UCHAMBUZI WA KITABU: UKIMWI KATIKA FASIHI YA KISWAHILI 1982 – 2006.
1. Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni UKIMWI KATIKA FASIHI YA KISWAHILI . Na kimeandikwa na Adrian K. Mutembei. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Taasisi ya Taaluma Za Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani ( ISBN): 978 9987 531 110. Kimechapwa mwaka 2009 kikiwa na kurasa 242 na anayekihakiki hapa ni Mimi Padri Privatus Karugendo.
11. Utangulizi
UKIMWI katika Fasihi ya Kiswahili ni kitabu cha aina yake, tunaweza kusema kwamba ni kitabu cha kwanza inachozungumza masuala ya UKIMWI kama yanavyojitokeza katika Fasihi ya Kiswahili. Kufuatana na kumbukumbu zilizopo, ushairi ndio utanzu wa kwanza wa fasihi kulijadili janga la UKIMWI hadharani kabla ya tanzu nyingine kufanya hivyo.
Ni ukweli usiopingika kwamba janga la UKIMWI limeleta changamoto nyingi katika jamii nyingi duniani kwa kuwa linazihusu sekta zote katika maisha ya mwanadamu. Mwandishi wa kitabu hiki anaangalia mchango wa fasihi ya Kiswahili (Ushairi) katika kukabiliana na changamoto za ugonjwa huu katika jamii ya Watanzania. Katika kazi hii mwandishi amechambua vipengele vya utamaduni, jinsia, uyatima, unyanyapaa na uelewa wa jamii kuhusu UKIMWI, na mwitikio wao kwa ujumla kuhusu janga hili.
Kitabu hiki pia kinaonesha kwa vitendo, uhusiano wa fasihi na jamii zilizoibua fasihi husika. Mwandishi anaonesha yale yaliyofikiriwa na jamii zetu kuhusu UKIMWI katika miaka ya mwanzoni mwa kutokea kwake. Analinganisha na yale yaliyotokea katika nchi nyingine kama vile Asia, Ulaya , Marekani na nchi nyingine za Afrika.
Kitabu kina sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni fikra. Sehemu hii inajadili kwa kina mawazo yanayotolewa na washairi kupitia katika mashairi yao. Sehemu hii ina sura sita. Sehemu ya pili ni ile ya mizani. Sehemu hii ina mashairi ambayo yamechambuliwa katika sehemu ya kwanza. Haya ni baadhi ya mashairi yaliyoandikwa kati ya mwaka 1982 na 2006. Mengi ya mashairi haya yalichapishwa katika magazeti mbalimbali ya Kiswahili, na machache yaliandikwa tu bila kuchapishwa.
Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu hiki, lakini baada kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu.
111. Mazingira yanayokizunguka kitabu
UKIMWI ni ugonjwa ulioisumbua dunia. Ni ugonjwa uliogusa kila sekta: Tumesikia UKIMWI na haki za Binadamu, UKIMWI na mazingira, UKIMWI na michezo, UKIMWI na utamaduni, UKIMWI na uchumi na sasa Mtembei anatuletea UKIMWI katika Fasihi ya Kiswahili.
Hii ni kazi ya aina yake na hasa pale Mwandishi, anapoyatumia mashairi kuelezea historia ya UKIMWI katika taifa letu. Anaonyesha mchango wa fasihi katika kupambana na ugonjwa huu; mchango chanya na mchango hasi.
Mugyabuso M.Mulokozi, Profesa na mtafiti wa fasihi katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, anasema hivi juu ya kitabu hiki:
“……. Ni kitabu cha kwanza katika Kiswahili kuujadili UKIMWI kwa kina kihistoria -kijamii na kuuhusisha na usawiri wake katika fasihi. Mwandishi, Dkt. A.K. Mutembei, ni mtafiti na mtaalamu wa fasihi na UKIMWI na kazi hii ni matokeo ya utafiti wake wa miaka mingi kuhusu tatizo hili….Kitabu hiki kinafaa kusomwa na watu wote wanaoshughulikia tatizo la UKIMWI, wakiwemo watafiti, wahamasishaji na hata waganga na wauguzi. Kitafaa pia kusomwa shuleni na vyuoni katika masomo ya fasihi na malezi ili kuhamasisha na kuelimisha wanafunzi na walimu kuhusu janga hili”
Naye Profesa Joe. L.P. Lugalla wa Chuo Kikuu cha Newa Hampshire anasema hivi:
“ Katika kitabu hiki, mwandishi anafahamu kwa kina mchango wa Washairi Andishi wa Kiswahili kuhusu janga la UKIMWI. Anavitalii kwa njia inayomvutia msomaji, vipengele vya unyanyapaa, uyatima, jinsia na utamaduni na jinsi vinavyoathiri harakati za kuondoa UKIMWI. Kitabu ni hazina kubwa na kinaweza kutumika katika sekta mbalimbali za elimu”
Profesa Charles Bwenge, wa Chuo Kiku cha Florida, Gainesville, anampongeza mwandishi wa kitabu hiki kwa maneno haya:
“ Kitabu hiki kinausogeza mbele Ushairi wa Kiswahili na kuuingiza katika uwanja mpya wa Afya ya Jamii. Mwandishi anaielezea dhima ya Washairi katika mapambano dhidi ya UKIMWI si katika Afrika Mashariki tu, bali duniani kote inapozungumzwa Lugha ya Kiswahili na kusomwa Fasihi ya Kiswahili.”
Naye Dkt Gideon Kwesigabo, wa Chuo Kikuu cha Muhimbili ana maoni haya juu ya kitabu hiki:
“ Umuhimu wa Kitabu hiki…..umo katika mtazamo wa aina yake wa kuliangalia uanga la UKIMWI kupitia katika Lugha na Fasihi ya Kiswahili. Ni Kitabu kinachononesha athari za UKIMWI katika maeneo mbalimbali ya maisha”.
Mwandishi mwenyewe anatuchorea mazingira yanayokizunguka kitabu chake kwa maneno haya:
“ Nadharia ya msingi inayosukuma mbele mjadala katika kitabu hiki ni ile inayoyaangalia mawazo au fikra za mwanadamu kama zenye nguvu na uwezo wa pekee. Hoja inayoangaliwa tokea mwanzo hadi mwisho ni ile inayoangalia fikra kama viumbe hai:
“ Fikra ni viumbe hai. Hutungwa, huzaliwa, hukua na kufa. Nyingine muda wa maisha yake huwa mfupi, hazidumu; na nyingine maisha yake huwa marefu. Hulelewa katika hatua mbalimbali za kukaa kwake na kuweza kuwaathiri watu. Husambaa na kuenea kutoka eneo moja hadi jingine, zikipingwa au kukubalika; na katika kuenea huko hubadilika, zikipunguzwa au kuongezwa kimo. Fasihi humwathiri binadamu, na binadamu huziathiri fikra. Na jinsi mwanadamu adumuvyo katika maisha ya mapambano, ndivyo fikra zake zibadilikavyo kuakisi ukweli wa wakati; nazo pengine huwa na umri mkubwa hata kumzidi mwanadamu, ambaye akiisha kufa, fikra zake huendelea kuwapo zikienea na kuwaathiri wengine” (Uk. 3).
Aldin Mutembei ana shahada za B.A. (Ualimu); M.A (Isimu) za Chuo kikuu cha Dar-es-salaam; M.A. na Phd (Chuo Kikuu cha Leiden, Uholanzi). Kwa sasa ni Mkurugenzi Mshiriki wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Ameandika vitabu vingine viwili: 1. Ushairi na UKIMWI Tanzania: Mabadiliko ya Sitiari na Metonimia katika jadi Simulizi za Wahaya (2001).
2. Kisiki Kikavu (2005)…. Itaendelea.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment