UHAKIKI WA KITABU: MAPINDUZI YA KILIMO KWA KUTUMIA ZANA BORA ZA KILIMO.
1. Rekodi za Kibibliografia
Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Mapinduzi ya Kilimo kwa Kutumia Zana Bora za Kilimo na kimetungwa na Pius B. Ngeze. Mchapishaji a kitabu hiki ni Tanzania Educational Publishers LTD na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN) 978 9987 07 032 9 Kimechapishwa mwaka huu wa 2010 kikiwa na kurasa 68. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. UTANGULIZI
Kitabu hiki kimekuja wakati muafaka. Leo hii wimbo wetu ni Kilimo kwanza. Hatuwezi kuanzisha mbio hizi za kilimo kwanza bila kuwa na ujuzi wa Mapinduzi ya Kilimo kwa kutumia zana bora za kilimo. Na kusema kweli hatuwezi kuendesha kilimo chenye tija kwa kuendelea kutumia jembe la mkono. Kitabu hiki kitasaidia kuwaelimisha na kuwashawishi watanzania kufanya mapinduzi katika kilimo chetu.
Matumizi ya Zana Bora za Kilimo ni sharti mojawapo la kuleta Mapinduzi ya kilimo nchini kama anavyosema Waziri wa Kilimo, Chakula na ushirika Mhe. Stephen Masato Wazira (Mb) “ Dhana ya Kilimo kwanza inatambua kuwa, Mapinduzi ya Kijani yanawezekana tu kwa kutumia maarifa na teknolojia za kisasa, hususan zana bora za kilimo’ (Julai, 2009).
Kuendelea kutumia zana duni au zenye uwezo mdogo kutaendelea kudumaza maendeleo ya kilimo nchini. Zana hizo duni ni hasa jembe la mkono. Zana hii imetumiwa tangu zama za kale, zaidi ya miaka 10,000 iliyopita. Uwezo wa zana hii ni wa kuhudumia heka moja kwa mwaka kwa familia moja.
Zana inayofuatia jembe la mkono ni plau inaotumiwa na wanyamakzi. Jozi ya wanyamakazi inaweza kufanya kazi kwa saa tano mfululizo kwa kipindi cha asubuhi. Baada ya hapo lazima wapumzike. Zana inayofuata ni trekta. Matrekta yanatengwa katika makundi kadhaa kwa kutegemea ukubwa na uwezo wake. Yapo matrekta madogo. Yapo matrekta ya ukubwa wa kati na yapo matrekta makubwa.
Mapinduzi ya Kilimo nchini yatapatikana pale wakulima wengi watakapokuwa na uwezo wa kutumia zana bora za kilimo ambazo zitawezesha kupata mavumo mengi.
Kitabu hiki ni mchango mkubwa katika kuleta mapinduzi ya kilimo katika taifa letu la Tanzania. Ni kitabu kizuri ambacho kinafaa kisomwe na wakulima, viongozi wao na Maofisa ugani.
Mwandishi wa kitabu hiki Mzee Pius Ngeze, ni mwanasiasa mkongwe aliyeamua kustaafu katika uwanja wa siasa na kujikita katika kuandika vitabu. Ameandika vitabu vingi na mwaka huu pekee, ametoa vitabu zaidi ya kumi na vitano. Yeye pia ni mtaalamu wa Kilimo, ndo maana ameamua kuwashirikisha watanzania wenzake elimu hii ili tuweze kwa nguvu zote kushiriki wimbo wetu wa Kilimo kwanza.
Kitabu hiki kinazo sura nane. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na thamini yake.
III. MUHTASARI WA KITABU
Kwa kifupi kitabu hiki kinaelezea historia ya kilimo, masharti ya kufanikisha mapinduzi ya kilimo nchini, maana ya shamba, muundo, majengo na mifumo kwenye shamba, maana shughuli na matatizo ya utumiaji nguvu ya binadamu katika kilimo, vyanzo vya nguvu katika kilimo, aina na kazi za zana na mashine za kilimo, kilimo cha kutumia wanyamakazi na kilimo cha kutumia matrekta.
Sura ya Kwanza inaelezea historia ya kilimo, watu wa kale, mwanzo wa ufugaji na ustawishaji wa mazao, zana za kale za kilimo na mwanzo wa vijiji.
Tunachofunza kwenye sura hii ni kwamba ili mwanadamu kuweza kubadili kabisa mfumo wake wa kuishi, kutoka kwenye kukusanya chakula kwenda kwenye kuzalisha chakula, watu wa kale walipaswa kufikiri jinsi ya kupata zana mpya. Mpaka hapo zana walizokuwa nazo hazikuwa imara, na zilikuwa kwa ajili ya kuvulia, kuwindia, kutegea wanyama na kuchimbia mizizi. Inaaminika kuwa zana ya kwanza ya kulimia ilikuwa ni kisu kilichochongwa gwa kutokana na jiwe gumu na kuingizwa katika mpini wa mti au mfupa.
Zana mpya nyingine zilifuata. Vijiti vya kuchimbia mizizi vilibadilishwa kuwa zana za kutayarishia mahali pa kupanda mbegu na kupalilia. Baadaye watu hao walivumbua moto na chuma. Nao huu ulikuwa uvumbuzi mkubwa na wa muhimu sana. Moto huo ulitumiwa kuota, kupikia na kufukuzia wanyama wakali. Moto huo ulitumika pia wakati wa kufua vyuma ili kutengeneza zana mbalimbali za kufanyia kazi, kama vile visu vya kuchinjia, mashoka na majembe ya mkono.. Hiki kilikuwa ni kipindi cha zana mpya.
Kuvumbua zana mpya za kilimo kulienda sambamba na uanzishwaji wa vijiji na watu kuishi kwenye makundi ya kifamilia na kikabila.. Na wakulima waligawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza lilihusika na ustawishaji wa mazao na kundi la pili lilifuga ng’ombe, mbuzi na kondoo. Wakulima walianza kustawisha aina kadhaa za mazao (uk.5).
Sura ya pili inajadili Masharti ya kufanikisha mapinduzi ya Kilimo nchini; ambayo ni Nchi yetu, Kilimo cha kisasa na mambo ya lazima kwa Maendeleo ya kilimo:
“ Lakini, sehemu kubwa ya nchi hupata milimita za mvua kuanzia 600 mpaka 1,200 kwa mwaka. Mvua ni moja ya mambo muhimu sana kwa maendeleo ya kilimo. Sehemu zenye mvua za kutosha na zinazoaminika hupata mazao mengi ya kilimo karibu kila mwaka. Na sehemu zisizo na mvua za kutosha hazipati mazao ya kutosha. Ili kuepuka njaa inayoweza kutokea, dawa ni kupanda mazao yanayoweza kustahimili ukame pamoja na yale mazao ambayo huuchukua muda mfupi kupevuka, kwa mfano mtama” ( uk.7).
“Mojawapo ya vipingamizi vikubwa vya maendeleo ya kilimo nchini ni wakulima wengi kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya maarifa ya kisasa ya kuendesha kilimo bora. Wakulima hawana budi kuelewa kwamba mimea na mifugo huhitaji kula chakula bora na cha kutosha, huhitaji maji, hewa, joto la kadiri, mwanga wa jua na mahali pa zuri pa kuweza kuishi ili kupata vitu hivyo..” ( uk.8).
Mambo ya lazima kwa maendeleo ya kilimo ni mengi lakini mwandishi anataja yale muhimu kama vile: Watu, Sera na utawala bora, Ardhi, Topografia, tabianchi na kufuata kanuni za kilimo bora.
Sura ya tatu inajadili maana ya shamba, miundo, majengo na mifumo kwenye shamba. Tunaelezwa kwamba ili eneo la ardhi liweze kuitwa shamba, lazima liwe na sifa zifuatazo: Ukubwa wa shamba ujulikane, shamba liwe na mipaka, shamba liwe linatumika na pawepo miundo au/na jengo la aina fulani.
Sura ya nne, inaelezea maana, shughuli na matatizo ya kutumia nguvu ya binadamu katika kilimo. Hapa mwandishi anasahihisha ile dhana ya kufikiri kwamba Kilimo maana yake ni ustawishaji wa mimea ya mazao tu. Maana kamili ya neno hili kilimo ni: Ustawishaji wa aina mbalimbali za mimea, kama vile mimea ya mazao ya kilimo, mimea ya kutoa nishati, mimea kwa ajili ya malisho na mifugo na mimea ya mapambo. Kilimo pia inamaanisha ufugaji wa aina mbalimbali za viumbe, kama vile wanyama wa: Ng’ombe, mbuzi, kondoo, sungura, nguruwe .n.k, ndege, kam vile kuku, bata, batamzinga n.k, viumbe wa majini kama vile samaki na mamba. Kilimo pia ni kumaanisha utunzaji wa mazingira na utafiti katika nyanja na vipengele mbalimbali vya uzalishaji, utafutaji wa masoko na uuzaji wa mazao ya kilimo nchini na katika nchi za nje na kilimo ni kumaanisha pia utafutaji na upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza kilimo.
Tunaelezwa kwamba shughuli za kilimo ni nyingi na zinahitaji nguvu kubwa. Ni vigumu kutumia nguvu za mwanadamu peke yake, tukabadilisha kilimo chetu. Kuna ulazima wa kutumia mashine ili kuleta mabadiliko ya haraka
Sura ya tano inajadili vyanzo vya nguvu katika kilimo ambavyo ni: Binadamu, wanyamakazi, mashine, upepo, maji, fueli, nishati Umeme, sola nishati na nishati atomi.
Sura ya sita inazungumzia aina, kazi za zana bora na mashine za kilimo; hatua za mapinduzi ya utengenezaji na matumizi ya zana za kilimo, maana ya kifaa, zana na mashine, aina na kazi za zana za kilimo.
Sura ya saba inaelezea juu ya kilimo cha kutumia wanyamakazi; historia ya plau, historia ya matumizi ya plau ya maksai nchini, masharti ya kufanikisha kilimo hiki, zana za kukokotwa na maksai, faida za kutumia maksai katika kilimo, mambo ya kuzingatia ili kilimo cha plau kifanikiwe, idadi ya maksai wanaotakiwa, uchaguzi wa maksai, kufundisha maksai kufanya kazi, utunzaji wa maksai na utunzaji wa plau na zana nyingine za maksai..
Sura ya nane inajadili juu ya kilimo cha kutumia matrekta; maana ya trekta, uzoefu wa matumizi ya matrekta nchini, faida za matrekta, mambo muhimu ya kuzingatia na mambo yanayoweza kusababisha matumizi ya matrekta kuleta faida.
Na mwisho kabisa ni marejeo ya vitabu alivyovitumia kuandaa kitabu hiki
IV TATHIMINI YA KITABU
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliyoifanya Mwandishi Mzee Pius Ngeze.
Ni lazima tuanze tathimini yetu kwa kumpongeza Mzee Ngeze kwa jitihada anazozifanya kuielimisha jamii. Mzee huyu alipotangaza kuachana na siasa, kila mtu alishangaa ni kwa nini aliamua kufanya hivyo akiwa na nguvu na wakati wenzake wote bado ndio kumekucha. Kumbe alitaka apate nafasi ya kutumia ujuzi wake kuwaelimisha watanzania wenzake. Na huu basi ungekuwa mwito kwa wataalamu wetu wote wanapostaafu, wasikae tu kuifurahi pensheni yao, bali watumie lugha nyepesi kuandika vitabu katika fani zao. Mzee Ngeze, ameandika upande wa Kilimo, tuna wazee wengine wengi kwenye fani mbali mbali za Afya, Elimu, Ufundi n.k.
Kitendo hiki cha kuandika vitabu ni cha kupongezwa na hii inaonyesha kwamba Mzee huyu ni kiongozi wa kweli. Tunavyofahamu Kiongozi, anaonyesha njia, anafundisha na kuelekeza. Kitabu cha Mapinduzi ya Kilimo kwa kutumia Zana Bora Za Kilimo ni kizuri na changamoto kwa wasomi. Haitoshi kusoma na kujigamba kwamba umesoma bila kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watu wa kawaida kule vijijini. Mzee Ngeze, amefanya kazi kubwa kuhakikisha elimu yake inasambaa na kuwafikia watu wengi.
Lugha iliyotumika kwenye kitabu hiki ni nyepesi na inaeleweka. Kila mtu atakayekisoma kitabu hiki ni lazima akubali kwamba tunahitaji mapinduzi makubwa katika kilimo chetu. Hatuwezi kukimbilia wimbo wa Kilimo kwanza, bila kuwafundisha na kuwashawishi wakulima wetu juu ya kufanya mapinduzi ya kilimo. Kama anavyosema Mzee Ngeze kwenye kitabu chake kwamba:
“ Mapinduzi ya Kilimo nchini yatapatikana pale wakulima wengi watakapokuwa na uwezo wa kutumia zana bora za kilimo ambazo zitawawezesha:
- Kulima na kuhudumia maeneo makubwa zaidi ya ardhi kuliko ilivyo sasa.
- Kuwahi majira ya kupanda mbegu au vipando,
- Kuyapalilia, kuvuna na kutayarisha mavuno mapema.
- Aidha, mapinduzi ya kilimo nchini yatatokana na; Kupanda mbegu bora ambazo huzaa sana, ni kinzani kwa magonjwa, wadudu na visumbufu vingine,
- Kutumia maji ya kumwagilia. Maji hayo yanaweza kutokana na; vyanzo vya maji asili, kama vile maziwa na mito,
- Vyanzo vya kuandaa au kujenga, kama vile mabwawa, uvunaji wa maji kwenye mapaa ya majumba au yale yanayotiririka, kudhibiti visumbufu vya mimea yaani wadudu waharibifu , kuzuia uharibifu wa mazingira kwa kupanda miti iliyo rafiki kwa ardhi, kuzuia mmomonyoko wa ardhi, wakulima na viongozi kujielimisha juu ya kanuni bora mpya za kilimo cha mazao wanayoyastawisha. Kila zao lina kanuni zake. Vitabu vinavyofaa vipo, lakini haviwafikii wakulima, viongozi wao na maofisa ugani. Iwapo elimu mpya iliyomo katika vitabu hivyo ili kuleta mapinduzi ya kilimo na
Kwamba wakulima kupata bei nzuri si chini ya asilimia 80 kwa mazao yao. Hii bei inayopatikana kwenye soko inawezekana kwa kuondoa mfumo wa uuzaji wa mazao wenye mlolongo wa matumizi na kudhibiti kiasi cha faida wanachokipata watayarishaji na wanunuzi wa mazao ya wakulima wanayouza nchini na katika nchi za nje.
Kitabu hiki kilivyoandikwa kinafaa kufundishia elimu ya kilimo katika shule za msingi na sekondari. Lakini pia kinafaa kwenye vyuo vyetu ambavyo mara nyingi masomo yanafundishwa kwa kingeleza, lakini maafisa kilimo wanakwenda kuwaelekeza wakulima kwa lugha ya Kiswahili. Hivyo kitabu hiki kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa maofisa wa kilimo.
V. HITIMSHO.
Kwa kuhitimisha, ningewashauri watanzania wakitafute kitabu hiki na kukinunua a kukisoma. Kitabu hiki ni muhimu sana kwa wakulima wote. Kinaelimisha na kufundisha. Kwa kujisomea mtu anaweza kuwa ujuzi wa kutumia zana bora katika kilimo.
Lakini pia kwa vile sasa hivi tunaimba wimbo wa Kilimo kwanza, huku tukishindwa mbinu za kuendesha kilimo kwanza, naishauri serikali kununua vitabu vingi vya Mapinduzi ya Kilimo kwa Kutumia Zana Bora za Kilimo na kuvisambaza nchi nzima. Ni matumaini yangu kwamba serikali itakuwa imefanya kitendo cha maendeleo. Hakuna mtu atakayesoma kitabu hiki na kuamua kuendelea na kilimo cha zana duni. Hii pia ni changamoto kwa serikali, maana watu wakisoma na kuelewa wataishinikiza serikali kutoa mitaji kwa wakulima ili waendeshe kilimo cha zana bora.
Hatuwezi kuimba Kilimo kwanza bila ya maandalizi. Na si kwamba kilimo kwanza kitakuja kama vile mvua za masika. Ni lazima watu wajitokeze kama alivyofanya Mzee Pius Ngeze, waandike vitabu, na wengine wafundishe, na wengine wabuni mbinu za kuenesha kilimo kwa njia za kiteknolojia. Kwa njia hii tunaweza kusonga mbele.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
Simu: 0754 633122
www.karugendo.com
1 comments:
Nimesoma uchambuzi/maoni ya kitabu yanapendeza. Tatizo lipo kwenye mikopo kwa wajasiriamali ambao hawana nyaraka zitakazowapeleka benki. Miye ni mkulima mjasiriamali namiliki trekta aina ya Ford 7500. Tabu halina trela wala jembe..... Napataje mkopo nafuu tabu inaanzia hapo!! Nipo kwa 0787519910 ama moddyguyz@yahoo.com.
Msaada kwenye tuta tafadhali!!
Post a Comment