UHAKIKI WA KITABU: MWANZO NA MWISHO WA UONGOZI WA KISIASA. 1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Mwanzo na Mwisho wa Uongozi wa Kisiasa na kimetungwa na Mzee Pius B. Ngeze. Mchapishaji wa kitabu hiki ni TANZANIA EDUCATIONAL PUBLISHERS LTD (TEPU) na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978-9987-07-010-7. Kimechapwa mwaka huu wa 2008 kikiwa na kurasa 46. Na anayekihakiki sasa katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. UTANGULIZI. Kitabu hiki Mwanzo na Mwisho wa Uongozi wa Kisiasa ni kati ya vitabu vitano vilivyozinduliwa na Kampuni ya Tanzania Educatinal Publishers Ltd, Mjini Bukoba hivi karibuni. Vitabu vingine ni Silaha 100 za Kiongozi , Wanyonge Wasinyongwe , Ushuhuda wa Muujiza wa 11 Mei 2007 na Maisha ya Alhaji Abubakari Rajabu Galiatano ambavyo tayari nimevifanyia uhakiki .Vitabu hivi vinapatikana kwenye duka la TEPU na Upendo Nyumba ya Kulala wageni, Bukoba mjini. Dar-es-Salaam, vitabu hivi vinapatikana Duka la TEPU lililopo makutano ya Mitaa ya John Rupia na Uhuru, Kariakoo. Mwanzo na Mwisho wa Uongozi wa Kisiasa ni kitabu chenye hotuba tatu za mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini. Naye ni ndugu Pius B. Ngeze aliyeongoza Chama Cha Mapinduzi katika Mkoa wa Kagera akiwa Mwenyekiti wa mkoa huo kwa miaka 25. Zimo pia makala za mahojiano na maoni ya magazeti kadhaa nchini. Hivyo kitabu hiki kinazo sura 8 na picha za Mwandishi na za matukio mbali mbali katika uongozi wake wa Kisiasa. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake. III. MUHTASARI WA KITABU. Hotuba ya kwanza ni ile ya kuwashukuru wajumbe waliomchagua kwa mara ya kwanza Septemba 21, 1977. Inaonyesha jinsi alivyoanza safari yake ya uongozi akizingatia “Ushirikishwaji” wimbo ambao leo hii unaimbwa na kila mmoja na ndilo hitaji la wakati tuliomo: “Kazi ya Uenyekiti wa Mkoa, hasa Mkoa huu wa Ziwa Magharibi, ni nzito na ngumu. Kwa sababu hiyo, nahitaji kuanzia sasa hivi ushirikiano wenu na viongozi wengine wa Chama, Serikalini, Mashirika ya Umma, Madhehebu ya Dini na wananchi wote kwa ujumla” (Uk 4). Hotuba ya pili ni ya kuaga Uenyekiti huo Oktoba 18,1997 na ya tatu ni ya Kuaga na Kung’atuka Uenyekiti wa Mkoa Septemba 10 2007 baada ya kuwa amerejea uongozini mwaka 2002. Sura ya tatu ni habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Rumuli, Februari, 2007: Ngeze Atangaza Kustaafu Uongozi. Sura ya nne ni habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Mtanzania,20 Machi, 2007: Ngeze Ang’atuka CCM. Sura ya tano, ni habari iliyoandikwa kwenye gazeti la RAI, Aprili 5-11,2007: Ngeze Aionya CCM na Fedha za Shetani: “ Mkongwe katika siasa za nchi yetu na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kagera, Pius Ngeze, amevionya vyama vya siasa nchini kuachana na mtindo wa kuombaomba fedha badala yake vibuni miradi yake kwani katika ombaomba vinaweza kupokea fedha za shetani…” (uk 22). Sura ya sita ni Mahojiano ya Pius Ngeze na Bw. Elia Mbonea, Mwandishi wa Habari, Gazeti la Rai, Aprili 5-11-2007: Ngeze, akisema “ Ninataka kupumzika, ni safari ndefu..” (Uk 25). Sura ya saba ni maoni ya Mhariri, Gazeti la Mtanzania, 5-11 Aprili, 2007: “Wengine wanasubiri Nini Kung’atuka?”: “….Tunachukua fursa hii kuwapongeza Ngeze na Ndejembi, kwa uamuzi wao wa busara. Uamuzi wa kung’atuka kwa hiari, unawajengea heshima kubwa mbele ya umma. Daima wataendelea kuheshimiwa, na kwa hakika ushauri wao utapokelewa na kutekelezwa na wale waliowaacha madarakani. Raha ya kung’atuka kwa hiari tumeiona kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pale alipoamua kuacha urais, na baadaye uenyekiti wa CCM..” (Uk 31). IV. TATHMINI YA KITABU. Kama tulivyoona kwenye vitabu vilivyotangulia, Mwandishi amefanikiwa sana kuweka uzoefu wake wa uongozi kwenye maandishi. Huu ni msaada mkubwa kwa kizazi cha leo na vizazi vijavyo. Mwandishi amefanikiwa pia kutufundisha kwamba “ Kilichoandikwa, kimeandikwa”. Kumbukumbu itabaki. Watakuja kusoma na kujifunza. Lakini pia, mwandishi anatufundisha juu ya hitaji la kujenga utamaduni wa kung’atuka. Kwamba wazee warithishe vijana. Wazee wengi wamekuwa na tabia ya kutotaka kuondoka madarakani, hadi wengine wanaondolewa kwa aibu ya kukataliwa kwa kura. Lakini, pia fundisho jingine ni kujenga utamaduni wa kusoma vitabu kwa kuandika vitabu. Daima tunasema watanzania hawana utamaduni wa kusoma. Watasoma nini kama hatuandiki vitabu? Badala ya kusoma mambo ya nje, tunaweza pia kusoma ya hapa nyumbani, kama vile kusoma maisha Ya Ngeze, Mzee Alhaji Abubakari Rajabu Galiatano na wengine wengi. V. HITIMISHO. Kwa kuhitimisha, napenda kuendelea kuwashawishi watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Na msisitizo ninauweka kwa viongozi na wale wanaotaka kuwa viongozi. Kitabu hiki kitawasaidia sana. Kwa upande mwingine, ningemshauri Mwandishi, kuandika zaidi juu ya Mchango wa wanawake katika uongozi wa Taifa letu na pia mchango wa wanawake katika uongozi wake. Kwenye orodha ya mwandishi ya watu karibia 30 waliomlea kisiasa, anatajwa mwanamke mmoja! Mama Kandika Kitu! Nina mashaka na hili. Nafikiri wako wanawake wengi lakini hawatajwi! Tukizingatia kwamba mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera, aliyepokea kijiti kutoka kwa Pius Ngeze, ni mwanamke, ni lazima mchango wao si haba! Lakini pia kuna Wanawake Mashuhuri katika Mkoa wa Kagera na taifa kwa ujumla ambao mchango wao katika uongozi na maendeleo ya taifa letu umesahaulika. Kuna akina mama walioujenga Mji wa Bukoba, kuna akina mama waliowasomesha baadhi ya wasomi wa Bukoba, kuna akina mama waliowazaa na kuwalea watu mashuhuri wa Kagera. Hawa noa kuna umuhimu wa kuandika historia ya maisha yao. Kwa vile Tanzania Educational Publishers LTD, ina mpango wa kuandika Maisha ya watu mashuhuri wa Mkoa wa Kagera, watakumbuka na wanawake pia. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment