UHAKIKI WA KITABU: MWALIMU MKUU WA WATU 1. Rekodi za Kibibliogarafia Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni “ Mwalimu Mkuu wa Watu” na kimetungwa na Paschally Boniface Mayega. Mchapishaji wa kibtabu hiki ni MPB Enterprises na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9976983387. Kimechapishwa mwaka 2006 kikiwa na kurasa 112.Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II.Utangulizi Hii ni hadidhi ya kubuni.Inaanaza kwa maneno ya unabii: “ Hii ni sauti ya mtu aliaye Nyikani.Itengenezeni njiaya Bwana.Yanyoosheni mapito yake.Kama nitasema kweli tupu siku zote kuna ubaya gani? Ukisema kweli daima kila aliye wa ukweli atakuheshimu. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu.Hapendenzi mbele ya binadamu wenye roho mbaya.Hukimbiwa hata na marafiki zake wenye roho nyepesi.Nikipatwa na mkosi kama huo, sitawaonea wivu watu wawezao kudumu na marafiki zao wote siku zote.Siwezi kuikana kweli kwa kuogopa upweke wa muda, nikanyimwa ushirika wa milele unaotazamiwa kutokea baadaya kushindwa kwa uongo” Kitabu hiki kinazo sura 23, sura zote ni fupi fupi zenye matukio ya kusisimua. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathimini yake, lakini baada ya kudokeza mazingia yanayokitangulia kitabu hiki. III. Mazingira yanayokizunguka kitabu Dokezo la mazingira ya kitabu hiki ni maneno ya mwandishi yaliyo mwanzoni mwa kitabu: “Kila kaya iache kibatari chake kikiwaka; Tumelishauri Jua lisitokee mpaka nchi itakaporudishwa kwa wananchi. Nenda katangaze neno hili.Usinitaje, kwa heri!”. Hadidhi hii ni ya nyakati hili tulizomo. Nyakati za uwekezaji, Ubinafsishaji, ubia na utandawazi.Ingawa mtunzi, anasisitiza kwamba ni hadidi ya kubuni: “ Maandiko haya ni ya kubuni.Hata nchi inayosimuliwa katika maandiko haya haipo, ni ya kufikirika tu.Hivyo, ikiwa itatokea baadhi ya majina yaliyotajwa katika maandiko haya k kufanana na majina halisi ya miji, vitu au watu waliopo ni bahati mbaya tu, na wala haikukusudiwa, kwani kama nilivyosema mwanzo Maandiko haya ni ya kubuni tu”. Bado kuna hali ya kushawishi na kuamini kwamba mazingira ya kitabu hiki ni Tanzania ya leo iliyo kwenye hatua ya uwekezaji, demokrasia ya vyama vingi na kiu ya kuwa na kiongozi mwenye dira na uzalendo wa kweli. Inawezekana kabisa riwaya hii ni ya kubuni. Lakini inaongelea Taifa letu. Hata kama ni kufanana tu, wahusika watakuwa na uhusiano wa karibu na watanzania. Majina yanayotumika kwenye riwaya hii yamefanana sana na yale tunayoyafahamu: Tibaijuka, anayetajwa kama Dada Tibaijuka!, Jakaya, anayetajwa kama Kaka Jakaya, Lyatonga, Pombe, Salim,Edward, Makamba,Azimio la Kijenge, Azimio la Mji Mkongwe,Mama Shamim,Sajenti Freeman,Luhigo, Tendwa, Hakimu Barnabasi, Luhanga,Jamuhuri Ya Muungano,Mwadilifu Freeman wa Hai, nk. Haiwezekani kuna nchi nyingine yenye kufanana na Tanzania, kiasi hiki! Baadaya ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari. IV. Muhtasari wa Kitabu Riwaya ya Mwalimu Mkuu, inahusu mapambano kati ya Mwalimu Mkuu Ngowe Boniface, wa Shule ya Msingi Kumwitu akisaidiwa na wanafunzi na wananchi dhidi ya mwekezaji Mzauzi Bw.Frederick de Witts, anayekingiwa kifua na kulindwa na Serikali. Sakata zima linaanza baada ya Mwalimu Mku wa Watu kupokea barua kutoka kwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Sehemu ya barua hiyo inasema hivi: “ Kwa muda mrefu sasa serikali imekuwa ikiivumilia tabi yako ya uchochezi.Unawashawishi wanafunzi na wananchi waichukie Serikali yao tukufu……Serikali inafuatilia kwa karibu sana nyendo zako.Unaitwa mkombozi! Unakomboa nani! Kutoka kwa nani? Fahamu kuwa huo ni uhaini. Adhabu ya uhaini ni kunyongwa mpaka ufe….Mwalimu mkuu gani wewe usiyeelewa hata sera ya uwekezaji, sera ya ubinafsishaji, sera ya ubia, sera ya utandawazi, sera ya ubabaishaji na sera zingine kama hizo? Mwekezaji ni mtu muhimu sana kuliko mtu yetote katika nchi hii, Amekuja kuboresha maisha yetu.Huyu ni mtu wa kulindwa sana…. Nimeelekezwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa sana ,Bwana Kafriko Mchumiatumbo, kukupa onyo kali…” (Uk wa 3&4) Frederick de Witts alikuwa mgeni aliyekuja nchini kuwekeza. Katika kuwekeza kwake alijenga kiwanda. Kiwanda cha kusindika nyama. Kiwanda hiki kilijengwa katika chanzo pekee cha mto Luzi. Mto ambao ulikuwa pekee katika eneo hilo kwa maji ya kunywa, kuoga na kazi nyingine. Pia mto Luzi, ulikuwa ndio tegemeo la wananchi kwa ajili ya uvuvi wa samaki wa kitoweo na biashara. Kiwanda hiki kilijengwa jirani kabisa na Shule ya Msingi ya Kumwitu. Moshi uliotoka katika Kiwanda hicho mara nyingi uliifunika kabisa shule ile na sehemu za makazi ya wananchi. Mara kadhaa ilibidi masomo yasimamishwe na wanafunzi kutoka nje shauri ya Moshi kujaa madarasani. Nje pia kulikuwa na moshi. Mafuta na kemikali zilizotoka katika kiwanda hicho zilitupwa katika mto Luzi na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Wananchi wa zehemu hiyo waliathirika kiafya, waliugua kikohozi kisichopona kutokana na moshi wa kiwanda, ngozi zao zilibabuka nk. Mwalimu Mkuu, alitaka kiwanda hicho kifungwe. Serikali, na hasa mawaziri waliokuwa wakipokea rushwa kutoka kwa msauzi, walitaka kiwanda hicho kiendelee! Mwandishi anaonyesha vizuri mawasiliano mabovu kati ya Mwekezaji na Rais wa nchi, na kati ya Rais na wananchi wake. Mwekezaji anatoa rushwa ya kumpelekea Rais, ili kumziba mdomo. Rushwa hiyo inaishia kwenye mifuko ya Waziri wa viwanda na Waziri Mkuu. Rais, anapata taarifa nzuri kwamba kiwanda ni kizuri na kinaleta faida kwa taifa, wakati kiwanda ni hatari kwa maisha ya wananchi. Malalamiko yanapozidi, Rais, anataka kukitembelea kiwanda. Waziri mkuu na waziri wa viwanda, wanamshauri msauzi kufunga kiwanda chake kwa muda, hadi rais atakapomaliza ziara yake. Mzauzi anakataa kufunga kiwanda: “Nimekubali kuwapeni ninyi mali ya kila aina ili nifanye shughuli zangu bila bughudha. Unaponiambia nifunge kiwanda changu unataka mimi nikueleweje? Niliwaambia sisi wawekezaji ni mtandao. Hao wenzangu nitawaambia nini? Nilishaambia kuwa Rais yupo na sisi, wewe unakuja kuniambia upuuzi? Mwalimu Mkuu atawashindaje wakati yeye hana jeshi, hana mamlaka yoyote.Sema nyinyi mnataka kuniletea kujua. Ukitaka kunijua mimi ni nani uliza nchi jirani. Wote walioleta mchezo huu unaoleta hawapo Duniani. Ohoooooo! Mnataka kucheza na moto……kamwambie huyo Waziri Mkuu wako na wenzio wote kuwa upuuzi wenu huu haukubaliki. Kitaondoka chochote hata matumbo au mapafu yenu lakini mimi nitabaki na kiwanda changu. Nimekuja hapa kuishi na si vinginevyo.” (Uk 47). Mwandishi wa riwaya, anaonyesha jinsi jitihada za Mwalimu Mkuu na wananchi, za kukifunga kiwanda hicho kwa amani zinashindikana. Rushwa, na mawasiliano mabovu kati ya ya Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, mwekezaji na wananchi- utawala mbovu- inasababisha Mwaimu Mkuu, wanafunzi na wananchi kutumia nguvu kukifunga kiwanda cha mzauzi. Kama ilivyo kwa mapambano yoyote yale ya ukombozi wa umma, nguvu ya wananchi inashinda. Mzauzi anashindwa na serikali inashindwa lakini baada ya kumwaga damu nyingi. Swali linabaki ni nani atakuwa kiongozi wa nchi?Mwalimu Mkuu wa watu au nani? Mwalimu Mkuu anapendekeza katiba mpya na mambo ya kuzigantia.Pia anatoa majina ya watu saba wenye sifa za kuwa viongozi.Ni nani atachaguliwa kati ya hawa saba.Mwandishi anamalizia hadidhi yake kwa kutoa ahadi ya kuandika kitabu kingine: “ Je, Rais aliyechaguliwa alikidhi matarajio ya waliomchagu?”. V. Tathmini ya Kitabu Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliyoifanya Bwana Paschally Boniface Mayega. Ingawa mwandishi anasema hadidhi hii ni ya kubuni, lakini ukweli ni kwamba amefanikiwa kiasi kikubwa kubuni hadidhi inayoeleza maisha ya kila siku ya mtanzania.Matazito ya kuelewa sera za ubnafsishaji, uwekezaji na utandawazi ni makubwa. Tunashuhudia magomvi hadi vifo kati ya wananchi na wawekezaji kwenye machimbo ya madini. Wananchi wanalalamika kwamba machimbo hayana faida kwao. Kama hawawezi kuuza nyanya zao, ndizi zao, maziwa yao nk, kila kitu kinatoka Afrika ya kusini, kwanini wasilalamike? Kama mwenye mali, mwananchi, hana pesa ya kumpeleka mtoto shule wala kununua dawa, wakati mwekezaji anaishi Dar-es-salaam, na kufanya kazi kila siku Kahama, ana uwezo wa kusafiri kila siku kwa ndege, kwa nini mtu hata kama hakusoma, asitilie shaka uwekezaji? Kuna mambo mengi ya kuhoji juu ya uwekezaji. Wananchi wanapiga kelele, lakini hakuna anayejitokeza kutoa majibu. Hadi leo wananchi wa Igoma na Kisesa,Mwanza, wanaendelea uathirika na harufu mbaya inayotoka kwenye viwanda vya kusindika minofu ya samaki. Kwa vile viwanda hivi ni vya wawekezaji hakuna anayesema, watu wanaendelea kuathirika na mazingira yanaharibika! Kuna ugomvi mkubwa kati ya wavuvi wadogo wadogo na wawekezaji wa viwanda vya kusindika minofu ya samaki. Ugomvi huu unasababisha mambo mengi: mauaji, uvuvi haramu, wananchi kushindwa kumudu bei ya samaki nk. Bila busara na hekima, ugomvi huu unaweza uelekea kwa Mwalimu Mkuu wa Watu! Baadhi ya watu wanaunga mkono sera nzima ya uwekazji. Baadhi wanapinga! Hawa wanaopinga hawapingi uwekezaji, bali wanapinga jinsi uwekezaji unavyoendeshwa, mfano kujenga kiwanda kwenye makazi ya watu, kuchimba madini yetu na kutuachia mashimo na watu wachache kunufaika na uwekezaji. Wananchi walio wengi hawajui faida na hasara za uwekezaji. Wanachokiona ni moshi unaoathiri afya zao, ni harufu mbaya inayotoka kwenye viwanda, ni maisha bora na ya starehe ya wawekezaji, ni kutozwa kodi kubwa, ni kuzuiwa kuingia ziwani kuvua kwa vile ziwa ni la wawekezaji, ni kuzuiwa kuwinda kwa vile misitu yote ni ya wawekezaji. Ni kuzuiwa kutumia uwanja kwa vile mwekezaji ameukarabati. Haya na mengine yasipopata maelezo ya kina, yakifanyiwa mzaha, ni kweli Mwalimu Mkuu, wanafunzi na wananchi watapambana na kushinda! Nimpongeze mwandishi kwa ubunifu wake wa kuelezea mambo mazito kwa hadidhi. VI.Hitimisho. Ingawa riwaya hii ni nzuri, na ningependa kuwashauri watanzania wote kuisoma, mimi binafsi nina tatizo kidogo nayo.Niliogopeswa na mwisho wake, inaishia katika kumwaga damu ya watu wengi.Sipendi vita! Ninachukia aina yoyote ile ya umwagaji damu hata kama inabeba nembo ya ukombozi. Kumwaga damu ni kuyapoteza maisha, na maisha yakishapotea hayarudi! Sipendi kuamini kwamba nchi yetu imeishiwa na watu wenye busara, hekima na uzalendo kiasi cha kulitelekeza taifa letu kwenye dimbwi la damu. Bado nina imani kwamba tunaweza kutanzua matatizo yetu kwa njia ya amani. Ingawa wakati mwingine ni ujinga kufumbia macho kilio kama cha Mwalimu Mkuu na vilio vingine kama kile kilichotolewa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Freeman Mbowe, aliyoitoa wakati akikubali kuteuliwa na Chama chake cha CHADEMA, kugombea urais wa Taifa letu la Tanzania, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Freeman, alisema kwamba Taifa letu limemwagiwa mafuta ya taa. Kwamba panahitajika kichaa mmoja kuwasha moto. Kwamba wale wanaoishi Mbezi, Oysterbay na Mikocheni watajikuta Ubungo na kuungana na wenzao wa Manzese, wakielekea kwenye makambi ya wakimbizi Kibaha!Inatisha! Lakini kuna ukweli! Wakati tunajenga tabia ya kujisomea vitabu, basi orodha yetu iwe na kitabu hiki cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment