UHAKIKI WA KITABU: KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2010. I. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA. Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Kuelekea uchaguzi Mkuu 2010 na kimetungwa na Dkt.Godfrey B.R. Swai. Amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 – 9987 – 9050 – 1- 0 kimechapishwa mwaka huu wa 2010 kikiwa na kurasa 36. Anayekihakiki sasa hivi ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. UTANGULIZI Kitabu hiki cha Kuelekea uchaguzi Mkuu 2010, kinakuja kwetu wakati tunajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka huu. Mwandishi anayaweka mbele yetu matatizo mawili ya kimsingi na sugu katika Taifa letu. Tatizo la kwanza ni utawala mbovu uliokithiri kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali na fedha za wananchi. Tatizo la pili ni hali ngumu ya maisha duni ya jamii na kupuuzwa kwa mipango ya ustawi wa jamii. Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010 kinachunguza na kupendekeza ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania. Hii ni pamoja na kutanabahisha hatua tano za kuchagua viongozi adilifu kwenye uchaguzi Mkuu wa 2010. Viongozi hawa ndio watakaowajibika na ujenzi wa Mustakabali mpya wa Katiba bora ya utawala wa kidemokrasia na ufanisi bora wa mpango wa maendeleo wa muda mrefu kwa maisha bora ya Watanzania wote. Kitabu hiki kinalenga kutukumbusha kwamba Watanzania tutakuwa tunaelekea uchaguzi mkuu wa 2010 kwa mara ya kumi tangu tupate uhuru nusu karne iliyopita. Itabidi, wakati huu tufanye uamuzi sahihi wa kuchagua viongozi adilifu, wenye itikadi, sera, malengo na mpango bora kwa maisha bora ya jamii. Na kwamba wakati ndio huu: “Kura yako ndiyo ufunguo wa Maisha bora”. Kitabu hiki kina sura sita. Sura ya kwanza ni utangulizi. Sura ya pili inabainisha matatizo sugu ya utawala na maendeleo ya wazalendo. Sura ya tatu inachambua chanzo na kiini cha matatizo sugu. Sura ya nne inabainisha njia za ufumbuzi wa matatizo na ujenzi wa mustakabali mpya. Sura ya tano inaelezea taswira ya mustakabali mpya. Sura ya sita inaainisha hatua za uchaguzi wa Mustakabali mpya wa wazalendo kwenye uchaguzi Mkuu wa 2010. Sura ya saba ni hitimisho. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu hiki, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu chenyewe. III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi. Tutawachagua wabunge, madiwani na Rais. Uchaguzi Mkuu utakuwa na wapiga kura takriban milioni 20 ambao ndiyo idadi ya Watanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi. Wazalendo takriban milioni 15 wenye umri wa zaidi ya miaka 21 wana haki kikatiba ya kugombea nafasi 181 za viti vya Ubunge, Wazalendo takriban milioni 4 wenye umri zaidi ya miaka 40 wana haki ya kugombea nafasi moja ya Urais. Ubunge na Urais ni wito wa ujenzi wa Mustakabali mpya wa mpango bora wa maendeleo na maisha bora ya jamii kwa unyenyekevu na kuheshimu katiba mpya ya wazalendo. Tuna vyama kama 18 vya siasa ambavyo vinajipanga kushinda uchaguzi mkuu na kuliongoza taifa letu kwa sera zake. Kuna malalamiko kwamba chama cha CCM kina nguvu kubwa kuliko vyama vingine na kinatumia nguvu za dola kuwashawishi wapiga kura. Kuna malalamiko ya muda mrefu ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Mbali na malalamiko hayo niliyoyataja, watu wengi ndani na nje ya Tanzania wamekuwa wakijiuliza ni kwa nini Tanzania inaendelea kuwa maskini miaka 45 baada ya uhuru? Nchi zilizopata uhuru wakati mmoja na Tanzania, zinaongoza kwa kasi ya ukuaji wa uchumi duniani na jamii zao wanafurahia maisha bora. Kwanini Tanzania imeshindwa kujenga maisha bora kwa watu wake? Ni katika muktadha huu, mwandishi wa kitabu hiki kidogo ameamua kutuleta Ilani ya Wazalendo inayobainisha kwa muhtasari, chimbuko la matatizo sugu ya utawala, uongozi na maendeleo ya jamii ya Tanzania, mapendekezo ya ufumbuzi wake, namna ya kuyatatua na kujijengea ujenzi wa mustakabali mpya wa kujihakikishia maisha bora. Ilani hii inasisitiza kwamba Wazalendo ndio pekee wamiliki wa utawala na Katiba ya Taifa lao la Tanzania na ndio wenye wajibu na jukumu la kuchunguza kiini cha matatizo sugu, ufumbuzi na kujijengea mustakabali wa maisha bora ya jamii. Vyama vya siasa, Tume za uchaguzi, Rais na viongozi wa chama tawala na Serikali ni vyombo na wakala waliopewa dhamana na Wazalendo. Mwandishi ni Mtanzania, Daktari wa Binadamu na Bingwa wa Afya ya Jamii, mtafiti, mshauri na mwandishi wa vitabu. Ni mwandishi wa kitabu cha Jikomboe kinachohusu mapambano dhidi ya ugonjwa, mlipuko na janga la UKIMWI. Kitabu kinapatikana duka la vitabu la TPH, mtaa wa Samora. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari. IV. MUHTASARI WA KITABU. Sura ya kwanza inaelezea hatua tatu ambazo Tanzania imepitia katika harakati ya kujiendeleza kwa kujijengea maisha bora. Mwandishi anaelezea hatua ya kwanza kwamba ni ile iliyoanzia katika Bonde la Olduvai takriban miaka milioni mbili iliyopita, ambapo wazalendo waliishi kwa uhuru, kujitawala na kujiendeleza. Miaka 200,000 iliyopita wazalendo hawa waliibuka kuwa binadamu wa kisasa na miaka 5,000 iliyopita walianza kufanya biashara na wageni kutoka mabara ya mashariki ya mbali. Hatua ya pili ni ile ya wazalendo kutawaliwa wa wageni na harakati za wazalendo kujikomboa kwa kuanzisha vyama vya wananchi vya wafanyakazi na ushirika wa wakulima kwa ajili ya kutetea haki na masilahi yao kutoka kwa wakoloni. Baadaye vyama hivi vya wananchi viligeuka kuwa vyama vya siasa. Uchaguzi Mkuu wa 1960, ulikuwa ni wa vyama vingi vya siasa ambapo itikadi na sera za chama cha TANU zilichaguliwa na wazalendo kwa ubora wake. Hatua ya tatu ya wazalendo wa Tanzania kujiendeleza kwa kujijengea maisha bora imeanza baada ya Uhuru hadi leo hii. “ Tangu uhuru, Wazalendo wamekuwa wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha duni, kwa takriban nusu karne. Isitoshe uongozi wa chama pekee tawala cha TANU/CCM tangu uhuru unatuhumiwa kwa uporaji wa mali, fedha, kukithiri kwa rushwa na ubadhirifu. Ni dhahiri kwamba Wazalendo wanakabiliwa na matatizo sugu na muda mrefu ya kupuuzwa kwa lengo kuu la katiba, utawala na uongozi ambalo ni ustawi na maisha bora kwa jamii. Kulikoni? “ ( Uk wa 2). Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba Wazalendo wa Tanzania kama binadamu wengine popote duniani wana silika ya kujiendeleza kwa kujijengea maisha bora. Sura ya pili inabainisha matatizo sugu ya utawala na maendeleo ya wazalendo. Tunaelezwa kwenye sura hii kwamba matatizo sugu ya maendeleo ya Wazalendo yamejikita kwenye mapungufu ya Katiba, mfumo na ujenzi wa utawala, uongozi, maendeleo kwa maisha bora ya jamii: “ Wazalendo wamekuwa na mfumo wa utawala wa kidemokrasia kwa mwaka mmoja (1961- 1962), Pili, Katiba ya mfumo wa utawala wa Jamhuri na Rais kwa jumla ya miaka 48......” Mwandishi anatuonyesha jinsi matatizo sugu ya wazalendo yanavyochimbuka kwenye mabadiliko ya Katiba. Ni kwamba Katiba yetu imebadilika mara nne, bila kuwashirikisha wazalendo. Mabadiliko ya kwanza yalifanyika 1962, miezi sita baada ya uhuru na kuunda utawala wa Jamhuri na Rais. Mabadiliko ya pili ya Katiba yalibuniwa mwezi mmoja tu baada ya kuundwa kwa Jamhuri. Viongozi wa chama tawala cha TANU walifanya uamuzi wa kuunda serikali ya chama kimoja; bila rasimu ya kuelewesha na kuomba ridhaa ya wazalendo. Mabadiliko ya tatu ni yale yaliyoingiza Azimio la Arusha, pia bila kuomba ridhaa ya wananchi. Na mabadiliko ya nne ya katiba ni yale yaliyoingiza mfumo wa siasa za vyama vingi na soko huria. Hapa kulikuwa na aina fulani ya kuwashirikisha wazalendo: “ Rais aliteua Tume ya Nyalali ya kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu kuendeleza mfumo wa chama kimoja au vyama vingi vya Siasa. Asilimia 77.2 ya wazalendo 36,299 waliohojiwa walichagua kuendelea na mfumo wa chama kimoja na silimia 21.5 walipendekeza mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa maelezo kwamba hauepukiki. Tume ilitoa mapendekezo takriban 50 pamoja na sheria 40 zinazohitajika kufutwa au kufanyiwa marekebisho. Rais alichangua mapendekezo machache, k.f., kurejeshwa vyama vingi vya siasa na kusitisha siasa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Rais alipuuza mapendekezo mengi ya kimsingi kuhusu kurekebisha Katiba, haki za binadamu, kupanua utawala wa demokrasia, kupunguza madaraka ya Rais, ujenzi wa utawala bora, kuunda tume mpya ya uchaguzi, uhuru wa vyombo vya dola, elimu ya uraia, muungano kuwajibika kwa Bunge, kupanua uhuru wa Serikali za Mitaa” (Uk 10). Maoni ya mwandishi ni kwamba viongozi wa chama cha TANU ni wa kulaumiwa kwa kubadili Katiba bila uelewa, ridhaa ya wazalendo na kutojali ustawi wa jamii. Viongozi wa CCM ni wa kulaumiwa kwa kupuuza mapendekezo ya Tume ya Nyalali, kuendeleza utawala mbovu na hali ngumu ya maisha duni ya jamii. Sura ya tatu inachambua matatizo sugu ya wazalendo. Na uchambuzi huu umejikita kwenye mzunguko hasi na hatari wa vyombo vya ujenzi wa utawala na ustawi wa jamii: Mzunguko huu ni: Katiba duni, Maisha duni, Mpango duni, Utawala mbovu, Sera duni, Uchaguzi duni: “ Matokeo ya itikadi na sera duni za vyama vya siasa pamoja na uchaguzi duni ni ujenzi wa utawala mbovu na uongozi. Matokeo ya utawala mbovu na uongozi ni Katiba duni, mipango duni na maisha duni ya jamii. Hatima ya mzunguko hatari ni kithiri ya matatizo, mauti, majanga na maangamizi ya jamii” (Uk 23). Sura ya nne inajadili ufumbuzi wa matatizo sugu. Hapa mwandishi anashauri tufanye kinyume cha sura ya tatu. Badala ya kuendeleza mzunguko hasi na hatari, tuanzishe mzunguko chanya wenye neema na matumaini. Mzunguko huu ni Sera bora, uchaguzi bora, Utawala bora, Katiba bora, Mipango bora, maisha bora: “ Kwa hapa tulipo na kwa kuzingatia historia yetu na hali halisi, ujenzi wa Mustakabali mpya utakuwa na awamu mbili, Awamu ya kwanza ni ujenzi wa vyombo vya utawala bora na uongozi adilifu, Awamu ya pili ni kutayarisha na kusimika Katiba mpya ya utawala bora kwa kidemokrasia ya wazalendo.” (Uk 25). Mwandisi anaendelea kusisitiza kwamba: “ Tume ya Uchaguzi bora ndio ishara ya kwanza ya ujenzi wa Mustakabali mpya wa maisha bora. Tume ya uchaguzi duni ni ishara ya kuendelea na mzunguko hatari wa matatizo na mauti milele. Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyopo inatiliwa shaka kutokana na kwanza, uteuzi wake kuwa chini ya Rais ambaye ni Mwenyekiti wa chama kimojawapo cha siasa, wagombea na washindani kwenye uchaguzi mkuu” ( Uk 25). Ujumbe muhimu kwenye sura hii ni kwamba Tume ya uchaguzi ndiyo yenye ufunguo wa mlango wa kwanza wa ujenzi wa Mustakabali mpya. Siyo busara kwa Wazalendo kuendelea na Uchaguzi Mkuu chini ya Tume inayotiliwa shaka; ni kufuru ya kuganga matatizo sugu kwa mchezo wa kuigiza. Sura ya Tano inaelezea taswira ya Mustakabali mpya. Tunaelezwa kwamba taswira ya Mustakabali mpya ni mwisho wa fikra, matatizo, msamiati na istilahi za umaskini, ujinga, magonjwa, rushwa na ufisadi. Itakuwa mwanzo wa kuwajibika na lengo kuu la ushindani wa maendeleo na maisha bora ya kila mzalendo na jamii kwenye dunia ya leo na kesho. Ujumbe muhimu kwenye sura hii ni kwamba Mustakabali mpya ndiyo mwisho wa Katiba duni yenye kubadilishwa kila mara na mwanzo wa Katiba mpya ya wazalendo yenye kusimika Haki za Binadamu, ujenzi wa utawala wa kidemokrasia na uongozi adilifu, kanuni na malengo ya mpango wa maendeleo ya muda mrefu kwa maisha bora ya kila Mtanzania na jamii. Sura ya sita inaainisha hatua za uchaguzi wa Mustakabali mpya wa wazalendo kwenye uchaguzi Mkuu wa 2010. Jambo la msingi analosisitiza mwandishi ni hatua ya wazalendo kujiandikisha kupiga kura na kuhakikisha wanaitumia kura kama silaha yao ya kuleta maisha bora. Muhimu zaidi ni wazalendo kuhakikisha wanadai tume huru kabla ya uchaguzi mkuu; wanadai taarifa ya mali na fedha za vyama vya siasa; wanadai Ilani, Itikadi na Sera za Mustakabali Mpya; wanadai rasimu kutayarisha katiba mpya na kudai rasimu ya kutayarisha mpango wa maendeleo. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba wakati tunajiandaa kwa uchaguzi mkuu ni muhimu kuhakikisha wazalendo wanajiandikisha, ni muhimu pia kudai Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Sura ya saba ni Hitimisho. Mwandishi anahitimisha kitabu chake kwa kusema hivi: “ Kila jambo na wakati wake. Babu zetu walipigana vita na wageni wavamizi, waporaji wa ardhi na maliasili. Baba zetu walipigana na waporaji wa kiloni na kurejesha uhuru bila fursa ya kujijengea maisha bora. Jukumu na wajibu wa kizazi cha karne ya 21 ni kujenga Mustakabali Mpya wa maendeleo kwa maisha bora ya jamii kwa milenia mpya. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010 na chini ya Tume bora ya Uchaguzi, wazalendo watachagua chama cha siasa chenye itikadi, sera bora na viongozi adilifu wa kuwajibika na ujenzi wa Mustakabali mpya” ( Uk. 35). V. TATHMINI YA KITABU. Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Dakt. Godfrey Swai. Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana kutokana na hoja anazoziibua na changamoto kubwa ya uchaguzi mkuu katika taifa letu. Pili, mwandishi amefanikiwa vizuri kuelezea matatizo sugu ya wazalendo. Ametuelezea kwamba matatizo haya yamejikita kwenye mapungufu ya Katiba, mfumo wa ujenzi wa utawala, uongozi, maendeleo kwa maisha bora ya jamii. Ameelezea vizuri mabadiliko ya katiba yetu na athari zake: Mabadiliko ya kwanza ya Katiba yaliyozaa Utawala wa Jamhuri na Chama kimoja ameyafananisha na utawala mithili ya Simba dume, tofauti na twiga, utawala kabla ya mabadiliko ya katiba. Ubunifu wake wa kuweka picha za twiga na simba kwenye kitabu chake unasaidia kumvutia msomaji na kumsaidia kutafakari zaidi. Mabadiliko ya pili ya katiba yaliyozaa Jamhuri na Chama pekee tawala anayafananisha na Faru, na kutuwekea picha ya mnyama huyo! : “ Rais akawa pia ni Mwenyekiti wa chama pekee tawala na mamlaka ya “mungu mdogo”; utawala wa nguvu mithili ya faru. Haki za Binadamu hazikuingizwa katika Katiba.....” (Uk 6). Mabadiliko ya tatu ya katiba yaliyozaa Jamhuri, Chama pekee na Ujamaa na Kujitegemea anaufananisha na Tembo. Ametuwekea picha ya Tembo, na hii inasaidia msomaji kufikiri kwa kina. Ni wakati huu Rais, viongozi wa chama pekee tawala na serikali walianza kusimamia njia kuu za uchumi wa wazalendo, kuhodhi madaraka ya vyombo vya maendeleo ya wazalendo. Serikali za mitaa zilivunjwa 1972, pia viongozi walivunja na kuhodhi madaraka ya vyama vya ushirika vya wakulima. Mabadiliko ya nne ya katiba yaliyozaa Jamhuri, vyama vingi vya siasa na Soko huria yalitokana na kurejeshwa kwa vyama vingi vya siasa bila uelewa na ridhaa ya wazalendo. Chanzo cha mabadiliko haya ilikuwa shinikizo la Shirika la Fedha la Dunia.... Vingozi wa chama tawala na serikali walibuni na kutekeleza Azimio la Zanzibar ambalo liliwapa “Ruksa” ya kujihusisha na biashara za soko huria na mabepari kwa njia za uwakala, hisa, ubia n.k. Matokeo yake ni kuunganisha mfumo wa ujenzi wa utawala na tamaa za kuhodhi madaraka, biashara, uporaji wa mali, fedha na ufisadi; utawala mithili ya Nyati. Ametuwekea picha ya Nyati, kutusaidia kufikiri na kutafakari kwa makini. Matumizi ya wanyama mbali mbali kuelezea hali fulani katika jamii yetu, kimekuwa ni kivutio kikubwa katika kitabu hiki. Ubunifu wake huu unafunga kazi pale anapofananisha taswira ya Mustakabali mpya na Tausi. Ametuwekea picha ya tausi nzuri yenye kuvuta hisia za msomaji na kumfanya afikirie Tanzania yenye neema kwa kutumia uhuru wake wa kupiga kura. Tatu, mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuelezea na kuchambua matatizo sugu ya wazalendo kwa kutumia picha ya mzunguko hasi na wa hatari wa: Katiba duni, Mipango duni, Maisha duni, Sera duni, uchaguzi Duni na Utawala duni na baadaye kuelezea kwa ufasaha mkubwa mzunguko chanya na wenye neema wa: Sera bora, Maisha bora, Mipango bora, Katiba bora, utawala bora na uchaguzi bora. Nne mwandishi, ambaye ni msomi, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuelezea mambo magumu ya uchumi na siasa kwa maneno mepesi ya kueleweka kwa kila mwananchi. Hata kule vijijini watu wanaweza kukisoma kitabu hiki na kukijadili. Pamoja na kumpongeza mwandishi kwa kazi kubwa aliyofanya na kuiwasilisha kwetu kwa ufupi kwenye kitabu chenye kurasa 36 tu, ningependekeza abadilishe jina la kitabu. Badala ya Kusema Tanzania Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010; Aseme Tanzania Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, maana yale yote anayoyapendekeza ya Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi hayawezi kufanyika kwa muda mfupi huu uliobakia. Ni wazi kabisa kwamba uchaguzi ujao utafanyika katika mfumo wa zamani unaozaa mzunguko hasi na wa hatari. VI. HITIMISHO. Kwa kuhitimisha, napenda nimpongeze Dkt. Dodfrey Swai, kwa kazi yake nzuri. Pia niwaombe watanzania wakitafute kitabu hiki na kukisoma. Ni bora wazalendo wakafahamu ni kwa nini wanapiga kura na ni kwa nini tuwe na viongozi mbali mbali kila baada ya muda fulani. Kwa upande mwingine ningewashauri watanzania wote watakaofanikiwa kukisoma kitabu hiki, tuunde jukwaa la kujadili changamoto alizoziibua Dkt Godfrey Swai. Tujadili umuhimu wa kuwa na katiba mpya na umuhimu wa kuwa na tume huru ya uchaguzi. Haya ni mambo muhimu sana katika mchakato wetu wa kutafuta maisha bora kwa kila Mtanzania; haya ni mambo muhimu ya kutusaidia kuzuia mzunguko hasi na wa hatari na kuanzisha mzunguko chanya, wenye neema na kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment