UHAKIKI WA KITABU: MPE MANENO YAKE.
1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA.
Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Mpe maneno yake na kimetungwa na Freddy Macha. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Limited na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 411 320. Kimechapishwa mwaka 2006 kikiwa na kurasa 188. Na anayekihakiki sasa hivi kwenye safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. UTANGULIZI.
Mpe Maneno Yake ni mkusanyiko wa visa mbali mbali vilivyosibu na kuibuka sehemu tofauti alizoishi na kusafiri Freddy Macha, katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Kwa mtu anayesoma Mwananchi Jumapili, atakuwa amevizoea visa hivi vya Freddy Macha, vyenye ucheshi na kejeli na kuficha masuala muhimu ya kijamii, hasa yale yanayowakumba watu wa hali duni.
Visa hivi ni vifupi vifupi na vingine viko kwenye mtindo wa barua, hivyo havimchoshi msomaji, bali vinavunja mbavu, vinasisimua na wakati huohuo vinaumiza kichwa. Kwenye dibaji Freddy Macha, anatoa nukuu mbali mbali za kuwaandaa wasomaji wake:
“Sumu ya neno ni neno” hii ni methali Kiswahili, “ Huwezi kujua kamwe maneno uliyoyatamka yataleta maana gani kwako mwenyewe au kwa mtu mwigine; ama ulimwengu wa maneno utakayoyaumba utakuwaje. Lolote lile laweza kutokea. Tatizo la kukaa kimya ni kwamba tunajua nini hasa kitatokea” haya ni maneno ya Hanif Kureishi, mtunzi wa riwaya mwenye asili ya Kihindi, yaliyoandikwa katika gazeti la The Guarian (Uingereza Juni 2003),
“ Jambo ninalotaka kuleta katika ushairi wa kiswashili ni utumiaji wa lugha ya kawaida; lugha itumiwayo na watu katika mazungumzo yao ya kawaida ya kila siku” Haya ni maneno ya Euphrase Kezilahabi, mwandishi, mwanataaluma na mwanafasihi wa lugha ya Kiswahili, kutoka utangulizi wa mkusanyiko wake wa tenzi “kichomi” 19774.
Kwa kuendelea kumwandaa msomaji Freddy Macha, anasema: “ Hata hivyo, nimezikusanya hadithi na visa hivi kutokana na dhamira zake kwa kuamini, kwa kiasi kikubwa , ziko dhamira ambazo ni kama nyuzi za rangi mbalimbali zinazojitokeza kwenye nguo popote nilipokuwa na wawakati wowote. Ninawaachia wasomaji kujaribu kutambua nyuzi hizi na hata zingine kwa kukubaliana na maneno ya Hanifu Kureishi na wenzake hapo juu”
Kitabu hiki kinazo sura tano. Kila sura imegawanyika katika visa mbali mabli vilivyotokea sehemu tofauti tofauti duniani. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki cha Freddy Macha.
III.
MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU
Freddy Macha, alianza uandishi alipokuwa akifanya kazi na magazeti ya Uhuru na mzalendo na baadaye kuwa mwanasafu wa gazeti la kila Jumapili la Sunday News hadi mwaka 1984. Vitabu vyake viwili vya Kiswahili, Twen’zetu Ulaya na Mwanamuziki Remmy ongala vilichapishwa mwaka 1984, na 1986. Amewahi kushinda tuzo kadhaa za uandishi ikiwemo ushairi – BBC mwaka 1981 na hadithi fupi fupi, Jumuiya ya madola mwaka 1996, mjini Lonon.
Huyu ni mmoja wa waasisi wa kikundi cha muziki, mashairi na tamthiliya na ngoma cha “Sayari”. Amesafiri na kuishi nchi nyingi duniani. Amesomea muziki, michezo na usingaji, Brazili a Kanada hadi mwaka 1995. Sasa hivi anaishi London, Uingereza. Anafanya kazi ya kufunisha, ukalimani, michezo, maigizo, sinema na muziki, anaongoza bendi ya Kitoto. Pamoja na kuishi nje ya nchi, Freddy Macha, anaendelea kuandika makala ya visa na mikasa ya kijamii katika gazeti la Mwananchi Jumapili.
Freddy Macha, ni msanii wa kweli. Visa, anavyoviandika vinafichua ukweli huu. Ni vigumu mtu kukataa kwamba visa hivi havikutokea. Hata kama havikutokea, mafundisho yake yanamgusa mtu na kumfundisha. Mfano visa vingi vya Ulaya, Brazili na Canada, vinalenga kutufundisha kulipenda taifa letu, kupenda uafrika wetu na kujivunia nchi yetu kuliko kukimbilia nchi za nje.
Jambo la kushangaza, na laba kuna jambo la kujifunza hapa; chuki anayoionyesha Freddy Macha, kwa maisha ya Ulaya na kwingineko nje ya Tanzania, huwezi kuamini kwamba yeye bado anaenelea kuishi Lonon, Uingereza. Hata hivyo ni vigumu kupinga ukweli anaouweka mbele ya jamii, na hasa jamii yetu ya Kitanzania. Baaaya ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa Muhtasari.
IV. MUTHASARI WA KITABU
Sura ya kwanza inabeba kichwa cha habari Waswahili Bwana. Sura hii ina visa saba. Vitano vilitokea Dar-es-salaam na viwili vilitokea London. Kabla ya visa, vilivyokwenye sura hii Freddy Macha, kama kawaida yake ya kufundisha, anatoa nukuu chache ambazo ni kama muhtasari wa sura au ujumbe muhimu unaobebwa na sura nzima: “…Ehe, nilikuwa nakwambia kuwa watoto wetu wanajua uvumbuzi. Wanapata mshawasha wa kuunda kutokana na mazingira na vitu ambavyo vinawachokonoa mawazo. Mabati, makopo, karatasi, tope, vijiti, visoda, chupa na kadhalika. Mwanao anapenda nini?” Haya yanatoka kwenye utenzi wa “Madaladala(Aprili 1986), wa mwafrika Merinyo,
“Ukubwa wako ulikuwa katika udogo wako
Umeishi kama watu wengi wasiotajwa
Wasiokumbukwa, ambao ndio huumba
Mashujaa na watakatifu..” kutoka kwenye Shairi la Mulokozi, “Kumbukumu ya Ezra Chemere”,
“Penye njaa hakuna sheria”, Maandishi ya ukuta wa barabara ya kwenda uwanja wa mpira wa Marakana, Rio de Janeiro, Brasil,(1994).
Visa vilivyotokea Dar-es-salaam, katika sura hii vinajikita katika maisha ya watoto yatima, ushirikina, mfano wa Paka Mweusi: “ Paka mweusi
Paka jama! Kiumbe mzuri, paka jamaa!... Amegeuzwa kuwa shetani..” (Uk.8), kisa hiki cha paka mweusi kinatufunulia ukweli tunaoishi nao wa kuamini majini, hata paka,na hasa paka mweusi anachukuliwa kuwa ni jini! Visa vingine vinagusia mahusiano na maisha ya uswahilini, manyanyaso wanayowapata watu wanaofanya kazi kwa wahindi na mbinu ambazo watu wanafanya kuwaibia wahindi katika biashara zao na hasa biashara za mahoteli. Kazi nyingi, mshahara kidogo, chanzo cha kukoswa uaminifu!
Visa viwili vya Lonon, vinaongelea mikasa inayowakumba waafrika wanaokwenda kuishi nchi za wangine. Ni vituko vya mapenzi na maisha yote kwa ujumla.
Sura ya pili inabeba kichwa cha habari: Kwaheri Bongo. Sura hii ina visa mchangayiko, vile vya Dar-es-salaam na vya nchi za Ulaya. Sura hii ndiyo ina kisa kinachobeba jina la kitabu: Mpe maneno yake kisa kinachoanza na nukuu kutoka kwa Shabaan Robert: “Usitumie lafidhi,
Kwa watu kuwaudhi,
Lugha humpa hadhi
Kutumia ajuaye…” (Uk. 77).
Kwa kumwandaa msomaji, Freddy Macha, anatoa nukuu mbali mbali kabla ya kuanza kuporomosha visa na vituko: “ Ukiona kwako kunaungua, kwa mwenzio kunateketea” hiii ni methali ya Kiswahili,
“ Baada ya kufanikiwa kupata kile ulichokitaka kwa kazi ngumu, sasa chukua muda mrefu kukifaidi” Ni kutoka mkusanyiko wa maandishi ya H.Jackson Brown, yanayosisitiza namna ya kupata mafanikio katika maisha.
“Usikasirikie ulikoangukia, kasirikia ulikojikwaa” hii ni methali ya kihehe.
“Nafuta machozi na moyo unazidi kulia” Haya ni maanishi kwnye khanga, na “Kanga hazai ugenini” Methali ya Kiswahili. Nukuu zote hizi zinapatikana Uk.76.
Kisa kinachovunja mbavu kwenye sura hii ni kile cha Bwana Halmashauri. Anapata barua ya siri ya kumteua kuwa balozi nchi za nje. Maisha yake yasiyokuwa ya uadilifu yanamtinga kiasi anashindwa kupata muda wa kusoma barua yake yake ya siri, hadi anakufa kwa ajali kabla ya kusoma barua hiyo.
Sura hii ina visa vya nchi mbali mbali. Kinachovutia pia hapa ni barua za Yusufu Pigalaza, kwenda kwa rafiki yake Johnny Nyau. Yusufu Pigalaza, anaishi Denmark na Sweden na Johnny Nyau, anaishi Dar. Barua hizi ni ujumbe kwa wale wanaofikiri kwenda ulaya ni kuukata: “Nnafanya kazi mkahawa mmoja hapa Stockholm unaitwa Macdonalds. Wamarekani. Misosi yenyewe utabloo lakini ndoo noti unaipata leo kesho ishayeyuka. Nna kibonge cha chumba lakini maisha Scandinavia bob, ghali..” (Uk.105).
Barua hizi katika sura hizi, zinatoka nchi mbali mbali: Denmark, Sweden, Italia na Ujerumani. Mwandishi ana lengo la kuonyesha jinsi mtu anavyolazimika kuhama nchi hadi nyingine akitafuta pesa. Maisha ni magumu, ni lazima mtu ahame kila wakati na wakati mwingine anashindwa kurudi nyumbani kwa kushindwa kupata pesa za kumtosha kurudi.
Sura ya tatu inabeba kichwa cha habari Wazungu Bwana. Sura hii ina visa vinne. Visa viwili vya Ujerumani, kimoja cha Amerika na kingine cha London. Kama kawaida yake, Freddy Macha, anamwandaa msomaji kwa sura hii kwa kutoa nukuu mbali mbali, mfano anatoa nukuu ya maandishi aliyoyasoma kwenye mlango wa choo, Herning, Denmark, 1986:
“ Doo!
Taa za mji zinag’ara, nzuri,
Za kuvutia
Lakini wakati wa bomu la nuklia
Litakapoanguka
Mji mzima utaonekana kama unakunya
Unaharisha” (Uk 116).
Nukuu nyingine ni ile ya Alice Walker, mwandishi na mpiganiaji haki za wanawake, mmarekani mwenye asili ya Kiafrika: “ Bila pesa zako mwenyewe, katika jamii ya kibepari, huna uhuru wa kujitegemea hata kidogo” (uk.116).
Sura ya nne inabeba kichwa cha habari Kuonana; kuoneana. Sura hii ina visa vinne; kisa kimoja ni cha Dar-es-salaam, kule Msasani. Ni kisa cha mbwa watatu. Hapa kuna vunja mbavu, lakini na mafundisho juu yake. Je Mbwa wakipandana yanakuwa ni mahaba? Je ndege wanayafahamu mahaba? Mbona wanaimba wakati wa kupandana? Je mahaba ya Mbwa ni mwenye nguvu mpishe? Je mahaba ya mwanadamu hayana mwenye nguvu mpishe? Hivyo nivyo visa vya Freddy Macha. Kama kawaida, anatoa nukuu mbali mbali za kumwandaa mtu kusoma visa vipya kwenye sura hii: “ Imani yangu ni kuwa kama mtu hakupendi wewe ulivyo, bali anakupenda kwa kile unachojaribu kuwa, uhusiano wenu hautadumu. Lakini ukiwa ulivyo bila kujifanya sijui kitu gani, baada ya muda yuko mtu wa hakika atakuenzi ulivyo” (Uk. 140), Haya ni maneno ya mwanamziki Berry Gordy.
Kisa cha pili katika sura hii kilitokea Kopenhangen, Denmark,1984, kinaelezea Disko la Ulaya. Hapa fundisho ni lilelile. Ulaya ni ulaya, ina mambo yake. Mswahili, hata akiishi miaka mingapi, bado ataendelea kuwa mgeni. Haya yanajitokeza kwenye nukuu anayoitoa Freddy Macha, mwanzoni mwa sura hii ya nne: “Sio vizuri kuishi muda mrefu katika nchi ya Wazungu” Haya ni maneno ya Mtabaruka, mshairi na mpiganaji wa falsafa ya afya, urasta na mila za watu weusi Jamaika.
Kisa cha chatu katika sura hii ya nne kilitokea kule Quebec, Kanada Novembea 12,1994. Kisa hiki kinaitwa Uzuri wa Tufaha: “ Wewe houni Bwana…. Juzi juzi mama yangu alitutembelea. Akasema nchi hizi za kizungu ni kama tufaha la kupendeza nje. Unajua tufaha sio? Ushawahi kukuta moja nje zuri sana kumbe ndani ukilikata limeoza? Watu nyumbani wanasikia Marekani, Kanada, Ulaya, lakini si chchote, si lolote. Tunda zuri nje lakini ndani hamna kitu. Ndiyo utapata fedha, utapata elimu lakini sidhani kama watu wa hapa wana furaha sana. Ndiyo maana wazungu wengi wanajiua. Watu huku hawaamini sana Mungu au dini au tambiko. Kila mtu na lwake.” (Uk. 156-157).
Kisa cha nne katika sura hii kilitokea kule Konstanz, Ujerumani, 1987. Hiki kinaitwa, Mturuki, waparaguay na Mimi. Katika kisa hiki Freddy, anajaribu kulinganisha mtu mweusi na wageni wengine kule Ulaya. Ingawa rangi nyeusi inakuwa kama kigezo cha mtu mweusi kuonekana ni mtu wa chini, lakini ukweli ni kwamba wakati mwingine mtu mweusi anakuwa ana uwezo kama weupe na wakati mwingine kuwa juu yao. Unakuta mtu mweusi anaongea lugha zaidi ya tatu au nne, wakati weupe wanaongea lugha moja tu! Nukuu, mwanzoni mwa sura inafafanua kisa hiki vizuri:
“ Mara alipokaa kwenye hoteli hizi, wakati wa chai ya asubuhi au chakula cha mchana bustanini, yaani buffet, wazungu wote walimtupia macho ya kumlaumu vile Mungu alivyomuumba. Lakini punde yaligeuka kuwa macho ya mshangao na wivu walipoona alivyovalia, gari aliloendesha na bakshishi nono alizowaachia wahudumu. Lugha zao pia alizitafuna, ama Kiingereza, Kireno na Kifaransa, ambapo ni wachache kati yao walizifahamu zote”(Uk 140). Haya ni maneno ya Harold Mhando, kwenye riwaya ya Rubi.
Sura ya tano na ya mwisho, inabeba kichwa cha habari: Maisha mapya. Sura hii ina visa vya Brazil. Nukuu zilizokwenye mwanzo wa sura hii zinatoa muhtasari wa visa hivi vya Brazil: “ Nyumbani si pangoni, kama pango la wanyang’anyi. Nyumbani ni mahali ambapo watu wanaishi kwa furaha, mume na mke, watoto wa nyumba ile wote wakiishi kwa furaha” Haya ni maneno ya Mchungaji Anaeli.A.Macha.
“Miye hujitazama ndani ya roho yangu. Sijali nje kuna nini. Macho yangu huchunguza ndani kuna hisi nini. Sijali kwamba watu wanasema nini, maana n’nachokitaka ni mambo ya haki. Unajua tena.” Maneno ya Bob Marley.
“Kitu gani ninatafuta katika maisha haya? Umuhimu! Hicho ndicho ninachotafuta, bwana. Nataka nisimame sawia na watu wa mataifa mengine. Kwa vile unapotembea barabarani na watu wa nchi nyingine, hupewi chapa au muhuri… na ili uwe mtu mkubwa unahitaji taifa kubwa. Ndiyo maana huwa nasema Afrika sisemi Naijeria, Togo au Senegal…” Maneno ya Fela Anikulapo Kuti.
Muhtasari wa visa vya Freddy Macha, unajikita kwenye nukuu ya Fela Anikulapo Kuti, hapo juu. Ingawa ni visa mseto, lakini lengo lake ni kusisitiza thamani ya Mwafrika. Ni kuonyesha thamani ya mwafrika sambamba na watu wengine duniani. Nukuu ya Albet Einstein, anayoitoa ukrasa wa 170, inaonyesha wazi nia yake: “Jaribu usiwe mtu wa mafanikio,bali mtu mwenye thamani”.
V. TATHMINI YA KITABU
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Freddy Macha.
Awali ya yote lazima niseme kwamba visa katika kitabu hiki vinavunja mbavu, vinasisimua na wakati huohuo vinafundisha. Mtu atakisoma kitabu hiki akicheka kuanzia ukrasa wa kwanza hadi wa mwisho, lakini hawezi kutoka mikono mitupu.
Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kubainisha na kisha kutoa majibu kamilifu kwa changamoto zinazowakabili watu wa chini hapa Tanzania, na zile zinazowakabili vijana wanaokimbilia nchi za nje.
Tatu, mwandishi ambaye ni msanii, mwandishi, mwalimu,mkalimani, mwanamichezo, japo kwa njia ya mzunguko unaoambatana na ucheshi na utani mwingi, amefanikiwa kufanya tathmini ya maisha ya watu wa hali duni, maisha ya mwafrika akiwa nchi za wengine na kufichua uongo wa kile kinachobatizwa utandawazi.
Nne, mwandishi amefanikiwa kukifanya kitabu chake kiwe cha kuaminika kwa kutumia mbinu mbalimbali. Kwa mfano amefanikiwa kuthibitisha hoja zake kwa kunukuu mistari ya kutoka kwenye maandishi ya watu mashuhuri, nyimbo, mabango nk. Pia, kule kutaja sehemu ambako visa vilitokea, inaongeza nguvu kitabu chake kuaminika zaidi. Inaonekana si vichesho tu, mtu huyu ameishi kwenye nchi hizi, anasoma vitabu vingi na ni mdadisi wa mambo mengi. Mfano: “ Miaka ya Uhai wa mwanadamu huwa haifikii mia moja; Hata hivyo imejaa huzuni zenye miaka elfu moja” maneno ya Bruce Lee.
“ Hakuna kitu cha ajabu kama kunya katika choo kilichojengwa kwa mabao” Haya ni maanishi ya Kiingereza ndani ya choo kilichopo “ Horombo Hut” Mlima Kilimanjaro.
“Kama ninavyopenda kuwambia watu wa Montgromery, Uhasama mji huu si kati ya watu weupe na weusi. Uhasama kimsingi ni kati ya haki na kutokuwa na haki, baina ya nguvu za mwangaza na zile za giza..”
Nukuu hizi na nyingine nyingi, zinamfanya msomaji, kuviangalia visa na vichesho vya Freddy Macha,kwa jicho la kutafakari.
VI. HITIMISHO.
Kwa kuhitimisha basi, niseme hiki ni kitabu cha kusoma. Kitabu hiki kinamfaa kila mtu katika jamii yetu. Kinafaa mashuleni, kwenye familia, vijiweni na sehemu za kazi. Freddy Macha, anagusia karibu nyaja zote za maisha. Visa vyake na vichekesho vinabeba ujumbe mzito. Inakuwa vigumu kushindwa kuamini kama visa hivi ni vya kweli ama ni vya kutunga. Vile vya Dar-esalaam, ni maisha ya kila siku ya watu wa hali ya chini. Vile vya Ulaya, America, Canada na Brazil, ni changamoto zinazowapata waafrika. Mtu, aliyesafiri nje ya nchi, ataviona visa hivi kuwa vya kweli na vinatoa fundisho.
Hata leo hii ukisoma visa vya Freddy Macha, kwenye gazeti la Mwanachi, vimebeba ujumbe kwa mtanzania, kwamba asitamani nchi za wangeni. Maisha bora na mazuri yako Tanzania! Yeye na familia yake, wanaendelea kuishi London! Maana yake ni nini? Ni ule msemo wa “Sikiliza mafundisho yangu na wala si matendo yangu”. Au anajifanisha na Fela Anikulapo Kuti : “ Kitu gani ninatafuta katika maisha haya? Umuhimu! Hicho ndicho ninachotafuta, bwana. Nataka nisimame sawia na watu wa mataifa mengine. Kwa vile unapotembea barabarani na watu wanchi nyingine, hupewi chapa au muhuri.. na ili uwe mtu mkubwa unahitaji taifa kubwa. Ndo maana huwa nasema Afrika sisemi Naijeria, Togo au Senegal..”
Hata hivyo, Freddy Macha, yuko wazi kiasi cha kujichambua yeye mwenyewe. Kukaa kwake Lonon , si kikwazo cha kusikiliza na kuzingatia nasaha zake. Yuko nje ya nchi, lakini uzalendo wake unajitokeza kwenye maandishi yake na maisha yake!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment