mwandishi, hakujikita katika kubuni tu. Sehemu
nyingi anazoziongelea, kama Moshi, Arusha, Tanga,
Tabora,Dar-es-salaam hadi Zambia, zipo na anazielezea
jinsi zilivyo. Ukisoma utasema kama hajaishi huko basi
amesoma sana juu ya sehemu hizo.Matukio yanayoongelewa
na mbinu zinazotumika, ni vitu vinavyotokea katika
jamii yetu. Kuwaonga mapolisi ni kitu kinachofanyika
kila wakati. Kuonga mpakani ni kitu kinachotokea kila
wakati. Hivyo si kubuni tu!
Nne, mwandishi anaonyesha amefanya utafiti juu ya
Pesa za Mawe. Mbinu zote anazoziongelea, zinaelekea
kuwa za kweli. Mfano anafichua mbinu ya kuuza mafuta
kwa magendo. Madreva wa magari ya mizigo wanaweka
matanki ya ziada kwenye magari yao. Mpakani wanafikiri
ni mafuta ya kutumia kwenye magari, kumbe ni mafuta ya
kuuza.
“Siku waliyopanga kuondoka pamoja, gari kama 12 kutoka
Tanzania, zote za kampuni moja, zilikuwa na nafasi
kwenye matanki yao. Walipanga kuongeza mafuta kwenye
gari nane, hivyo jumla ya lita 8,000 za dizeli
zilinunuliwa. Waliondoka Ndola asubuhi na saa saba
mchana walishafika mji mdogo wa mpakani wa
Kasumbalesa, wakiwa wamepitia miji ya Kitwe, Chingola
na Chililabombwe..” (Uk 38).
Pia kuna hili analoliongelea uk wa 25, linaelekea
kuwa kweli, maana kuna uvumi kwamba Serikali ya Uganda
inawapatia wananchi wake pesa za kununulia kahawa za
Tanzania kwa magendo:
“ Uvumi ambao labda ulikuwa ukweli ni kwamba fedha
nyingi walizokuwa nazo hao wageni, walipewa kama
mitaji na serikali zao, wakafanye biashara kokote
ulimwenguni na walirudisha sehemu ya faida kwenye
benki za kwao” (uk 25).
Tano, kwa bahati mbaya au kwa makusudi mazima
mwandishi, hapendekezi mbinu za kuzuia Pesa za Mawe.
Labda hili analiacha kwa msomaji. Yeye anachokoza
mawazo, ili watu wakisoma wajazie alipoachia. Pia,
hakupenda kutuonyesha mtoto aliyepata malezi mazuri
tofauti na Kala Ndezi, maisha yake yanachukua mkondo
gani. Je, malezi mazuri yanachochea moyo wa kizalendo?
Malezi mazuri yanamfanya mtu kulinda madini ya taifa
na kuhakikisha yanauzwa kwa njia ambazo zitaleta faida
kwa taifa letu. Labda na hili ametuachia sisi
wasomaji.
VI. HITIMISHO
Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri
watanzania kukisoma kitabu hiki cha Pesa za Mawe, ili
wafahamu jinsi madini yetu yanavyopitia njia za panya.
Ni imani yangu kwamba hadithi hii haikushuka kutoka
mbinguni. Inaongelea yale yanayotendeka katika taifa
letu. Hadithi hii inaweza kutusaidia kutafakari na
kujadiliana miongoni mwetu ni njia gani inalifaa taifa
letu Tanzania.
Lakini, kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa
kitabu hiki kufanya jambo moja zaidi katika uandishi
wake siku za usoni. Atuchoree akina Kala Ndezi,
wanaopambana kuzuia madini yetu yasipite njia za
panya. Pia, tuwaone akina Kala Ndezi, waliolelewa
kwenye familia zenye maadili mazuri. Kala Ndezi, ambao
si majambazi! Ni imani yangu kwamba nchi yetu ina
wazalendo, ina watu wanaokesha usiku na mchana
kuhakikisha taifa letu linatembea katika mwanga. Hawa
pia ni lazima waonekane katika tungo, nyimbo, hadithi
na historia ya taifa letu.
Mwisho, kabisa niwahimize watanzania kusoma na
kuandika. Jamii inayosoma vitabu na kuandika vitabu
inapiga hatua kubwa katika maendeleo.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment